Cha kufanya ikiwa macho yako yamepata maumivu baada ya kupatwa kwa jua

Chanzo cha picha, Getty Images
Kupatwa kwa jua kabisa ni tukio lililotokea siku ya Jumatatu huko Amerika Kaskazini na kulifuatiliwa na watu wengI, kama inavyokuwa mara nyingi wakati wa kupatwa kwa jua kote ulimwenguni, huku watu wakitafuta majibu mtandaoni juu ya nini cha kufanya ikiwa macho yatakuwa na maumivu.
Kabla ya tukio hilo, wakati ambapo Mwezi ulificha Jua, wataalamu walionya kwamba ilikuwa hatari kutazama Jua kwa macho moja kwa moja. Badala yake, walipendekeza kutumia miwani.
Lakini chochote kitakachotokea kwa sasa, kuna uwezekano ikawa macho yako yamedhurika, na kwa kawaida taratibu tu maumivu yataendelea kuisha yenyewe, wataalamu wa macho wanasema.
Lakini kuna uwezekano wa mtu kupata matatizo ya macho kama vile ‘Retinopathy’
Retinopathy ya jua ni shida ya kuona ambayo inaweza kutokea baada ya kutazama Jua kwa muda mrefu sana, wakati mwingine hata kwa sekunde tu.
Hali hiyo hutokea wakati kuna uharibifu wa retina, ambayo ni safu muhimu ya tishu iliyo ndani ya nyuma ya jicho. Retina ina seli zinazoweza kuhisi mwanga ambazo hubadilisha picha kabla ya kutumwa kwenye ubongo.
Lakini retina haina mishipa yenye kusababisha maumivu, ikimaanisha kuwa uchungu wowote hauwezekani kuwa ishara ya ugonjwa wa ‘retinopathy’, Chuo cha Marekani cha masuala ya macho kinasema.
Dalili za hali hiyo zinaweza kujumuisha uoni hafifu au dalili za upofu.
Kuhusu kwa nini hutokea - jicho la mwanadamu linaweza tu kustahimili "nguvu" fulani ya mwanga alieleza Profesa Bainbridge, mwenyekiti wa masomo ya retina katika Chuo Kikuu cha London College.
Kuangalia moja kwa moja kwenye Jua - hata tu juu ya Jua lililofichwa na Mwezi - kunaweza kuwa na madhara.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Profesa Bainbridge aliambia BBC kwamba yeyote anayekabiliwa na hilo anapaswa kutafuta matibabu - lakini iwe haraka kuzuia uharibifu wa kudumu wa jicho.
Wataalamu wengine walikubali kwamba hii sio kawaida. Kulikuwa na takriban ripoti 100 kote Marekani na Canada kufuatia kupatwa kwa jua kwa mwaka wa 2017, kulingana na ripoti ya mwaka jana ya Chama cha Wanaanga Marekani.
Profesa Bainbridge, ambaye pia ni daktari wa macho katika Hospitali ya Macho ya Moorfields ya London, anakumbuka kuona wagonjwa kadhaa waliokuwa na dalili hizi baada ya Uingereza kupatwa kabisa na jua mwaka wa 1999.
"Kwa kawaida mambo yanaimarika hatua kwa hatua, ingawa baadhi ya watu walikuwa na madhara ya kudumu," alisema. Hakuna matibabu, ndiyo sababu msisitizo uko katika kuzuia.
Lakini kupatwa kwa jua kwa jumla siku ya Jumatatu kulileta hatari zilizofichika, wataalamu wa huduma ya macho waliambia mshirika wa BBC wa Marekani, CBS News.
Ukweli ni kwamba Jua lilizuiliwa kwa kiasi kikubwa na hii ilimaanisha watu hawakuwa na "hisia ya asili ya mwangaza", alisema daktari wa macho Jason P Brinton.
Pia, watu wengi katika Amerika Kaskazini walishuhudia kupatwa kwa jua katika baadhi ya sehemu - lakini bado kuna uwezekano wa macho kudhurika.
Vile vile, kuna kile kinachofahamika kama – ‘keratopathy’ – athari ya "kuungua" kwenye konea, sehemu ya mbele ya uwazi ya jicho.
Hata hivyo, hii haitokei kutokana na kuangalia kidogo wakati wa kupatwa kwa jua, kulingana na Prof Bainbridge.
Husababishwa na kukabiliwa na mwanga mkali kwa muda mrefu, kawaida kwa wachomeleaji.
Kama ilivyo kwa retinopathy, hali hii hupona yenyewe.
Ikiwa una dalili kama vile maumivu ya kichwa baada ya kupatwa kwa jua, inawezekana pia kwamba unasumbuliwa na kile Prof Bainbridge anakiita athari ya pili.
Hii inaweza kutokea kutokana na macho kupata maumivu kwasababu ya kuangalia sehemu moja – wakati unajaribu kuzingatia kitu kilicho mbali kwa muda mrefu sana. Tena, mara nyingi tatizo hili pia hujitatua lenyewe baada ya muda.
Imefasiriwa na Asha Juma













