Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tangshan na Xuzhou: Hasira na maswali juu ya unyanyasaji wa wanawake China
Ilikuwa Ijumaa usiku yenye shughuli nyingi kwenye mgahawa mmoja wa nyama choma katika mji wa Tangshan nchini China. Kundi la wanawake walikuwa wakipata chakula cha jioni pamoja wakati mmoja wao alipofuatwa na mteja wa kiume.
Akiwa na hasira kutokana na kuguswa kwake, alisema "Toka". Kwa kujibu hilo, alimpiga kichwani na kumtupa chini.
Kisha marafiki zake wakaungana naye wakitumia viti na chupa kuwapiga wanawake hao ambao baadhi yao walitolewa nje na kupigwa teke la kichwa.
Ilikuwa ni mfano wa hivi karibuni zaidi wa unyanyasaji dhidi ya wanawake ambao uliukasirisha umma wa Wachina mwezi Januari, habari za mwanamke kukutwa amefungwa kwa minyororo kwenye kibanda zimezua hasira kama hizo.
Kesi zote mbili zimeanzisha mjadala mikubwa mitandao ikikosoa vitendo hivyo ambavyo havijawahi kushuhudiwa pamoja Pia wameibua maswali, hasa miongoni mwa wanawake vijana, kuhusu unyanyasaji wa wanawake na nguvu za wanaume.
"Imetuvuruga sana jinsi watu wa China wanavyoitazama jamii yao na haswa, kanuni za kijinsia na mila potofu inayoisisitiza," Pichamon Yeophantong, mtafiti wa China katika Chuo Kikuu cha New South Wales alisema.
Kuzuka kwa Vurugu.
Wanawake kushambuliwa hadharani na wapenzi wao "ni jambo la kawaida sana mtandaoni", anasema Kerry Allen, mchambuzi wa ufuatiliaji wa vyombo vya habari vya Uchina wa BBC.
"Ninaona picha karibu kila siku za unyanyasaji wa kinyumbani zilizorekodiwa kwa siri au mashambulizi ambayo yamechukuliwa kupitia picha za uchunguzi."
Utafiti wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2013 uliohusisha wanaume 1,000 katika kaunti moja katikati mwa China uligundua kuwa zaidi ya nusu walikiri kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono dhidi ya wapenzi wao idadi kama hiyo pia walisema watatumia vurugu kulinda heshima yao.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilihusisha ukatili wa kijinsia na kanuni za kijinsia zilizokita mizizi nchini China nchi ambayo unyanyasaji wa majumbani ulifanywa kuwa kosa la jinai mwaka 2016.
Katika jamii ya Kichina, "ugumu, uwezo wa kijinsia ... na matumizi ya nguvu katika baadhi ya matukio" yanabaki kuwa masuala ya wanaume, ilisema.
Lakini wachunguzi wa mambo wanasema pia kuna kusita kuingilia kati jambo ambalo bado linaonekana kuwa la faragha kati ya wanandoa.
Allen alisema kuwa alipokuwa akiishi nchini humo muongo mmoja uliopita alishuhudia mashambulizi kadhaa mchana kweupe ambapo "makundi ya watu [walikuwa] wakitazama tu".
Ndivyo ilivyotokea Tangshan, ingawa mwathiriwa hakumjua mshambuliaji. Ilikuwa vivyo hivyo huko Xuzhou pia, ambapo mwanamke alikuwa amefungwa minyororo shingoni mwake kwenye kibanda nje ya nyumba yake.
Mumewe alikuwa amedai kuwa alikuwa amefungwa kwa sababu ugonjwa wake wa akili ulimfanya kuwa tishio kwa wengine. Lakini uchunguzi wa polisi ulithibitisha tuhuma kwamba alisafirishwa kama bibi harusi katika miaka ya 1990.
Kanda hiyo iliibuka tu na kusambazwa mitandaoni baada ya mtengeneza maudhui ya video mtandaoni kumkuta alipotembelea kijiji hicho - ukweli ni kwamba imechukua muda mrefu kwake kugunduliwa na kuwashangaza watu sana.
"Yeye ni mtu, si kitu. Baada ya kupata watoto wanane zaidi ya miaka 20 anapatikana leo tu? Hakuna idara yoyote ya serikali iliyohusika ambayo haina hatia hapa," mtumiaji mmoja aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo.
Kudai mabadiliko
Wanawake wengi wa China walishangazwa na kiwango cha unyanyasaji ulioonyeshwa katika kesi za Tangshan na Xuzhou, hasa kutokana na viwango vya chini vya uhalifu wa China na viwango vya juu vya ufuatiliaji.
"Nikizungumza na kizazi kipya - wanafunzi wa vyuo vikuu, haswa, nimesikia wengi wao wakielezea mshtuko wa kweli kwamba unyanyasaji kama huo dhidi ya wanawake bado upo, ikiwa haukubaliwi, katika jamii ya kisasa ya Wachina," Dk Yeophantong alisema.
Wengi wanahoji mienendo ya kijinsia kwa mara ya kwanza, aliongeza.
Wito wa mabadiliko ya kijamii unaonekana kuwa maarufu zaidi kwa vijana wengi wa China ambao wanatumia mitandao ya kijamii na wanafahamu vyema harakati za kimataifa kama #MeToo.
Baadhi ya machapisho maarufu kwenye mtandao wa Weibo kuhusu kesi hizo mbili yanatia wasiwasi kuhusu jinsi wanawake wanavyotendewa katika jamii ambayo bado inakuza mawazo ya mfumo dume wa Confucian.
"Tunahitaji... kukiri kwamba bado kuna nguvu katika mazingira yetu ambazo zinaunga mkono, kuhimiza na kuwasukuma wanaume kushiriki katika unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake," insha moja ilieleza.
Wengi pia wameelezea kutoridhishwa na jinsi mamlaka imejibu kesi hizi, wakiwashutumu walio mamlakani kwa kudharau jukumu la jinsia.
Katika tukio la Tangshan, majibu ya awali ya polisi na vyombo vya habari yalionekana kuzingatia uhusiano wa washambuliaji na magenge ya ndani na historia yao ya uhalifu.
Ripoti moja ilisema mwanamke huyo alifikiwa tu kwa "mazungumzo". Lakini kwenye Weibo watumiaji wengi walipinga, wakisema ni unyanyasaji wa kijinsia.
Hasira juu ya mwanamke aliyefungwa pia ilisababisha vitendo vya nadra vya maandamano ya umma.
Katika matukio tofauti, wanawake wawili waliendesha gari kote nchini kujaribu kumwokoa. Waandamanaji waliokuwa wazi nyuso zao walijipiga picha na ishara na kuweka picha hizo mtandaoni. Duka moja la vitabu lilianzisha maonyesho ya fasihi ya harakati za wanawake.
Je, hii ni hatua ya mabadiliko?
"Wanawake wana hasira sasa na kusema. Lakini sina matumaini kwamba hii italeta mabadiliko ya kimsingi," Yaqiu Wang, mtafiti wa China katika shirika la Human Rights Watch. Katika kukabiliana na shinikizo kubwa la umma, mamlaka ilijibu kesi zote mbili kwa kuanzisha uchunguzi na vikosi kazi.
Huku kukiwa na hasira juu ya hali ya mwanamke huyo huko Xuzhou, waliahidi msako mkali wa usafirishaji haramu wa watu kwa kuongeza ukaguzi wa leseni za ndoa za kienyeji.
Baada ya shambulio la mgahawa, waliongeza doria za usiku huko Tangshan na kumfukuza kazi mkuu wa polisi wa eneo hilo. Wahusika wanaodaiwa katika kesi zote mbili wamekamatwa. Lakini Guo Jing, mfanyakazi wa kesi ya unyanyasaji wa majumbani nchini China, alisema ni kawaida kwa mamlaka kuchukulia uhalifu wa kijinsia kama matukio ya mara moja, kutatuliwa kwa kuwakamata na kuwaadhibu washtakiwa.
"Matukio haya hayatazamiwi kwa mtazamo wa kimuundo; hakuna mtazamo wa muda mrefu wala masuluhisho ya kitaasisi," aliiambia BBC Kichina.
Machi, baadhi ya wanachama National People's Congress walipendekeza kuimarishwa kwa sheria zinazolinda wanawake na kuongeza adhabu kwa biashara haramu ya binadamu.
Lakini haya bado hayajatokea na uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China haujaashiria mabadiliko yoyote. Wakati huo huo, udhibiti umeongezeka. Kufuatia shambulio la Tangshan, Weibo aliondoa akaunti ambazo "zilichochea makabiliano ya kijinsia".
Mazungumzo ya zamani kuhusu mwanamke aliyefungwa minyororo ambayo mara nyingi yalijumuisha mijadala kuhusu ubaguzi wa kijinsia pia yamefutwa.
Wang alisema ni vigumu kuendeleza uanaharakati kutokana na jinsi China imekuwa ikifuta makundi yake ya kutetea haki za kiraia katika miaka ya hivi karibuni.
Waangalizi wana wasiwasi kuwa ukandamizaji huo pia umeathiri harakati wa haki za wanawake: wanaharakati watetezi wa haki za wanawake wamekamatwa na mapambano ya hali ya juu ya MeToo mahakama yakitupiliwa mbali.
Kesi ya hivi karibuni inayomhusu mchezaji wa tenisi Peng Shuai pia imezua hofu kwamba wanaoshtaki unyanyasaji wa kingono wananyamazishwa.
"Nguvu zilizokuwapo ambazo zilishinikiza serikali kufanya vyema kuhusu masuala ya jinsia zimeondolewa," Wang alisema. "Haya yote yanaashiria mabaya kwa haki za wanawake nchini China."