Kwa nini vikosi vya Ukraine vimeshindwa kuvunja ulinzi wa Urusi?

Iliyochapishwa

Maoni katika vyombo vya habari vya Magharibi juu ya matukio ya hivi karibuni huko Ukraine yamejawa na kukata tamaa. Mashambulizi ya miezi mingi, hayajaleta ushindi wa haraka kwa jeshi la Ukraine. Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine vinapigana kila kilomita ya ardhi katika mikoa ya Zaporozhye na Donetsk na kujilinda katika mkoa wa Lugansk, ambapo jeshi la Urusi linajaribu kushambulia.

Miongoni mwa sababu za hali hii, wataalamu wanataja ni ulinzi ulioandaliwa vizuri wa jeshi la Urusi, mafunzo duni ya askari wa Ukraine, ukosefu wa aina fulani za silaha, pamoja na wingi wa askari wa Urusi.

Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine vilijaribu kutumia sana magari ya kivita ili kuvunja ulinzi wa Urusi, lakini vilitatizwa na mabomu ya chini ya ardhi. Vilevile matumizi ya helikopta na makombora, vyote havikutoa mafanikio ya haraka.

Kisha vikabadili mbinu, na kuanza kushambulia vituo vya mashambulizi vya Urusi na vituo vya kamandi. Makombora na rada zilifanikisha mbinu hii. Mfano, mashambulizi kwenye ghala za adui, kutatiza mawasiliano. Lengo la jumla la mashambulizi haya ni kumfanya adui ajilinde kwa njia ambayo ni faida zaidi kwa mshambuliaji.

Kwanini mafanikio yamekuwa magumu?

Sababu kuu ambayo wachambuzi wa Ukraine, Urusi na wale wa Magharibi wanaandika; ni ulinzi wa Urusi ulioandaliwa vizuri, kuna mabomu chini ya ardhi, ngome, mitaro na mahandaki. Haya yote yalijengwa katika miezi michache wakati Ukraine ikijiandaa kwa mashambulizi.

Disemba 2022, Urusi ilikuwa inajenga ngome katika eneo la Zaporozhye, ikisambaza mifuko ya saruji huko. Ulinzi kawaida hupangwa kwa mistari kadhaa, mstari mmoja unaweza kuwa kilomita kadhaa ya mstari mwingine. Kwa hiyo, hata baada ya kuvunja mstari mmoja, vikosi vitapaswa kuvunja mistari ya mbele kwa njia ile ile.

Baada ya Ukraine kukiri ni kazi ngumu kuvunja ulinzi wa Urusi. Walibadilisha mbinu ili kuvishinda vikosi vya Urusi kwa msaada wa silaha. Maana ya mabadiliko ya mbinu ni kwamba kwa vile ni askari ndio nguvu kuu inayohakikisha uimara wa ulinzi, basi ni muhimu kuwadhoofisha kwanza, na kisha itakuwa rahisi kukabiliana na vikwazo.

Mapema Agosti, gazeti la Marekani la New York Times lilichapisha makala ya uchambuzi ikisema wanajeshi wa Ukraine, walioandaliwa kwa ajili ya mashambulizi, walipewa mafunzo na nchi za Magharibi lakini hawakuwa na muda wa kutosha kupokea mafunzo.

Maafisa wa utawala wa Biden walitarajia kwamba brigedi tisa zilizofunzwa kutoka nchi za Magharibi, jumla ya askari 36,000, wangeonyesha njia ya vita ya Marekani ni bora kuliko ya Urusi. Wakati Urusi ina muundo wa amri wa kati, Wamarekani waliwafundisha Waukraine jinsi ya kuwapa askari wa cheo cha juu na wale wa kawaida, uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka kwenye uwanja wa vita.

Swali hapa sio ubora wa vifaa vya kijeshi, lakini kiwango cha mafunzo. Kama wataalamu wa kijeshi Franz Stefan Gadi na Michael Kofman wanavyosema katika makala iliyochapishwa katika jarida la Economist, askari wa Ukraine walijua mbinu za uendeshaji wa vita katika ngazi za chini, lakini matatizo yalianza kutokea juu ya kikosi.

Mbinu ya Magharibi

Moja ya faida za Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine, ambayo imezungumzwa sana katika miezi ya hivi karibuni, ni silaha za Magharibi na zana za kijeshi. Hata hivyo, faida hii kwa maana fulani ikawa hasara.

Kwa upande mmoja, mifumo mingi ambayo ilitolewa na inayotolewa kwa Ukraine ilitengenezwa hivi karibuni au ya kisasa, na ni bora kuliko ile iliyokuwa ikimilikiwa na Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine kabla ya uvamizi wa Urusi.

Baada ya uvamizi huo kuanza, washirika wa Ukraine walijaribu kuondosha mifumo ya silaha za mtindo wa Soviet - katika kesi hii, hakukuwa na haja ya kutumia muda wa mafunzo - walikuwa wanafahamu vizuri vifaa hivyo. Lakini hizi silaha za kisasa zinahitaji muda mwingi wa mafunzo.

Kama Andriy Tarasenko, mtaalamu wa silaha wa kutoka Ukraine, aliiambia BBC, magari ya kivita ya Soviet, yaliundwa tofauti kabisa na mifumo ya magari ya Magharibi. Kulingana na ye, magari ya kivita ya Soviet yaliundwa ndani ya mfumo wa teknolojia wa miaka ya 1950-60, wakati Umoja wa Kisovieti ulikuwa unajiandaa kupigana katika vita vya nyuklia.

"Kila kitu tunachotumia kwa sasa ni mashine iliyoundwa kwa tiknolojia ya miaka ya 1960, iliyoundwa kulingana na maono ya vita vya wakati huo,"alisema.

Mtaalam wa Kirusi, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa magari ya kivita ya Soviet na Magharibi yaliundwa ili kukabiliana, na kwa hiyo sifa zao mara nyingi zinatofautiana. Anasema, magari ya kivita ya Magharibi yaliundwa zaidi kwa vita vya kujihami, na kwa hivyo ni ya kujilinda zaidi na mazito.

Nini kinafuata?

Licha ya kukata tamaa kwa wachambuzi katika kutathmini matokeo ya askari wa Ukraine wakati wa mashambulizi, karibu wote wanaona kuwa Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine bado vina uwezo wa kusonga mbele.

Katika mahojiano na kituo cha Alexander Plushev, Michael Kofman alisema kuwa brigedi zisizo na mafunzo ya kutosha za vikikosi vya Ukraine, wanapata uzoefu wa mapigano katika vita, na ufanisi wao wa mapigano unaongezeka.

Wakati huo huo, makombora ya Ukraine yanashambulia mawasiliano, haswa, kwenye madaraja ambayo yanaunganisha Crimea na Bara. Hii ni katika mbinu za Marekani kutenganisha makundi ya wanajeshi.

‘’Licha ya mapungufu yote katika mafunzo na nyenzo na hasara iliyopatikana, vikosi vya wanajeshi vya Ukraine bado vina nafasi ya kuvunja ukuta wa ulinzi wa Urusi mapema au baadaye," Kofman anaamini.