Nyota ambao huenda wakashiriki kombe la Dunia kwa mara ya mwisho

Chanzo cha picha, Getty Images
Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wametawala soka kwa kizazi kimoja, lakini hii huenda ikawa nafasi yao ya mwisho kushinda Kombe la Dunia.
Wachezaji hao wawili wameshinda ubingwa na mataji yote katika ngazi ya vilabu, lakini wana taji moja tu la bara na timu za taifa za Argentina na Ureno, mtawalia.
Messi na Ronaldo ni miongoni mwa wachezaji mashuhuri ambao Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar linaweza kuwa la mwisho kwao kushiriki , na orodha hii inajumuisha:
Cristiano Ronaldo (Portugal)
Huwezi kamwe kupinga uwezekano wowote wa Ronaldo, lakini atakuwa na umri wa miaka 41 kufikia Kombe lijalo la Dunia, ikimaanisha kwamba Kombe la Dunia la Qatar huenda likawa la mwisho kwake.
Ronaldo alikuwa amethibitisha Septemba iliyopita kwamba hatastaafu baada ya Kombe la Dunia nchini Qatar, akielezea matumaini yake kwamba angecheza na Ureno kwa "miaka michache zaidi" - ni nani anajua nini kitatokea?
Mustakabali wake na klabu yake pia haujulikani kwa sasa, baada ya mahojiano na waandishi wa habari ambapo aliikosoa Manchester United.
Ronaldo pia alivunja rekodi nyingi katika Kombe la Mataifa ya Ulaya - kushiriki katika idadi kubwa zaidi ya matoleo ya mashindano hayo, kucheza mechi nyingi zaidi, na kufunga mabao mengi - na pia aliongoza Ureno kushinda taji hilo mnamo 2016.
Zaidi ya hayo, ndiye mfungaji bora katika timu ya taifa akiwa amefunga mabao 117 - yakiwemo mabao matatu (hat-trick) dhidi ya Uhispania kwenye Kombe la Dunia hivi karibuni nchini Urusi.
Mshambuliaji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 37 anachukuliwa kuwa mmoja wa wanasoka wakubwa zaidi katika historia, akifunga mabao 700 katika ngazi ya klabu, kushinda mataji zaidi ya 30 na kushinda taji la Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA mara tano. Lakini bila shaka hii ni nafasi ya mwisho ya kuongeza taji la Kombe la Dunia kwenye wasifu wake mzuri.
Lionel Messi (Argentina)
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa hakika, tunaweza kurudia mambo mengi tuliyosema hapo awali kuhusu Ronaldo tunapozungumza kuhusu Messi, ambaye atakuwa na umri wa miaka 39 wakati wa Kombe la Dunia lijalo.
Inasemekana ndiye mchezaji bora wa wakati wote, alifunga mabao 695 akiwa na Barcelona na Paris Saint-Germain, na alitajwa kuwa mchezaji bora wa dunia mara saba, ambayo ni rekodi ambayo hakuna mchezaji mwingine yeyote katika historia aliyeitangulia, na pia aliiongoza Argentina. kushinda Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini. (Copa America) katika toleo lake la hivi punde.
Lakini kushinda Kombe la Dunia nchini Qatar kungemweka Messi mwenye umri wa miaka 35 katika orodha ya wababe, pamoja na Pele na Diego Maradona, kwa wale wanaofikiria kushinda Kombe la Dunia kuwa kigezo kikuu cha kuamua mchezaji "bora zaidi".
Messi alijiunga na timu ya taifa ya Argentina kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia katika viwango vyake bora katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kufunga mabao 11 na kutengeneza mabao 14 katika michezo 18 akiwa na Paris Saint-Germain.
Hivi majuzi Messi alisema hilo litakuwa ni Kombe lake la mwisho la Dunia, lakini hakuna kilichothibitishwa bado, hasa kwa vile hapo awali alitangaza kustaafu soka la kimataifa na kisha kurejea tena kushiriki timu ya taifa ya Argentina.
Robert Lewandowski (Poland)

Chanzo cha picha, Getty Images
Hii itakuwa mara ya pili kwa nyota wa Poland Robert Lewandowski kucheza Kombe la Dunia, na huenda ikawa ya mwisho pia.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye alifunga mabao 18 katika mechi 19 akiwa na Barcelona msimu huu, alishindwa kufunga katika Kombe la Dunia lililopita nchini Urusi akiwa na Poland, ambao waliondolewa katika hatua ya makundi.
Nyota huyo wa zamani wa Bayern Munich alifunga mabao matano katika mechi 11 alizoichezea Poland kwenye michuano ya Uropa, lakini hii inaweza kuwa nafasi yake ya mwisho kufunga kwenye Kombe la Dunia.
Neymar (Brazil)
Neymar, 30, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye orodha hii, lakini tayari amesema kwamba Kombe la Dunia nchini Qatar huenda likawa ni ushiriki wake wa mwisho katika Kombe la Dunia.
"Nadhani ni Kombe langu la mwisho la Dunia," nyota huyo wa Brazil alisema mwaka jana. "Sijui kama nina nguvu ya kiakili ya kukabiliana na soka tena." Lakini baadaye alionyesha kuwa matamshi yake yalikuwa yametafsiriwa vibaya.
Lakini kuna uwezekano kwamba Neymar - ambaye alifunga mabao 13 na kusaidia mabao 11 akiwa na Paris Saint-Germain msimu huu - atajuta ikiwa ataamua kustaafu soka la kimataifa baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia, hasa kwa vile ni mmoja wa wachezaji mwenye vipaji vingi kizazi chake, na amefunga mabao 75 akiwa na nchi yake.
Luis Suarez (Uruguay)

Chanzo cha picha, Getty Images
Suarez ana umri wa miaka 35, hivyo - sawa na wachezaji wenzake wa zamani wa Barcelona Messi na Neymar - huu unaweza kuwa mwisho wa kushiriki Kombe la Dunia.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool, Barcelona na Atletico Madrid alikuwa amerejea katika kikosi chake cha kwanza, Nacional, ambacho alishinda nacho taji la ligi ya Uruguay.
Pengine kumbukumbu kuu ya Suarez katika Kombe la Dunia ni pale alipopokea kadi nyekundu baada ya kuchukua mpira kwa mkono kutoka kwenye mstari wa goli na kuinyima Ghana kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2010, na kisha kumng'ata beki wa Italia Giorgio Chiellini kwenye Kombe la Dunia la 2014.
Suarez sio nyota pekee wa Uruguay anayekaribia mwisho wa soka yake ya kimataifa, kama ilivyo kwa mshambuliaji wa Valencia Edinson Cavani, 35, na mlinzi wa Velez Sarsfield, Diego Godin, 36.
Luka Modric (Croatia)
Nyota wa Real Madrid Luka Modric ana umri wa miaka 37, na hili litakuwa kombe lake la nane kuu akiwa na timu ya taifa ya Croatia. Ripoti zinaonyesha kuwa atastaafu soka la kimataifa baada ya Kombe la Dunia - ingawa meneja wake alithibitisha kuwa ataendelea kucheza.
Modric alichukua jukumu kubwa katika kuiongoza nchi yake kutinga fainali ya Kombe la Dunia la 2018, ambayo walipoteza kwa Ufaransa.
Modric alishinda tuzo ya Mpira wa Dhahabu ya mchezaji bora katika mashindano hayo, na pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia.
Karim Benzema (France)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid atafikisha miaka 35 siku moja baada ya fainali ya Kombe la Dunia.
Benzema anashiriki michuano hii baada ya kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA 2022, baada ya kufunga mabao 44 katika michezo 46, ingawa alifunga mabao matano pekee msimu huu.
Hii itakuwa Kombe lake la pili la Dunia, baada ya kucheza Kombe la Dunia la 2014. Benzema aliondolewa kwenye kikosi cha Ufaransa kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2010, kisha akakosa mashindano ya Kombe la Dunia 2018 wakati wa kutengwa kwa karibu miaka sita kwenye timu ya taifa kwa kushiriki kwake katika kesi ya ulafi wa kanda ya ngono. .
Gareth Bale (Wales)

Chanzo cha picha, Reuters
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa gwiji wa Wales Gareth Bale kuonekana kwenye Kombe la Dunia - na inaweza pia kuwa ya mwisho.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alisema hana nia ya kustaafu baada ya Kombe la Dunia nchini Qatar, lakini atakuwa na umri wa miaka 37 kwenye Kombe lijalo la Dunia.
Bale alijiunga na klabu ya Marekani ya Los Angeles msimu uliopita wa joto baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Real Madrid. Ripoti zilidokeza kuwa huenda Bale angestaafu soka la kimataifa kama Wales wangeshindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Manuel Neuer (Germany)

Nyota wa Bayern Munich na Ujerumani Manuel Neuer ni mmoja wa makipa bora wa kizazi chake.
Neuer alishinda Kombe la Dunia la 2014 na alijumuishwa katika XI bora kwa mashindano hayo.
Sergio Busquets (Spain)
Busquets ni mmoja wa wachezaji bora katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, na amekuwa akiwasaidia wenzake katika klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania kusonga mbele ili kutekeleza majukumu yao ya kushambulia huku yeye akitekeleza majukumu yake ya ulinzi kwa ukamilifu.
Lakini ana umri wa miaka 34, na utimamu wake wa kimwili si kama ilivyokuwa zamani.
Itakuwa vigumu kuona mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2010 akitokea tena kwenye Kombe la Dunia miaka minne kutoka sasa.












