Baraza la ghuba lapongeza Oman kwa kuanzisha njia mbadala ya usafiri katika Mlango wa Hormuz
Chanzo cha picha, Eric Lee/POOL/AFP via Getty Images
Baraza la Ushirikiano la Ghuba, GCC, limepongeza hatua ya Oman ya kuanzisha njia ya muda ya usafiri wa baharini katika Mlango wa Hormuz na wakati huo huo kukosoa vitisho vya Iran dhidi ya uhuru wa usafiri katika mlango huo.
Katibu Mkuu wa GCC, Jassem Mohammed Al Badawi, alisema Ijumaa kuwa njia hiyo ya muda itasaidia kuwaondoa na kuwasafirisha zaidi ya mabaharia 11,000 waliokwama katika eneo hilo.
Oman ilitangaza Jumanne kuwa imeanzisha njia hiyo kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Bahari, IMO, ambalo ni wakala wa Umoja wa Mataifa.
Hatua hiyo imepingwa na Iran, huku Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi likisema kuwa njia pekee zinazoruhusiwa kupita katika Mlango wa Hormuz ni zile zilizotangazwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Usalama katika Mlango wa Hormuz hauwezi kuhakikishwa bila ushirikiano wetu - Iran
Chanzo cha picha, Stringer/Anadolu via Getty Images
Maelezo ya picha, Katika mji wa Bandar Abbas, usafiri wa boti ndogo kati ya bandari za kusini mwa Iran na Falme za Kiarabu ulirejea Alhamisi, Julai 24, baada ya mvutano katika eneo hilo kupungua.
Mvutano katika Mlango wa Hormuz unaendelea kuongezeka. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema usalama wa usafiri kupitia mlango huo hauwezi kuhakikishwa bila uratibu na Iran, akionya kuwa njia zozote za usafiri zinaweza kusitishwa ikiwa hakutakuwa na ushirikiano na Tehran.
Iran pia imekosoa taarifa ya pamoja iliyotolewa jana na Marekani na Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC), ikiitaja kuwa “ya kuingilia masuala ya wengine, isiyowajibika na yenye uchochezi”.
Katika taarifa yao ya mwisho, iliyotolewa baada ya mkutano uliofanyika Bahrain, Marekani na GCC zilipongeza uelewano wa hivi karibuni kati ya Iran na Marekani, huku zikikataa sera yoyote ya kutoza ada au kujaribu kudhibiti usafiri kupitia Mlango wa Hormuz.
Kiongozi wa Hezbollah ameitaka Israel kuondoka kikamilifu Lebanon bila masharti yoyote
Chanzo cha picha, Houssam Shbaro/Anadolu via Getty Images
Maelezo ya picha, Hotuba ya televisheni ya kiongozi wa Hezbollah Naim Qassem nchini Lebanon.
Kiongozi wa kundi la Hezbollah, Naim Qassem, amesema Israel haina njia nyingine isipokuwa kuondoka kikamilifu katika kila sehemu ya ardhi ya Lebanon, akisisitiza kuwa hakuna masharti yanayopaswa kuambatanishwa na hatua hiyo.
Katika hotuba yake ya televisheni wakati wa maadhimisho ya Ashura, Qassem alisema Lebanon haitakubali uhusiano wa kawaida na Israel wala hatua zozote ambazo zinaweza kuhalalisha uwepo wake katika ardhi ya Lebanon.
“Israel haina chaguo jingine isipokuwa kuondoka kabisa kutoka kwa kila ardhi ya Lebanon,” alisema.
Aliongeza kuwa kundi lake halitakubali “kurekebishwa kwa uhusiano, kusitishwa kwa uhasama, faida yoyote kwa Israel, wala uwepo wa sehemu yoyote ya Israel katika ardhi ya Lebanon.”
Kauli hiyo inakuja wakati maafisa wa Lebanon na Israel wakiendelea na mazungumzo ya moja kwa moja Washington, hatua ambayo imezua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa mahusiano ya mataifa hayo mawili.
Lebanon na Israel bado zipo katika mvutano wa muda mrefu, huku Hezbollah ikiwa na uhusiano wa karibu na Iran ambayo imekuwa ikisema inazingatia maslahi ya kundi hilo katika mazungumzo yake na Marekani.
Hasira Kenya baada ya video kuonesha polisi wakimkamata kwa nguvu mwanamume mwenye ulemavu
Chanzo cha picha, Asulaba/socials
Maelezo ya picha, Mwanamume aliye na ulemavu akibebwa na kupelekwa kwa gari la polisi Nakuru, Kenya
Wakenya wameeleza kutoridhishwa na kukasirishwa baada ya video kusambaa ikionyesha maafisa wa polisi wakimkamata kwa nguvu mwanamume mwenye ulemavu wakati wa maandamano ya kupinga serikali mjini Nakuru, yaliyofanyika jana Alhamisi.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya imekosolewa vikali baada ya tukio hilo linalomhusisha James Thuku, ambaye hutumia magongo kutembea, kuonekana akivutwa na kuangushwa chini kabla ya kuingizwa kwenye gari la polisi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Seneta Crystal Asige, Thuku alikamatwa na anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Nakuru kwa tuhuma za kuchochea vurugu.
“Nimeweza kuthibitisha kwamba alikamatwa na anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Nakuru. Jina lake ni James Thuku. Mashtaka: kuchochea vurugu,” Seneta Crystal Asige aliandika kwenye mtandao wa X.
Seneta huyo ameitaka mamlaka ya polisi kutoa maelezo kuhusu mazingira ya kukamatwa kwake.
Video hiyo iliyosambaa mitandaoni inaonyesha Thuku akijaribu kuvuka barabara akiwa ameandamana na mtu mwingine wakati wa maandamano. Gari la polisi aina ya Land Cruiser kisha linafika eneo hilo likiwa na maafisa zaidi ya kumi waliokuwa na silaha na vifaa vya kudhibiti vurugu.
Baada ya maafisa hao kushuka, mtu aliyekuwa akimsaidia Thuku anakimbia, na kumwacha akiwa peke yake. Thuku anaanguka chini wakati akijaribu kukwepa kukamatwa kabla ya kuburutwa na maafisa hao na kisha kuwekwa ndani ya gari la polisi.
Tukio hilo limeibua ukosoaji mkali kutoka kwa wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii, wengi wakilaani matumizi ya nguvu dhidi ya mtu mwenye ulemavu.
Wadau wa haki za binadamu wametoa wito wa uchunguzi huru kubaini iwapo taratibu za polisi zilizingatiwa na kama nguvu iliyotumika ilikuwa ya lazima katika tukio hilo.
Chanzo cha picha, Asulaba/Socials
Maelezo ya picha, Mwanamume akimsaidia mtu anayeishi na ulemavu kuvuka barabara kabla ya kukamatwa na maafisa wa polisi wakati wa maandamano ya Alhamisi
India yataka masharti bora ya ushuru kabla ya mkataba wa biashara na Marekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa BBC Monitoring, Waziri wa Biashara wa India, Piyush Goyal, amesema New Delhi haitasaini mkataba wa biashara wa pande mbili na Washington hadi kuwe na mfumo utakaohakikisha bidhaa za India zinapata ushindani wa juu zaidi katika ushuru wa forodha.
Akizungumza katika hafla moja jijini London, Goyal alisema, "Lengo kuu la mkataba wa biashara huria ni kukupa faida dhidi ya washindani wako."
Akirejelea makubaliano ya muda ya biashara yaliyotangazwa kati ya India na Marekani mwezi Februari, alisema: "Bila shaka tunahitaji sababu thabiti ya kutekeleza makubaliano ambayo tayari yamefikiwa."
Goyal alisema chini ya makubaliano hayo yanayopendekezwa, Marekani italazimika kuipa India masharti ya kibiashara yaliyo bora zaidi kuliko yale yanayotolewa kwa nchi kama Vietnam, Thailand, Philippines, Indonesia, Malaysia, China, Bangladesh na Sri Lanka.
Kauli zake zinakuja wakati India na Marekani zikifanya tathmini ya maendeleo ya makubaliano ya muda ya biashara yanayojumuisha masuala ya upatikanaji wa masoko, biashara ya kidijitali na minyororo ya ugavi.
Nchi hizo mbili zinafanya jitihada za kukamilisha makubaliano hayo kabla ya Julai 24, tarehe ambayo ushuru wa muda wa asilimia 10 uliowekwa na Washington unatarajiwa kuondolewa.
Makubaliano ya mpito kati ya Marekani na Iran yataruhusu ukaguzi wa vituo vya nyuklia vya Iran - IAEA
Chanzo cha picha, Getty Images
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, amesema mfumo "madhubuti" wa uhakiki unahitajika ili kuhakikisha Iran haiwezi kumiliki silaha za nyuklia baada ya vita vya Mashariki ya Kati.
Akizungumza na wanahabari nchini Japan, Grossi amesema anaamini lengo la makubaliano kati ya Marekani na Iran ni kuhakikisha Tehran haielekei katika kutengeneza silaha za nyuklia.
"Serikali ya Iran tayari imeweka wazi kuwa haina nia hiyo," alisema.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kauli pekee haitoshi.
"Tunahitaji kuanzisha mfumo imara sana wa uhakiki haraka iwezekanavyo," alisema.
Grossi pia amesema makubaliano ya mpito ya amani kati ya Marekani na Iran yataruhusu wakaguzi wa IAEA kurejea katika vituo vya nyuklia vya Iran.
Kauli hiyo imekuja baada ya Tehran kutangaza kwamba baadhi ya vituo muhimu vya nyuklia vitaendelea kufungwa na wakaguzi hawataruhusiwa hadi pale makubaliano ya mwisho na Marekani yatakapofikiwa na vikwazo vya kiuchumi kuondolewa.
"Kuna makubaliano, na ili yatekelezwe, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki utahitaji kupata fursa ya kufanya ukaguzi na kufikia vituo husika. Tunatumaini tutaweza kufanya hivyo hivi karibuni," Grossi alisema katika mkutano na waandishi wa habari nchini Japan.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka Iran. Hata hivyo, Tehran tayari imesema kurejea kwa wakaguzi wa nyuklia wa IAEA kutakuwa sehemu ya mazungumzo yanayoendelea kati yake na Marekani na pia sehemu ya makubaliano ya mwisho yanayoweza kufikiwa.
Kwa mujibu wa makubaliano ya awali yaliyofikiwa kati ya Iran na Marekani ili kumaliza vita, inatarajiwa kuwa nchi hizo mbili zitafikia makubaliano ya mwisho baada ya miezi miwili ya mazungumzo.
Unyanyasaji wa kingono wageuka sehemu ya maisha ya kila siku katika baadhi ya maeneo ya Sudan
Chanzo cha picha, Getty Images
Tahadhari: Makala haya yana maelezo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuyapata kuwa ya kusikitisha au ya kushtua.
Ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia bado vimeshamiri nchini Sudan, hata katika maeneo ambayo hayajaathiriwa moja kwa moja na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo, kulingana na ripoti mpya ya shirika la kimatibabu la Médecins Sans Frontières (MSF).
Ingawa ubakaji umeelezwa kuwa "alama rasmi" ya mzozo huo, ripoti hiyo inasema vitendo vingi vya unyanyasaji wa kijinsia vinafanywa na wanaume wenye silaha, mara nyingi vikisindikizwa na ukatili, udhalilishaji na vitendo vya kuwavunjia heshima waathiriwa.
Hata hivyo, MSF imesema ubakaji umeendelea kuwa sehemu "iliyofichika" ya maisha ya kila siku kwa jamii nyingi katika eneo la Darfur Magharibi, hata katika maeneo ambayo kwa sasa hayako mstari wa mbele wa mapigano.
Ripoti hii ndiyo pana zaidi kuwahi kutolewa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia katika vita vya Sudan ambavyo sasa vinakaribia kutimiza miaka mitatu.
Ripoti hiyo inategemea ushuhuda wa waathiriwa 3,396 waliotafuta matibabu katika vituo vinavyoungwa mkono na MSF katika maeneo ya Darfur Kaskazini na Darfur Kusini kati ya Januari 2024 na Novemba 2025.
Pande zote mbili zinazohusika katika mzozo huo, yaani jeshi la Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), zimekabiliwa na tuhuma za kufanya unyanyasaji wa kijinsia.
Hata hivyo, Darfur inachukuliwa kuwa ngome kuu ya RSF, na waathiriwa wengi waliobainisha waliowadhulumu walisema wahusika walikuwa wapiganaji wa kundi hilo.
Mashambulizi hayo mara nyingi yalihusisha wabakaji zaidi ya mmoja na yaliambatana na aina nyingine za ukatili mkubwa na vitisho, ikiwemo kupigwa na kushuhudia ndugu zao wakitishiwa kuuawa au kuuawa.
"Mara walitupeleka katika eneo la wazi," anasimulia mwanamke mmoja aliyenukuliwa katika ripoti hiyo. "Mwanaume wa kwanza alinibaka mara mbili, wa pili mara moja, wa tatu mara nne na wa nne mara moja."
Anaongeza: "Mbali na ubakaji, walitupiga kwa fimbo na kutuelekezea bunduki vichwani. Msichana mwingine mwenye umri wa miaka 15 pia alibakwa na wanaume watatu. Tulibakwa usiku kucha."
Jiji la Paris ladhibiti unywaji pombe kukabiliana na wimbi la joto Ulaya
Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka ya Ufaransa imepiga marufuku ya unywaji pombe hadharani na mauzo yake mjini Paris, katika jitihada za kupunguza shinikizo kwa hospitali za mji mkuu kipindi hiki cha joto kali.
Wakaazi wa Parisi wamezuiawa kunywa pombe hadharani kuanzia saa sita mchana Ijumaa hadi saa moja siku ya Jumamosi.
Agizo hilo litazingatiwa kuanzia Jumamosi hadi Jumapili.
Hali ya joto kali ambayo imesababisha Uhispania, Uingereza na Ufaransa kudorora kwa siku kadhaa inatarajiwa kuelekea upande wa mashariki, huku watabiri wa hali ya hewa nchini Ujerumani na Jamhuri ya Czech wakionya juu ya hali mbaya zaidi.
Halijoto nchini Ujerumani inaweza kufikia nyuzi joto 40 kote nchini siku ya leo Ijumaa.
Tahadhari ya hali mbaya ya hewa umetolewa katika sehemu kadhaa za Jamhuri ya Czech.
EU yawawekea raia wa Somalia vikwazo vya muda vya usafiri
Chanzo cha picha, Social
Umoja wa Ulaya (EU), umeweka vikwazo vya muda vinavyowazuia raia wa Somalia kupata viza ya Schengen, baada ya nchi hiyo kushindwa kutoa ushirikiano wa kuwarejesha nyumbani raia wake wanaoishi katika nchi wanachama wa umoja huo kinyume cha sheria.
Chini ya hatua hizo mpya, raia wa Somalia hawatastahiki tena viza ya Schengen, ambayo inawawezesha wamiliki kuzuru eneo la Schengen hadi muda wa viza utakapokamilika.
EU pia imeongeza muda wa kushughulikia maombi ya viza kwa raia wa Somalia kutoka siku 15 hadi siku 45.
Hatua hiyo mpya itawaathiri raia wa Somalia wanaotaka kuenda Ulaya kwa shughuli za kikazi, masomo, ziara za familia au utalii.
Umoja wa Ulaya pia umesitisha taratibu zilizorahisishwa za kuunga mkono hati zinazohitajika kwa ajili ya maombi ya viza, na imerejesha ada za viza kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na huduma nchini Somalia.
Marekani yadai meli mafuta ya Singapore ilishambuliwa na Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa Marekani ambao majina yao hayakutangazwa hadharani wameviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba shambulio la Alhamisi dhidi meli ya mafuta karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz lilitekelezwa na Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran IRGC.
Iran haijatoa tamko lolote kuhusiana na madai haya, lakini jeshi la majini la IRGC lilionya Jumatano usiku kwamba meli yoyote itakayopitia Mlango-Bahari wa Hormuz lazima ishirikiane na vikosi vya Irani.
Siku ya Alhamisi Mamlaka mpya ya Usimamizi ya Mlango Bahari wa Hormuz ilionya kwamba "haiwezi kuzihakikishia uslama meli zinazotumia njia ambazo hazijaidhinishwa".
Mashirika ya habari ya Iran yaliandika siku ya Alhamisi usiku: "Kujibu maswali yanayoulizwa mara kwa mara, Mamlaka ya Njia ya Majini katika Ghuba ya Uajemi (PGSA) imetangaza kwamba meli zozote zinazopita nje ya mfumo uliowekwa na mamlaka hii haitapewa dhamana ya usalama na hazitapewa bima na majukumu yanayohusiana nayo.
Tangazo la shirika hilo pia lilisisitiza kuwa: "Hasara itakayotokana na usafiri kupitia njia zisizo rasmi itasimamiwa na mmiliki, mwendeshaji, na nahodha wa chombo."
Onyo la IRGC Jumatano usiku lilikuja baada ya Oman kutangaza, wakati wa ziara ya wziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio katika nchi kadhaa za Ghuba, kwamba ilikuwa imeunda njia mpya ya baharini ili kurahisisha meli kupita kwenye Mlango -Bahari wa Hormuz.
Taarifa hizo ziliungwa mkono na Bahrain, lakini huenda Jeshi la majini la IRGC "lilikerwa" na hatua kwa kuundwa kwa njia hiyo.
Hata hivyo Iran bado haijakubali rasmi au kukana kuhusika na shambulio dhidi ya meli hiyo ya Singapore.
Mfalme Charles afichua kodi aliyolipa mwaka 2024-25
Chanzo cha picha, Getty Images
Mfalme Charles amekuwa mfalme wa kwanza wa Uingereza kuweka adharani malipo ya kodi yake.
Mfalme Charles alilipa dola milioni 17 kutokana na mapato yake binafsi katika mwaka wa kodi ulioishia Machi, 2025.
Mfalme Charles amelipa takriban dola milioni arobaini kama kodi tangu alipokuwa Mfalme mnamo mwaka wa 2022.
Mwanafalme William, pia ameweka wazi maelezo yake ya kodi, William alilipa dola milioni 10 katika mwaka uliopita wa kodi.
Kando na hayo, imebainika kuwa Mfalme Charles na Malkia Camilla hawaishi tena katika Ikulu ya Buckingham Palace licha ya jengo hilo kufanyiwa ukarabati ambao tayari umegharimu dola za Marekani milioni 430 itakapokamilika mwaka ujao.
Badala yake, watasaliai katika jumba jirani la Clarence.
Wataendelea kutumia Kasri la Buckingham shughuli za kiserikali.
Kombe la Dunia 2026: Ivory Coast yafuzu raundi ya pili baada ya kuilaza Curacao
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Nicolas Pepe
Ivory Coast imefuzu kwa hatua ya muondoano kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia baada ya Nicolas Pepe kufunga mabao mawili na kuwaondoa Curacao.
Wenyeji Ivory Coast walihitaji alama moja tu ili kufika hatua ya 32, baada ya kutoka katika hatua ya makundi katika mechi zao tatu zilizopita za Kombe la Dunia.
Na walionyesha ujasiri wao kwa bao baada ya dakika saba tu mabeki wa Curacao walishikwa wavuni na kuondolewa na Yan Diomande, ambaye alimuandalia mpira safi Pepe.
Katika dakika ya 65, mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Pepe - ambaye aliachwa nje ya kikosi cha Ivory Coast kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu - alipata la pili alipopachika wavuni kwa mguu wa kushoto na kumpita kipa wa Curacao, Eloy Room.
Hii inamaanisha kuwa Ivory Coast inamaliza nafasi ya pili katika Kundi E ikiwa na alama sita, ikishinda mechi mbili za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Tetemeko la ardhi Venezuela: Waokoaji mbioni kuwatafuta manusura, idadi ya waliofariki ikifikia 235
Chanzo cha picha, Getty Images
Waokoaji wanapekua vifusi watafuta walionusurika matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyokumba maeneo ya karibu na mji mkuu wa Venezuela na kusababisha vifo vya takribani watu 235 na kuwajeruhi zaidi ya 1,500.
Katika Caracas na mji wa karibu wa pwani wa La
Guaira, watu walisikika wakiomba msaada kutoka chini ya vifusi vya majengo
yaliyoporomoka.
Tetemeko la kwanza la ukubwa wa 7.2 lilifuatiwa
sekunde chache baadaye na lingine lenye nguvu zaidi ya 7.5, kulingana na
Utafiti wa Jiolojia wa Marekani (USGS), na kusababisha uharibifu mkubwa zaidi.
Watu wengi zaidi wanahofiwa kufariki, huku wengine
wakiwa wameachwa bila makao au kulala barabarani kwa kuogopa kurejea kwenye
majengo yaliyoharibiwa baada ya mkasa huo.
Matetemeko ya ardhi yalitokea saa kumi na mbili na
dakika ne kwa saa za ndani(22:04 GMT) siku ya Jumatano - sikukuu ya kitaifa
nchini Venezuela, kumaanisha kuwa watu walikuwa nyumbani ikilinganishwa na siku
ya kawaida ya juma.
Siku ya Alhamisi Rais wa Bunge la Venezuela Jorge
Rodríguez, aliripoti kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka, baada ya Rais wa
mpito wa nchi hiyo Delcy Rodríguez kutangaza hali ya dharura.
Nchi kadhaa zimeahidi kusaidia juhudi za uokoaji,
huku Marekani ikiahidi msaada wa dola milioni 150. Jeshi la Marekani linatuma
meli za usafiri na ndege kusaidia shughuli ya uokoaji na "operesheni za msaada
wadharura", ilisema katika taarifa.
Jorge Rodríguez alisema majengo 250 yameharibiwa au
kupotea, hasa La Guaira, ambapo BBC ilithibitisha picha za hoteli ya ghorofa 10
iliyoharibiwa na kuwa vifusi. Siku ya Alhamisi, watu walikuwa wakitafuta
wapendwa huko.
Juan Ortiz ameiambia BBC kwamba mmoja wa marafiki
zake wa karibu amethibitishwa kufariki, mwingine anaaminika kuwa chini ya
vifusi, na takribani watu 20 anaowafahamu wanaoishi katika eneo la pwani hawajulikani
waliko.
"Ninakabiliwa na mshtuko na kuchanganyikiwa, nasikitika
kwamba siwezi kusaidia," mwanafunzi wa matibabu mjini Caracas alisema.
UN yasitisha mpango wa uokoaji wa Mlango wa Bahari wa Hormuz baada ya meli ya mizigo kushambuliwa
Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Umoja
wa Mataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) limesitisha mpango wa kuwahamisha zaidi
ya mabaharia 11,000 waliokuwa wamekwama kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz baada ya
meli ya mizigo iliyokuwa ikipita kwenye njia hiyo ya majini kushambuliwa.
Mkuu wa IMO
Arsenio Dominguez alisema boti kadhaa tayari zimeondolewa, lakini shirika hilo
lilitaka kuhakikisha kuwa "usalama" utaendelea
kudumishwa.
Shirika la
usalama wa baharini la Uingereza UKMTO liliripoti siku ya Alhamisi kuna meli ambayo imeshambuliwa kwa "kifaa kisichojulikana" maili 7.5 kusini-mashariki mwa bandari ya Dahit ya Oman. Hakuna majeruhi walioripotiwa.
Kampuni ya
usimamizi wa hatari za baharini ya Vanguard ilisema meli hiyo, yenye bendera ya
Singapore, Ever Lovely, iliendelea na safari licha ya shambulio hilo.
Maafisa wa
Marekani walisema Iran ilishambulia meli hiyo, kwa mujibu wa ripoti
za vyombo vya habari vya Marekani. Chombo kilichoundwa na Iran kusimamia mkondo
wa bahari kilisema meli zinazopita nje ya njia zilizotengwa hazitahakikishiwa usalama.
Katika chapisho
kwenye X, Mamlaka ya Mlango-Bahari ya Ghuba ya Uajemi (PGSA) ilisema:
"Madhara yoyote yanayotokana na utumiaji wa njia zisizoidhinishwa itakuwa
jukumu la mmiliki, mwendeshaji na bwana wa meli".
Mamia ya meli na
maelfu ya mabaharia wamekwama katika Ghuba tangu Februari kwa sababu ya vita vya
Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Juhudi za
kuwahamisha Umoja wa Mataifa zilitangazwa Jumanne baada ya kufunguliwa tena
kwa mlango wa bahari huo, huku Dominguez akisema "operesheni hiyo
kubwa" ilikuwa na ushirikiano wa Iran, Oman, Marekani, mataifa mengine ya
pwani katika eneo hilo na sekta ya bahari.