Kutana na maduka ya ughaibuni yanayounganisha watu na nchi zao

SHOPS

Chanzo cha picha, POPAT MITHAI & FARSAN

Iliyochapishwa

Katika duka la familia la vyakula la Popat Mithai & Farsan, linalomilikiwa na Vijaya Popat na wafanyakazi wake wote wanawake mara nyingi huwa na shughuli nyingi sana kushughulikia wateja wa lugha nyingi kiasi cha kukosa muda wa kukaa chini, achilia mbali kuzungumza na mwandishi wa habari.

Bi Popat alianzisha biashara hii huko Leicester mwaka 2011 ili kuuza peremende na vyakula vya Kihindi, ikikuwa kutoka wafanyakazi wawili hadi wafanyakazi 15 leo. Huduma kupitia mtandao ilizinduliwa mnamo 2018.

Ikihudumia watu wa Asia Kusini katika jiji la Midlands Mashariki na maeneo ya mbali zaidi, mauzo yaliongezeka wakati wa janga la corona, kwani wateja walitafuta chakula cha faraja zaidi - ladha ambazo wao au mababu zao walileta Uingereza kutoka nchini mwao zikiwemo India, Pakistan, Bangladesh na Sri Lanka.

Mtoto wa Bi Popat Shyam alizungumza na BBC. "Mama yangu anajulikana sana katika jamii kama mtu anayeendesha biashara," anasema. "Na wote wanataka kuongea naye haswa ili kuona kama anaweza kutoa vitu fulani."

POPAT MITHAI & FARSAN

Chanzo cha picha, POPAT MITHAI & FARSAN

Maelezo ya picha, Biashara ya Popat Mithai & Farsan ya mtandaoni imesaidia kuhudumia wateja wake katika maeneo mbaimbali ya Uingereza.

Anaongeza kuwa sio wahamiaji wa kizazi cha kwanza tu, au wale ambao wamehamia Uingereza hivi karibuni, wanaounda msingi wa wateja wake. Badala yake pia kizazi cha pili, ambao huenda wananunua chakula cha familia zao, na wanazidi kuongezeka mtandaoni.

"Mauzo ya mtandaoni sasa yanachukua takriban robo moja hadi theluthi moja ya mauzo yote ya biashara."

Mbali na kuagiza bidhaa kutoka Asia Kusini, duka pia hununua bidhaa kutoka Kenya. Kenya ilitangaza mwezi Septemba kuwa itaunda wizara mpya kwa ajili ya Wakenya wanaoishi nje ya nchi, na Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kwamba atauambia Mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika utakaofanyika mwezi ujao mjini Washington kwamba anataka "kukuza uhusiano wa wageni wanaoishi nchini humo".

pizza

Chanzo cha picha, Google

Maelezo ya picha, Pizza ni chakula maarufu duniani, asili yake ni Italia

Lakini watu wnaaoishi nje ya nje zao duniani ni wengi kiasi gani? Hivi sasa kuna watu milioni 281 ambao wanaishi katika nchi tofauti na zile ambazo walizaliwa, kwa mujibu wa Ripoti ya Uhamiaji Duniani ya 2022 kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM).

Idadi hiyo ni sawa na 3.6% ya idadi ya watu duniani, au mtu mmoja kati ya 30. Na haijumuishi watoto ambao watu hao wanao ambao wamezaliwa katika nchi yao ya ugenini, wala haijumuishi vizazi vya wahamiaji wa zamani.

Idadi kamili ni vigumu sana kuhesabu kwa sabababu ya utambulisho wa kitamaduni wa mtu. Hata IOM ilisema mnamo 2020 kwamba "kwa sasa hakuna majaribio ya kufanya sensa ya idadi ya watu wanaoishi nje ya nchi kwa kila sekunde".

Biashara ya kimataifa

Jambo la hakika, ni kwamba msukumo wa ujasiriamali kwa wageni wakiwemo wahamiaji umekuwa ukitambuliwa kwa muda mrefu. Ripoti ya mwaka 2010 ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ilisema kuwa wajasiriamali wahamiaji walikuwa na elimu bora kuliko wenzao asilia, na wana uwezekano mkubwa wa kuunda biashara mpya.

Na mara nyingi makampuni au biashara nyingi za wageni zinahusika katika uingizaji wa chakula, nguo au bidhaa nyingine kutoka nchi zao za asili, kama anavyofanya Vijaya Popat mzaliwa wa India na duka lake linalostawi huko Leicester.

Duka hilo, na mengine kama hayo, yalichangia mauzo ya nje ya India kwenda Uingereza jumla ya $10.4bn mwaka jana. Akiwa Paris, Olivier Habiyambere anasaidia kukuza mauzo ya Kenya hadi Ulaya. Yeye ndiye mwanzilishi wa tovuti ya Kenyan Diaspora Market, ambayo huagiza chakula na nguo kwa wingi kutoka nchi hiyo ya Kiafrika, na kisha kuziuza kwa wateja katika bara la Ulaya.

OLIVIER HABIYAMBERE

Chanzo cha picha, OLIVIER HABIYAMBERE

Maelezo ya picha, Olivier Habiyambere anasema biashara kupitia Kenyan Diaspora Market imekuwa kupitia njia ya mdomo tu

Bwana Habiyambere, ambaye alilelewa nchini Kenya, alipata wazo la biashara hiyo alipohamia Paris kusoma na kukutana na watu wengine kutoka Kenya na Afrika Mashariki. "Kila mtu alitaka bidhaa za Kenya, lakini suala lilikuwa kuleta bidhaa hizo kutoka Kenya hadi hapa," anasema. "Watu wangeweza kuchukua bidhaa walipoenda Kenya, lakini wasingeweza kufanya hivyo kila mwaka."

Kwa hivyo alizindua biashara hiyo mnamo Aprili 2022 ili kuwapa Wakenya wanaoishi barani Ulaya njia rahisi ya kununua bidhaa kutoka nyumbani.

Bwana Habiyambere anaongeza kuwa biashara imekua polepole, ikisaidiwa na jamii za Wakenya kueneza habari kupitia vikundi vya WhatsApp.

KENYAN DIASPORA MARKET

Chanzo cha picha, KENYAN DIASPORA MARKET

Maelezo ya picha, Kenyan Diaspora Market inauza Ulaya mamia ya bidhaa kama hizi kutoka Kenya na nchi zingine za Afrika Mashariki.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati Kenyan Diaspora Market inalenga wahamiaji wa Kenya, tovuti yenye makao yake Glasgow ya Agora Greek Delicacies sasa ina wateja wengi wasio Wagiriki kuliko wale kutoka katika jumuiya za Wagiriki za Uingereza.

Ilianzishwa muongo mmoja uliopita na mume na mke Christina Lyropoulou na Michael Sofianos, ambao walikuwa walikwenda kusoma nchini Uingereza.

Sasa wameajiri watu 14 na kusambaza vyakula na vinywaji vya Kigiriki vinavyoagizwa kutoka nje kwenda kwenye migahawa, watu binafsi, na biashara nyinginezo.

"Tulianza kuipanua biashara kwa watu wa Uingereza - wale wanaosafiri kwenda Ugiriki au walikuwa na marafiki wa Ugiriki," anasema Bi Lyropoulou.

"Na duka letu la mtandaoni lilishuhudia ongezeko la mauzo ya karibu 1000% katika miezi ya kwanza ya zuio la kutotoka nje kwa sababu ya corona."

Prof Pragya Agarwal, mwanasayansi katika Chuo Kikuu cha Loughborough, mara kwa mara hununua bidhaa zinazotoka India alikozaliwa kwa ajili yake na familia yake nchini Uingereza.

CHRISTINA LYROPOULOU

Chanzo cha picha, CHRISTINA LYROPOULOU

Maelezo ya picha, Christina Lyropoulou alishuhudia biashara yake ikikua sana kipindi cha corona

"Kwangu mimi binafsi, ni juu ya kudumisha uhusiano na nchi ya mama, nchi ya baba - vyovyote unavyoweza kuita," anasema. Anacheka anapoelezea mapenzi yake ya embe za Kihindi, na anakiri mara kwa mara alikuwa akiagiza kutoka kwa duka fulani mtandaoni ili kupata embe, haswa wakati wa janga.

"Hicho ndicho nilichokuwa nakula wakati nakua nchini India kila msimu wa joto - na kila siku baada ya mlo."

Maria Elo, ni profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa Denmark ambaye ana idadi ya vitabu na makala kuhusu watu wanaoishi ng'ambo na biashara.

Anasema ni muhimu kufahamu muundo unaotokea wakati wowote jamii hiyo inapojadiliwa, huku wahamiaji mara nyingi wakielezewa katika mojawapo ya njia mbili.

Simulizi moja ni kwamba uhamiaji na ughaibuni ni tatizo. Prof Elo anaelezea hilo kama "mtazamo wenye mapungufu" na wenye maana hasi. Lakini anaongeza pia kuna simulizi chanya, ambayo inahusisha "biashara na uchumi".

Anaongeza kuwa utafiti unaonyesha kuwa wafanyabiashara wanaoishi nje ni muhimu kwa biashara zinazovuka mipaka. "Sote tunakula pizza leo, ingawa sisi sio wote waitaliano na hilo ni jambo ambalo limepita muda mrefu uliopita."