Siku ya Dunia ni nini, na ni yapi mafanikio yake?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

By Mark Poynting & Maddie Molloy

BBC News Climate & Science

Kila mwaka, mamilioni ya watu duniani kote hukusanyika kwa ajili ya Siku ya Dunia kusherehekea harakati za mazingira.

Maadhimisho ya siku hii yalinza mwaka 1970 nchini Marekani, na sasa imekuwa siku inayoadhimishwa duniani kote.

Siku ya Dunia ni nini na ni lini inaadhimishwa?

Siku ya Dunia ni tukio la kimataifa ambalo linalenga kuonyesha umuhimu wa kuyalinda mazingira.

Hufanyika kila mwaka tarehe 22 Aprili.

Ilianzishwa mwaka 1970 na Gaylord Nelson, seneta wa Marekani na mwanamazingira, na Denis Hayes, mwanafunzi aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Harvard.

Wote wawili walikuwa na wasiwasi juu ya uharibifu wa mazingira nchini Marekani, kama vile athari ya umwagikaji mkubwa wa mafuta mnamo 1969 huko Santa Barbara, California.

Walianzisha Siku ya Dunia kama njia ya kuwashirikisha umma na kushinikiza masuala ya kijani kwa ajenda ya kitaifa.

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Siku ya Kwanza ya Dunia ilivutia umati mkubwa wa watu, kama vile hawa huko Philadelphia, Pennsylvania.

Siku ya kwanza ya dunia ilishuhudia watu milioni 20 kote Marekani wakiingia mitaani.

Ilianza kuwa tukio la kimataifa mwaka 1990, na sasa inahusisha zaidi ya watu bilioni moja wa rika tofauti katika nchi karibu 200, kulingana na waandaaji.

"Kuadhimisha Siku ya Dunia mara nyingi ni hatua ya kwanza ya mazingira kwa watu wengi," anasema rais wa Earthday.org, Kathleen Rogers.

Nini kinatokea katika Siku ya Dunia mwaka 2024?

Kauli mbiu ya mwaka wa2024, "Planet vs. Plastics", inalenga kuongeza uelewa wa madhara ya uchafuzi wa plastiki kwa afya ya binadamu na sayari.

Matukio ya awali yameshughulikia masuala mbalimbali ya mazingira, kuanzia mabadiliko ya hali ya hewa na nishati safi hadi kulinda spishi na faida za upandaji miti.

Lengo la mwaka huu linakuja kabla ya mkataba wa kihistoria wa Umoja wa Mataifa juu ya plastiki, ambao unatarajiwa kukubaliwa mwishoni mwa 2024.

Zaidi ya nchi 50, ikiwa ni pamoja na Uingereza, zimetoa wito wa kukomesha uchafuzi wa mazingira wa plastiki ifikapo mwaka 2040.

Lakini waandalizi wa Siku ya Dunia wanataka kwenda mbali zaidi, na wanatoa wito wa kupunguzwa kwa 60% katika uzalishaji wa plastiki zote ifikiapo mwaka 2040.

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Unaweza kujitolea kwa kusafisha taka za plastiki ufukweni

Siku ya Dunia imeweza kuleta mafanikio gani?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ndani ya miaka michache tangu kuanzishwa kwa Siku ya kwanza ya Dunia mwaka wa 1970, Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Marekani lilikuwa limeanzishwa, na sheria kadhaa za mazingira - kama vile Sheria ya Hewa Safi - zilianzishwa au kuimarisha juhudi za utunzi wa mazingira.

Matukio ya hivi karibuni yamejumuisha kupanda mamia ya mamilioni ya miti, kusaidia wakulima na mbinu endelevu za kilimo, na kuanzisha miradi ya kujifunza kuhusu hali ya hewa kote duniani.

Baadhi ya waangalizi pia wanataja umuhimu wa Siku ya Dunia katika kushinikiza masuala ya mazingira nyuma ya ajenda za kitaifa na kimataifa.

"Kwa masuala mengi yanayosababisha changamoto zetu za kimazingira chini ya orodha ya kipaumbele kwa jamii, matukio kama Siku ya Dunia yanatukumbusha kuhusu athari za muda mrefu na muda mfupi za uharibifu wa mazingira," anasema Yvo de Boer, mkuu wa zamani wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa.

Mwaka 2016, Siku ya Dunia ilichaguliwa kwa ajili ya kutiwa saini rasmi kwa mkataba wa kihistoria wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, ambao ulikubaliwa mwishoni mwa mwaka 2015.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa nchi zote duniani kukubaliana kwa pamoja ili kujaribu kupunguza ongezeko la joto duniani.

Wakosoaji wanasema nini kuhusu Siku ya Dunia?

Baadhi ya wakosoaji wanaonya kuwa mafanikio haya yanatoa hisia za uongo za maendeleo.

Viashiria vingi vya mazingira – kuanzia kuongezeka kwa joto la ulimwengu hadi kutoweka kwa spishi - vinabadilika haraka kutokana na shughuli za binadamu. Juhudi hadi sasa zimepungua sana katika kusimamisha au kubadilisha mwenendo huu.

Baadhi ya watu binafsi na makampuni pia wamekuwa wakishutumiwa kwa kutumia Siku ya Dunia kama fursa ya kupotosha sifa zao za mazingira, bila kufanya mabadiliko halisi ambayo yanahitajika.

Kwa mfano, mwanaharakati Greta Thunberg aliandika kwenye Twitter mnamo mwaka 2022 kwamba Siku ya Dunia "imegeuka kuwa fursa kwa watu walio madarakani kuchapisha 'upendo' wao kwa sayari, wakati huo huo kuiharibu kwa kasi kubwa".

Tabia hii imeitwa ‘’greenwashing’’

"Sote tunajua kuwa ‘’greenwashing’’ inayofanyika na inakasirisha," muandaaji wa Siku ya Dunia Bi Rogers aliiambia BBC.

"Sio suala ambalo tumesababisha, lakini tunajua Siku ya Dunia hutumiwa kwa njia ya mbaya na baadhi ya biashara [kupotosha] kutumia maadili uendelevu kwa faida yao wenyewe."

"Serikali zinahitaji kuchukua hatua madhubuti na kupambana na biashara yoyote au sekta inayodawanganya watumiaji."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah