WARIDI WA BBC - Ninaishi bila bega na mkono kwa sababu ya Saratani.

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Esther Nyambura atafikisha miaka 39 mwezi ujao wa Disemba. Anatarajia kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa namna yoyote ile na kwa furaha kwa kutambua safari ngumu aliyopitia kutokana na mihangaiko ya ugonjwa wa saratani uliogundulika tangu akiwa na umri wa miaka 23.

"Muda mfupi baada ya kuolewa na kujifungua mtoto wangu wa kwanza nilianza kuwa na uchungu usiokuwa wa kawaida , ilikuwa ni mwaka wa 2007. Nilikuwa nahisi uchungu upande wa kulia wa mkono wangu karibu na mabega yangu . Ni uchungu ambao ulikuwa hauachi kuuma licha ya kumeza madawa ya uchungu kwa miezi mitatu" anakumbuka Esther.

Kutokana na kwamba uchungu huo uliendelea kuwa mkali zaidi na kuhangaisha maisha yake akiwa na mtoto mdogo , aliamua kufanya uchunguzi wa kiafya katika hospitali moja ambako alipigwa picha za XRAY , na vilevile uchunguzi wa kina katika maeneo yaliokuwa na eneo alilokuwa anasikia maumivu makali.

Baada ya uchunguzi huo wa kwanza matokeo yalionyesha kwamba alikuwa na aina ya saratani ambayo huathiri mifupa. Mwanadada huyu anasema kwamba baada ya kupewa matokeo hayo hakuanza matibabu yoyote kwani pia uchungu mwingi aliokuwa nao ulianza kuondoka ghafla.

"Kwa hiyo niliendelea na maisha yangu, na kusahau matokeo hayo, kwani uchungu ulitokomea kabisa. Hadi miaka michache baadaye , ambapo uchungu huo ulirudi kwa kasi mno na kuamua nirejee tena hospitalini, nilipofanyiwa uchunguzi wa mara ya pili ilidhihirika kuwa nina saratani ijulikanayo kama 'osteosarcoma' inayoanzia ndani ya mifupa ya binadamu"aliongezea.

Wakati huo Esther anasema kwamba alielezwa na wataalam waliokuwa wanamshugulikia kwamba angetolewa mfupa wa Saratani na kupachikwa chuma maalum, ila mwanamke huyu hakuchukulia uamuzi huo kwa uchanya aliukataa kata kata.

Na kwa kuwa yeye hakuelewa mengi kuhusu saratani inayoangamiza mifupa, na pia hali ya kuwa na dukuduku kuhusiana na matokeo ya kwamba alikuwa na saratani , aliendelea kutafuta maoni mbalimbali na matibabu tofauti. Alikuwa na matumaini kwamba angeelezwa matokeo tofauti kinyume na kwamba alikuwa na saratani.

"Nadhani kwamba nilipoteza muda mwingi wakati huo, hadi wakati nilishika ujauzito wa pili wa mtoto wangu wa kike ,ilikuwa ni mwaka wa 2012 , miaka mitano baada ya kupashwa taarifa kwamba nilikuwa na saratanı..Mkono wangu ulianza kuvimba mara nne zaidi ya mkono wa binadamu "anakumbuka Esther

Mwanamke huyu anasema kwamba ilikuwa changamoto hata kutembea kutokana na kuvimba kwa mkono na uchungu mwingi aliokuwa nao. Mwaka wa 2013 alihangaishwa na uchungu zaidi na alipofanyiwa uchunguzi mwengine alipatikana na saratani ya mifupa ijulikanayo kama Chandrosarcoma .

Alianzishwa matibabu ya miale ijulikanayo kama radiotheraphy baada ya miezi mitatu ule mkono wa kulia uliokuwa umevimba ulipasuka na kuanza kutoa maji yaliokuwa na uvundo wa ajabu.

"Ilifikia mahali mkono ulionekana hauna maana kabisa , ulikuwa umeoza hadi hata mimi nikaamini kwamba hauwezi kuokolewa tena , mkono umekuwa msumbufu, hata nikimeza madawa haupoi , sikuwa na amani hata kidogo" anasema Esther .

Kufikia hapo aliamua kwamba afadhali mkono uondolewe kabisa badala ya mateso aliokuwa nayo , mkono wenyewe ulinyofolewa kutoka sehemu inayoshikana na bega lake .

"Nilipoamka baada ya upasuaji nilijikuta bila mkono wangu wa kulia, mimi nilihisi kana kwamba nimeondolewa mzigo mkubwa sana , kiasi cha kwamba waliokuja kunifariji hospitali walikuwa wanashangaa ni kwanini ninafuraha na kicheko bila mkono wa kulia? anakumbuka Esther

Esther alikuwa ameshakubali hali ya kuishi bila mkono wa kulia , anasema kwamba kilichompa nguvu ni watoto wake wawili na mume wake ambaye daima alisimama kidete kumfariji na kuhakikisha amepata matibabu stahiki.

"Nilifahamu kwamba licha ya kuwa nitaishi bila mkono wa kulia , ningehakikisha kwamba nimeandalia jamii yangu kila kitu na mkono wa kushoto na mimi nilikataa kujichukulia kama mlemavu"anasema Esther

Mwanadada huyu anasema kamba kujikubali alivyo kulipelekea yeye kupona haraka na kuendelea na shughuli zake .

Mwaka wa 2019 miaka 5 baada ya kutolewa mkono wa kulia, uchungu ulianza kumnyemelea tena sehemu ya juu ya mkono uliyokatwa , mwezi wa Oktoba mwaka huo ilielekea kwamba saratani hio ilikuwa imerejea. Mwaka wa 2020 iliamuliwa kwamba nilazima angekatwa bega lote la épande wa kushoto.

"Nilisalia na sehemu kubwa ya upande wangu wa kushoto kukiwa na shimo kubwa .Nilifahamu kuwa saratani huwa ina endelea kula mtu hata zaidi wakati anaendelea kuishi bila kutafuta suluhu , ndio maana nilikubali niishi bila bega na mkono wote upande wa kulia"Esther anatema

Bilashaka maisha yalibadilika anasema Esther, hasa wakati jamii ilikuwa inahangaikia kutafuta pesa za matibabu, anasema kwamba kuna jamaa na marafiki walitoroka na kuingia mitini. Esther anasema kwamba ugonjwa wa saratani ulimpatia nafasi ya kuelewa ni nani mwandani wake na ni akina nani walikuwa tu wanaigiza kuwa marafiki.

Esther anasema kwamba ni muhimu kujikubakali ikiwa utafahamishwa una saratani .

"Ukielezwa una saratani wakati mwingine unakuta watu hawakubali matokeo hayo, utakuta mtu ameanza kujaribu dawa na aina ya matibabu tofauti. Usisikilize mawaidha mengi au nasaha bila mwelekeo . Mara utaambiwa jaribu ushirikina watu wengine wanalenga watu wenye saratani na kuwaambia kwamba pengine hujalipa madeni kwa wazee au wazazi , kwamba upeleke mbuzi nyumbani hapana .!!"anasema Esther.

Esther anatupilia mbali dhana potofu na kusema kwamba saratani haibagui weupe au weusi, wakubwa kwa wadogo, ikibisha hodi ni sharti ishughulikiwe kwa kasi ila lazima mtu ajikubali.

Imekuwa ni safari ndefu ya miaka 16 ya mwanamke huyu kupigania maisha yake. Kwa haya yote anasema kwamba mume wake amekuwa nguzo dhabiti katika kujikubali , kujipenda na kujithamini. Kwa upeo wa Esther maisha ni zawadi kutoka kwa mola na ni muhimu kushukuru kwa afya kila uchao .

Licha ya hayo yote mwanadada huyu hupendelea kuingia vyumba vya mazoezi , ambapo hupiga mazoezi , kama njia ya kuboresha mwili wake .

Esther anaamini kwamba saratani sio mwishio wa maisha, bali ni mwanzo wa kuona jinsi maisha yanakuwa ya maana hasa anapoangalia nyuma na kufikiria pandashuka ambazo amezipitia , hana budi ila kutabasamu huku akichukua hatua moja kwa nyengine kiła uchao akiwapa matumaini wahanga wote wa saratani.