Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani imeisaidia Ukraine kwa kiasi gani mpaka sasa?
Msaada kwa Ukraine limekuwa suala nyeti tangu Donald Trump alipojikuta akirejea katika Ikulu ya White House.
Rais Trump ametoa madai kadhaa kuhusu ni kiasi gani Marekani imetumia ikilinganishwa na nchi za Ulaya.
Hata hivyo, baadhi ya madai yake yanatiliwa shaka - bila ushahidi wa kuyathibitisha.
Je, Marekani imetumia dola bilioni 300-350 kuisaidia Ukraine?
Rais Trump amedai hivi mara kadhaa - ikiwa ni pamoja na alipomkaribisha Rais wa Ufaransa Macron kwenye Ikulu ya White House wiki hii.
Jibu fupi: Takwimu zinaonyesha kwamba kiasi halisi kilichotumika ni kidogo zaidi.
BBC Verify haikuweza kupata ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.
Kuna hesabu tofauti kuhusu matumizi ya Marekani nchini Ukraine au yanayohusiana na Ukraine - na inaonesha kiasi cha chini zaidi.
Taasis ya Kiel yenye makao yake Ujerumani inayofuatilia msaada unaopelekwa Ukraine. Ilikadiria kuwa Marekani ilitumia dola bilioni 119.7 (£94.3bn) kwa msaada kati ya Januari 2022 na Desemba 2024.
Wengine wamefikia kiasi kikubwa zaidi - lakini kwa maana pana ya kile kinachohesabiwa kama matumizi kwa Ukraine.
Idara ya Ulinzi ya Marekani imetoa takwimu ikizingatia matumizi yote kwenye Operesheni Atlantic Resolve - ambayo ilianzishwa baada ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Inasema kuwa dola bilioni 182.8 zimeidhinishwa - kiasi kinachojumuisha mafunzo ya kijeshi ya Marekani barani Ulaya na hifadhi mpya za ulinzi za Marekani.
Hata hivyo, takwimu zote hizi ni za chini kuliko alivyodai rais.
Tuliuliza Ikulu ya White House kuhusu msingi wa madai ya dola bilioni 350. Hadi sasa, haijatoa kauli yoyote.
Je, Marekani imetumia dola bilioni 200 zaidi kuliko Ulaya?
Rais Trump amedai: "Tumeweka zaidi ya dola bilioni 300 na Ulaya imetumia takriban dola bilioni 100 - hiyo ni tofauti kubwa."
Jibu: Takwimu zinaonyesha kuwa Ulaya imetumia zaidi inapojumuisha msaada wote na, kama ilivyoelezwa hapo juu, hatuwezi kupata ushahidi wa takwimu za dola bilioni 300.
Marekani ni mfadhili mkubwa zaidi wa Ukraine, kwa mbali. Hata hivyo, Ulaya kwa ujumla imetumia fedha nyingi zaidi kuliko Marekani, kulingana na Taasisi ya Kiel.
Hii inajumuisha msaada kutoka kwa Umoja wa Ulaya, lakini pia kutoka kwenye mikataba ya pande mbili yaani kwa nchi za Ulaya, ndani na nje ya EU. Inahusisha msaada wa kijeshi, kifedha na kibinadamu.
Inakadiriwa kuwa kuanzia Januari 24, 2022 hadi mwishoni mwa 2024, Ulaya kwa ujumla ilitumia dola bilioni 138.7 kwa Ukraine. Katika kipindi hicho hicho, Marekani itatumia dola bilioni 119.7, kwa mujibu wa takwimu zao.
Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte alitoa hoja kama hiyo, akiiongeza Canada kwenye hesabu yake.
Bwana Rutte alisema Februari 2025: "Mnamo 2024, Shirikisho la NATO lilipeleka msaada wa usalama wa zaidi ya euro bilioni 50 kwa Ukraine – karibu 60% ya hii ikitoka Ulaya na Canada."
Tuliomba takwimu za NATO, lakini walisema kuwa ni siri.
Je Ulaya italipwa pesa zake wakati Marekani haitalipwa?
Hii ni kauli aliyotoa Rais Trump alipomkaribisha Rais Macron.Ambayo ilimfanya Rais Macron kukubali, akisema kuwa Ulaya na Marekani zilitoa kwa pamoja mikopo na misaada.
Jibu fupi: EU imetoa mikopo, lakini pia misaada.
Rais Macron yuko sahihi, kwa mujibu wa takwimu za Kiel. Lakini wanaamini kuwa Rais Trump pia ana hoja; Marekani imetuma misaada zaidi, huku EU ikituma mikopo zaidi.
Hata hivyo, kuna takwimu tofauti huko nje.
Umoja wa Ulaya unasema nchi za EU zimetoa msaada wa karibu $145bn hadi sasa na kwamba ni 35% tu ya hiyo imekuwa mikopo. Kama vile Idara ya Ulinzi ya Marekani, EU imetumia ufafanuzi zaidi wa kile kinachozingatiwa kuwa kama msaada kwa Ukraine.
Mikopo ya EU itakuwa kwa masharti nafuu - kwa hivyo Ukraine itakuwa ikilipa riba kidogo kuliko kawaida.
Aidha nyakati nyingine, Ukraine haitarajiwi kulipa chochote, huku malipo yakitokana na mapato ya mali ya Urusi iliyowekewa vikwazo.
Tunachoweza kusema ni kwamba misaada kwa Ukraine imekuwa ni pamoja na mikopo na ruzuku.
Uingereza imetoa kiasi gani kwa Ukraine?
Uingereza ni mojawapo ya serikali zinazoifadhili Ukraine.
Lakini nchi pekee ambazo zimetoa zaidi ni Marekani na Ujerumani, kulingana na data ya Kiel.
Lakini michango ya Uingereza ni kiwango ndogo sana kuliko Marekani.
Hilo linazua swali kwa Uingereza na nchi nyingine za Ulaya; ikiwa Marekani itaondoa sehemu kubwa ya ufadhili wake kwa Ukraine, je mataifa mengine yanaweza kuleta tofauti hiyo?
Hilo litahitaji nyongeza kubwa ya michango yao.