Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nini kitatokea baada ya kile kinachoitwa kura ya maoni ya Urusi nchini Ukraine?
Watu katika mikoa minne ya Ukraine inayoshikiliwa na Urusi wamepiga kura katika kile kinachojulikana kama kura ya maoni kuhusu kujiunga na Urusi, ambapo serikali ya Kyiv na washirika wake wa Magharibi wanapuuzia na kusema kuwa ni udanganyifu.
Kura hizi ambazo zimekataliwa kuwa si halali na Ukraine pamoja na Magharibi zimefanyika katika maeneo manne yanayoshikiliwa na Urusi kusini na mashariki mwa nchi, ambayo yanaunda takriban 15% ya eneo la Ukraine.
Maafisa walioteuliwa na Moscow katika mikoa hiyo sasa wanadai kuungwa mkono kabisa na wale walioshiriki katika kura hizo za kujiunga na Urusi.
Mashirika ya habari yanayoendeshwa na utawala unaounga mkono Kremlin huko Donetsk na Luhansk yanaripoti kwamba hadi 99.23% ya watu walipiga kura ya kuunga mkono Urusi, asilimia kubwa ambayo si ya kawaida katika kura ya aina hii.
Kumekuwa na madai mengi ya vitisho huku maafisa wa uchaguzi wakienda nyumba hadi nyumba wakiandamana na walinzi wenye silaha.
Kuna uvumi wa kimataifa kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin anaweza kutangaza matokeo wakati wa hotuba katika kikao cha pamoja cha bunge la Urusi siku ya Ijumaa.
Mnamo Machi 2014, alitangaza kwamba rasi ya Crimea ya Ukraine imetwaliwa siku chache tu baada ya kura ya maoni ambayo vile vile haikutambuliwa kufanyika.
Ni sehemu gani za Ukraine zinaweza kujiunga na Urusi?
Kura hizo zilizoitishwa miezi saba baada ya Urusi kuvamia Ukraine, zilianza baada ya kutolewa kwa taarifa ndani ya siku chache tu na zilifanyika kati ya tarehe 23 na 27 Septemba.
Kura za maoni zinajiri wakati ambapo mashambulizi ya Ukraine yakirudisha tena maeneo mengi yaliyotekwa tangu uvamizi huo ulipoanza Februari 24.
Takriban watu milioni nne kutoka mikoa ya mashariki ya Donetsk na Luhansk (ambayo mara nyingi hujulikana kama Donbas) na mikoa ya kusini ya Kherson na Zaporizhzhia walitakiwa kupiga kura zao.
Watu kutoka eneo hilo, wakiwemo wakimbizi, ambao sasa wametawanyika kote Urusi wameweza kupiga kura katika mamia ya vituo vya kupigia kura huko.
Watu walipigia kura kwa ajili ya nini?
Hakuna upigaji kura wa kielektroniki na maswali kwenye karatasi za kupigia kura yametofautiana kulingana na eneo.
Hii ni kwa sababu wanaounga mkono Urusi wanaotaka kujitenga wamekuwa wakiendesha sehemu za Donetsk na Luhansk tangu 2014, walipofanya kura za maoni za uhuru ambazo hazitambuliki kimataifa.
Wapiga kura huko wameulizwa ikiwa "wanaunga mkono kujiunga kwa jamhuri yao kwa Urusi kama shirikisho".
Katika sehemu za Kherson na Zaporizhzhia zinazokaliwa na majeshi ya Urusi tangu uvamizi wa 2022, watu wanaulizwa ikiwa "wanapenda kujitenga kwa eneo hilo kutoka Ukraine, kuunda nchi huru na baadaye kujiunga na Urusi kama shirikisho".
Karatasi za kupigia kura huko zimechapishwa katika Kiukraine na Kirusi, ambapo katika mikoa miwili ya mashariki imechapishwa kwa Kirusi pekee.
Je, kura ilipangwaje?
Upigaji kura umefanyika katika mamia ya vituo vya kupigia kura, vikilindwa vikali na vikosi vya usalama vinavyoungwa mkono na Urusi, katika maeneo hayo manne
Kura hiyo pia "ilipangwa katika jumuiya na kwa njia ya nyumba kwa nyumba kwa sababu za usalama", shirika la habari la serikali la Urusi Tass linaripoti.
Maafisa wa uchaguzi wakisindikizwa na wanajeshi waliojihami wamegonga milango ya makazi ya watu ambapo wakazi walipiga kura mbele ya wanajeshi waliokuwa wamebeba bunduki.
"Lazima ujibu kwa maneno na askari aweke alama kwenye karatasi na kulihifadhi," mwanamke mmoja huko Enerhodar aliambia BBC.
Kwa hiyo, bunduki zilikuwepo kwa ajili ya kuwalinda wananchi walipokuwa wakipiga kura, au kuwashinikiza wapige kura? Hilo lilikuwa ni swali lililopita vichwani mwa watu.
Mwanamke mmoja alieleza BBC jinsi wazazi wake walivyopiga kura katika mji wa Melitopol katika eneo la Zaporizhzhia.
"Washiriki" wawili wa eneo hilo walikuwa wamefika na wanajeshi wawili wa Urusi kwenye ghorofa yao ili kuwapa karatasi ya kupigia kura kusaini, alisema.
"Baba yangu aliweka 'Hapana' [kujiunga na Urusi]," mwanamke huyo alisema. "Mama yangu alisimama karibu, na kuuliza nini kitatokea kwa kuweka 'Hapana'. Wakasema, 'Hakuna'."
Mwandishi wa habari wa Ukraine Maxim Eristavi alitweet na kusema kwamba familia yake "imelazimishwa kupiga kura kwa mtutu wa bunduki" kusini mwa Ukraine.
Ukosefu wa faragha unaonekana.
Picha kutoka kwa vyombo vya habari rasmi vya ndani na habari zimeonesha karatasi za kura zikijazwa mbele ya kila mtu, na kuwekwa zikiwa zimefunuliwa kwenye masanduku ya kura yaliyo wazi
Kura za maoni zimefanyika bila waangalizi huru.
Pia kumekuwa na ukosefu wa kanuni za maadili na utekelezaji wa viwango.
Wapiga kura walipewa muda mfupi wa kuelewa kura hizo za maoni zinazopingwa zilihusu nini.
Urusi inataka nini katika kura hizo?
Baadhi ya wataalam wanaona kura za maoni kama nyenzo ya propaganda ya Urusi ili kupata uungwaji mkono wa umma wakati ambapo wanajeshi wake wanapambana kushikilia ardhi huko Ukraine.
Akizungumza na shirika la habari la Associated Press, gavana aliye uhamishoni katika eneo la Luhansk - Serhiy Haidai alisema Warusi walikuwa wakitumia mchakato huo kama kisingizio cha kutafuta nyumba za wanaume ambao wangeweza kuwandikisha kama wanajeshi.
Pia alisema walikuwa wakitafuta "chochote cha kutiliwa shaka na kinachounga mkono Ukraine".
Je, nini kitatokea baada ya matokeo ya 'kura za maoni'?
Wengine wanaona kura za maoni kama jaribio la Kremlin kuanzisha upya vita.
Ikiwa Urusi itachukua maeneo haya inaweza kupeleka mzozo katika kiwango kipya na hatari zaidi, huku Moscow ikionyesha juhudi zozote za Ukraine kuyarudisha maeneo hayo kama shambulizi dhidi ya eneo lake huru.
Kuunganisha maeneo hayo kunaipa Urusi fursa ya kujilinda na kulipiza kisasi dhidi ya mashambulio yoyote ya Ukraine huko.
Rais Putin hivi karibuni alidokeza uwezo wake wa kutumia silaha za nyuklia kutetea ardhi ya nchi hiyo.
Mwitikio wa dunia
Kumekuwa na kilio cha kimataifa juu ya kura hizi za maoni.
Nchi nyingi za magharibi zimeshutumu kura hiyo kuwa ni kinyume cha sheria. Shirika la kimataifa la OSCE na vyombo vya habari vya Urusi tayari vimesema kuwa kura ya Ndiyo imeshinda.
Serbia, ambayo ina uhusiano wa karibu na Moscow na ni miongoni mwa nchi chache za Ulaya ambazo hazijajiunga na vikwazo dhidi ya Urusi, imetangaza kutotambua matokeo ya upigaji kura.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Serbia Nikola Selakovic alisema kuwa kufanya hivyo kutakuwa "kinyume kabisa" na sera ya nchi yake ya "kuhifadhi uadilifu wa eneo na mamlaka na... kanuni ya kutokiuka mipaka".
Mbele ya upinzani wa kimataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesisitiza kuwa kura hizo zilikuwa "udhihirisho wa mapenzi" ya watu ambao wameishi katika mikoa hiyo.
Alithibitisha kuwa iwapo mikoa hiyo minne itajiunga na Urusi watakuwa na ulinzi sawa na sehemu nyingine yoyote ya eneo lake, ikiwa ni pamoja na ulinzi kwa silaha za nyuklia.
Ikulu ya White House inasema Marekani haitawahi kutambua "eneo hilo la Ukraine kama kitu kingine chochote isipokuwa sehemu ya Ukraine".
Kwa maoni ya Rais Biden, "kura ya maoni ni udanganyifu, kisingizio cha uwongo cha kujaribu kunyakua sehemu za Ukraine kwa nguvu katika ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa".
Uingereza imejibu kwa vikwazo vipya vinavyolenga maafisa wakuu wa Urusi waliohusika katika kutekeleza kura hiyo miongoni mwa wengine.