Ferdinand Waititu: Gavana wa kwanza kuondolewa madarakani Kenya

    • Author, Wanyama wa Chebusiri
    • Nafasi, BBC Africa, Nairobi
  • Iliyochapishwa

Bunge la seneti la Kenya limepiga kura ya kumuondoa madarakani gavana wa jimbo la Kiambu Ferdinand Waititu maarufu Babayao kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Katika hatua ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na ghamu nchini Kenya, maseneta 27 kati ya 38 waliopiga kura usiku wa kuamkia Alhamisi, waliidhinisha hoja ya kumwondoa mamlakani Waititu iliyopitishwa na bunge la kaunti ya Kiambu mnamo Disemba mwaka 2019.

Safari ya kumfurusha madarakani Ferdinand Waititu ilianza mwaka jana katika kaunti yake ya kiambu wakati madiwani walipopiga kura ya kutokuwa na imani naye.

Madiwani wa Jimbo la Kiambu walidai kuwa Bw Waititu alijihusisha na ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka, ukiukaji wa katiba na sheria nyinginezo, mashtaka ambayo yaliidhinishwa na Seneti.

Inadaiwa kwamba bw Babayao alitumia ushawishi wake kujinufaisha kifedha, kutoa zabuni za mamilioni ya pesa kwa kampuni za jamaa wake kutoa hudumu katika kaunti ya Kiambu.

Madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi

Mwaka 2019 Waititu, mke wake Susan Wangari Ndung'u na binti yao, Monica Njeri walishtakiwa kortini kwa kuchukua zabuni ya pesa za Kenya Shilingi milioni 588 (sawa na dola 6,000,000) bila ya kufuata sheria.

Hatua ya serikali ya Kiambu kuzipa kampuni zinazomilikiwa na watu wa familia ya Waititu zabuni inakwenda kinyume na sehemu ya 66 (8A) ya Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Bidhaa za Umma 2015.

Sehemu hiyo inasema: "Mtu au jamaa za mtu wanapopewa zabuni katika asasi anayosimamia atakuwa, ametenda kosa kwa mujibu wa sheria ya ununuzi na uuzaji bidhaa."

Bw Ferdinand Waititu ni gavana wa kwanza kupigwa kalamu na bunge la seneti nchini Kenya kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Kufurushwa kwa Bw Waititu kunafanyika wakati ambapo serikali inaonekana kuimarisha vita dhidi ya ufisadi ambao umekithiri hasa miongoni mwa maafisa wa serikali ya kitaifa na za majimbo.

Wachanganuzi wa mambo wanasema kwamba hatua ya bunge la seneti ya kumtimua gavana Waititu ofisisni inatuma ujumbe wa tahadhari kwa vigogo ambao wanakabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

Mafunzo kutokana na kufurushwa kwa Babayao

Mwanasheria ambaye pia ni mchambuzi wa maswala ya kijamii na kisiasa Daktari Alutalala Mukhwana anasema kutimuliwa kwa Bw Waititu ni ishara kwamba vita dhidi ya matumizi mabaya ya pesa za umma vimeanza kuzaa matunda.

"Sasa maafisa wa serikali, wabunge na hata magavana itabidi wawe waangalifu katika matumizi ya pesa za umma. Na taua ya seneti pia itatoa changamoto kwa idara ya mahakama kuongeza kasi ya kushughulikia kikamilifu kesi za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi miongoni mwa maafisa wa serikali" anasema Dkt Alutalala Mukhwana.

Magavana wengine wanne wanakabiliwa na mashataka ya kuhusu madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka miongoni mwao gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko kwa jina maarufu Sonko

Rais Uhuru Kenyatta kila mara ameshtumu idara ya mahakama nchini Kenya kwa madai kwamba haisaidii utawala wake kupambana na ufisadi uliokolea serikalini.

Kwa upande mwingine, jaji mkuu wa kenya amelalamikia vikali kuhusu hatua ya serikali ya kupunguza bajeti dhidi ya idara ya mahakama, jambo ambalo anasema, linavuruga shughuli na usimamizi na utekelezwaji wa haki.

Pia, idara ya mahakama inanyoshea kidole kitengo cha usimamizi wa mashtaka ya uma kwa ushahidi hafifu dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi, jambo ambalo limesababisha kesi nyingi kutupiliwa mbali.