Polisi wa Australia wakamata tani 2.7 za kokeni iliyofichwa kwenye maghala ya siri

Chanzo cha picha, Australian Federal Police
Polisi wa Australia wamekamata tani 2.7 za kokeni, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa nchini humo.
Dawa hizo za kulevya, zenye thamani inayokadiriwa kufikia dola za Australia milioni 816 (takriban pauni milioni 433), ziligunduliwa Ijumaa katika vyumba vya siri vilivyofichwa chini ya sakafu bandia ndani ya makontena matatu ya usafirishaji kwenye eneo la Londonderry, magharibi mwa mji wa Sydney.
Wanaume wawili wenye umri wa miaka 21 na 25 walikamatwa eneo la tukio baada ya kudaiwa kujaribu kuwatoroka polisi. Wameshtakiwa kwa kumiliki kiasi kikubwa cha dawa za kulevya zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria.
Polisi wanasema kokeni hiyo ilisafirishwa kwa magendo kuingia Australia kupitia mji mdogo wa Midge Point, ulioko Kaskazini mwa jimbo la Queensland, kwa maagizo ya kundi la uhalifu uliopangwa.
Wanaume hao wawili waliwekwa rumande baada ya kufikishwa mahakamani Jumamosi, na wanaweza kukabiliwa na kifungo cha maisha gerezani iwapo watapatikana na hatia.
Polisi walisema uvamizi huo ulikuwa sehemu ya operesheni iliyopewa jina la Operation Minjiang, ambayo ilianzishwa mwezi Mei baada ya kilo 40 za kokeni kupatikana zikielea majini karibu na sehemu ya kushushia boti katika Midge Point.
Wiki iliyopita, watu wengine sita katika majimbo ya Queensland na New South Wales walikamatwa na kushtakiwa kutokana na uchunguzi ulioanzishwa kufuatia ugunduzi huo.
Aidha, chombo kikubwa cha majini kinachoshukiwa kuwa sehemu ya mtandao wa usafirishaji wa dawa hizo kwa magendo kimezuiliwa katika visiwa vya Solomon.


















