Mzozo wa Loliondo: Miaka 30 ya machungu na matumaini
Na Yusuph Mazimu
BBC Swahili,Dar es Salaam

Vitu viwili vinavyolitambulisha zaidi eneo la Loliondo, Kaskazini mwa Tanzania hasa katika miaka ya hivi karibuni ni:
Kwanza, kuibuka kwa Mzee Ambilikile Mwasapile maarufu kama babu wa Loliondo, ambaye mwishoni mwa mwaka 2010 na mwanzoni mwa 2011 kupitia tiba yake ya ‘kikombe cha babu’ alichokuwa anadai kinatibu magonjwa mbalimbali makubwa alikusanya maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya Tanzania waliokwenda kunywa dawa Loliondo, akiwemo Rais John Magufuli, wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi katika serikali ya awamu ya 4 ya Rais Jakaya Kikwete.
Jambo la pili linalolitambulisha eneo la Loliondo ni mgogoro wa ardhi.
Babu wa Loliondo amefariki Julai, 2021 baada ya kuishi kwa miaka 86, lakini mgogoro wa Loliondo umeendelea kudumu mpaka hii leo ukiishi kwa miaka karibu 30. Mzozo unaonekana kuleta matumaini ya mipango ya serikali kwenye uwekezaji lakini machungu kwa wanaoathiriwa na hatua za aina hiyo.
Nini kiini cha mzozo huu hasa?
Ujio wa muwekezaji Ortello Business Corporation (OBC) ulibadilisha maisha ya kawaida yaliyozoeleka katika Eneo la Loliondo. Mwaka 1992 chini ya Brigedia Mohamed Abdulrahim Al-Ali, kutoka falme za kiarabu (UAE) kwa upande wa OBC na Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, zilisaini mkataba huo ulioonekana kama chanzo cha mizozo yote iliyofuata huko Loliondo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mkataba ulikuwa ni wa shughuli za uwindaji, lakini wakazi wa Loliondo hasa wa vijiji nane vilivyokuwa vinaguswa kwa namna moja ama nyingine ambao wengi wao ni wafugaji wa jamii ya kimasai walipinga uwekezaji huo.
Wakilalamika kutoshirikishwa katika hatua za mwanzo za mkataba na kuelewa kinachoendelea, na hilo likaibua kile kilichoitwa ‘Loliondo Gate Scandal’, skendo iliyoonekana kama kuna watu ndani ya Serikali wanaojaribu kuuza ardhi ya Lolilondo kwa mwekezaji.
Baada ya wananchi kuzidi kumpinga mwekezaji, mwaka 2008 serikali na mwekezaji walikuja na mkataba uliolezwa kuwa ‘shirikishi ili kupunguza ukinzani.
Ulikuwa mkataba kati ya mwekezaji OBC na halmashauri ya kijiji, kwa vijiji husika ambapo ulielezwa kuwa na kipengele kilichomtaka mwekezaji, OBC kulipa wanakijiji shilingi milioni 25, kwa sharti la wanakijiji kuondoka kwenye eneo la mkakati la uwekezaji.
Kwa mujibu wa Muungano wa watetezi wa haki za binadamu, kupitia ripoti yao ya haki za binadamu iliyoitwa ‘Loliondo joint fact finding mission’, huu ndio ulikuwa msingi wa kuhamisha wakazi wa eneo la karibu na Pori tengefu Loliondo, zoezi lililolalamikiwa kuvunja haki za binadamu.

Machungu ya Loliondo
Baada ya Mwaka 2008, kusainiwa kwa mkataba ulioonekana ‘shirikishi’ ukimuhusisha mwekezaji na vijiji, mwaka 2009 Serikali ilianza utekelezaji wa uwekezaji huo, kwa kuwaondoa wakazi na mifugo katika eneo la kimkakati la uwekezaji.
Kwa mujibu wa ripoti ya Muungano wa Mashirika yasiyo yakiserikali watetezi wa haki za binadamu iliyotoka mwaka 2015, zoezi hilo la kuwaondoa wakazi wa Loliondo kwa nguvu liliathiri wanakijiji zaidi ya 4,000, na maboma zaidi ya 300 yalichomwa moto.
Baada ya hapo matukio ya ukinzani yaliendelea karibu kila wakati. Lakini waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Hamis Kaghasheki kupitia sheria ya uhifadhi ya mwaka 2009, alieleza azma ya serikali ya kupunguza ukubwa wa eneo la Pori Tengefu la Loliondo kutoka Kilomita za Mraba 4,000 hadi 1,500 na kupandisha hadhi kutoka pori tengefu hadi kuwa pori la akiba.
Tangazo hilo halikueleweka na kusababisha wanakijiji wa jamii ya kimasai kukusanyika Dodoma, bungee likiendelea, kabla ya Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda kuingilia kati na kueleza kuwa eneo hilo ni la wamasai kwa ajili ya shughuli zao za kijami na kiuchumi.
Mwaka 2017, Serikali ilitoa tangazo maalmu la kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi ya Serengeti na mpaka wa pori tengefu la Loliondo, tangazo ambalo liliendelea kuibua wasiwasi na kuwa chanzo cha mizozo zaidi katika eneo hilo iliyoendelea kudumu mpaka leo.
Mwaka huo huo wa 2017, kifo kilichotokana na kupigwa risasi kwa Pormoson Losso, mkazi wa kijiji cha Ololosokwan, Loliondo kiliibua hasira zaidi, ingawa Wizara ya Maliasili na Utalii ilikana kwa kuwa kilitokea kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa zoezi la kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi, zoezi lililoanza Agosti 13, 2017.
Wiki moja iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mogella alithibitisha kifo cha askari polisi mmoja aliyeuawa kwa kupigwa na mshale akisimamia ulinzi wakati wa zoezi la uwekaji mipaka kati ya vijiji na eneo la pori Tengefu Loliondo.
Hatua ya kusababisha kifo, majeruhi, uharibifu wa mali na madhara mengine ya kimazingira, kisaikoloji, kiuchumi na kijamii yanatia wasiwasi zaidi kuhusu mustakabili wa wakazi wa eneo hilo, watumishi wa serikali, ikolojia ya wanyama na uwepo wa pori tengefu la Loliondo.
Ukubwa wa suala hili umeanza kuonekana, si tu kwa mashirika ya haki za binadamu, wanaharakati na vyombo vya habari kuripoti mara kadhaa, lakini kujiingiza kwa Umoja wa Mataifa (UN), kunaleta picha tofauti.
Kupitia jukwaa lake la kudumu la masuala ya wenyeji ama watu wa asili, Umoja huo umeitaka Tanzania kuondoa maafisa wake wa usalama Loliondo ili kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji unaodaiwa kufanyika katika eneo hilo.
Kauli ya serikali na Matumaini ya kutekeleza mpango wake
Kwa muda mrefu mpango na nia ya serikali ya Tanzania katika mapori tengefu na hifadhi zake ikiwemo Ngorongoro, Serengeti na Pori Tengefu Loliondo ni kulinda maeneo hayo, ikiwemo kuondoa maboma na mifugo pamoja na kuweka mipaka na alama ili kutenganisha maeneo hayo na yale ya vijiji kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Zoezi la sasa la uwekaji wa alama Loliondo lililosababisha kifo cha askari mmoja, na baadhi ya wanakijiji kujeruhiwa katika rabsha za kupinga zoezi hilo, ni muendelezo wa nia ya serikali ya kulinda maeneo hayo ya hifadhi.
Hata hivyo, msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipozungumza na BBC mara mbili alisisitiza hali ni shwari Loliondo na kwamba kilichotokea hadi kusababisha mauaji ni wakazi kuwafuata askari polisi na si polisi kuwafuata wakazi, wakati wa zoezi la kuweka mipaka, umabali wa takribani kilomita 8, kutoka yalipo makazi ya watu.
Tangu mwishoni mwa juma lilimalizika Juni 12, picha za video, ripoti na picha kadhaa mnato zilizagaa zikionesha wakazi wakikimbia huku na huko, baadhi yao wakiwa wamejeruhiwa na wengine wakitajwa kukimbilia nchi jirani ya Kenya kwa matibabu.

Awali akizungumza bungeni mjini Dodoma Ijuma Juni 10, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema ‘hakuna mapambano yoyote, hakuna askari yeyote aliyekwenda huko kwenye kijiji kutishia, kwa sababu katika mipango yote hakuna kijiji kinaondoka, hakuna mwananchi anayeondolewa, wananchi wa Loliondo watulie’, alisema Majaliwa na kuongeza.
Waziri Majaliwa akaongeza‘ eneo lile ni letu sote na tutaliratibu vizuri baada ya kuweka hizo alama, kuashiria tu kwamba huku ndani ndo tumehifadhi, tuweze kuratibu kwa pamoja, hayo ndiyo malengo ya serikali kwa eneo la Loliondo’, alisema.
Lengo hasa la serikali kuendelea na zoezi hilo la Loliondo ni kutokanana na umuhimu wake kwa ikolojia na uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania.
Suluhu ya mzozo huu ni ipi?
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwahi kuunda kamati iliyopokea mapendekezo kadhaa kutoka kwa wakazi, wahifadhi na wadau wengine wanaohusika na iliyakusanya mapendekezo kadhaa, likiwamo la kuanzisha Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) au kuanzisha mamlaka kamili ya uhifadhi wa eneo hilo ambayo itaihusisha Serikali na jamii.
Mapendekezo hayo yanatajwa yanaweza kusaidia kuleta ahueni ya mzozo huo, huku Kituo cha Sheria na haki za binadamu nchini Tanzania, LHRC kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wake, Fulgence Massawe, kiliiambia BBC kwamba kunahitajika uwazi zaidi katika mzozo wa Loliondo kaskazini mwa nchi hiyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Raphael Kugesha, ambaye mbali ya kuwa mtaalam wa masuala ya jamii, amefanya kazi kwenye sekta ya utalii kwa zaidi ya miaka 10.
‘Nia ya Serikali ni njema, inataka kulinda hifadhi na mapori tengefu, ambapo mapato yake yanatumika kwa maendeleo yetu, sasa usipolinda hifadhi na pori tengefu kama la Loliondo, unahatarisha uwepo wake, lakini ni lazima ushirikishwaji uwe mkubwa sana, kwa sababu zoezi linakwenda kuathiri watu walioishi kwa muda mrefu na waliozoea mazingira yale’.
Samwel Nangiria alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema ‘mgogoro huu umechukua sura hiyo kwa sababu, serikali imeshindwa kutengeneza mazingira mazuri ya majadiliano, kukutana na viongozi wa kiserikali au kisiasa (Loliondo) na kuongea nao haitoshi’.

Matukio muhimu ya kihistoria ya mzozo wa Loliondo
Mwaka 1992: Kusainiwa mkataba wa uwekezaji katika eneo la Loliondo kati ya mwekezaji Ortello Business Corporation (OBC) na Serikali.
Mwaka 2008: Kusainiwa kwa mkataba mwingine baada ya mazungumzo kati ya OBC na vijiji ili wananchi wapishe eneo la mkakati la uwekezaji kuruhusu uwekezaji kuendelea. Wapo wananchi waliokataa na wapo waliokubali
Mwaka 2009: Kuondolewa kwa wakazi na maboma ya wananchi wa jamii ya kimasai, yaliyoonekana yako ndani ya eneo pori tengefu. Maboma 300 yanadaiwa yalichomwa moto na wakazi takriban 4,000 kupisha shughuli uwekezaji.
Mwaka 2013: Serikali kupendekeza kutengwa kwa hekari 2,500 kusalia kwa wananchi na 1,500 kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.
2016: Kamati ya Kamani
Naibu waziri wa Maliasili na utaliii wakati huo, Ramo Makani alitangaza kuunda kamati kushughulikia mgogoro wa Loliondo.
Mwaka 2017: Kulitokea kwa rabsha zingine za mzozo huo kufuatia zoezi la serikali kuodoa mifugo na makazi, na kusababisha baadhi ya watu kufungua kesi kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).
Mwaka 2017: Vijiji vinne vilifungua shauri namba 15 la mwaka 2017 kuiomba mahakama ya haki ya Afrika Mashariki , EACJ kuizuia Serikali kuacha kufanya jambo lolote katika eneo hilo hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Mwaka 2018: Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) yatoa uamuzi wa zuio la kuwahamisha wakazi wa maeneo yenye mzozo huko Loliondo kwa kuwa ni kinyime cha sheria.
Juni, 2022 : Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, katika hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo, aonesha azma ya Serikali kuendelea kumega eneo la pori tengefu la Loliondo kwa kupandisha hadhi kwenda kuwa pori la akiba. Licha ya uwepo wa kesi iliyofunguliwa na vijiji vinne vya Loliondo kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki, ambayo hukumu yake itakuwa Juni 22, mwaka huu.
Juni 10, 2022: Kwatokea purukushani kati ya askari wa jeshi la Polisi na baadhi ya wakazi kutoka katika vijiji 14. Ikaripotiwa baadaye kuuawa kwa askari polisi mmoja.
Juni 12: 2022 Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, asisitiza hali ni shwari Loliondo, na kilichotokea hadi kusababisha mauaji ya askari polisi ni wakazi kuwafuata polisi na si polisi kuwafuata wakazi, wakati wa zoezi la kuweka mipaka, katika eneo lililopo kilometa 8, kutoka yalipo makazi ya watu.















