Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Benki ya dunia yaiorodhesha Tanzania kuwa taifa lenye uchumi wa kipato cha kati
Benki ya Dunia imeiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati.
Hatua hii inajiri miaka mitano kabla ya ruwaza ya maendeleo ya taifa hilo ambapo ilikuwa imelenga kuafikia kiwango hicho kufikia 2025.
Na kufuatia hatua hiyo rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewapongeza wananchi wa taifa hillo kwa mafanikio hayo.
Katika chapisho aliloliweka katika mtandao wake wa twitter rais Magufuli amesema kwamba : ''Huu ni ushindi mkubwa na kazi kubwa tumeifanya, tulipanga kuingia katika uchumi wa kati ifikiapo mwaka 2025 lakini tumefanikiwa.''
Je ni vigezo gani vinavyotumiwa na benki ya dunia
Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya siasa kutoka Tanzania Deus Kibamba benki hiyo hutazama pato la taifa kwa mfano kupitia jumla ya utajiri wa raslimali na ule wa kifedha na kugawanya na idadi ya watu wa Tanzania.
Amesema kwamba mataifa yenye kipato cha kati ya dola 1,006 hadi dola 3,955 kwa mtu mmoja hutajwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati, lakini yaliyo na uchumi mdogo huku yale yenye kipato cha kati ya dola 3,956 hadi dola 12,235 yakidaiwa kuwa mataifa yenye kipato cha kati yenye uchumi unaoimarika.
Lakini je hii ina maana gani kwa taifa la Tanzania?
Kulingana namchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Tanzania Deus Kibamba, ni kwamba taifa hilo linaelekea kuimarika kiuchumi.
Kibamba anasema ni ishara kwamba siasa za taifa hilo zinaenda sambamba na ukuaji wa chumi wa taifa hilo na kwamba sifa hiyo italisaidia taifa hilo kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni hatua ambayo italifanya kuimarika zaidi kiuchumi.
Hatahivyo amesema kwamba Watanzania hawapaswi kufikiria kwamba mifuko yao tayari itaanza kufaidika kutokana na hilo, na badala yake akasema wanahitajika kufanya bidii zaidi ili kuboresha uchumi.
Je ni lipi lililosababisha Tanzania kuwekwa katika orodha hiyo?
Kulingana na Kibamba hatua ya uongozi uliopo kudhibiti matumizi ya fedha mbali na kukabiliana na ufujaji wa fedha ni miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na serikali kufikia malengo hayo yaliyotarajiwa mwaka 2025.
Kulingana na benki ya dunia mataifa yenye kipato cha kati ndio yenye asilimia 75 ya idadi ya watu mbali na asilimia 62 ya watu masikini duniani.