Urusi yafanya 'kura ya maoni' katika maeneo iliyoyateka Ukraine

Askari

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Urusi iliruhusu vyombo vya habari katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, kikiwemo hiki cha Luhansk, ambapo mwanajeshi alipiga kura yake
Iliyochapishwa

Raia wa Ukraine wameripoti kuwa wanajeshi waliojihami wakienda nyumba kwa nyumba katika maeneo ya nchi hiyo yaliyotekwa kukusanya kile walioita "kura za maoni" za kujiunga na Urusi.

"Lazima ujibu kwa maneno ili askari aweke alama kwenye karatasi na kuhifadhi," mwanamke mmoja huko Enerhodar aliambia BBC.

Kusini mwa Kherson, walinzi wa Urusi walisimama na sanduku la kura katikati ya jiji kukusanya kura za watu.

Upigaji kura wa nyumba kwa nyumba ni wa "usalama", vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vinasema.

"Upigaji kura wa ana kwa ana utafanyika tarehe 27 Septemba pekee," Tass iliripoti.

"Siku nyingine, upigaji kura utafanywa kijumuiya na kwa njia ya nyumba kwa nyumba."

Mwanamke mmoja huko Melitopol aliambia BBC kwamba "washiriki" wawili wa ndani walifika na askari wawili wa Kirusi kwenye nyumba ya wazazi wake, ili kuwapa kura ya kutia saini.

"Baba yangu aliweka alama ya 'hapana' [kupinga kujiunga na Urusi]," mwanamke huyo alisema.

"Mama yangu alisimama karibu, na kuuliza nini kitatokea kwa kuweka alma ya 'kupinga'. Wakasema, 'Hakuna'. "Mama sasa ana wasiwasi kwamba Warusi watawatesa."

Uwepo wa watu wenye silaha wanaoendesha kura hiyo unakinzana na msisitizo wa Moscow kwamba huu ni mchakato huru au wa haki.

Maelezo ya video, Mtoto asikika akilia 'kwaheri baba' huku babake raia wa Urusi akienda vitani Ukraine
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wataalamu wanasema kura hizo za maoni zinazofanyika kwa muda wa siku tano, zitairuhusu Urusi kudai - kinyume cha sheria - maeneo manne yanayokaliwa kwa mabavu au inayokaliwa kwa kiasi fulani ya Ukraine kuwa yao.

"Kunyakuliwa" huko kusingetambuliwa kimataifa, lakini kunaweza kuifanya Urusi kudai kwamba eneo lake linashambuliwa na silaha za Magharibi zinazotolewa kwa Ukraine, hali ambayo inaweza kuzidisha vita.

Rais wa Marekani Joe Biden alizitaja kura hizo za maoni kama "uzushi", akisema ni "kisingizio cha uwongo" kujaribu kuteka sehemu za Ukraine kwa nguvu kinyume na sheria za kimataifa.

"Marekani kamwe haitatambua eneo la Ukraine kama kitu kingine chochote isipokuwa sehemu ya Ukraine," alisema.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, James Cleverly, alisema Uingereza ina ushahidi kwamba maafisa wa Urusi tayari wameweka na"kubuni idadi ya wapiga kura na viwango vya kuidhinishwa kwa kura hizi za uwongo".

Bw Cleverly alisema Urusi inapanga kurasimisha unyakuzi wake wa mikoa minne - Luhansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhzhia - mwishoni mwa mwezi.

Masanduku ya kura yakilindwa na askari wenye silaha huko Luhansk

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Masanduku ya kura yakilindwa na askari wenye silaha huko Luhansk

Chanzo kimoja huko Kherson kiliiambia BBC kuwa hakuna juhudi za umma kuhimiza upigaji kura, mbali na tangazo kwenye shirika la habari la Urusi kwamba watu wanaweza kupiga kura katika jengo la bandari, ambalo lilikuwa halitumiki kwa miaka 10.

Mwanamke mwingine huko Kherson alisema aliona "wanamgambo wenye silaha" nje ya jengo ambalo kura zilionekana kupigwa.

Alijifanya kusahau pasi yake ya kusafiria, kwa hivyo hakulazimika kupiga kura.

Mwanamke huyo alisema marafiki na familia yake wote walikuwa wakipinga kura hiyo ya maoni.

"Hatujui maisha yetu yatakuwaje baada ya kura hii ya maoni," alisema. "Ni vigumu sana kuelewa wanachotaka kufanya."

Kyiv inasema kura za maoni hazitabadilisha chochote, na vikosi vyake vitaendelea kushinikiza kukomboa maeneo yote.