Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Yaliyomkuta Msuva ni darasa tosha kwa wachezaji wa Afrika Mashariki
Na Yusuph Mazimu
BBC Swahili
Wiki hii Shirikisho la Soka la duniani (FIFA) limeiagiza klabu ya Wydad Athletic ya Morocco kumlipa kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva zaidi ya Dola za Kimarekani 700,000 (Tsh. zaidi ya bilioni 1.6), kwa kukiuka mkataba.
Uamuzi huo wa FIFA umekuja miezi 7 baada ya Msuva kufungua kesi ya madai ya malipo dhidi ya klabu hiyo aliyokuwa akiichezea na hatimaye kushinda.
Msuva aliyesaini mkataba wa miaka minne kuchezea timu hiyo, alilazimika kuusitisha mkataba wake Desemba mwaka jana kutokana na kuidai klabu hiyo malimbikizo ya mishahara pamoja na pesa za usajili.
Wydad ina siku 7 za kukata rufaa uamuzi huo na kama haijakata rufaa itapaswa kumlipa Msuva kiasi hicho cha fedha ndani ya siku 45.
Si mara ya kwanza kusikia taarifa za aina hii, za wachezaji wa mataifa ya Afrika hasa Afrika Mashariki kusotea maslahi yao na wakati mwingine kusitisha ndoto zao za kucheza nje, kwa sababu ya masuala ya malipo.
Tulisikia maneno mengi, wakati huo Shomari Kapombe, beki kisiki wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, anaachana na Klabu ya Cannes ya Ufaransa.
Soka la kulipwa vs Soka la kutupwa Afrika
Ni rahisi kuwalaumu wachezaji wanaokataa kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi zao lakini usipuuze mitazamo yao ya maisha 'magumu' wanayopitia na kusimuliwa na watu kama akina Msuva.
Msuva anatuonyesha aina mbili za soka zilizopo, ambazo mchezaji anapaswa kuzifahamu..... soka la kulipwa ambalo amelitamani na ambalo wanaoishi nalo wachezaji wengi ulaya unaowasikia, kina Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Harry Kane, Pierre-Emerick Aubameyangna wengine na soka hili la changamoto za kuanzia asubuhi, mchana na jioni.
'ilifika kipindi nampigia simu rais (wa timu), nionane nae alikuwa hapokei, na sometime ananambia njoo nyumbani kwangu na nafika nyumbani kwake na sometime yuko ndani, getini pale anawaambia walinzi waaambie sipo nyumbani nimetoka', Msuva anayasema maisha yake huko Morocco mbele ya wanahabari.
Ukiyasikiliza maneno ya Simon Msuva utagundua kwamba, alikuwa sehemuya soka la kutupwa, na sio soka la kulipwa. Hatujasikia uongozi wa Wydad kujibu hili moja kwa moja ila mara kadhaa umeeleza kufuata utaratibu wote wa haki kwa wachezaji wake.
'bado mataifa mengi Afrika, soka ni burudani, mtu (kiongozi au mshabiki) akiburudika inatosha, hajali kuhusu mburudishaji ambaye ni mchezaji, sasa wamiliki na viongozi wako mbali na soka la leo linalotaka mchezaji kupewa thamani ya kwanza kuliko chochote kwenye timu', anasema Salim Amin, mchambuzi wa soka, anayeishi Ujerumani na aliyewahi kuwa kiongozi wa timu ya Sinza Stars ya Dar es Salaam.
Amin anasema, kwa Ulaya mchezaji wa kulipwa anapewa heshima kubwa kutokana na misingi ya soka lenyewe lilivyojengwa, linathamini na kuheshimu utu na kila mtu.
'Lakini kwa Afrika, mataifa ya Kaskazini, yanahitaji muarobaini, ingawa soka lao liko juu, kuna vitendo vingi vinavyokiuka misingi ya soka la kulipwa', alisema.
Wachezaji wengi wanaficha 'masaibu yao'
Msuva ana maumivu kwa kauli na maneno yake. Pengine Msuva amekaa na maumivu haya kwa muda mrefu. Alienda kucheza soka la kulipwa Morocco karibu miaka mitano iliyopita, ambapo alianza mwaka 2017 akiwa na Difaâ Hassani El Jadidi kabla ya kutua Wydad AC.
Ameshindwa kuvumilia na sasa ameweza kujitoa mhanga na kusema aliyoyapitia, akiweka wazi matatizo haya hayakuwa kwake pekee bali kwa wachezaji wengi.
'na haya maumivu sio ya kwangu mimi (pekee), wameshashitaki wachezaji wengi wa kiafrika, na wengine wamesamehe hadi hela (zao)', anasema.
Lakini wangapi hawasemi, kwa aibu , fedheha ama sababu zingine mbalimbali?wanaogopa nini?
'hakuna woga wala aibu, ni uelewa mdogo tu wa haya mambo, lazima wakubali kujifunza kupitia makosa ya wengine, na wasichoke kuwa wawazi na kukubali kukosea, itawasidia wengine kujifunza', anasema Amin
Jasmine Razack ambaye husaidia wanamichezo wa Tanzania kisheria, anafichua uwepo wa wachezaji wengine wa Tanzania wanaopitia masaibu kama ya Msuva akimtaja pia Mwanahamis Omari, mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake Tanzania, Twiga stars ambaye alikuwa Morocco akichezea Chabab Atlas ya ligi kuu ya wanawake nchini humo.
' suala la Mwanahamisi liliniumiza sana sana sana, Mwanahamisi kapitia mazito naweza kusema zaidi ya Simon', anasema Jasmine.
Nyota huyo wa Twiga Stars amerejea Tanzania, akikata tamaa ya maslahi yake kutoka kwa Wamorocco hao, na sasa anasaidiwa na Jasmine kuhusu maslahi yake kama ilivyo kwa Msuva.
'Mikataba, lugha, usimamizi, uwazi, taarifa na uelewa ni msiba kwa wachezaji wetu'
Jasmine na Salim wote wanakubaliana kwamba, kinachowaumiza wachezaji wengi wa Afrika Mashariki kuhusu soka la Kulipwa, ni ulaghai unaotumika kwa mawakala, mameneja ama wanaosaka wachezaji.
'Tanzania ni shamba la bibi,; anasema Jasmine akirejea udanganyifu wa mawakala wanaokuja nchini humo kuchukua wachezaji na kuwalaghai na kuwapeleka kucheza soka la kulipwa.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Amin ambaye anakiri kwamba kwa nchi za Ulaya angalau kiasi fulani visa vya namna hii ya Msuva, vimepungua.
'Huku (Ulaya) kuna unafuu kiasi, tofauti na Afrika, kwa sababu soka huku ni biashara, uchumi na taaaluma iliyopiga hatua kubwa, kuna sheria na kanuni ambazo zinawabana sana na watu wanajua haki zao na wajibu wao, na mengi yanawekwa wazi', anasema.
Wachezaji wengi Afrika Mashariki wanao wachezaji wengi wa kujifunza kuhusu soka la kulipwa. Kenya inao wachezaji walifanya vyema kwenye soka la kulipwa Ulaya kama nahodha wake wa zamani, Dennis Oliech, Victor Wanyama na nahodha wa wakati huu Michael Olunga Ogada.
Ukiacha Msuva, Tanzania inao nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta anayecheza Ulaya, Thomas Ulimwengu aliyeko TP Mazembe ya DRC au vijana wanaochipukia kama Kelvin John (Genk-Ubelgiji), Ben Starkie (Spalding- Uingereza), Haji Mnoga (Weymouth-Uingereza) na Novatus Dismas anayekipiga Zulte Waregem.
Uganda inaye mtu kama Dennis Onyango au Emanuel Okwi, hawa wanaweza kuwa funzo kubwa Namna walivyoishi na kubebwa na misingi ya soka la kulipwa Ulaya, ni funzo kwa wachezaji wengi wazawa wanaoweza kujifunza kupitia wao.
Amin anasema serikali za Afrika zikichukulia kama taaluma, zitajenga mazingira ya vilabu na wasimamizi , waendeshaji wa mpira kujenga misingi ya kuheshimu mkataba na yote kuhusu mchezaji.
Hili litasaidia kuwa na soka la kulipwa linalokaribia sawa na Ulaya, na kuwafanya wachezaji kuishi kifalme.
Ingawa haipaswi Serikali kuingilia masuala ya michezo, Jasmine anafikiria zaidi akitaka wadau wote kimamlaka; 'naomba tujaribu kufuatilia wachezaji wetu waliokuwa nje ya nchi, wanayoyapitia muwape support (muwaunge mkono), tujaribu kuwapigania, tuweke umoja tujaribu kuwasaidia hawa vijana
Analolitaja Jasmine linajengewa misngi na Amin anayetajwa masuala matano wanayokosa wachezaji wengi wazawa wa Afrika Mashariki na kujikuta wakikumbwa na masaibu.
'Mikataba, lugha, usimamizi, uwazi, taarifa na uelewa duni ni msiba kwa wachezaji wetu'.
Anachojaribu kusema Amin ni kwamba wachezaji wengfi wanaingia mikataba wasiyoielewa vyema kisheria, mingine inatumia lugha za kigeni wasizozifahamu vyema, hawana uelewa na hawana pia watu wazuri wa mpira wa kuwasimamia masuala yao.
Ukiacha hayo hawawi wawazi, wanafichaficha mambo yao mengi, lakini sasa hatua ya nyota mkubwa wa soka la Tanzania ambaye ni kioo na anayefuatiliwa sana pengine sawa na Mbwana Samatta, inatoa somo kwa wachezaji wa Afrika Mshariki, kufikiria mara mbili mbili kabla ya kukubali kutia saini kucheza soka la kulipwa hasa Afrika.