'Mke wangu na watoto wametekwa nyara na Hamas'

Yoni Asher anasema alimtambua mke wake Doron (C) na binti zake Aviv (kushoto) na Raz (kulia) wakiwa wamepakiwa kwenye lori na wanamgambo.

Chanzo cha picha, YONI ASHER

Maelezo ya picha, Yoni Asher anasema alimtambua mke wake Doron (katikati) na binti zake Aviv (kushoto) na Raz (kulia) wakiwa wamepakiwa kwenye lori na wanamgambo.
Iliyochapishwa

Familia zimesimulia kwa hofu kubwa kuhusu wapendwa wao ambao wanasadikiwa kutekwa nyara na Hamas, baada ya kundi hilo la wanamgambo kushambulia Israel.

Jeshi la Israel linakadiria makumi ya watu wakiwemo raia wa kigeni wametekwa na kupelekwa hadi Gaza. Hizi ni baadhi ya simulizi.

'Ninajaribu kuwa mtulivu'

Kitu cha kwanza kilichomfanya Yoni Asheri kushuku kuwa familia yake ilikuwa ndani ya Gaza ni kufuatilia simu ya mkononi ya mke wake.

Mkewe Doron na watoto wao wawili Raz, 5, na Aviv, 3, walikuwa wakiishi na jamaa zao karibu na mpaka na Gaza wakati wanamgambo hao waliposhambulia.

Yoni aliambia BBC: "Jumamosi, mwendo wa saa 10:30 asubuhi, ndio mara ya mwisho nilizungumza na mke wangu kwa simu. Aliniambia kuwa magaidi kutoka Hamas waliingia ndani ya nyumba hiyo.

"Walikuwa kwenye chumba kilicho salama, kisha simu ikakatwa. Baadaye, nilifanikiwa kumpata kwa simu yake na ilikuwa ndani ya Gaza".

Baadaye siku hiyo, hofu yake kubwa ilithibitishwa alipotambua familia yake ikionyeshwa kwa ufupi kwenye video ya watu wakipakiwa nyuma ya lori.

"Katika video hiyo nilimtambua mke wangu na binti zangu wawili, watoto wangu wawili wadogo," alisema.

"Sijui wanashikiliwa kwa masharti gani au hali gani lakini unajua, hali inazidi kuwa mbaya."

Kwa sasa, kama familia zingine, kile Yoni alicho nacho ni matumaini. "Ninajaribu kuwa mtulivu. Nataka kuamini kuwa kuna mawasiliano kati ya wanadiplomasia wanaofanya mazungumzo au kitu lakini hatujui chochote - hilo ndilo jambo gumu zaidi".

'Ni kama sinema ya kutisha'

tt

Chanzo cha picha, NOAM SAGI

Maelezo ya picha, Noam alikuwa akimtarajia mama yake mjini London wiki ijayo kwa siku yake ya kuzaliwa ya 75.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Noam Sagi alisema moyo wake ulishtuka wakati vyombo vya habari vya Palestina vilipoanza kutangaza kutoka mbele ya nyumba ya mama yake mwenye umri wa miaka 74, karibu mita 400 kutoka mpaka na Gaza.

Jumamosi mchana, Jeshi la Israel liliingia kwenye makazi ya bibi wa watoto sita Ada Sagi na kukuta madoa ya damu - lakini ajuza huyo hakuwepo, alielezea.

Akizungumza na BBC Radio 4, Bw Sagi - anayeishi London - alisema anahisi mama yake, ambaye anafundisha Kiarabu, alikuwa miongoni mwa waliotekwa nyara.

"Tunamzungumzia ajuza wa miaka 74, ambaye aliingia kwenye chumba salama na [sasa] hayupo", alisema.

"Hayupo kwenye orodha ya waliofariki, hayuko kwenye orodha ya waliojeruhiwa, na ni jumuiya ndogo... watu 350 na wote wanafahamiana, kwa hivyo wamepitia mchakato wa kutambua kila mtu."

Jamii inaripoti kwamba wazee na vijana wametekwa nyara, kulingana na Bw Sagi, ambaye alisema hakuna uthibitisho rasmi wa mahali mamake aliko. Alidokeza kwamba hangeweza kukimbia mbali kufuatia baada ya kufanyiwa upasuaji wa kimatibabu hivi majuzi.

"Inaonekana kama sinema ya kutisha, ni ngumu kuelezea", Bwana Sagi aliendelea.

"Hebu fikiria kijiji cha kupendeza, cha mashambani hapa Uingereza na watu wanaendelea na maisha yao ya kawaida ... kisha ghafla unatekwa kutoka kwa nyumba yako.

"Unahisi kama ndoto na sio ya kweli ... hujui la kufanya... inasikitisha sana kufikiria kuwa kitu kama hiki kinaweza kufanyika. Hata katika vita kuna sheria, na tunazungumza juu ya wanaume wa miaka ya 20 na 30 ambao wanaingia kwenye nyumba ya ajuza na kumteka yeye pamoja na majirani zake."

Aliongeza kuwa anahofia afya ya mama yake, ambaye anahitaji dawa.

Mkewe Michal, ambaye pia alizungumza na BBC, alisema Ada alikuwa na mzio.

"Bila ya dawa zake, hatujui ataendelea kuishi kwa muda gani," alisema. "Ninajaribu kutofikiria mabaya, ni ngumu kufikiria hivyo."

Bw Sagi, ambaye anaamini atamwona mamake tena, alisema alikuwa akimtarajia mjini London wiki ijayo kwa siku yake ya kuzaliwa ya 75.

Alimtaja kama mwanamke mwenye nguvu, msukumo na wa ajabu, akiongeza kuwa alimwamini "kukabiliana na hali hiyo".