Virusi vya Corona: Boris Johnson amesema 'hali ingeweza kwenda mrama'

Chanzo cha picha, Twitter/@BorisJohnson via REUTERS
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametoka hospitali baada ya kupona virusi vya corona lakini atapumzika kwanza kabla ya kuanza kurejelelea majukumu yake, kulingana na msemaji wa serikali.
Bwana Johnson, 55, alipelekwa St Thomas' hospital, mjini London, Jumapili - siku ya 10 baada ya kupatatikana na virusi hivyo.
Alikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku tatu kabla ya kurejeshwa kwenye wadi ya kawaida Alhamisi.
Kulingana na taarifa iliyotolewa, Waziri Mkuu ataendelea kupumzika katika makazi ya Chequers.
"Kulingana na ushauri wa timu yake ya matibabu, Waziri Mkuu hatarejea mara moja kazini. Na pia anatoa shukrani zake kwa kila mmoja katika hospitali ya St Thomas kwa uangalizi mzuri aliopokea.
"Na pia maombi yake ni kwa wote walioathirika na ugonjwa huu."
Idadi ya watu waliokufa kwa virusi vya corona hospitali nchini Uingereza inasemekana kupitia 10,000 hadi kufikia Jumapili.
"Hali ingeweza kwenda mrama"
Bw Johnson amesema hali yake "ingeweza kwenda mrama" katika ujumbe wa kuwashukuru wahudumu wa afya waliompatia matibabu.
Amesema katika ujumbe uliopakiwa kwenye mtandao wa Twitter kuwa ameshuhudia "ujasiri binafsi" mkubwa kutoka kwa wafanyakazi wa hospitali ambao wapo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya janga la corona.


Bw Johnson amesema manesi wawili - Jenny kutoka New Zealand na Luis kutoka Ureno - walisimama pembeni ya kitanda chake kwa saa 48 ngumu zaidi akiwa hospitali huku akiwataja wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo ambao walimpa huduma kwa juma moja lilopita na kuwashukuru.
Amesema wahudumu wa afya "wamekuwa wakiendelea kujiweka katika hatari dhidi ya kirusi hatari".
"Ninatoa shukrani kwa ujasiri huu, kujitoa kwao, namna wanavyofanya kazi kwa bidii ni kitu ambacho hakiwezi kushindwa," amesema.

Daktari Ian Abbs, mkuu wa hospitali ya St Thomas, amesema: "Pongezi nyingi kwa timu ya wataalamu wa tiba, pamoja na kila mmoja kwa ujumla kwamba tumeweza kutoa huduma bora kwa waziri mkuu wakati huohuo tukiendelea kutoa huduma za kiwango cha juu kwa wagonjwa wengine tuliokuwa nao.
"Wakati ni haki kusherehekea habari hizi njema, moja kwa moja mawazo yetu tunayaelekeza kwa wale ambao bado wanahitaji usaidizi wetu wakati huu.
"Kwa niaba ya kila mmoja katika hospitali ya St Thomas, natoa wito kwa watu kusalia majumbani na kusaidia kuokoa maisha na kulinda wafanyakazi wote wa afya."

Chanzo cha picha, Reuters
Mchumba wa waziri mkuu, Carrie Symonds, amabaye anatarajiwa kujifungua katika kipindi cha miezi miwili ijayo, amesema kwenye mtandao wa Twitter: "Shukran pia kwa kila mmoja aliyetuma ujumbe wa kheri kutia moyo. Leo hii najihisi mwenye bahati.
"Wiki jana kulikuwa na wakati tulikuwa gizani kabisa. Niko pamoja na wale walio katika hali kama hii, walio na wasiwasi juu ya wapendwa wao ambao ni wagonjwa.
"Nawashukuru zaidi wahudumu wa afya. Wafanyakazi katika hospitali ya St Thomas wamefanyakazi ya kipekee. Siwezi kuwalipa kwa kile walichofanya na sitaacha kuwashukuru."
Bi Symonds amekuwa akijitenga baada ya kuonesha dalili za virusi vya corona lakini bado hajapimwa.


Chanzo cha picha, Reuters
Toka mwaka 1921 Chequers ni makazi rasmi ya waziri mkuu wa Uingereza nje ya jiji la London.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab kwa sasa ndiye anayekaimu nafasi ya kuongoza serikali huku wasidizi wa karibu wakitajia Bw Johnson kurejea kazini walau baada ya mwezi mmoja.
Baba wa waizir mkuu Bw, Stanley Johnson, amemtaka mtoto wake achukue muda ili kupumzika.












