Wafanyakazi wa umma waingiwa na hofu baada ya shambulio la Al Shabaab

Iliyochapishwa

Idadi kubwa ya walimu katika kaunti ya Garissa nchini Kenya wametishia kuhama eneo hilo wakihofia usalama wao kwasababu ya mashambulizi zaidi ambayo yamekuwa yakitekelezwa na kundi la AlShabaab.

Wapiganaji wa Al Shabaab wameshambulia Kenya mara sita tangu mwishoni mwa mwezi Desemba hadi sasa na zaidi ya watu 25 wameuawa.

Miongoni mwa waliouawa katika mashambulio ya hivi karibuni katika eneo la Garissa ni walimu 3 na wanafunzi 3, huku serikali ikisisitiza kuwa imeimarisha usalama.

Miongoni mwa walimu ambao wamezungumza na BBC ni Lucy Wanjiru.

Lucy anajiona mwenye bahati kuwa hai pamoja na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili.

Yeye ni miongoni mwa wachache waliowahi kuvamiwa na wapiganaji wa Alshabaab na kuishi kutoa ushuhuda.

Lucy ana kumbukumbu ya usiku wa manane mwezi huu wa Januari alipoamshwa na sauti za milio ya risasi. Alijificha chini ya kitanda huku mwanae mwenye umri wa miaka miwili akimkumbatia.

Alinusurika kifo akiwa na walimu wenzake wawili wa kike huku wenzao watatu wa kiume wakiuawa.

''Wakati wanakijiji walipokuja walituambia kwamba baadhi ya walimu wenzako wamekufa. Tulikuwa tunalia, kisha wakaanza kutuuliza, kwanini munalia, Mungu amewaokoa. Munastahili kwa na furaha. Lakini kwasababu ya mfadhaiko...''amesema Lucy Wanjiru huku akiwa anabubujikwa na machozi.

Nisingependa kuwa sehemu hiyo tena. Nimepata msongo wa mawazo, wenzetu wameuawa, siwezi kurejea katika taasisi niliyokuwa na kuendesha shughuli zangu katika chumba ambacho nilikuwa na walimu wenzangu ambao kwa sasa wamekufa, Wanjiru ameongeza.

Shule ya msingi ya Kamuthe ilivamiwa. Hali ya huzuni ikatanda shuleni humo polisi walipowasili kuchukua miili ya wafu. Shule ya Kamuthe ilidhaniwa kuwa salama.

Iko umbali ya kilomita 200 kutoka mpaka wa Somalia na kuna kituo cha polisi. Hata hivyo wanamgambo wa Alshaabab walivamia shule hiyo na kuchoma kituo hicho cha polisi.

Wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi wa umma

Ni jambo la kawaida kwa shambulio kama hilo kuibua wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi wa Umma katika eneo hilo.

Waalimu kutoka maeneo mbalimbali ya Garissa wamekua wakimiminika katika ofisi ya tume ya huduma kwa walimu nchini Kenya (TSC) kuomba kuhamishwa huku baadhi wakiwa tayari wamefungasha virago.

Wengi wameomba kupelekwa katika maeneo mengine ya nchi. Hata hivyo tume hiyo inawahamisha walimu hao katika shule zingine ndani ya Garissa.

''Tayari tuna upungufu mkubwa wa waalimu hususan katika kaunti hii. Kwahiyo, iwapo waalimu hawa wataondoka katika kaunti hii, tutakuwa tunatafuta kuwa na janga la kitaifa haswa,''Andrew Mwanthi, Mkurugenzi wa tume ya kuajiri walimu eneo la Garissa.

Kila aina ya maafisa wako katika eneo hilo kwa sababu za kiusalama. Na huenda hofu hiyo ikaongezeka baada ya walimu kushambuliwa.

Hata hivyo, kila kinachostahili kufanyika ni kujaribu kujiweka katika hali zao.

Tayari kuna mpango wa kuanzisha huduma za utoaji ushauri kwa ajili ya walimu walioathirika. Pengine sio wengi watakaokubaliana na kauli hiyo lakini serikali inakabiliwa na kibarua kigumu.

Zaidi ya nusu ya idadi ya wafanyakazi wa umma kama walimu, madaktari, na wauguzi kutoka sehemu zingine za nchi.

Lakini hawa ni watu ambao wanahisi kwamba wanalengwa na kundi la Al Shabaab na hivyo basi linataka kuondoka sehemu hiyo.

Ni hali tete kwa serikali kwasababu ya huduma za msingi wanazotoa.

Hatua iliyochukuliwa na serikali

Serikali imetuma vikosi vya wanajeshi kupambana na Alshabaab katika maeneo yanayopakana na Somalia.

Lakini watu 26 wameuawa tangu mwishoni mwa Desemba hadi sasa. Wakenya wengi wanaoishi na kufanya kazi katika kaunti zinazopakana na Somalia wameingiwa na wasiwasi na kuhoji ikiwa wako salama.

Vita dhidi ya ugaidi vinabadilika na kundi la Al Shabaab limefanikiwa kulaghai watu na kufanya kile wanachoweza nchini kenya.

Garissa kama kaunti ni pana ikiwa na ukubwa wa karibia kilomita 46,000 za mraba na ingawa kuna maafisa wengi wa usalama, bado mashambulio kama haya yamekuwa yakitokea katika kaunti hiyo.

''Garissa kama kaunti, tayari tumeweka mipango ya kukabiliana na misimamo mikali. Ili kushinda vita dhidi ya ugaidi, kunahitajika juhudi za kila mmoja katika jamii, watu wa eneo na maafisa wa usalama'', amesema Samuel Njuguna ndiye Naibu wa kamishna, Kaunti ya Garissa.

Kwa kiwango kikubwa Kenya ni nchi salama lakini mashambulio ya kila mara yanayotekelezwa na wapiganaji wa Alshabaab yanaendelea kusababisha hofu.