Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Coronavirus: Uganda yathibitisha kesi 18 za coronavirus
Uganda imeripoti kuwa na kesi mpya nne za maambukizi ya virusi vya corona na hivyo kufanya taifa hilo kuwa na jumla ya maambukizi ya wagonjwa 18.
Rais Yoweri Museveni alisema kuwa visa hivyo vimegunduliwa baada ya watu 197 waliowasili kutoka Dubai kupimwa siku ya Alhamisi.
Watu wengi waliokutwa na maambukizi nchini Uganda walikuwa wanatokea Dubai.
Kwa sasa biashara katika mji mkuu wa Uganda na nchi nzima kwa ujumla zimesitishwa baada ya rais kuweka katazo la usafiri wa umma kwa kipindi cha wiki mbili kuanzia Jumatano iliyopita.
Suala la uchumi kushuka ndio jambo ambalo wengi walilalamikia na vilevile watu kushindwa kujimudu na maisha yao ya kila siku kwa kushindwa kupata kipato chao cha kila siku wakati serikali haijatoa msaada wowote.
Kumekuwa na purukushani nyingi mitaani kwa polisi kufukuza raia kuondoka mitaani.
Rais Yoweri Museveni alitangaza usiku wa Jumatano kupiga marufuku ya usafiri wote wa umma kote nchini humo ili kuzuwia kusambaa kwa coronavirus.
Hii imeleta athari kubwa kwa mamilioni ya watu -na situ kwasababu inazuwia matembezi yao bali pia kwasababu inaathiri mapato ya baadhi ya watu wengi waliomo hatarini zaidi.
Watu hawawezi kufika kazini au katika biashara zao, hii ikimaanisha kuwa hawana kipato cha kuwawezesha kuishi.
Wafanyakazi au vibarua wanaopokea malipo ya kila siku kulingana na kazi wanayoifanya pia wanaumia.
Masoko yameamrishwa kuuza bidhaa za chakula pekee.
Biashara za maduka, usafiri na majumba ya kibiashara mjini Kampala vimefungwa .
Leo asubuhi video ilianza kusambaa ya vikosi vya usalama vikiutawanya umati wa wauzaji wa bidhaa na watu katikakati ya jiji la Kampala.
Polisi na wanajeshi wameshutumiwa kutumia nguvu kupita kiasi , ambapo walionekana wakiwapiga watu mitaani.
Waandishi wa habari wanasema kuwa ingawa maduka hayapaswi kufungwa kulingana na maagizo ya rais , vikosi vya usalama vimefunga biashara zote mjini Kampala isipokua maduka ya jumla na migahawa ya chakula.