Virusi vya corona: Johnson azungumzia 'mipango ya dharura' iliyowekwa wakati anatibiwa

Chanzo cha picha, AFP
Boris Johnson ameweka wazi kwamba mipango ya dharura ilikuwa imefanywa wakati alipokuwa mgonjwa sana hospitali akiugua ugonjwa wa virusi vya corona.
Katika mahojiano na gazeti la the Sun leo Jumapili, Waziri Mkuu amesema aliwekewa lita nyingi za oksijeni ili kumwezesha kuwa hai.
Anasema uwepo wake katika hospitali ya St Thomas huko London ulimwacha akiwa na hamu ya kutaka wengine wasitaabike kama ilivyotokea kwake na kuhakikisha Uingereza inarejea katika hali yake ya kawaida.
Awali, mchumba wake, Carrie Symonds, alisema mtoto wao wa kiume amepewa jina la Wilfred Lawrie Nicholas Johnson.
Majina hayo yakiwa yametokana na babu yao na madaktari wawili waliomtibu waziri mkuu Johnson alipokuwa hospitali kwasababu ya virusi vya corona, Bi. Symonds aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram.
Kijana wao alizaliwa Jumatano, wiki kadhaa baada ya Bwana Johnson kutoka hospitali alipokuwa anatibiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Katika mahojiano yake kwenye gazeti hilo, waziri mkuu alielezea alivyounganishwa kwenye nyaya kadha kufuatilia hali yake na kubainika kwamba "viashiria vilkuwa vinaenda katika upande usio sahihi".
"Ulikuwa wakati mgumu sana, hilo siwezi kupinga," amenukuliwa akisema, akiongeza kwamba kila wakati alikuwa anajiuliza: "Nitawezaje kuepuka hili?"


Bwana Johnson alibainika kuwa na virusi vya corona Machi 26 na kulazwa hospitali siku 10 baadae. Siku iliyofuata, alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
"Ilikuwa vigumu kuamini kwamba ndani ya siku chache tu, hali ya afya ilikuwa imezorota kiasi kile," waziri mkuu ameliambia gazeti la the Sun Jumapili.
"Madaktari walikuwa wamefanya maandalizi yote kuhusu kile kitakachofanyika iwapo hali itaendelea kuwa mbaya."
Kupona kwake, anasema kulitookana na huduma bora aliopata.
Bwana Johnson anasema alijihisi mwenye bahati hasa ikizingatiwa kwamba wengi bado wanataabika, na kuongeza: "na iwapo utaniuliza mimi, 'Je nimepata msukumo wa kuhakikisha wengine hawapitii tabu hii? ' Ndio, bila shaka uo ndio ikweli.
"Lakini pia nimepata msukumo wa kutaka kuhakikisha nchi yetu inarejea katika hali yake ya kawaida, kuwa imara tena na nina uhakika tutafika tu."
Wagonjwa kidogo bado wamelazwa
Idadi kamili ya waliokufa kwa magonjwa yenye kuhusishwa na virusi vya corona nchini Uingereza hadi kufikia sasa ni 28,131 - ikiwa ni ongezeko la watu 621 kutokea Ijumaa.
Hata hivyo, naibu afisa wa matibabu Uingereza Dkt Jenny Harries anasema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa hospitali kwasababu ya virusi hivyo imepungua kwa asilimia 13 katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Jumamosi, serikali iliahidi kutoa Euro milioni 76 kusaidia watoto walio katika hatari, waathirika wa dhuluma za nyumbani na utumwa mambo leo, waliokwamba majumbani kipindi cha kutekeleza amri ya kutotoka nje.
Taarifa hiyo imefuatia taarifa kwamba kuna ongezeko la ghasia majumbani wiki za hivi karibuni tangu hatua ya kusalia ndani ilipotolewa.

Chanzo cha picha, Carrie Symonds
Bwana Johnson amerejelea kazi yake serikali tangu Jumapili iliyopita. Lakini alikuwa Downing Street kwa siku chache tu kabla ya Bi. Symonds kujifungua.
Alipotuma picha ya mtoto wao kwenye akaunti ya Instagram, alisema jina la pili ya katikati, Nicholas, lilitokana na "Dkt. Nick Price na Dkt. Nick Hart - madaktari wawili walionusuru maisha ya Boris.
Hilo likatoa picha ya jinsi mambo yalivyokuwa wakati waziri mkuu anaumwa baada ya kupata virusi vya corona, amesema mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa BBC Jonathan Blake.
Dkt. Nick Price na Profesa Nick Hart waliwapa hongera zao Waziri mkuu na Bi. Symonds.
Walisema kwenye taarifa: "Tunashukuru kutambuliwa kwetu kwa namna hii, na shukrani kubwa tunatoa kwa timu nzima ya wataalamu tulioshirikiana nao katika hospitali ya St Thomas na kuhakikisha kwamba kila mgonjwa anapokea huduma bora.
"Tunatakia familia hii mpya afya njema na furaha tele."
Matukio mengine:
- Uhispania ilitangaza kuwa kuvaa barakoa itakuwa lazima kwa wote wanaotumia usafiri wa umma kuanzia Jumatatu na kampuni ya Eurostar pia inawataka abiria wao kufunika nyuso zao
- Utafiti umebaini aina fulani ya vipele vinavyowaathiri wagonjwa wa virusi vya corona
- Wawakilishi wa bodi ya kibiashara ya taifa wametoa wito kwa mawaziri kuweka mipango ya kuhakikisha ulegezaji wa masharti ya kusalia ndani kunatekelezwa kwa makini.
- Aliyekuwa mkuu wa jeshi la mbunge Richard Dannatt na aliyekuwa mkuu wa jeshi la ulinzi jenerali David Richards wametoa wito wahudumu wa afya kupewa pesa za ziada












