Ugonjwa uliwaokoa maelfu ya Wayahudi dhidi ya ugaidi wa Hitler

Iliyochapishwa

Tukio hili linaweza kuonekana kama filamu ya Hollywood, lakini ni tukio la kweli la wakati wa vita vya pili vya dunia. Mwishoni mwa 1943 huko Roma - wakati huo, vikosi vya jeshi la Ujerumani la Nazi, kwa msaada wa askari, wafanyabiashara na wanasiasa, waliteka mji mkuu wa Italia baada ya kumpindua mshirika wao - mfashisti Benito Mussolini.

Baada ya kuuteka wa mji wa 'Eternal City, askari wa Adolf Hitler walianza kutafuta Wayahudi wa jiji hilo. Wayahudi walikuwa wameepuka mateso ya kikatili na kuangamizwa katika sehemu nyingine za Ulaya kabla ya askari wa Hitler kuanza msako.

Habari juu ya kambi za mateso zenye kutisha zilianza kuzunguzwa, na Wayahudi wengi walitafuta kimbilio katika makanisa, nyumba za watawa za Kikristo, na hata hospitali zinazosimamiwa na Kanisa Katoliki ili kuepuka kupelekwa kwenye kambi za mateso.

Katika moja ya vituo hivi vya afya, madaktari watatu waliwakaribisha makumi ya watu na kuwagundua kuwa wana ugonjwa mbaya. Hakuna mtu aliyejua chochote kuhusu ugonjwa huo kabla, kwa sababu ugonjwa huo haukuwepo.

Dawa ya msingi na hatari

Alfajiri ya Oktoba 16, 1943 katika mji mkuu wa Italia. Wanajeshi wa Ujerumani walivamia eneo la Wayahudi kilomita tatu tu kutoka Vatikani. Walikamata zaidi ya watu 1,000 wakiwemo wanaume, wanawake na watoto. Baadhi ya waliobahatika kutoroka na kufika katika hospitali ya San Juan Cabilita.

Kituo hicho kiko kwenye kisiwa kidogo katikati ya Mto Tiber na kinatazamana na Sinagogi Kuu katika mji mkuu wa Italia.

Wanazi waliendelea na msako wao na kufika hospitali. Giovanni Borromeo, wakati huo alikuwa mkurugenzi wa hospitali hiyo na Mkatoliki, aliwakaribisha maofisa hao waliovalia sare na kuwaruhusu kufanya uchunguzi.

Hata hivyo, wanapofika kwenye chumba, Borromeo anawaonya kuwa katika chumba hicho wagonjwa wenye dalili za ugonjwa wa ajabu na hatari wanatengwa na wanachunguzwa. Borromeo aliwaambia ni ugonjwa unaoambukiza sana. Unaathiri mfumo wa neva wa binadamu na kusababisha kifo.

Dk. Vittorio Sacerdotti aliiambia BBC mwaka wa 2004, "tuliuita ugonjwa wa K. Wakifikiri ulikuwa ugonjwa fulani kama kansa au kifua kikuu, Wanazi walikimbia kama sungura.”

Pamoja na Sacerdotti na Borromeo wakati huo alikuwepo Adriano Ossini, daktari wa Kiitaliano na mpinga ufashisti na muundaji wa mbinu hii. Mbinu yake iliokoa maisha ya makumi ya Wayahudi. Daktari huyo wa Kiyahudi aliajiriwa na Borromeo kufanya kazi katika hospitali ya Kirumi licha ya kupigwa marufuku na sheria zilizotungwa katika miaka ya 1930 kwa idhini ya Mussolini.

Mwandishi na kasisi Mhispania Jesus Sánchez Adalid aliiambia BBC, "ugonjwa wa K ulipewa jina hilo ili kutoa hisia kuwa ni hatari kama vile kifua kikuu. Kifua kikuu kilikuwa tatizo kubwa kwa wanajeshi wengi wa Hitler huko Hungaria na Poland wakati huo."

Riwaya ya Jesus Sanchez Adalid 'A Light in the Night of Rome' ilichapishwa mapema mwezi huu. Ni hadithi ya mapenzi kati ya msichana tajiri na kijana wa Kiyahudi na hadithi hiyo ya mapenzi inajitokeza wakati wa matukio haya ya kihistoria.

Hali ilivyokuwa

Borromeo, Sacerdotti na Ossini walicheza mchezo mzuri. Walianza kuweka rekodi za matibabu za Wayahudi ambao walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo unaodaiwa. Walihitaji watu wengi wa nje na wa ndani. Timu yao kisha ikawa kubwa. Ilijumuisha pia mkuu wa San Juan de Dios ambaye alisimamia hospitali hiyo.

Ingawa Wanazi walikaa mbali kwa sababu ya ugonjwa huu unaodaiwa kuwa mbaya, madaktari waliendelea kuwa macho na kuwaelekeza Wayahudi juu ya nini cha kufanya ikiwa Wanazi wangerudi.

Gabrielle Sonnino alikuwa na umri wa miaka minne wakati kisa hicho kilipotokea na 'kulazwa' katika hospitali ya Kikatoliki. "Madaktari walituambia ikiwa Wajerumani watarudi, ilibidi tuongeze nguvu zetu zote na kukohoa na kujifanya tu wagonjwa sana," Gabriel alieleza katika runinga ya umma ya Ujerumani 2019.

Sánchez Adalid anasema “Wajerumani walituma madaktari kuthibitisha ugonjwa huo, lakini waliridhika na maelezo ya madaktari wa Italia. Huenda madaktari hao walihisi hakukuwa na haja ya kuhatarisha kuambukizwa au kupoteza wakati katika hospitali iliyojaa wagonjwa."

Aliongeza "kama madaktari wa Ujerumani wangewachunguza wagonjwa wanaodaiwa, wangegundua uongo huo, lakini hawakugundua."

Mnamo Mei, 1944, askari wa Nazi walikuja hospitalini na kuikagua, lakini walipokuwa wakipita vyumba ambavyo Wayahudi walikuwa wametengwa, walisikia kikohozi kikubwa cha wagonjwa.

Mwezi mmoja baadaye, vikosi vya Washirika viliikomboa Roma na wagonjwa waliosalia waliachiliwa.

Wanahistoria na mamlaka mbalimbali wamethibitisha matukio yaliyotokea katika hospitali ya Kirumi. Borromeo alitunukiwa tuzo maalum mwaka 2004 na kituo cha kumbukumbu cha 'Holocaust' cha Israeli 'Yad Vashem'. Tuzo hii maalum hutolewa kwa wale tu waliookoa au kusaidia watu wa Kiyahudi wakati wa Vita vya pili vya dunia.

Wala haiko wazi ni maisha ngapi ambayo ugonjwa huo umeokoa. "Hatujui idadi kamili ya watu waliohifadhiwa katika hospitali, kwa sababu hospitali ilikuwa daraja la kutoroka," alisema Sánchez Adali

Sánchez alitumia miaka miwili kutafiti kumbukumbu za kituo hicho pamoja na Wakfu wa Shoah na Yad Vashem ili kuandika riwaya hiyo.

Sánchez Adalid anasema baadhi ya wagonjwa hao wanaodaiwa kuugua K walihamia Amerika Kusini baada ya kumalizika kwa vita. Hospitali hii ilikuwa moja ya mahali ambapo Kanisa Katoliki liliokoa Wayahudi.

Aliongeza, “nimeambiwa maofisa wa polisi wa Wanazi, walishangaa kupata watawa 70 katika baadhi ya nyumba za watawa walipofika Roma. Wengi wao hawakuwa watawa, bali Wayahudi waliojificha. Watawa hao walitoa sababu za ajabu za kuwapotosha Wanazi. Walisema Roma ni mji mkuu wa Ukatoliki, ni dhahiri kuna watawa wengi."

Hospitali haikuwa tu mahali pa ulinzi kwa Wayahudi.

"Hofu ya Wanazi ilifanya hospitali hiyo kuwa kituo cha kijasusi, mahali pa mawasiliano na pia mahali pa kukutana upinzani," anasema Sánchez Adalid.

Redio Victoria pia ilirusha matangazo kutoka hospitali hii. Redio Victoria, iliendeshwa na Wamarekani wenye asili ya Kiitaliano.

Sánchez Adalid anakiri kwamba “ubora wa kibinadamu hujitokeza na kumea katika nyakati mbaya zaidi za historia ya binadamu.” Jambo ambalo utafiti wake umethibitisha.