Tanzania: Serikali haijakwenda kuwaondoa Wamasai Loliondo au Ngorongoro’ - Msigwa
Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amekanusha madai kwamba serijkali inatumia nguvu kuwaondoa wakaazi wa jamii ya wamasai kutoka ardhi zao huko Loliondo na Ngorongoro.
Akizungumza na BBC Swahili kuhusu taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotaka serikali kuondoa polisi katika maeneo hayo na kutotumia nguvu katika zoezi hilo Msigwa amesema wanaondoka maeneo hayo wanafanya hivyo kwa hiari baada ya kuzungumza na serikali kuhusu umuhiu wa kuhifadhi mazingira .
Kupitia taarifa ,Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wenyeji ama watu wa asili limeeleza kusikitishwa kwake na juhudi zinazoendelea za kuwaondoa zaidi ya Wamasai 70,000 wa tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro, Tanzania kutoka eneo la kilomita za mraba 1,500, ambazo ni ardhi ya vijiji iliyosajiliwa kisheria.
Jukwaa hilo limesema kwamba mnamo Juni 8, lilipata taarifa kuwa polisi wa Tanzania kwa kutumia nguvu, ikiwa ni pamoja na kutumia silaha kiholela, waliwaondoa kwa nguvu Wamasai katika ardhi zao na kusababisha makumi ya watu kujeruhiwa huku baadhi ya watu wakikimbilia msituni.
Pia iliripotiwa matukio mbalimbali ya kukamatwa kwa viongozi wa jamii hiyo, wakiwemo Madiwani wa Vijiji na Wenyeviti. Umoja wa mataifa unataja vitendo hivi kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu na za Wamasai wa Loliondo.
