Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Man Utd: Ole Gunnar Solskjaer awakosoa baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo wakati akiwa kocha Old Trafford
Ole Gunnar Solskjaer amekosoa tabia ya baadhi ya wachezaji wakati wake kama meneja wa Manchester United, akisema hawakuwa wazuri kama walivyofikiria.
Solskjaer alifutwa kazi Novemba 2021 baada ya kuhudumu kwa takriban miaka mitatu.
Mrithi wake Erik ten Hag amesema "hakukuwa na utamaduni mzuri" alipowasili Old Trafford Mei 2022.
"Wengine hawakuwa wazuri kama mtazamo wao wenyewe," Solskjaer, 50, aliiambia The Athletic.
Mshambuliaji huyo huyo wa zamani wa United na Norway aliongeza: "Sitataja majina, lakini nilisikitishwa sana wakati baadhi yao walikataa nafasi ya kuwa nahodha.
"Pia nilisikitishwa wakati wengine walisema hawatacheza au kufanya mazoezi kwa sababu walitaka kuondoka kwa lazima."
Man United ya Solskjaer ilimaliza nafasi ya pili katika msimu wa 2020-21 na kupoteza fainali ya Ligi ya Europa kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Villarreal.
Mwanzoni mwa msimu uliofuata alimsajili fowadi wa Uingereza Jadon Sancho na beki wa Ufaransa Raphael Varane, na kumsajili tena mshambuliaji wa zamani wa United na mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or mara tano Cristiano Ronaldo.
Lakini alifutwa kazi baada ya mechi 12 za Premier League katika kampeni mpya alipopoteza kwa mabao 4-1 kwa klabu ya Watford.
"Unapokuwa na kikundi unahitaji kila mtu kuwa na mwelekeo mmoja," aliongeza. "Wakati mambo hayaendi sawa, niliona wachezaji fulani na wakijigamba.
"Ni kazi nzuri lakini ngumu"
Ten Hag amelazimika kushughulika na masuala mengi ya nje ya uwanja msimu huu, huku Jadon Sancho akifanya mazoezi nje ya kikosi cha kwanza na winga wa Brazil Antony akichelewesha kurejea Old Trafford ili "kushughulikia tuhuma" za unyanyasaji dhidi yake.
Mason Greenwood amejiunga na klabu ya ligi kuu ya Uhispania Getafe kwa mkopo kufuatia uchunguzi wa ndani wa klabu baada ya mashtaka ya uhalifu dhidi yake, ikiwemo kujaribu kumbaka na kushambulia, kutupiliwa mbali.
Kwa kuongezea, umiliki wa kilabu bado haujatatuliwa baada ya familia ya Glazer kusema kuwa walikuwa wakifikiria kuiuza kwani "wanatafuta njia mbadala" mnamo Novemba 2022.
Shinikizo linaongezeka kwa Ten Hag, huku United wakiwa wamepoteza mechi tatu kati ya tano za mwanzo za Ligi Kuu msimu huu.
Alipoulizwa kama ana huruma na Ten Hag, Solskjaer alisema: "Najua anachopitia. Ni kazi nzuri, lakini ni ngumu.
"Unashirikiana na wanadamu , shida zao zote Pamoja na asili - hii sio simulizi ya kompyuta.
"Lakini wengi ni wataalamu wazuri ambao wanataka kufanya vizuri. Wengine wanafikiria juu ya nambari moja kwanza, lakini wengi wanafikiria kuhusu klabu."
Kumekuwa na maandamano ya mashabiki dhidi ya umiliki wa Glazer lakini Solskjaer aliwataja kama "waaminifu na wenye kutaka maendeleo" katika mazungumzo ambayo amekuwa nao .
"Ilinibidi kuwa mvumilivu na mwenye nguvu kiakili . Na wamemuunga mkono meneja wa sasa," aliongeza.
Kurudi kwa Ronaldo 'ilikuwa hatua mbaya'
Solskjaer alimsajili tena Ronaldo - mnamo 31 Agosti 2021, miaka 12 baada ya nyota huyo wa Ureno kuondoka kwenda Real Madrid.
Lakini kurejea Old Trafford kuligeuka kuwa hatua mbaya pale alipoikosoa klabu hiyo na kusema "hana heshima" kwa meneja Ten Hag, jambo ambalo lilipelekea Ronaldo kuondoka na kujiunga na Al-Nasr, nchini Saudi Arabia, mwezi Disemba.
"Ulikuwa uamuzi ambao ulikuwa mgumu sana kuukataa na nilihisi kwamba tulipaswa kuuchukua, lakini ikawa si sawa," Solskjaer alisema kuhusu kurejea kwa Ronaldo.
"Ilikuwa vyema wakati [Ronaldo] aliposajiliwa na mashabiki walihisi hivyo kwenye mechi dhidi ya Newcastle, Old Trafford [baada ya Ronaldo kufunga mara mbili katika ushindi wa 4-1].
"Bado alikuwa mmoja wa wafungaji bora zaidi duniani, alikuwa akionekana kuwa na nguvu."
Haaland, Rice, Bellingham na Kane wote walitafutwa kusajiliwa
Solskjaer pia alifichua kuwa klabu hiyo haikuweza kuwanunua wachezaji aliowatajia.
Walijumuisha mshambuliaji wa Manchester City Erling Haaland, kabla ya kujiunga na RB Salzburg mwaka 2019, kiungo wa kati wa Arsenal Declan Rice, ambaye alisajiliwa na The Gunners kwa mkataba wa pauni milioni 100 kutoka West Ham mwezi Julai na Jude Bellingham, aliyejiunga na Real Madrid kutoka Borussia Dortmund msimu huu wa joto.
Alipoulizwa ni wachezaji gani alijaribu kusajili, Solskjaer alisema: "Erling Haaland, kabla hajacheza mechi yake ya kwanza na Salzburg.
"Declan Rice hangegharimu kile alichokifanya msimu wa joto. Tulimjadili Moises Caicedo, lakini tulihisi tunahitaji wachezaji walio tayari kwa wakati huo.
"Tulimtaka Jude Bellingham vibaya - ni mchezaji wa Man United - lakini ninaheshimu alichagua Dortmund. Labda hiyo ilikuwa busara."
Akimzungumzia nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza, Harry Kane, aliyehamia Bayern Munich msimu huu kutoka Tottenham, aliongeza: "Ningemsajili Kane kila siku ya wiki na ufahamu wangu ulikuwa kwamba alitaka kuja, lakini klabu haikuwa na bajeti kutokana na vikwazo vya kifedha kutoka Covid-19.