Msichana wa Gaza,12, aliyepoteza familia yake yote kwa usiku mmoja

Katika video iliyorekodiwa na mwokozi wa Kipalestina, sauti inatoka chini ya vilima vya saruji iliyovunjwa.
"Mimi ni Alma."
"Usinisaidie kwanza. Nisaidie mama na baba yangu. Na tafadhali nisaidie kaka yangu Tarazan. Ni mtoto mchanga, ana miezi 18."
Ni asubuhi tarehe 2 Desemba 2023, na Alma Jaroor, 12, amezikwa chini ya vifusi vya jengo la ghorofa tano katikati mwa jiji la Gaza kwa zaidi ya saa tatu.
"Nataka kuwaona kaka na dada zangu," anapiga kelele. "Nawatamani."
Lakini mwokozi anamfikia Alma kwanza, na anatoka nje - bila kusaidiwa - kutoka kati ya vibao vya zege vilivyochongoka na paa za chuma zilizosokotwa.
Amefunikwa na vumbi lakini hana majeraha makubwa.
Wanauliza familia yake iko wapi. Anaelekeza kwenye kifusi upande wake wa kulia na kushoto.
Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo yaweza kuwaathiri baadhi ya wasomaji
Miezi mitatu baadaye, Alma anaiambia BBC hadithi yake, kwa kirefu na kwa kina.
Mjomba wake Msami ameketi karibu. Anajihifadhi pamoja naye na familia yake katika hema huko Rafah, kusini mwa Gaza.
Maneno yake ni mafuriko ya hofu na hasara.
"Nakumbuka niliamka chini ya kifusi. Niliangalia iPad yangu, nikaona ni 09:00. Nilitarajia kaka yangu Tarazan bado yuko hai. Nilikuwa nikimpigia simu, na nikiwa na matumaini kwamba mmoja wao atakuwa hai.
"Nilisikia harufu ya damu. Ilikuwa ikinidondoka. Nilikuwa nikipiga kelele ili mtu yeyote atuokoe. Nilikuwa nikisikia wengine wakiita pia."
Lakini baada ya Alma kuokolewa, aliona mabaki ya Tarazan.

Chanzo cha picha, Family handout
"Niliinua blanketi lililokuwa limemfunika. Nilimkuta katika hali isiyoweza kufikirika," anasema, "kichwa chake kimekatwa." Kwa hili yeye hunyamaza, akisumbuliwa na kile ambacho hawezi kukiona.
"Natamani kifo baada ya kumuona kaka yangu hivyo," anasema. "Alikuwa na umri wa miezi 18 tu. Amefanya nini katika vita hivi?"
Tarazan haikuwa hasara pekee. Familia yake yote ilikuwa imetoweka, waliuawa kwa pamoja - wazazi wake Mohammed, 35, na Naema, 38; kaka Ghanem, 14, na Kinan, 6; na dada yake Reehab, 11.
Wazazi wa Alma walikuwa wamejaribu kwa bidii kushinda mashambulizi ya Israeli na kuwaweka watoto wao salama. Anatuambia eneo la kwanza ambalo familia ilikimbilia lilipigwa kwa bomu, na la pili. Na katika sehemu ya tatu, bomu lilitua juu yao.
Jamaa wanasema jengo walimokuwa wamelala liliangushwa na mashambulizi ya anga ya Israel. Jeshi la Israeli lilituambia kuwa halingeweza kutoa maoni juu ya dai hili bila kuratibu jengo hilo.

Chanzo cha picha, Family handout
"Tulikuwa na furaha pamoja kama familia," Alma anasema. "Tulikuwa tunakumbatiana tukiwa na hofu. Natamani ningewashika wote. Sikuwa na muda wa kutosha nao."
Na bado anasubiri kuzika. Mwili wa Tarazan pekee ndio uliopatikana.
"Kulikuwa na wakimbizi 140 [Wagaza waliohamishwa na vita] katika jengo hilo, na ni baadhi tu ya miili iliyopatikana," anasema.
"Miili ya familia yangu inaoza chini ya vifusi. Ninatamani kuwaona na kuwapa mazishi yanayofaa."
Wakati fulani, Alma anaweza kusahau - kwa muda tu - yote hayo amepoteza.
Anakaa kwenye sakafu baridi ya hema pamoja na binamu zake wachanga. Wanatengeneza tiara kutoka kwa mabaki ya plastiki na kwa kufikiria. Alma anajiunga, akipiga soga na kutabasamu.
Yeye halii tena wakati wote, anasema, kwa sababu anajua kwamba wazazi wake "wana furaha huko waliko ‘mbinguni’".
Amepata faraja na familia ya mjombake Sami, lakini si usalama.

Chanzo cha picha, Family handout
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kama kila mtoto huko Gaza, anaweza kuuawa dakika yoyote. Hasa walio hatarini ni wale wa Rafah, ambapo Israel inaendelea kutishia mashambulizi ya ardhini. Ni nyumbani kwa Wapalestina milioni 1.4.
Vita huko Gaza vilichochewa na mashambulio ya Hamas dhidi ya Israeli tarehe 7 Oktoba, ambayo yaliua karibu Waisraeli 1,200, wengi wao wakiwa raia.
Tangu wakati huo, watoto wa Gaza wamelipa gharama mbaya sana.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, linasema watoto 13,000 huko Gaza wameuawa na Israel tangu vita hivyo vilipoanza, kiwango cha mauaji kinachoelezwa kuwa ni cha "kushangaza".
Maafisa wa wizara ya afya katika eneo linaloendeshwa na Hamas wanasema kuwa jumla ya vifo katika vita hivyo ni angalau watu 31,923. Shirika la Afya Ulimwenguni linachukulia takwimu zao kama "za kuaminika" na linasema takwimu halisi zinaweza kuwa kubwa zaidi.
Israel inasema inafanya kila iwezalo kupunguza vifo vya raia.
Wapalestina wanapinga kwamba mabomu mengi yamerushwa kwenye majengo ya makazi yaliyojaa watu waliokimbia makazi yao, na kuua familia kama za Alma.
Ndugu zake wanatuonyesha picha. Inaonyesha Alma akitabasamu, akiwa amezungukwa na kundi la binamu vijana sita. Wote sasa wamefariki, isipokuwa yeye. Waliuawa katika shambulio la Disemba 2, pamoja na familia yake ya karibu.

Chanzo cha picha, Family handout
Ni Almas wangapi waliopo kwa sasa, walioibiwa mama na baba zao?
Vita hivyo vimesababisha mayatima wasiopungua 20,000 kufikia mwisho wa Februari, kulingana na taarifa za awali zilizokusanywa na watafiti kutoka Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Palestina. Ni shirika huru lisilo la kiserikali linaloungwa mkono na EU ambalo linafanya kazi mashinani huko Gaza.
Idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi, kulingana na kituo hicho, lakini hilo haliwezi kuthibitishwa kwa sababu ya ugumu na hatari ya kupata habari huko Gaza.
Kabla ya vita kuchukua kila kitu, alipenda kuimba, na alikuwa na matumaini ya kuwa daktari - kama baba yake alivyomtaka.
"Nilikuwa na ndoto ambazo nilitaka kuzitimiza," Alma anasema, "lakini sasa sina ndoto tena. Ninahisi uchungu moyoni mwangu na utakaa nami kwa maisha yangu yote, kwa sababu walikuwa familia yangu, wazazi wangu, dada yangu na kaka zangu. Na wote walifariki kwa usiku mmoja."
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi












