Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: 'Picha ya video ' ilivyosababisha kifo cha mume wangu
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Mwaka huu Anne Sharon Hegnhof na mumewe ambaye ni wa asili ya Denmark wangekuwa wanasherehekea miaka kumi ya ndoa ambayo ameitaja kuwa na huba na upendo, ila tukio la mwaka wa 2018 lilizima ndoto za sherehe hiyo baada ya ajali mbaya kuwakuta wakiwa likizo nchini Uhispania.
Mnamo tarehe 21 mwezi Julai mwaka wa 2018, Anne na mumewe kwa jina Hegnhof pamoja na watu wengine katika jamii yao walikuwa wameingia nchini Uhispania kwa mapumziko. Jamii yake Anne ilikuwa na msisimko kwa sababu nyakati za mapumziko ulikuwa wakati wa kujuliana hali pamoja na kutangamana .
"Tulikuwa na desturi ya aina yake katika ndoa yetu , kila mwaka tulikuwa tunatenga muda wa kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. Kwa hiyo kila mwaka tulikuwa tunasafiri karibu mara tano tukielekea nchi mbalimbali tukijivinjari na kuwa pamoja," anakumbuka Anne.
Kulingana na mwanadada huyu, walikuwa wameingia nchi ya Uhispania wiki mmoja kabla ya ajali iliyobadilisha mkondo wa maisha yake. Wakiwa wamesalia na wiki nyingine moja kabla ya kurejea kwao nchini Denmark, Anne anakumbuka nyakati za asubuhi siku hiyo walifanya mipango ya jinsi wangejivinjari kwa kutembelea ufuo wa bahari mbali na mipango ya mume wake ya kuingia sokoni kununua zawadi.
Ila mipango yao haikutimia kwani mambo yalibadilika wakiwa njiani kuelekea baharini. Anne anasema kwamba yeye na mume wake walikuwa ndani ya gari moja dogo huku jamaa wengine wakiwa kwenye gari iliyokuwa imetangulia.
"Katika nchi hiyo kuna kuna mandhari ya kupendeza mijini na hata maeneo yaliyo nje ya mji. Nikiwa ndani ya gari nilipotizama nje nilitambua eneo mmoja ambalo lilikuwa na muonekano kama wa mji mmoja ulio nchi yangu ya asili Kenya .Nilianza kuashiria kwa mikono nikimuonesha mume wangu eneo hilo huku nikipiga picha za 'selfie' huku gari likiwa katika mwendo wa pole pole . lakini ghafla , tulisikia kishindo kikubwa , na hapo ndipo maisha yangu yakabadilika, "anakumbuka Anne.
Mwanadada huyo anasema kwamba alipoteza fahamu kutoka siku ajali ilipotokea hadi wiki mbili zilizofuatia. Alikuwa amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi akiwa amepoteza fahamu.
Katika kipindi hicho anasimulia matukio ya kuelezwa na mashahidi na watu mbalimbali . Kwanza ajali iliyowapata ilisababishwa na trela kubwa ambayo lilipoteza mwelekeo katika sehemu ya mteremko ,na kuligonga gari walimokuwa Anne na mume wake. Habari ni kwamba mume wake alifariki papo hapo , huku yeye akipata majeraha karibu sehemu zote za mwili .
Kulingana na walioshuhudia waliozungumza na Anne na video zilizonaswa katika eneo hilo, ni kwamba mumewe alifariki papo hapo, ila mwanadada huyo hakuwa amepoteza fahamu wakati huo lakini alikuwa na majeraha mabaya ambapo sehemu ya tumbo lale ilikuwa imepasuka huku mkono pamoja na sehemu za mgongo na kichwa zikiwa zimepata majereha mabaya.
Habari za kifo cha mumewe
Baada ya wiki mbili mwanadada huyu alirejesha fahamu na kitu cha kwanza alichouliza ni 'yuko wapi mume wangu?' wakati anauliza kuhusu hali ya mumewe alikuwa bado hajafahamu kwamba alikuwa hospitalini.
Kutokana na mwangaza mwingi aliokuwa anaushuhudia, alianza kupambana kusimama wima huku akijaribu kung'oa nyaya na mirija mingi iliyokuwa imepandikizwa mwilini mwake kama sehemu ya matibabu yake .Kulingana na Anne ilibidi wahudumu wamchome sindano ya kupata usingizi ghafla kutokana na mahangaiko aliyoamka nayo.
''Nilipopata ufahamu nilikuwa bado sielewi niko wapi, nilidhani kwamba nilikuwa nimewasili mbinguni kutokana na mwanga, pamoja na kuwaona wahudumu waliovalia nguo nyeupe.
Ni tukio ambalo siwezi kulielezea. Nilikuwa sina uwezo wa kuzungumza, wale wahudumu walinipa tarakilishi ndogo ambayo nilitumia kuandika ujumbe wangu na swali nililouliza ni, yuko wapi mume wangu? Wale wahudumu walinijibu papo hapo kwamba mume wangu alifariki kwenye ajali "anakumbuka Anne.
Mwanadada huyu anasema kwamba alikuwa haamini taarifa alizokuwa anapata kutoka kwa wahudumu, na aliwaeleza wahudumu hao kwamba taarifa hizo hazikuwa na ukweli wowote .
Katika muda huo wakati yuko bado hospitalini, Anne anasema kwamba alipokea mgeni ambaye ni mmoja wa swahibu wake wa karibu, anasema kwamba alishangaa ni vipi amefika hospitalini.
Anne anasema alianza kwa kumuuliza ikiwa ni kweli mume wake ameaga dunia , huku akilia, alimueleza kuwa ni kweli na kwamba asizidi kulia. Mume wa Anne alikuwa anafahamika kwa jina lengine Yens , swahibu wake akamuenleza kuwa Yens yuko mahali salama, akazidi kumfariji huku akimwekea mojawapo wa wimbo aliokuwa anaupenda ili umtulize. Ni matukio yaliokuwa yanafanyika kwa haraka sana Anne asingeng'amua cha kufanya.
''Swahibu wangu alinieleza ni lazima angefika hospitalini ili kuniwakilisha katika kutambulishwa kwangu, kwani wakati wa ajali sikuwa na cheti chochote cha mtu kufahamu mimi ni nani.
Baada ya wiki kadhaa , nilianza kuwaeleza wahudumu wangu pale hospitalini kwamba nilihitaji kurejea nchini Denmark. Tatizo lililokuwa ni kwamba hatukuwa tunaelewana katika mawasiliano yetu, wale walikuwa wanazunguma kihispania na mimi nilikuwa sielewi". Anasema Anne.
Mwanadada huyu anasema kwamba kabla hajaondoka nchini Uhispania , alikuwa ametoa ombi la kupata fursa ya kuona mwili wa marehemu mume wake katika chumba cha kuhifadhi maiti, ni ombi ambalo lilikubaliwa. Licha ya kwamba hakuwa na uwezo wa kutembea aliwekwa kwenye kiti cha magurudumu na kuwasilishwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti kwa ajili ya kumuona mume wake. Ni mojawapo ya siku ambazo hatazisahau maishani.
Alipoingia ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti alimokuwa mume wake, Anne anasema alikuwa ameomba muda kukaa naye na kuzungumza naye kwa mara ya mwisho. Ila wale wahudumu wakamueleza kuwa hawangekubali kumpa nafasi pekee yake kutokana na hali yake kisaikolojia. Muhudumu alisimama kando karibu na mlango . Akamuona mume wake kana kwamba alikuwa amelala, akamsemesha tu huku akilia, alikaa hapo kwa takriban dakika 30.
Baada ya hapo mipango ya kusafirisha Anne, pamoja na maiti ya mume wake hadi nchini Denmark ilianza, na hatimaye alisafirishwa kutumia ndege ya matibabu kutoka Uhispania hadi nchini Denmark
Anne anasema kwamba akiwa hospitalini nchini uhispania alikuwa amefanyiwa upasauaji mara 16 katika sehemu mbali mbali za mwili ila mgongo wake ulikuwa haujaguswa. Madaktari walikuwa wamesema kwamba mwili wake ulikuwa umehimili upasuaji baada ya mwingine na kwa hiyo alihitaji muda kabla ya upasuaji mwingine kufanywa.
Alipotua uwanja wa ndege nchini Denmark, walikuwa wamekubaliana kwamba Anne hakuwa tayari kurejea nyumbani kwake na alihitaji kukaa kwenye makao maalum ya uangalizi wa wagonjwa kama yeye.
Vile vile kulikuwa na wasiwasi kwamba Anne alikuwa anapitia kipindi kizito cha kukubali mabadiliko mengi yaliotokana na ajali .
Mwanadada huyu anasema kwamba hakuhisi akiwa nyumbani wakati akiwa nje ya makao yake, na aliwasihi wahudumu wa afya pamoja na watoto wake kwamba aendelee na matibabu akiwa nyumbani. Baada ya siku tano alirejea nyumbani kwake na kuchukua uamuzi wa kuupumzisha mwili wa mume wake .
Marehemu alikuwa mwenye asili ya nchi mbili Uswidi na Denmark na kulingana na mwanadada huyu mume wake alikuwa ameshatoa wosia wa kwamba endapo angefariki mabaki yake yarejeshwe nchini Uswidi .
"Mume wangu alikuwa ni Daktari ,alikuwa mtu wa kusafiri sana. Kuna wakati aliniambia kwamba iwapo siku moja nitasafiri na nikose kurudi nyumbani basi ningependelea mabaki yangu yarejeshwe nchini Sweden. Kwa hiyo mimi niliona ni muhimu niheshimu wosia wa mume wangu."anasema Anne.
Na hatimaye Anne aliongoza jamii ya marehemu mumewe katika kuchoma maiti yake kulingana na matakwa yake na hatimaye mabaki yake kusafrishwa hadi nchini Uswidi.
Kukubali
Anne anasema kwamba haikuwa rahisi kukubali matukio ya ajali hiyo iliyobadilisha maisha yake kabisa. Mwanadada huyu anakubali kwamba kukubali hatima imekuwa ni safari, iliyohusu kukataa , kuwa na hasira , kuwa na huzuni, kuwa na mawazo ya kujitoa uhai na kadhalika pamoja na hali ya kuishi na sonona ya siku nyingi.
Anasema kwamba kwa sasa amekubali hali yake, na anaona kana kwamba amepewa nafasi ya pili ya kuishi.
"Baada ya ajali iliyosababisha kifo cha mume wangu, nilikuwa siamini tena kwamba kuna Mwenyezi Mungu. Nilikuwa najiuliza ni Mungu yupi atasababisha hali hii ya majonzi na kifo kwa mtu niliyemthamini sana? Ila kwa sasa ninaamini kuna Mungu, ninaamini kwamba kwa kibali chake amenipa nafasi ya pili ya kuishi tena. Na kwa hilo mimi nimekubali matukio ya kale na sasa nina matumaini makubwa zaidi".
Maisha ya mwanadada huyu yamepiga hatua na anasema kwamba siri ya kuishi hatua baada ya nyingine imefanikishwa na jamii na marafiki wanaomshughulikia na kumjali. Pia mwanadada huyu anasema kwamba alipata fursa nyingine ya mahaba na kwa sasa anaye mpenzi ambaye yuko karibu naye sana.
"Siumii sana kama zamani , kwa hivi sasa nimeanza mahusiano mengine mapya, mwenza wangu amekuwa mtu muhimu katika maisha yangu , ananifariji na ananipenda sana na ninaamini hata yeye amechangia kupona kwangu kisaikolojia "anasema.
Anne alizaliwa nchini Kenya , ambapo mama yake ni raia wa Kenya na baba ni Raia wa Tanzania. Alipata malezi yake hadi kukamilisha chuo akiwa nchini Kenya. Anne anasema kwamba wazazi wake walifariki kwenye ajali na akasalia yatima. Bibi yake ndiye aliyemlea ila hata yeye alifariki kabla kufika utu uzima.
Alikutana na mume wake Yens katika hospitali moja jijini Nairobi wakati alikuwa anamtembelea rafiki wake aliyekuwa anaugua. Kwa upande mwngine mume wake naye alikuwa anafanya kazi ya udaktari hapo japo kwa muda.
Mapenzi yalikolea hadi walipofunga ndoa mwaka wa 2011 . Kama Yatima Anne anasema kwamba anapendelea sana kutembelea makao ya watoto wasiokuwa na wazazi kama njia ya kuhusika na maisha yao kwani anaelewa upweke na matatizo yanayoandamana na watoto yatima .