Tanzania kwa nini Namibia?

Chanzo cha picha, Ikulu
Namibia si miongoni mwa washirika wakubwa wa biashara wa Tanzania.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024 za The Observatory of Economic Complexity (OEC), Tanzania iliuza bidhaa za thamani ya dola za Marekani milioni 2.38 kwenda Namibia, huku Namibia ikiuza bidhaa za thamani ya dola milioni 5.96 kwenda Tanzania.
Hata hivyo, katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita, marais wa Tanzania na Namibia wamekutana mara kadhaa, wamefanya ziara za pande zote na kuendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wao.
Tanzania kwa nini Namibia?
Swali hilo linaweza kuonekana rahisi. Lakini jibu lake linaeleza mengi kuhusu namna ambavyo Tanzania inavyoitazama nafasi ya Afrika katika uchumi wa dunia.
Wiki hii, Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, anafanya ziara nyingine nchini Tanzania na kutoa ujumbe ambao unaweza kueleza kwa nini uhusiano huo unaonekana kupewa uzito mkubwa.
"Ukombozi wetu wa kisiasa umekamilika kwa kiasi kikubwa. Ukombozi wetu wa kiuchumi bado haujakamilika," alisema.
Kauli hiyo inaweza kuwa ndiyo ufunguo wa kuelewa kwa nini Tanzania na Namibia zinaonekana kuharakisha ushirikiano wao katika biashara, uwekezaji, nishati, madini na maendeleo ya viwanda.
"Biashara ndogo leo, fursa kubwa kesho"

Chanzo cha picha, MFA via CGTN AFRICA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa kuangalia takwimu za sasa, biashara kati ya Tanzania na Namibia bado ni ndogo. Bidhaa kuu zilizouzwa kutoka Tanzania kwenda Namibia mwaka 2024 zilijumuisha tumbaku iliyosindikwa, magari ya mizigo na magari madogo. Namibia kwa upande wake iliuza zaidi bia, mvinyo na vinywaji vikali kwenda Tanzania.
Lakini viongozi wa nchi hizo mbili wanaonekana kutazama zaidi fursa zilizopo kuliko hali ilivyo sasa.
Katika mazungumzo yao Dar es Salaam, Samia na Nandi-Ndaitwah walikubaliana kuongeza ushirikiano katika biashara, uwekezaji, usalama wa chakula, mifugo, madini, gesi asilia na uchumi wa buluu.
"Kweli biashara ndogo leo, lakini fursa kubwa kesho, kwa sababu ya uhitaji na mazingira ya sasa ya diplomasia ya nchi za Magharibi", anasema mchambuzi Salim Amin.
Namibia imekuwa moja ya nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya mafuta na gesi baada ya ugunduzi wa rasilimali mpya katika miaka ya karibuni. Pia imejipambanua katika miradi ya nishati jadidifu na uzalishaji wa green hydrogen.
Kwa upande wake, Tanzania ina akiba kubwa ya gesi asilia, bandari za kimkakati na soko kubwa la ndani.
Kwa hiyo, kwa viongozi wa nchi hizo mbili, ushirikiano huo unaonekana kuwa uwekezaji wa baadaye kuliko kutazama takwimu za leo pekee.
Uhusiano wa Tanzania na Namibia

Chanzo cha picha, Okeri
Uhusiano wa Tanzania na Namibia una mizizi mirefu kuliko biashara. Wakati Namibia ikipigania uhuru wake, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zilizotoa hifadhi, elimu na msaada wa kisiasa kwa wapigania uhuru wa taifa hilo.
Akikumbuka historia hiyo, Rais Nandi-Ndaitwah alisema wananchi wa Namibia hawatausahau mchango wa Tanzania.
"Watu wa Namibia hawajawahi kusahau msaada huo na hawatausahau kamwe," alisema. Hata Rais Nandi-Ndaitwah mwenyewe wakati huo, aliishi Magomeni, Dar es Salaam na katika ziara hii ameitembelea nyumba aliyokuwa kiishi.
Wakati kizazi cha viongozi kama Julius Nyerere na Sam Nujoma kilipigania uhuru wa kisiasa, viongozi wa kizazi cha sasa wanaonekana kuzungumzia zaidi kesho kuliko jana. Katika hotuba yake, Nandi-Ndaitwah alisema Afrika haiwezi kuendelea kuuza malighafi na kuagiza bidhaa zilizoongezwa thamani kutoka nje ya bara huku ikitarajia kupata maendeleo ya kudumu.
Aliyataja viwanda, uongezaji thamani, ubunifu, teknolojia na ajira kama maeneo muhimu katika hatua inayofuata ya maendeleo ya Afrika.
Siku chache kabla ya kuwasili Tanzania, rais huyo alizindua kitabu chake Building Namibia's Future: President Netumbo Nandi-Ndaitwah's Roadmap to Unity, Prosperity and Transformation, kinachosisisitiza umoja, ustawi na mageuzi ya kiuchumi.
Mtazamo huo unaendana na hoja ambazo zimekuwa zikitolewa kwa miaka mingi na watetezi wa umoja wa Afrika, akiwemo Profesa Patrick Lumumba wa Kenya, ambaye amekuwa akisisitiza kuwa bara hilo haliwezi kupata nguvu kamili za kiuchumi bila kuongeza ushirikiano wa ndani na kupunguza utegemezi wa nje.
Diplomasia ya uchumi ya Tanzania na biashara ya Afrika

Chanzo cha picha, URT/TZ Embassy
Tangu aingie madarakani mwaka 2021, Rais Samia ameongeza ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kikanda na kimataifa kwa msisitizo mkubwa katika biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.
Sasa anaeleweka zaidi, hasa baada ya misimamo ya washirika wa jadi kama Umoja wa Ulaya na Marekani kuhusu kuangalia upya mahusiano na misaada kutokana na kile wanaxchokiita kukiukwa kwa masuala ya haki za binadamu.
Mbali na kuimarisha mahusiano na majirani kama Kenya, Uganda na Burundi, Tanzania imeendelea kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kikanda kupitia SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Kwa mujibu wa Afreximbank na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA), biashara ya ndani ya Afrika bado ni ndogo ikilinganishwa na maeneo mengine ya dunia, jambo linalozuia bara hilo kunufaika kikamilifu na soko lake la watu zaidi ya bilioni 1.4.
Kwa mchumi Beatrice Kimaro, changamoto hiyo ndiyo inayopaswa kuwa kitovu cha mjadala wa viongozi wa Afrika.
"Afrika bado inafanya biashara kubwa zaidi na mabara mengine kuliko inavyofanya yenyewe kwa yenyewe. Nchi za Afrika zinapaswa kutumia fursa za AfCFTA kuongeza biashara za ndani ya bara na kujenga uchumi unaotegemea ushirikiano wa Waafrika wenyewe," anasema.
Kwa upande wa sekta binafsi, Rhoda Magoiga wa Jukwaa la Kilimo Tanzania anaona dalili za matumaini katika ushirikiano huo.
"Tunauona uwekezaji unakwenda kutokea kwa kuwa tumepata wadau wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo," anasema.
Kwa mujibu wake, ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Namibia unaweza kusaidia kuongeza uwekezaji katika uzalishaji na usindikaji wa mazao, jambo ambalo linaweza kuwagusa moja kwa moja wakulima na wafanyabiashara wa kawaida.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa urafiki wa kisiasa pekee hauwezi kutosha kuongeza biashara kati ya nchi hizo mbili.
Huenda jibu la swali la "Tanzania kwa nini Namibia?" lisipatikane katika takwimu za biashara za leo, bali katika matokeo yatakayopatikana miaka michache ijayo ikiwa ahadi za viongozi hao na ziara zao, zitageuzwa kuwa uwekezaji, biashara na fursa za kiuchumi kwa wananchi wa nchi zote mbili.














