Ndingi Mwana a'Nzeki: Askofu aliyekiri kusema uongo mara moja azikwa Kenya

Aliyekuwa mshindi wa tuzo la Nobel nchini Kenya marehemu waangari Maathai na askofu Ndingi Mwana a'Nzeki

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aliyekuwa mshindi wa tuzo la Nobel nchini Kenya marehemu waangari Maathai na askofu Ndingi Mwana a'Nzeki
Iliyochapishwa

Askofu Ndingi Mwana a'Nzeki, ambaye amefariki akiwa na miaka 89 amezikwa leo Jumanne jijini Nairobi baada ya kuishi maisha marefu yenye kumbukumbu tele ikiwemo za kupambania haki na Amani nchini Kenya.

Yeye mwenyewe amekiri katika uhai wake kuwa alisema uongo mara moja tu.

Ni wakati ule ambao alimsaidia mshindi wa tuzo ya Nobel Peace Prof. Wangari Maathai kukwepa vikosi vya usalama wakati serikali ilikuwa inakiuka haki za binadamu kwa wanaharakati mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Askofu Mwana a'Nzeki alikuwa sehemu ya mpango wa kutoroka ambao Prof Maathai alijifanya kuwa mgonjwa na mwanamke wa kiislamu wa jamii ya Kisomali kabla ya kusimamishwa na maafisa wa polisi kwa muda katika eneo la ukaguzi, kabla ya kuendeshwa kwa kwa km 200 mpaka nyumbani kwake katika mji wa Nakuru.

Prof Maathai, alikuwa mwanaharakati maarufu wa masuala ya haki za binadamu na mazingira, siku hiyo alikuwa amevalia vazi la hijabu akiwa na dereva wake ambaye alikuwa padre, walilazimishwa kusimama katika barabara iliyokuwa imefungwa.

Askofu Ndingi Mwana a'Nzeki alikuwa akiomba katika kanisa la Holy Famili Basilica Nairobi

Chanzo cha picha, Getty Images

Polisi aliuliza "anaumwa huyu?" Padre alijibu kuwa ndio, na afisa akawaruhusu kuendelea na safari.

Siku iliyofuata Prof Maathai na askofu huyo waliambatana na kuitisha mkutano.

'Unakufa mara moja tu'

Mamlaka ilikataza mkutano huo lakini askofu alikaidi na kuendelea jambo ambalo lilipata wafuasi wengi na kufanya serikali ya rais Daniel arap Moi kudhalilishwa.

Askofu Maurice Crowley, ambaye alikuwa anamjua askofu huyo huyo kwa miaka 40, anamkumbuka kama mtu aliyekuwa shujaa duniani, ambaye si muoga na hakuwa na kinyongo.

"Alikuwa rafiki hata kwa wale ambao angeliwaona kuwa ni wakosefu ili kuwafundisha namna ya kufanya mambo sawa, na watu walikuwa wanamsikiliza,"Askofu Crowley aliongeza.

Wafuasi wa Askofu Mwana a'Nzeki watamkumbuka kwa jitihada zake za kukabiliana na zilizolipuka katika maeneo ya Rift Valley mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Makumi elfu ya watu walihamishwa kutoka kwenye makazi yao kwa nguvu na khofu naye alikodisha malori na kuwabeba na kuwapatia hifadhi kwenye makanisa.

Askofu Mwana a'Nzeki alikuwa ni mtu wa kupaza sauti yake, akikituhumu chama tawala cha wakati huo cha Kanu, kuwa kilikuwa kinatumia vurugu dhidi ya wapinzani wake ili kubaki madarakani.

"Nina taarifa kuwa vijana wamepatiwa mafunzo ili kuwafanyia vurugu na kuwatimua wale ambao hawakiungi mkono chama cha Kanu.... Serikali inabidi iingilie kati kwa kutumia katiba ili kuhakikisha kuwa wanatoa ulinzi," alisema hayo kwenye misa kanisani.

Rafiki zake walimuonya na kumwambia kuwa anahatarisha maisha yake na kuwapuuzia kwa kusema: "Mtu anakufa mara moja."

Katika mahojiano mwaka 2000, Askofu Mwana a'Nzeki alisema kuwa kipindi kile klikuwa katika wakati mgumu zaidi wa maisha yake.

"Nimeona watu wasio na hatia wakinyanyaswa… na kuuliwa. Nyumba zikiwa zinachomwa huku watu wakikanusha maoni yangu," alisema.

Vita viliwashinikiza makumi ya maelfu ya watu kutoroka nyumba zao

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukiachilia harakati zake za kupambania haki na amani, askofu Mwana a'Nzeki alikuwa kinara wa kutunza utamaduni wa Afrika ndani ya kanisa Katoliki.

Muonekano wake wa mavazi ulikuwa tofauti na maaskofu wengine wa katoliki, alikuwa anavaa kofia aliyopewa na rafiki yake wa Ethiopia.

Padre Lawrence Njoroge, ambaye alifanya naye kazi alisema kuwa alifurahia muziki wa Afrika na muziki wa kale hususani vibao vya Fadhili William, Fundi Konde, Amadeus Mozart na Ludwig van Beethoven".

Utata wa matumizi ya kondomu

Askofu Mwana a'Nzeki alikuwa mtetezi wa ndoa za kiafrika akitaka zitambuliwe na kanisa Katoliki.

"Waumini wengi walikuwa wamefunga ndoa zao za kimila na kutokana na sababu mbalimbali walikuwa hawajafunga ndoa kanisani. Aliandika katika chapisho lake mwaka 1994.

Licha ya jitihada za kuleta mabadiliko askofu Mwana a'Nzeki alishindwa kuwashawishi watu kufunga ndoa kanisani, na kwa tafsiri ya kanisa lake, kuendelea kutenda dhambi.

Askofu Ndingi alikosana na wanaharakati kuhusu jinsi ya kukabiliana na virusi vya HIV/Aids

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Askofu Ndingi alikosana na wanaharakati kuhusu jinsi ya kukabiliana na virusi vya HIV/Aids

Askofu Ndingi alijulikana pia kwa kupinga sana matumizi ya kondomu, licha ya kwamba Shirika la Afya Duniani (WHO) liliwataka watu kutumia ili kujikinga na maradhi ya ngono na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

"Ukimwi... umekua kwa kasi kwa sababu ya upatikanaji rahisi wa kondomu ," aliwaambia watu mwaka 2003, na kusababisha taharuki miongoni mwa wanaharakati kuwa wamekatazwa kusambaza kondomu kwa sababu zinapingwa kanisa Katoliki.

Askofu Mwana a'Nzeki, alizaliwa siku ya Krismasi mwaka 1931,alikuwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watano. Alipata upadri mwaka 1961, na alikuwa akilihudumia kanisa mpaka alipostaafu mwaka 2007.

Alifariki Machi 30, kutokana na matatizo ya kiafya na uzee. Amezikwa Nairobi katika eneo la kanisa la Holy Family Minor Basilica.

Misa yake itakuwa katika kanisa basilica, lakini kutokana na mlipuko wa corona, mazishi yake yamehudhuriwa na watu 100 tu na waumini wake wakifuatilia mazishi kwenye televisheni.