India: Mtoto afariki tumboni baada ya mwanamume kumshambulia mwanamke mjamzito tumboni

Iliyochapishwa

Polisi nchini India wanasema mwanamke mjamzito ambaye anadaiwa kukatwa tumbo na mume wake amezaa mtoto wa kiume aliyefariki tumboni.

Familia ya mwanamke huyo inadai kuwa mwanamume huyo alimshambulia akitaka kujua jinsia ya mtoto.

Wanasema wanandoa hao wana watoto watano wa kike na kwamba mwanamume huyo amekuwa akimhangaisha mke wake amzalie mtoto wa kiume.

Mwanamume huyo ambaye tayari amekamatwa amekanusha madai ya kumshambulia makusudi mke wake akisema ilikuwa ni ajali.

Kisa hicho kilitokea katika wilaya ya Badaun,Uttar Pradesh, jumbo la India lilili na watu wengi zaidi kaskazini mwa nchi.

Maafisa wameiambia BBC kwamba mwanamke aliyejeruhiwa anaendelea kupokea matibabu na kwamba hali yake imeimarika katika hospitali ya mji mkuu wa Delhi.

Kwa mujibu wa ndugu yake, mwanamke huyo alipelekwa Delhi siku ya Jumapili kufuatia ushauri wa daktari kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya sana.

Mume wake aliambia vyombo vya habari nchini kuwa alimrushia upanga lakini hakujua itamuuimiza vibaya hivyo.

"Nina watt watano wa kike, mwanangu mmoja wa kiume amefariki. Najua watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Sasa chochote kitakachotokea,kitatokea."

Polisi wanaendelea na uchunguzi.

Hamu ya baadhi ya wasabi nchini India kupata watt wa kiume badala ya watoto wa kike imefanya watoto wengi wa kike kuuawa kabla ama baada ya kuzaliwa.

Wasichana milioni 46 walitoweka India katika kipindi cha miaka 50, kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Juni ya mfuko wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia idadi ya watu(UNFPA).

Kila mwaka, watoto wa kike karibu 460,000 wanauawa kupitia utoaji mimba huku vifo vingi vya watoto wa kike wanaozaliwa na kutelekezwa baada ya kuzaliwa vikiripotiwa.

Mwaka 2018 ripoti ya serikali ya India ilisema hamu ya kutaka watoto wa kiume imechangia kuzaliwa kwa watoto milioni 21 wa kike ambao "hawatakikani".

Ripoti hiyo ya Wizara ya Fedha ilibaini kuwa wanandoa wengi wanaendelea kuzaa hadi wapate mtoto wa kiume.

Mchambuzi Geeta Panday

Anahusika na masuala ya wanawake wa India na jamii

India ni nchi ambayo kwa muda mrefu imekabiliwa na utamaduni wa kupendelea mtoto wa kiume kuliko wa kike.

Hali hiyo inatokana na imani kwamba mtoto wa kiume atatunza familia na kuikimu kifedha na Pia kupeleka mbele jana la familia.

Mtoto wa kike kwa upande mwingine ataolewa na kuondoka huku familia ikitarajiwa kulipa mahari ya kiwango kikubwa.

Upendeleo huo wa watoto wa kiume umeimarishwa na teknolojia ya uteuzi wa kijinsia kabla ya mtoto kuzaliwa ambayo umeathiri vibaya uwiano wa kijinsia kwa miaka mingi ambapo mamilioni ya wasichana wameuawa wakiwa tumboni au baada ya kuzaliwa kwa kutelekezwa makusudi.

Mnamo mwaka 1961, kwa kila watoto wavulana 1,000 walio chini ya miaka saba, kulikuwa na wasichana 976. Kulingana na sensa ya mwisho 2011, idadi hiyo ilikuwa imeshuka hadi 914.

Wanaharakati wa kutetea haki wanasema ni ''mauaji ya kiholela'' Waziri Mkuu wa zamani Manmohan Singh alielezea suala hilo la kubagua jinsia ya kike kama "aibu ya kitaifa " na kutoa wito wa kufanyika "harakati" za kuokoa wasichana.

Waziri Mkuu Narendra Modi pia ameshauri Wahindi "wasiwatukuze watoto wa kiume pekee" na pia "wasiwaue mabinti zao kwa matumaini ya kupata mvulana".

Miaka Mitano iliyopita alizindua kampeni ya Beti Bachao, Beti Padhao (muokoe binti, msomeshe binti) - kwa lengo la kuokoa watoto wa kike. Katika kampeini nyingine aliwaomba kina baba kupiga picha za selfie na mabinti zao na kumtumia.

Lakini hakuna hata kampeni moja iliyofanya kazi.Wataalamu wanasema ili mambo yabadilike, Wahindi lazima wakabiliane na upendeleo wao mbaya wa watoto wa kime kuliko wa kike katika jamii na kushawishi familia kusherehekea mabinti zao kadri wanavyo washerehekea watoto wao wa kiume.