Wahalifu na wakwepa vikwazo wanavyoitumia mianya ya kisheria Uingereza

SS
    • Author, James Oliver, Will Dahlgreen, James Melley & Andy Verity
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa

Kampuni ya Alpha Consulting yenye makao yake Seychelles ilisaidia kuunda zaidi ya ubia 900 chini Uingereza. Vilevile iliunda kampuni zaidi ya 200 na kuficha wamiliki wake wa kweli.

Uchunguzi wa BBC, ikishirikiana na shirika la Finance Uncovered na Shirika la Utangazaji la Ushelisheli umechambua hati za kampuni ya Alpha na maelfu ya rekodi za kampuni hiyo.

Na kuwatambua baadhi ya watu ambao walinufaika kisiri na kazi ya kampuni hiyo, yenye makao yake makuu katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi.

Yevgeny Prigozhin

S

Chanzo cha picha, US TREASURY

Maelezo ya picha, Ndege binafsi na boti la kifakhari vinavyomilikiwa na hayati Yevgeny Prigozhin

Yevgeny Prigozhin, bosi wa Kundi la Wagner aliyefariki katikati ya mwaka huu, alikuwa mmoja wa wale waliofaidika na huduma za Alpha.

Kampuni yake ya Beratex Group Ltd iliwekewa vikwazo na Marekani mwaka 2019, baada ya kuficha umiliki wa ndege yake ya kibinafsi na boti la starehe.

Hati zilizovuja - zilizopatikana na Muungano wa Kimataifa wa Wanahabari wa Uchunguzi na kuchunguzwa katika sakata la Pandora Papers 2021 - zinaonyesha Alpha ilisaidia kuanzishwa Beratex huko Ushelisheli, na mmiliki akitajwa kuwa mama mkwe wa bosi huyo.

Mtu wa Karibu na Putin

A

Chanzo cha picha, LUTHER DENIS

Maelezo ya picha, Raia wa Seychelles Luther Denis

Leonid Reiman, rafiki wa karibu na mshirika wa Rais Putin, alikuwa mteja wa Alpha. 2006 akiwa waziri wa mawasiliano wa Urusi, Reiman alipatikana na mahakama ya Uswizi kuwa mmiliki wa siri wa kampuni iliyopokea malipo ya ufisadi.

Mtaalamu wa kupambana na utakatishaji fedha Graham Barrow anasema huu ni ukiukaji wa sheria ikiwa unafanya biashara kwa kujua na mtu ambaye anahusishwa na pesa chafu.

Alpha inasema ilifanya ukaguzi wote unaohitajika kwa Reiman na haikupata habari kwamba ni mtu aliyehusika katika utapeli wa pesa. Inasema kampuni hiyo haifanyi kazi na wateja au watu ambao wamehusika katika makossa.’

Uchunguzi huo pia unaonyesha Alpha inayoendeshwa na mfanyabiashara Mrusi anayeitwa Victoria Valkovskaya, ilisaidia kuunda ubia huko Uingereza, Wales na Ireland Kaskazini tangu 2017.

Ni aina ya ubia mdogo ambao kwa kawaida huundwa na watu wawili au zaidi ili kumiliki na kuendesha biashara pamoja, inaweza pia kutumiwa kukwepa kanuni za uwazi.

Sheria isiyo na Meno

SX

Chanzo cha picha, CENGIZ TOKGOZ

Maelezo ya picha, Meli ya mafuta ya Delfi

Baada ya sheria kuanzishwa mwaka wa 2016 inayotaka kampuni za Uingereza kutangaza ni nani anazimiliki, kulikuwa na ongezeko kubwa la usajili kupitia ubia, ambao hauna ulazima wa kusajiliwa.

Sharti la kusajili ubia liliongezwa Scotland mwaka mmoja baadaye baada ya kufichuliwa kuwa zilikuwa zikitumika zaidi kwa utakatishaji wa pesa na uhalifu mwingine.

Lakini mwaka jana, BBC na Finance Uncovered zilifichua ongezeko la matumizi ya ubia nchini Uingereza na ushahidi unaonyesha baadhi ya wabia wanahusika na ulaghai, ugaidi na utakatishaji fedha .

Kevin Hollinrake, waziri mdogo wa biashara, alipuuzilia mbali wasiwasi kuhusu mwanya huo, akiiambia House of Commons "watu wa ubia hawawezi kumiliki mali kwa jina lao."

Mama wa Mwanasiasa wa Ukraine

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa Alpha ilisaidia kuunda kampuni ndogo ambazo zilitumiwa kupata mali na kuficha wamiliki wake - ikiwa ni pamoja na meli ya mafuta, Delfi, ambayo ilichafua pwani ya Ukraine baada ya kuharibika mwaka wa 2019.

Uchunguzi wa serikali ulipata hati zinazomtambulisha mmiliki wa meli hiyo ni kampuni ya ubia iliopo Cardiff, Uingereza kwa jina la Mister Drake PC.

Kama makampuni mengi ambayo Alpha ilisaidia kuanzisha, meli hiyo ilionekana kumilikiwa kwa sehemu moja na raia wa Ushelisheli ambaye kwenye karatasi amesajiliwa kama mjasiriamali.

Kufuatia ajali hiyo, mahakama ilimtoza faini Drake PC - lakini haijawahi kumtambua mmiliki halisi na faini hiyo haijawahi kulipwa.

Uchunguzi wetu ulipata hati za ndani za Alpha ambazo zimrikodi mmiliki wa Drake PC kama Alla Kovtunova, mama wa mwanasiasa wa zamani wa chama kilichopigwa marufuku nchini Ukraine kinachounga mkono Urusi.

Baroness Kramer, msemaji wa Hazina ya Liberal Democrat katika House of Lords, alisema ni jambo la kushangaza kuwa serikali haijatumia muswada wake wa uhalifu wa kiuchumi kufunga kila mwanya.

Meli ya Ostra

AS

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Septemba 2020, Luther Denis alitajwa kwenye makaratasi ya ushirika mwingine, Cilkon PC, ambayo inahusika na kuendesha meli ya mafuta iitwayo Ostra.

Chini ya jina tofauti, Ostra ilikiuka vikwazo dhidi ya Syria mwaka wa 2019. Ushirikiano wa Denis ulihusika katika kuendesha meli hiyo baada ya mmiliki wake aliyesajiliwa, kampuni ya Kirusi iitwayo Rustanker, kuwekewa vikwazo kwa kujaribu kukwepa marufuku ya Marekani ya biashara ya mafuta na Venezuela. .

Uchunguzi wetu ulifuatiliaji taarifa za Ostra katika kipindi cha baada Denis kuchukua nafasi. Tuligundua GPS ilikuwa imezimwa kwa muda wa wiki tatu mwezi Septemba mwaka jana, na kutoweka katika ufuo wa Venezuela.

Bockmann anasema meli "zinazima GPS ili kuficha mahali zinapakia na kupakua mizigo yao, "ili kudanganya na kukwepa mamlaka yoyote ya udhibiti ambayo inafuatilia meli hizi."

BBC iliwaandikia Cilkon na Rustanker lakini haikupata jibu. Pia tulimwandikia Denis lakini alikataa kutoa maoni yake.

Ufichuzi Mwingine

SAZ

Chanzo cha picha, VICTORIA VALKOVSKAYA

Maelezo ya picha, Kampuni ya Alpha inamilikiwa na mfanyabiashara raia wa Urusi, Victoria Valkovskaya

Ushirikiano mwingine Alpha Consulting ilisaidia kuanzisha ni pamoja na:

Green Line LP, kampuni ambayo iliuza dawa za moyo kinyume cha sheria kwa kutangaza tiba ambayo haijathibitishwa

NIC International Services LP, iliendesha paperwriter.com, tovuti inayowaandikia insha wanafunzi - huduma ambayo ni kinyume cha sheria nchini Uingereza.

Histol Corporate LP, kampuni inayotuhumiwa kuhusika katika "udanganyifu mkubwa" nchini Urusi. Maafisa wawili wa Urusi wanadaiwa kuagiza kemikali kwa ajili ya sekta ya ulinzi kwa bei ya juu.

BBC ilijaribu kuwasiliana na kampuni hizi lakini haikupokea jibu. Alpha ilisema haifahamu shughuli zozote za kampuni hizi.

Marekani

DDD

Chanzo cha picha, DEMOCRATIC PARTY OF ALBANIA

Maelezo ya picha, Lulzim Basha na d Donald Trump

Machi 2017, kampuni ya Biniatta Trade LP, ilimlipa mtu mwenye ushawishi nchini Marekani kwa niaba ya Lulzim Basha, kiongozi wa Chama cha Demokrasia cha Albania.

Mtu huyo aliwaunganisha na wanasiasa wa chama cha Republican, ambapo Basha aliweza kupata fursa ya kupiga picha na Rais wa wakati huo Donald Trump - iliyotumiwa baadaye katika kampeni za uchaguzi wa Albania.

Ripoti za mwaka jana zilidokeza kwamba majasusi wa Marekani wanaamini kuwa kampeni ya uchaguzi ya Basha, ambaye kauli mbiu yake ilikuwa Make Albania Great Again, iliungwa mkono kwa siri na Urusi kwa dola 500,000.

Umiliki wa Biniatta ulifichwa lakini nyaraka za Alpha zilizovuja ni pamoja na makubaliano ya mwaka wa 2015, wakati ushirikiano huo ulipoanzishwa, ambao ulimtaja mmiliki kuwa raia wa Kirusi anayeitwa Maxim Trofimets.

Kujibu Tuhuma

D
Maelezo ya picha, Alpha imetengeneza zaidi ya kampuni 200 zilizosajiliwa Uingereza

BBC ilijaribu kuwasiliana na Trofimets na Basha lakini hawakujibu. Bi Valkovskaya, mkurugenzi mkuu wa Alpha, alikanusha kampuni yake kuhusika katika shughuli zozote zisizo halali.

Alpha Consulting ilisema "kuhusika kwake katika kampuni ndogo nchini Uingereza ni katika kutoa ushauri na usaidizi wa kusajili na kuunda kampuni kwa mujibu wa kanuni za Uingereza".

"Haishiriki, au haihusiki kwa lolote katika usimamizi, uendeshaji au maamuzi ya wateja au makampuni inayoisaidia kuiunda," ilisema. Alpha pia ilisema inazingatia taratibu za kupambana na utakatishaji fedha.

Mwezi uliopita Visiwa vya Shelisheli viliwekwa kwenye orodha nyeusi ya Umoja wa Ulaya.