Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mamilioni ya watu kufungiwa laini zao za simu Tanzania
Mamilioni ya watu wanaomiliki simu za mkononi nchini Tanzania wanakabiliwa na tishio la kukosa mawasiliano ya simu kutokana na kufungwa kwa laini zao za simu ambazo zitakuwa hazijasajiliwa kwa alama za vidole ifikapo saa nne usiku wa leo Jumatatu Januari 20, 2020.
Tanzania ni taifa la hivi punde la Afrika kukumbatia utambulisho wa kidijitali ambao unaendelea kuwa maarufu barani humo.
Afisa mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA Semu Mwakyanjala ameiambia BBC hakuna uwezekano wa muda huo kuongezwa.
Amesema kufikia Jumatano Januari 15, jumla ya laini 27,287,091 zilikuwa zimesajiliwa wiki iliyopita, ambayo ni sawa na asilimia 56 ya watu 48, 717, 967 ambao wana laini za simu.
Hii inamaanisha laini 21,430,876 ambazo ni sawa na (44%) zilikuwa hazijasajiliwa kwa mfumo huo mpya, hali inayowaweka katika hatari ya kusitishiwa huduma endapo mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) itazima mawasiliano.
"Mpango haujabadilika. Laini za simu ambazo hazijasajiliwa zitazimwa," alisema.
Huku hayo yakijiri kwa majuma kadhaa kumeshuhudiwa milolongo mirefu ya watu katika vituo mbalimbali vya mamlaka za vitambulisho vya taifa NIDA kwa ajili ya kupata nambari zao ambazo ni kigezo katika kukamilisha zoezi la usajili kwa alama za vidole.
Zikiwa zimesalia chini ya saa kumi kabla ya muda wa mwisho uliowekwa, zaidi ya watu milioni 20 walikuwa hawajasajili laini zao za simu.
Baadhi yao wameikosoa serikali kwa kutowapatia muda wa kutosha kukamilisha usajili huo.
Hata hivyo mamlaka ya mawasiliano nchini humo TCRA ambayo inasimamaia mchakato huo imewalaumu watu kwa kusubiri hadi dakika za mwisho kujisajili,
Nchini Tanzania simu hazitumiki kama njia ya mawasiliano bali pia zinatumika kama benki kuweka na kutoa pesa, kumaanisha laini zikizimwa itakuwa na athari ya kiuchumi.
Unaweza kutazama mchakato wa usajili unavyoendelea
''Wakati tunasajili laini lazima tujue lengo ni nini, kwa kuwa watu milioni 24 wako kwenye mifumo ya kibenki kwa njia ya mtandao wa simu hivyo kwa masuala ya usalama ni muhimu kukamilisha zoezi hilo kwa kuwa serikali imeamua kuboresha mifumo na kuboresha usalama wa mtumiaji wa simu''. Alisema Bw. Mwakyanjala.
Siku ya Alhamisi wiki iliyopita TCRA ilitoa wito kwa Watanzania waliokamilisha usajili wa laini zao kuzihakiki upya.
Katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Mkurugenzi mkuu wa TCRA, James Kilaba amesema mchakato huo unapaswa kufanyika kabla ya simu ambazo hazijasajiliwa kuzimwa Januari 20, 2020.
Muongozo huo wa kuhakiki unasemaje?
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na TCRA:
- Kila aliye na laini ya simu anastahili kuhakiki kwa kupiga simu kwenda *106#
- Muda wa mwisho wa Januari 20, 2020 unawahusu wale ambao wana laini za simu lakini hawakutumia kitambulisho cha taifa(Nida) na kuthibitishwa kwa alama ya vidole.
- Watakaokasitishiwa huduma za simu Januari 20 wanaweza kuendelea na utaratibu wa usajili ili waweze kurudisha laini zao.
- Wale wanaonunua upya laini za simu wanaweza kuzisajili wakati wowote kwa kutumia stakabadhi zinazohitajika
- Wanadiplomasia ambao hawajakamilisha usajili wa laini zao za simu zinazotumika katika vifaa vyao vya mawasiliano wanatakiwa kuendelea na utaratibu waliopewa.