Coronavirus: Watakaopotosha wa jamii kuhusu corona kuwajibishwa Tanzania

Rais Magufuli amekemea tabia ya watu kufanya mzaha na kutisha wengine kupitia mitandao ya kijamii

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais Magufuli amekemea tabia ya watu kufanya mzaha na kutisha wengine kupitia mitandao ya kijamii
Iliyochapishwa

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amekemea tabia ya watu kufanya mzaha na kutisha wengine kupitia mitandao ya kijamii juu ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Badala yake Rais Magufuli amewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuzingatia mbinu zinazozuia kusambaa kwa ugonjwa huo.

"Watu tusitishane, tunatishana mno. Niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa Madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa Corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu" amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumapili alipohudhuria Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuagiza kwamba wapotoshaji kuhusu Corona na wafanyabiashara wanaopandisha bei kiholela kwa bidhaa za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa corona wachukuliwe hatua kali.

Maelezo ya video, Coronavirus: Utajuaje kuwa umeathirika na virusi?

Tangu kuibuka kwa ugonjwa wa homa ya mapafu, Corona, mitandao ya kijamii na vyanzo vingine ya habari vimekuwa vikijaa na taarifa mbalimbali zikiwemo zinazokinzana na zile za wataalamu wa afya.

Sanjari na hilo, katika baadhi ya maduka yanayouza bidhaa kama barakoa na vitakasha mikono (sanitizer) bei ya bidhaa hizo imeonekana kupanda maradufu, ikilinganishwa na ile iliyokuwepo awali kabla ya kuibuka kwa ugonjwa wa Corona.

Kufuatia hayo, Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) na wakuu wa mikoa kufuatilia hali hizi na kuwawajibisha wale wote watakaobainika kuhusika ama katika kupotosha jamii kuhusu Corona au kupandisha bidhaa zinazohusiana na Corona

Majaliwa ameyatoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza nna Wakuu wa Mikoa yote nchini, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa kwa njia video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Upotoshaji katika mataifa mengine Afrika

Nchi zingine barani Afrika kama vile Kenya na Afrika Kusini wamefanya upotoshaji wa taarifa za Corona kuwa kinyume na sheria na wanaothibitika kufanya hivyo huweza kushitakiwa.

Katika mazungumzo yake na viongozi Majaliwa ameelekeza pia kwamba wanaohusika na kutoa taarifa za ugonjwa wa Corona ni Wizara ya Afya, yeye mwenyewe Waziri Mkuu na itakapobidi Rais.

Amewataka pia wakuu wa mikoa kuongeza jitihada za kutoa elimu zaidi kuhusu ugonjwa wa Corona na kuwahimiza kubuni mbinu mbalimbali ambazo zitawezesha kufikisha taarifa kwa wananchi wengi zaidi iwezekanavyo.

"Nendeni kwenye maeneo ya mikusanyiko, vituo vya mabasi kutoa elimu kwa umma na kuwaondoa hofu. Upande wa maofisini, viwandani na kwenye mgodi kuwe na utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyakazi kila siku asubuhi watumie hata robo saa kabla ya kuanza kazi waelekezwe namna ya kujikinga," amesema Majaliwa.

Unachohitajika kufanya ili kuzia mambukizi ya virusi hivi

Hadi hivi sasa, Tanzania imetangaza wagonjwa 12 waliothibitika kuambukizwa ugonjwa wa Corona. Mamlaka zimesema wagonjwa wote hawa wapo chini ya usimamizi wa karibu na uangalizi wa wote wanaoaminika kuwa wamekutana nao kwa namna moja au nyingine.

Kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo nchini, mamlaka zimechukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kufunga shule, vyuo na vyuo vikuu, kupiga marufuku mikusanyiko mikubwa ya umma na kuhimiza watu kuzingatia kanuni za usafi, hasa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni.

Hata kama maambuki nchini Tanzania hayajafikia kiwango cha juu kama kilichoshuhudiwa katika nchi zingine barani Ulaya na Asia, athari za kiuchumi za ugonjwa huo zimeanza kuonekana nchini Tanzania, hasa upande wa visiwa vya Zanzibar.

Mwishoni mwa wiki hii, Waziri wa Utalii Visiwani Zanzibar Mahmoud Thabit alisema kwamba takribani asilimia 95 ya hoteli zote za kitalii visiwani humo zimefungwa na kwamba asilimia tano iliyosalia, zinatarajiwa kufungwa kufikia mwishoni mwa wiki ijayo.

Hali hiyo inatarajiwa kuathiri uchumi wa Zanzibar kwa kiasi kikubwa kutokana na utegemezi wa visiwa hivyo katika sekta ya utalii kuingiza fedha za kigeni na kuchangia katika bajeti kuu.

Kwa mujibu wa baadhi ya takwimu, zaidi ya asilimia 60 ya fedha za kigeni na bajeti kuu ya Zanzibar inategemea sekta ya utalii.

Hatua zilizochukuliwa na mataifa ya Africa kukabiliana na coronavirus