Virusi vya corona:Serikali Kenya yaapa kuwakamata watu 50 waliotoroka karantini

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC News Swahili
  • Iliyochapishwa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa watu wote 50 waliotoroka kutoka kwenye kituo cha karantini cha watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona mjini Nairobi watakamatwa tena na kurejeshwa tena kwenye vituo hivyo ili waendelee kujitenga kufuatia mlipuko wa Corona.

Akizungumza na kituo kimoja cha redio nchini Kenya, Bw. Kenyatta amesema: ''Tutawatafuta watu wote 50 waliotoroka kituo cha karantini na kuhakikisha wanajitenga kutokana na mlipuko wa Covid -19 wa virusi vya corona''.

Kauli hiyo ya rais wa Kenya inakuja baada video ya watu wasiojulika kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii nchini Kenya ikionyesha watu wakitoroka kituo cha karantini katika Chuo cha mafunzo ya tiba cha Kenya (KMTC).

''Msako wa kuwakamata watu 50 waliotoroka karantini unaendelea,Wakenya waheshimu hatua za kukabiliana na Covid-19.'', alisema rais Kenyatta.

Watu hao walioonekana wakikwea ukuta wa jengo la Chuo hicho na kudondoka kwenye barabara ya Mbagadhi na kisha kuondoka kwa mwendo wa kasi na kuchangamana na wapitanjia wengine na baadae kutoweka.

Kituo cha Karantini katika kilikua na jumla ya watu 200 waliotengwa baada ya kubainika kuwa walikutana na watu waliokuwa na virusi vya corona pamoja na wale waliokiuka amri za kutotoka nje na kutosogeleana.

Inaaminiwa kuwa baadhi walitoroka Jumatatu usiku wakati mvua ilipokua inanyesha na waliosalia wakatoroka wakati wa kifungua kinywa wakati ambao maafisa wa usalama wanakua na shughuli nyingi.

Baadhi ya Wakenya wanaunga mkono hatua ya watu hao kutoroka kwenye kituo cha karantini.

Mmoja wao ni Royn Kean ambaye kupitia mtandao wa Twitter anasema ''Ninawaunga mkono, unawezaje kunilazimisha kulipia karantini''.

Sababu za kutoroka

Baadhi ya watu waliokaa katika maeneo ya karantini wamekua wakilalamika kupitia vyombo vya habari juu ya maisha katika vituo hivyo ambayo wanasema ni ghali kutokana na kwamba wamelazimishwa kujilipia gharama za malazi na chakula.

Wengine wanahofia kuwa kuwekwa katika vituo hivyo bila maambukizi ya corona kunawaweka katika hatari ya kuambukizwa na wenye virusi hivyo ambao wanalazimika kuishi nao katika karantini.

Baadhi wanasema kuwa wasi wasi wa kusubiri kwa muda mrefu kupimwa ili kujua matokeo yao ikiwa wana virusi au la ni jambo linalowaathiri kisaikolojia.

Hata hivyo picha za kituo cha karantini kilichotorokwa na watu 50 zinaonekana kama bweni la kawaida la shule ya sekondari , huku vitanda vyake vikiwa na vyandarua vilivyoning'inizwa vitandani.

Serikali ya Kenya imekua ikikosolewa na makundi mbali mbali kwa kuwaweka washukiwa wa maambukizi ya corona katika maeneo yanayofanana na mahabusu.

Baadhi ya vituo hivyo vya karantini vimetajwa kuwa na hali asipostahili mtu kuishi na kwamba vinawaweka watu waliomo katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya corona.

Ukatili unaodaiwa kufanywa na maafisa wa usalama.

Shirika lakimataifa la haki za binadamu Human Rights Watch linasema kuwa watu takriban sita wamekufa kutokana na ghasia za polisi katika kipindi cha siku 10 tangu serikali ilipotangaza sharia ya kutotoka nje kuanzia saa moja jioni nchini Kenya tarehe 27 Machi,2020 ili kudhibiti kusambaa kwa Covid-19, Human Rights Watch.

Kulingana na Shirika hilo, polisi bila sababu wamekua wakiwapiga risasi na kuwapiga watu masokoni au wanapokua wakirejea nyumbani kutoka kazini, hata kabla ya kuanza kwa kipindi cha marufuku hiyo.

Human Rights Watch linasema polisi wamekua wakiingia kwa nguvu katika nyumba na maduka ya watu.

Kufuatia ukosoaji kutoka makundi mbalimbali juu ya ukatili uliofanywa na polisi katika nguvu katika kaunti ya Mombas, likiwemo shirika la Human Rights Watch, Rais Uhuru Kenyatta aliomba msamaha wa jumla juu ya matumizi ya nguvu yaliyofanywa na polisi, lakini hakuwaagiza polisi kuacha unyanyasaji , linasema shirika hilo katika ripoti yake.

"Inatisha kwamba watu wanapoteza maisha yao kwa kile kinachosemekana kuwa wanalindwa na maambukizi ," amesema Otsieno Namwaya, mtafiti wa ngazi ya juu wa Human rights Watch barani Afrika "Ukatili wa polisi sio tu unakiuka sharia ;bali pia hausaidii katika vita dhidi ya kuenea kwa virusi ."

Hatua zilizochukuliwa hivi karibuni kudhibiti coronavirus

Hatua za dharura zilizochukuliwa ni pamoja na kufungwa kwa baa zote na wenye hoteli kuruhusiwa tu kuuza chakula cha kwenda kula nyumbani.

Ibada za Kanisa na Sala za pamoja Misikitini zimesitishwa huku mazishi ya kiruhusiwa kuhudhuriwa na familia ya marehemu pekee.

Sherehe za harusi pia zimepigwa marufuku.

Masharti mengine ya kuzuia maambukizi Kenya

  • Marufuku ya usafiri wa kuingia na nkutoka Nairobi na miji mingingine mitatu pwani ya Kenya ambayo ina visa vya juu vya maambukizi ya virusi vya corona.
  • Ndege za kimataifa zilisitishwa kuanzia Jumatano Machi 25 ispokuwa ile ya kubeba mizigo.
  • Wageni wote wanaongia nchini kutoka mataifa yaliyoathiriwa watalazimika kujitenga binafsi kwa gharama zao.
  • Wakenya katika mataifa ya kigeni wametakiwa kufuata muongozo wa nchi husika
  • Atakayekiuka maagizo ya karantini atakamatwa kama afisa wa ngazi ya juu wa serikali aliyetiwa mbaroni pwani ya Kenya.