Viongozi wa upinzani Kenya kuwakumbuka wahanga wa Juni 25
Viongozi wa upinzani nchini Kenya wanatarajiwa kuandamana hadi bungeni kuweka shada la maua kuwakumbuka wahanga wa maandamano ya Juni 25, 2024.
Hata hivyo, polisi wamefunga barabara kuu zinazoelekea Bunge la Kitaifa na Seneti.
Maadhimisho ya Juni 25 yanakuja miaka miwili tangu maelfu ya Wakenya wengi wao vijana kulivunja Bunge wakati wa maandamano ya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya ushuru, katika mojawapo ya changamoto kubwa kwa mamlaka ya serikali katika historia ya hivi majuzi nchini.
Kilichoanza kama upinzani kwa Muswada wa Fedha kilibadilika na kuwa vuguvugu pana lililochochewa na kufadhaika kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, ukosefu wa ajira, ufisadi na ukatili wa polisi na utawala mbaya.
Maandamano hayo yaliandaliwa kupitia mitandao ya kijamii na bila uongozi rasmi wa kisiasa, na kuanzisha enzi mpya ya uanaharakati wa vijana nchini Kenya.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema zaidi ya watu 60 waliuawa wakati wa maandamano ya 2024 na ukandamizaji wa usalama uliofuata.
Wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa 2025, watu wengine 16 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa maandamano mapya na mapigano na polisi.
Waandalizi wanasema matukio ya mwaka huu hayakusudiwi tu kuwakumbuka waliofariki, bali pia kutoa wito wa kuwajibishwa kwa maafisia wa waliohusika na vifo vinavyohusiana na maandamano, majeraha na madai ya unyanyasaji wa polisi.
Serikali ilisema itaruhusu maandamano ya amani lakini ikaonya kuwa itachukua hatua kali dhidi ya wale watakaofanya uhalifu na ghasia.
"Kesho ni siku ya kawaida ya kazi na shule," Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen alisema kabla ya maandamano.
"Serikali inaheshimu haki za kikatiba za Wakenya wote kukusanyika kwa amani kwa sababu yoyote ile, siku yoyote, wakati wowote.
Watu binafsi au makundi yoyote yanayotaka kutumia maandamano halali kuzua vurugu, kufanya uporaji, kuharibu mali, kuvuruga biashara, au kufanya vitendo vyovyote vya uhalifu, hata hivyo, yatachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria," Murkomen aliongeza.




























