Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Utafiti waonesha kuna umuhimu wa kuvuna manii kutoka kwa waliokufa
Kuvuna mbegu za kiume kutoka kwa wanaume waliokufa kunastahili kuruhusiwa, utafiti umeonesha.
Utafiti uliochapishwa na Jarida la maadili ya kitabibu, limedai kwamba kuchukuliwa kwa mbegu za kiume baada ya mtu kufa kunaweza kuruhusiwa kimaadili kama njia ya kuongeza akiba ya manii iliyopo.
Mwaka 2017 nchini Uingereza, watoto 2,345 walizaliwa kutokana na mbegu za kiume zilizokuwa zimehifadhiwa.
Hata hivyo, kuna upungufu wa watu wanaojitolea kuchangia mbegu za kiume kote nchini humo kwasababu ya sheria kali.
Mbegu za kiume zinaweza kuchukuliwa baada ya mtu kufa kupitia kifaa cha kusisimua misuli cha kielektroniki ambacho kinawekwa kwenye tezi ya kibofu au kupitia upasuaji na baadaye zinagandishwa.
Ushahidi unaonesha kwamba uvunaji wa mbegu za kiume kutoka kwa wanaume waliokufa bado kunaweza kuchangia ujauzito na kupatikana kwa watoto wenye afya njema hata wakati ikiwa zitavunwa saa 48 baada ya mtu kufa.
Pia unaweza kusoma:
Kupitia utafiti uliofanywa na Dr. Nathan Hodson, kutoka chuo kikuu cha Leicester, na Dr Joshua Parker, kutoka Hospitali ya Wythenshawe ya Manchester ulidai kwamba njia kama hizo zinaweza kufananishwa na wanaojitolea kutoa viungo vyao kwa hiari.
"Ikiwa inakubalika kimaadili kwa mtu kutoa kiungo chake ili kusaidia mwingine anayetaabika na ugonjwa fulani, hakuna sababu utoaji wa mbegu za kiume kutopanuliwa zaidi na kuangaziwa kwa misingi ya kusaidia ambao ni tasa ama wagumba," utafiti umeeleza.
Hata hivyo, hilo linaweza kuzua maswali mengi kuhusu ridhaa ya mtu binafsi na familia, na pia kuna wasiwasi wa kimaadili unaozingira mtu aliyejitolea ambaye hataki kutajwa, wameongeza.
Mwaka 2014, hifadhi ya taifa ya mbegu za kiume Uingereza, ilifunguliwa mji wa Birmingham kwa usaidizi wa ufadhili wa serikali wa pauni 77,000.
Chini ya miaka miwili baadaye, kituo hicho cha hifadhi ya mbegu za kiume kilikuwa kimefungwa na kuacha kabisa kutafuta wanaotaka kutoa mbegu zao za kiume. Hiyo ni kwasababu, watu 9 pekee ndiyo walitia saini makubaliano hayo baada ya kituo hicho kufunguliwa, na wengine wakajitoa baadaye.
Tangu 2005, sheria inasema kwamba watu wanaotaka kutoa mbegu zao za kiume nchini Uingereza lazima wakubali watoto wao watakaozaliwa kwa mbegu walizochangisha wanaweza kuwasiliana nao wanapotimiza miaka 18.
'Kukabili unanyanyapaa'
Jeffrey Ingold, aliyekuwa akitoa mbegu zake jijini London, ameiambia BBC kwamba anaamini kuwa kuruhusu watu kutoa mbegu za kiume kwa hiari baada ya wao kufa kunaweza kufanya wanaume wengi zaidi kuanza kutafakari suala la kuwa miongoni mwa wanaojitolea kuchagia kwa hiari.
"Kuanzisha mfumo utakaowezesha watu kuchangia mbegu zao za kiume kuwa sawa na wanaotoa viungo vya mwili kwa hiari ni kitu kizuri," amesema. "kwangu, kuchangia mbegu za kiume kwa hiari hakuna uhusiano wowote na jeni bali ni kusaidia marafiki walio kwenye uhitaji.
"Pia ninafikiri kwamba kuwa na mchakato kama huu kunaweza kuwa njia moja ya kukabiliana na unyanyapaa au fikra zilizopo katika jamii kuhusu uchangiaji wa mbegu za kiume."
Aliongeza: "Ikiwa watu wanaweza kufahamu zaidi kuhusu mchakato huu na kuweza kufanya maamuzi yenye tija zaidi, ikiwa anataka kuwa mchangiaji wa mbegu za kiume, nafikiri watu wengi zaidi wangeamua kufanya hivyo."
'Kesi ya awali ya uzazi wa mbegu za kiume zilizogandishwa'
Mwaka 1997, mwanamke mmoja alishinda kesi ya kutumia mbegu za kiume za mumewe aliyekufa.
Stephen Blood alipata ugonjwa wa utando wa ubongo February 1995, miezi miwili baada ya kujaribu kuanza familia na mke wake Diane.
Alipoteza fahamu kwa muda mrefu na kuaga dunia kabla ya kukubali kwa maandishi kwamba mbegu zake za kiume zitumike, lakini tayari mbegu zake zilikuwa zimetolewa mara mbili kwa ombi la mkewe.
Mwaka 1990 Shirika la Uzazi na Viini-tete, lilimpiga marufuku mke wa Blood kutumia mbegu za kiume za mumewe bila ya idhini yake ambaye tayari alikuwa amekufa.
Hata hivyo, mahakama ya rufaa baadaye ilitoa uamuzi kwamba Bi. Blood aruhusiwe kupata matibabu ya uzazi ndani ya Jumuiya ya Ulaya lakini siyo Uingereza.
Bi. Blood alifanikiwa kuzaa mtoto wa kiume Joel - kwa kutumia mbegu za kiume za mumewe zilizokuwa zimegandishwa mwaka 2002 na mwaka uliofuata akashinda kesi kwamba mumewe aliyemuoa baadaye atambulike rasmi kama baba mzazi wa mtoto wake.