Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahakama ya kimataifa yaitaka Myanmar kuzuia mauaji ya kimbari
Mahakama ya Umoja wa mataifa imeamrisha hatua zichukuliwe kuzuia mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar, na kupinga hoja ya kiongozi wa nchi hiyo Aung San Suu Kyi.
Uamuzi huo umetolewa licha ya kiongozi huyo kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi uliopita kutetea serikali yake dhidi ya madai ya mauaji ya kimbari.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa vitendo vya mauaji ya kimbari vinaweza kutokea tena.
Watu hao walihatarisha maisha yao katika bahari na hata kutembea kwa umbali mrefu. Zaidi ya watu 700,000 walihamia nchi jirani ya Bangladesh baada ya maelfu kuuliwa kwenye machafuko yaliyotokea Agosti 2017.
Umoja wa mataifa umeonya kwamba mauaji zaidi huenda yakatokea.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na taifa la Gambia, imetoa wito wa hatua za dharura kuchukuliwa dhidi ya jeshi la Myanmar hadi uchunguzi kamili utakapoanzishwa.
Myanmar, taifa ambalo waumini wengi ni wa Kibuddha, limekuwa likisisitiza kwamba kampeni yake ya kijeshi ilikuwa ni kukabiliana na tishio kubwa lililokuwepo katika jimbo la Rakhine.
katika taarifa yake ya kujitetea katika mahakama ya kimataifa huko the Hague, Aung San Suu Kyi ameelezea vurugu zilizotokea kama mapigano ya ndani kwa ndani yaliyosababishwa na wanamgambo wa Rohingya baada ya wao kuanza kuvamia vituo vya usalama vya serikali.
Mahakama imesema nini?
Jopo la mahakimu 17 katika mahakama ya kimataifa, Alhamisi, limepiga kura kwa kauli moja kuagiza Myanmar kuchukua hatua kuzuia mauaji ya kimbari ambayo wamesema bado yanaweza kuweka kabila la Rohingya kuwa katika hatari.
Hilo ni pamoja na kuzuia mauaji na kusababisha maafa makubwa ya kimwili au kiakili kwa watu wa kundi hilo pamoja na kuhifadhi ushahidi wa kile ambacho kinaweza kuchukuliwa kama mauaji ya kimbari ambayo tayari yameshatokea.
Rais hakimu Abdulqawi Ahmed Yusuf amesema Myanmar inastahili kuripoti kwa mahakama hiyo ndani ya kipindi cha miezi minne kuelezea vile ilivyotekeleza agizo hilo la mahakama.
Umauzi huo unatekelezwa na pande zote mbili pia hakuna anayeweza kukata rufaa lakini mahakama haina uwezo wa kuutekeleza uamuzi wenyewe.
Hatma ya Aung San Suu Kyi ni ipi?
Na Nick Beake, mwandishi wa BBC News, Myanmar
Umuzi huo umefuta kabisa kile ambacho Aung San Suu Kyi alikuwa amesalia nacho katika hadhi ya kimataifa.
Kumbuka kwamba, hakuwa na haja ya kwenda yeye mwenyewe katika mahakama ya kimataifa na kuwa mtetezi wa moja kwa moja wa serikali yake. Lakini aliamua kwenda yeye binafsi na kutoa hoja zake na kusema kwamba katika vurugu zilizotokea, hakukuwa na mauaji ya halaiki, ubakaji wala matukio ya uchomaji wa makazi.
Hata wale wakosoaji wake wakubwa ambao walikuwa wakikubali kwamba hadhibiti jeshi la Myanmar ambalo bado lina nguvu lakini kwasasa, amevunja ukuta uliopo kati yake na majenerali kwa kujaribu na kushindwa kuthibitisha sababu za kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya Rohingya.
Hadi kufikia sasa, Myanmar imekuwa haitekelezi uamuzi wa mahakama ya kimataifa lakini je wakati umewadia wa kutekeleza umauiz wa sasa ulitolewa na mahakama hiyo?
Katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti moja la Uingereza, Aung San Suu Kyi alihoji ikiwa mfumo wa haki wa kimataifa una uwezo wa kupuuza simulizi zisizokuwa na msingi za makundi ya kutetea haki za kibinadamu na wachunguzi wa Umoja wa mataifa wanaopinga nchi yake.
Lakini baada ya kutoa hoja zake katika mahakama ya kimataifa, je Aung San Suu Kyi ataamua kujitenga?
Msimamo wa Myanmar?
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo Desemba, Suu Kyi aliitaka mahakama ya kimataifa kutupilia mbali kesi hiyo na kuuielezea kama "isiyo na ushahidi na yenye kupotosha".
Na katika makala ya gazeti la Financial Times iliyochapishwa muda mfupi kabla ya uamuzi wa mahakama, alisema makundi ya kutetea haki za kibinadamu yameshutumu Myanmar kwa misingi ya taarifa bila ya kufanywa kwa uchunguzi wa uhalifu unaosemekana".
"Shutuma za kimataifa zimekuwa na athari hasa kwa juhudi za Myanmar za kuleta uthabiti katika jimbo la Rakhine," amesema.
"Imekuwa ikikandamiza juhudi za ndani za kuanzisha ushirikiano kati ya jeshi na serikali ya kiraia."
Matamshi yake yameonekana kuunga mkono taarifa za awali za jopo la serikali ambazo ziliashiria kuunga mkono kwamba huenda kulitekelezwa uhalifu wa kivita na watu binafsi lakini ikaongeza kwamba hakukuwa na nia ya kutekeleza mauaji ya kimbari.
Hata hivyo, mwandishi wa BBC Anna Holligan, ambaye yuko The Hague, anasema kuja kwa Suu Kyi katika mahakama ya kimataifa Desemba, kulionesha kwamba ametambua umuhimu wa kesi hiyo na kwasasa itakuwa vigumu kwa Myanmar kupuuza uamuzi uliotolewa.
Rohigya ni kina nani?
Idadi ya watu wa kabila la Rohingya, lilikuwa karibia milioni moja mwanzoni mwa 2017 nchini Myanmar. Ni moja ya makabila machache nchini humo.
Waislamu wa Rohingya ndiyo jamii kubwa zaidi ya Waislamu Myanmar, wengi wao wakiwa wanaishi jimbo la Rakhine.
Lakini serikali ya Myanmar imekataa kuwapa uraia, na haiwatambua kama watu wa nchi hiyo badala yake inawachukulia kama wahamiaji wa Bangladesh.
Mamia ya wakimbizi wa Warohingya wamekimbilia Bangladesh katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita lakini madhila yao yalianza Agosti 25, 2017 baada ya wanamgambo wanaojiita Arsa kuanzisha mashambulizi katika zaidi ya vituo 30 vya polisi.
Raia wa Rohingya wanaowasili Bangladesh wanasema walitoroka baada ya vikosi vinavyoungwa mkono na waumini wa Kibuddha, kujibu mashambulizi kwa kuchoma moto vijiji vyao na kuwaua.
Serikali inadai kwamba oparesheni dhidi ya wanamgambo ilimalizika Septemba 5, 2017 lakini wachambuzi wa picha za setilaiti za kundi la haki za kibinadamu la Human Rights watch, limesema mamia ya vijiji vilichomwa baadaye mwaka huo.
Huku zaidi ya nusu milioni ya Rohigya ikiaminika kwamba bado wanaishi katika jimbo la Rakhine, wachunguzi wa kimataifa wameonya kwamba kuna uwezekano mkubwa wa mauaji hayo ya kimbari kutokea tena.