Ni kwanini mitandao gushi ya propaganda ya Uganda iliiba sura yake?

Chanzo cha picha, Jared Wolfe
Uchunguzi wa BBC umebaini mtandao wa akaunti bandia za mitandao ya kijamii nchini Uganda. Chini ya utambulisho bandia , walieneza propagandaza kuunga mkono serikali na kutoa vitisho vinavyowalenga wakosoaji . Lakini watu walio nyuma yake ni akina nani?
Sio jambo la kawaida kila siku kupiga picha ya selfie na Rais wa Uganda aliyehudumu kwa muda mrefu, Yoweri Museveni. Wakati fursa hiyo ilipotokea, Dkt Jamechia Hoyle alipiga picha hiyo.
Yeye ni mshauri mwandamizi nchini Marekani, anayehusika na masuala ya usalama wa afya duniani. Mnamo Oktoba 2017, alikuwa amesafiri kwenda mji mkuu wa Uganda, Kampala, kuhudhuria mkutano wa kimataifa.
Rais Museveni alikuwepo kwa ajili ya kuwakaribisha wageni wake.
Akipitia kwenye umati wa watu Dkt Hoyle aaliweza kumfikia rais huku akiwa na simu ya smartphone mkononi. "Alikuwa na furaha sana kuzungumza nasi na kuchukua picha," anakumbuka.
Walipomuona Dkt Hoyle na rais, wakiwa na nyuso za tabasamu wakijiandaa kwa ajili ya picha, wapiga picha hawakuweza kuvumilia – nao pia walilchukua picha hiyo.

Chanzo cha picha, Twitter/Don Wanyama
Miaka minne baadaye, picha hii halisi imetumika kuunda akaunti bandia ya mitandao ya kijamii inayolenga kueneza propaganda za serikali na kuwalenga wakosoaji wa serikali.
Dkt Hoyle hivi karibuni aligundua kuhusu hilo, baada ya BBC kuwasiliana naye.
"Kuona picha yangu mwenyewe na kisha kuelewa muktadha wa baadhi ya mambo ambayo yalishirikishwa... Sikuweza kuamini hivyo," alisema. "Kwa kweli nilikuwa nimerudishwa nyuma."
'Jamechia Feki' aliingia
Akaunti hiyo bandia kwa kutumia picha ya Dkt Hoyle iliundwa kwenye X, ikiitwa Twitter zamani kabla ya kubadilishwa jina, mnamo Oktoba 2021.
Mwanzoni akaunti hiyo ilionekana kutokuwa na maslahi nje ya siasa za Uganda, mara kwa mara ikituma sifa kwa serikali ya Uganda na sera zake.

Maneno makali zaidi - ikiwa ni pamoja na vitisho vya mara kwa mara - yalielekezwa kwa wafuasi wa upinzani na wakosoaji wa serikali.
"Tunajua mnaunga mkono vitendo vya kigaidi", akaunti hiyo ilichapisha bila kuwasilisha ushahidi wowote, kujibu ujumbe wa Twitter kutoka kwa kiongozi wa upinzani Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi.
"Utakufa", uliandikwa ujumbe tofauti wa twitter ulioelekezwa kwa Hillary Innocent Taylor Seguya, mwanaharakati wa mazingira wa Uganda anayeishi Marekani na mwanachama wa chama cha Bw Wine, Jukwaa la Umoja wa Kitaifa.
Katika mitandao ya kijamii, Bw Seguya amejulikana kwa ukosoaji wake wa moja ya miradi mikubwa ya Uganda: Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Chanzo cha picha, Hillary Innocent Taylor Seguya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mradi huo utakapokamilika, bomba hilo lenye thamani ya dola bilioni 3.5 litaunganisha viwanja vya uchimbaji mafuta ya Uganda na bandari ya Tanzania ya Tanga, katika njia ya kilomita 1,445 (maili 898).
Kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa ya Total Energies inamiliki karibu theluthi mbili ya mradi huo, huku hisa zilizobaki zikigawanyika kati ya kampuni za mafuta za Uganda na Tanzania, pamoja na kampuni ya nishati ya China.
Wanaounga mkono mradi huo wanasema utatengeneza maelfu ya ajira na kuzalisha mamilioni ya mapato ya mafuta.
Lakini wakosoaji wanasema kuwa EACOP inaweza kuwa na athari kubwa kwa jamii za wenyeji, kwani utakuwa na athari kubwa kwa mazingira.
Maandamano dhidi ya bomba hilo yamefanyika kote nchini Uganda, na wakati mwingine kusababisha kukamatwa – kwa watu kulingana na makundi ya haki za binadamu.
"Wanaharakati wamekuwa wakinyamazishwa nyumbani," anasema Bw Seguya. "Ninatumia fursa yangu, kama mtu ambaye yuko Marekani... Kuhamasisha makundi yanayoweza kuishinikiza serikali kutoka sehemu mbalimbali za dunia."
Lakini kauli ya Bw Seguya dhidi ya serikali na miradi kama EACOP zimekumbwa na athari.
"Waendesha kampeni gushi wa mtandaoni wananishambulia kila siku ," anasema. "Wanaendelea kuniita kama adui wa maendeleo nchini Uganda na Afrika. Wakati mwingine wananiita 'kibaraka anayeungwa mkono na Marekani' au aliyenunuliwa."

Akaunti hiyo ya "feki ya Jamechia" ilikuwa moja tu ya matukio kadhaa ya kumshambulia, kumnyanyasa, na wakati mwingine kumtishia Bw Seguya.
Lakini, kwa uchunguzi wa karibu, maelezo yote yalionekana kufanana kwa kila mmoja.
Wote walidai kuwa raia wa Uganda - mara nyingi wanawake - ambao akaunti zao zilionekana kuwa na lengo pekee la kumsifu rais sifa na kuwapinga wakosoaji.
Kituo cha Habari cha Uganda, ambacho kinashughulikia mawasiliano ya umma kwa niaba ya serikali, hakikujibu maombi yetu ya kulitaka kutoa maoni.
Kuchipuka kwa akaunti za mitandao bandia
Kwa kuchunguza tabia za akaunti hizo, BBC iliweza kugundua akaunti bandia 200 za mitandao ya kijamii zinazofanya kazi kwenye mtandao wa X na Facebook (ingawa hatimaye umezuiwa nchini Uganda tangu 2021).
Idadi kubwa ya akaunti hizi zilitumia picha zilizoibiwa kama picha za wasifu - mara nyingi picha za mitandao ya kijamii ya mifano, washawishi, na waigizaji kutoka ulimwenguni kote. Lakini hakuna hata jina moja la watumiaji lililotumiwa na picha hizo zilionekana kuhusiana na watu halisi kutoka nchini Uganda au Tanzania

Akaunti hizi mara nyingi zilichapisha yaliyomo sawa ndani ya dakika kwa kila mmoja. Kwa kuangalia tarehe wakati wao walikuwa kuundwa, sisi pia kutulibaini kwamba jumbe hizo nyingi zilikuwa zimewekwa siku hiyo hiyo.
Hii inaonyesha kwamba, wakati zinaweza kuonekana kama akaunti tofauti, ukweli ni kwamba watoa ujumbe wamekuwa wakifanya kazi pamoja.
Haijulikani jinsi mtandao huu ulivyofanikiwa katika kubadilisha maoni ya watu juu ya serikali, kwani machapisho yake machache sana yalipata idadi kubwa ya watu waliweka alama za kupenda, kutoa maoni, au hisia.
Je, mtandao huu unaweza kushindwa kutimiza dhamira yake basi? Sio kwa kiasi kikubwa, wataalamu wanasema.
"[Lengo lao] linaweza kuwa kushinikiza ujumbe huko nje - ikiwa watu wanajihusisha nao ni aina ya kutokuwa na maana, mradi watu wameuona," anasema Tessa Knight, mshiriki wa Taasisi ya Utafiti wa Digital wa Baraza la Atlantic ambaye anachunguza habari za uongo.
Ni nani anayeendesha mtandao huu wa akaunti?
Ilipowasiliana na BBC, kampuni ya Meta iliondoa akaunti nyingi za Facebook tulizozitambua.
Meta inaamini kuwa watu wanaohusishwa na Kituo cha mashauriano ya Wananchi wa Serikali (GCIC) - shirika la serikali ya Uganda - huenda walikuwa ndio waliokua wakiendesha akaunti kadhaa zilizoondolewa.
Kampuni hiyo haikutoa ushahidi ulioonekana kuwa kituo hicho kiliunga mkono madai hayo. Na matokeo yake, BBC haijaweza kuthibitisha kwa uhuru.
Lakini katika taarifa yake, GCIC ilikanusha madai hayo, ikisema kuwa akaunti za shirika hilo "hazifanyi kazi kwenye Facebook".
Sio mara ya kwanza kwa shirika hilo kushutumiwa kuendesha kile Meta inachokielezea kama "operesheni za ushawishi": mnamo 2021, kampuni mama - Facebook ilichukua hatua dhidi ya mamia ya akaunti ambazo ilisema zilihusishwa na GCIC.
X haikujibu maombi yetu ya kutoa maoni na jukwaa hilo halikuchukua hatua yoyote dhidi ya akaunti yoyote iliyotambuliwa na uchunguzi wa BBC.
Ilipoulizwa ikiwa inatambua akaunti yoyote kwenye X, GCIC ilisema: "tunatambua akaunti za wafanyakazi wetu ambao masharti yao ya kumbukumbu ni pamoja na kusambaza habari za ukweli kuhusu mipango ya serikali. Tunatambua tu na kuwajibika kwa akaunti za wafanyakazi wetu waliokusudiwa kufanya kazi."
GCIC haikujibu maswali ya kufuatilia kujaribu kufafanua ikiwa akaunti zilizotambuliwa ziliendeshwa na wafanyakazi wa serikali.
Bw Seguya anasema "hajashangazwa" na kuwepo kwa mtandao huu, lakini anamtaka yeyote aliye nyuma yake kuzingatia gharama za kibinadamu za kampeni yao dhidi ya wakosoaji.
"Huenda hawajui athari mbaya wanazotengeneza kwa afya ya akili ya mtu kwa kutuma vitisho kama hivyo kwa watu kama mimi na wanaharakati tofauti.
"Waache kuwanyamazisha wapinzani. Maoni tofauti ni demokrasia."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












