Je ni nini kinachoendelea kati ya Urusi, Marekani na Afghanistan?

Iliyochapishwa

Je tunazipokeaje taarifa za siku za hivi karibu kwamba ujasusi wa kijeshi wa Urusi umekuwa ukilipa kundi la Taliban kuua wanajeshi wa Marekani na nchi zingine za Ulaya? Je taarifa hizo zina ukweli gani? Na je zinaweza kuhakikiwa vipi? Na je zina umuhimu gani?

Kitu cha kwanza kinachojitokeza bayana ni kwamba wahusika wote wakuu waliotajwa katika ripoti hiyo wamekataa kuhusika katika suala hilo.

Serikali ya Urusi imepuuzilia mbali taarifa hizo sawa na Taliban walivyofanya.

Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha vikali kuwa na ufahamu kuhusu suala hilo - huku vyanzo vya habari katika Ikulu ya White House vikiambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba ripoti hiyo haikumfikia rais wala naibu wake kwa sababu idara ya intelijensia haikuafikiana kuhusu uchunguzi wa madai hayo.

Hata hivyo, mashirika makubwa ya habari nchini Marekani yameangazia ripoti kadhaa zikinukuu vyanzo vingi, ikionyesha kuwa tathmini ya ujasusi inaashiria kwamba maajenti wa Urusi walikuwa wakiwalipa Taliban kuwaua wanajeshi wa Marekani au wa muungano nchini Afghanistan tangu mwezi Machi; na kwamba pesa nyingi zilikuwa zimekamatwa katika shambulio la Marekani; hali ambayo inaashiria kwamba huenda waliuawa kutokana na hatua hiyo.

Vyanzo hivi pia vinaonyesha kuwa tathmini ya ujasusi iliwasilishwa hadi viwango vya juu zaidi vya uongozi, pamoja na kutajwa katika mkutano wa kila siku wa rais.

Wakosoaji wa Bw. Trump - mbali na mgombea wa rais wa Democratic, Joe Biden - wametumia ripoti hizi kuangazia maoni yao tena kwamba Bwana Trump hajaonesha utashi wa kisiasa kutetea masilahi ya Marekani.

Lakini jambo la kufurahisha zaidi, ni kwamba hata watu wengine muhimu wa Republican wanaibua maswali - Mwakilishi Liz Cheney wa Wyoming akiuliza swali lisiloweza kuepukika ni nani alijua juu ya tathmini hiyo na ni lini waliijua?

Ni wakati wa malipo?

Lakini kwa nini Urusi ichukue hatua kama hiyo? Huenda, ina sababu kadhaa.

Urusi ina uhusiano wa karibu na Taliban kwa sababu nzuri. Inaona juhudi za Marekani nchini Afghanistan zinaendelea kufifia. Inahofia sana kuongezeka kwa makundi yenye itikadi kali ya Kiislam katika eneo hilo na yamekuwa yakisambaa kuelekea upande wake. Na inaonelea Taliban kama moja ya makundi ambayo huenda yakawaletea shida.

Moscow inaaminiwa kuwasaidia viongozi muhimu wa Taliban kwa silaha na fedha. Na wakati huo pia inaendeleza uhusiano na serikali ya Afghanistan na kwa maneno mapana inaunga mkono mpango wa amani wa Afghanistan, inaangalia maslahi ya usalama wake, ikihofia mambo yatakavyokuwa siku za usoni endapo Afghanistan haitakuwa na hali ya utulivu.

Lakini Urusi pia inapiga vita nchi za Magharibi. Hii inazingatia mambo mengi: Mashambulio ya kimtandao; kampeini za upotoshaji; kuingilia uchaguzi; kufadhili watu wenye misimamo mikali ndani ya nchi za magharibi na kadhalika.

Wakati mwingine, hatua hizo zimeishia kuwa makabiliano ya moja kwa moja: Kwa mfano jaribio la mauaji yaliyotibuka dhidi ya afisa wake wa zamani wa kijasusi kwa kutumia sumu ya neva nchini Uingereza katika mji wa Salisbury, na shambulio la wanajeshi wa Urusi dhidi ya ngome za Marekani nchini Syria baada ya mashambulio ya angani ya Marekani kudaiwa kuwaua raia kadhaa wa Urusi.

Urusi chini ya rais Vladimir Putini imepambana kuimarisha hadhi yake tangu kuanguka kwa muungano wa Sovieti. Hatua ya Marekani kuunga mkono wapiganaji wa Afghanistan inasadikiwa ilichangia Moscow kuondoka nchini humo miaka ya 1980.

Kuna madai kwamba baadhi ya viongozi nchini Urusi huenda hawana mpango wa kulipiza kisasi Marekani kwa kulemaza juhudi zao za zamani na sasa hivi.

Kutoeleweka

Tukio hili pia litakuwa na athari kwa uhusiano wa sasa kati ya Marekani na Urusi. Sera ya Marekani kwa Moscow inakabiliwa na hali ya sintofahamu tangu madai yalipoibuka kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2016.

Pia kuna suala la Marekani kwa upande mmoja kuwa na hofu kuhusu hatua ya Urusi kuimarisha nguvu zake za nyuklia na kutilia shaka mpango wa mpaka wake Mashariki ya kati na kwingineko.

Utawala huu unashirikiana na Urusi kwa njia ya kushangaza, kwa mfano kuhusu madai yake ya kuingilia kampeni ya uchaguzi wa Marekani.

Hali ya kutoeleweka pia inachangiwa na hulka ya rais Trump mwenyewe, ambaye wengi wanamuona kama anawahusudu viongozi wa kiimla.

Kando na hilo, jinsi ambavyo anashughuikia ripoti ya intelijensia anayopewa pia imeleta mabadiliko katika mchakato wa uundaji wa sera za kigeni ndani ya utawala wake.

Vigezo vyote hivi vinaongezea uzito hoja ya upande wa Democratic na Warepublican wenye misimamo mikali, kama vile mshauri wa zamani wa masuala ya usalama wa kitaifa John Bolton, ambaye analalamika hakuna muelekeo maalum wa kuleta pamoja maoni, na kuongeza kuwa yote hayo yanatokana na uongozi kutoka ngazi ya juu.

Taarifa hizi zinajiri wakati ambapo Marekani inajiandaa kwa uchaguzi mkuu kumaanisha zitachukuwa muda kufifia. Hata ikitiliwa shaka endapo kuna kifo chochote kitakachohusishwa na madai ya Urusi kulipa Taliban kushambulia vikosi vya Marekani nchini Afghanistan, itakuwa mwanzo wa mzozo mpya kati ya Marekani na Urusi tangu kumalizika kwa enzi ya vita baridi.

Ikizingatiwa kuwa madai hayo yanatokea wakati ambapo Bw. Trump anaendelea na kampeini ya kugombea muhula wa pili madarakani huku umaarufu wake ukididimia kutokana na jinsi alivyoshughulikia janga la corona na maandamano ya Black Lives Matter bila shaka itaongezea uzito.

Kwa sababu kuna hali ambayo marafiki na maadui wa Washington watalazimika kutilia maanani: kuna uwezekano kwamba rais Trump huenda akashindwa katika uchaguzi. Kando na hilo athari ya kimatibabu, kijamii na kiuchumi iliyotokana na janga la corona, bado inaendelea kuzua mjadala.

Urusi na China zinaongeza juhudi za kujinadi kama mataifa yaliyo na ushawishi mkubwa kikanda, japo dhamira ya Beijing huenda ikawa dhamira ya kutafuta ushawishi zaidi kimataifa. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatathmini uwezekano wa kuleta pamoja eneo la ukanda wa magharibi.

Serikali ya Uingereza inaendeleza juhudi za kufikia kile inachoonelea kuwa faida itakayotokana na hatua yao kujiondoa katika muungano wa Ulaya maarufu Brexit na kufanyia kazi upya sera zake za kigeni chini ya kauli mbiu ya Uingereza ya kimataifa "Global Britain".

Kwa miezi michache ijayo nchi zote hizi zitalazimika kujumuisha katika mipango yao hatua itakayochukuliwa na Marekani: kwa kuzingatia utawala uliopo sasa madarakani na ule unaotarajiwa kuingia uongozini mwezi Januari.

Na utawala wa Biden endapo atashinda uchaguzi haitarajiwi kuwa karibu na Urusi ikiwa taarifa ya nchini hiyo kuwafadhili Taliban itathibitishwa kuwa kweli .