Je, Rais Kenyatta atamteua nani kuwa mrithi wake mwaka wa 2022?..

    • Author, Hezron Mogambi,
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu Cha Nairobi
  • Iliyochapishwa

Ikiwa kuna swala ambalo linatawala mazungumzo na siasa za Kenya ni suala la atakayemrithi Rais Uhuru Kenyatta baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Hili linatokana na uhusiano kati ya Rais Kenyatta na naibu wake, William Ruto, ambao umekuwa ukidorora tangu Machi, 2018 wakati Rais Kenyatta alipoanza kushirikiana na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila odinga.

Tofauti kati ya Rais Kenyatta na naibu wake, William Ruto, zimekuwa zikiendelea kuonekana hadharani. Huku Rais Kenyatta akishikilia kuzingatia shughuli za kimaendeleo, naibu wake amekuwa akijipigia upatu na kuzuru maeneo mbali mbali kujitayarisha kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Hali hii imewafanya wawili hawa waliokuwa marafiki wa karibu kisiasa tangu walipochaguliwa mwaka wa 2013 kila mmoja kuonekana kuchukua mkondo tofauti. Tofauti hizi, zimepelekea Rais Kenyatta kuchukua hatua kadhaa ambazo zinaonyesha kuwa amebadili nia kumhusu naibu wake kuwa mrithi kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Ushirikiano kati ya Rais Uhuru na Raila Odinga

Ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Raila Odinga umepelekea Bwana Ruto kuonekana kutengwa kwenye shughuli za serikali na hata za chama tawala cha Jubilee. Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta ameonekana kuhusiana zaidi na Raila Odinga kwenye siasa, shughuli rasmi na katika bunge la Kenya ambapo vyama vyao sasa vinashirikiana wazi wazi.

Itakumbukwa kwamba miezi kadhaa iliyopita, Rais Kenyatta alichukua usimamizi dhabiti wa bunge la kitaifa na lile la seneti ambapo kwa sasa mabunge haya hayana upande wa upinzani. Naibu wa Spika wa bunge la seneti, kiongozi wa wengi na kamati zake zimefanyiwa mabadiliko makubwa. Hali hii imekumba bunge la kitaifa ambapo kiongozi wa wengi na naibu wake na kamati zake pia zimefanyiwa mchujo.

Pigo kwa Ruto

Tofauti hizi zimepelekea mabadiliko kwenye uongozi wa seneti na bunge la kitaifa ambapo wandani wa naibu rais William Ruto wameondolewa. Miezi ya hivi karibuni, kumekuwepo na tofauti ambapo zimejitokeza hadharani kati ya rais na naibu wake jambo ambalo limewafanya wengi kushuku kwamba huenda William Ruto asiwe kwenye mahesabu ya Rais Kenyatta kuhusiana na uchaguzi wa mwaka wa 2022 pamoja na atakayekuwa mrithi wake baada ya kuhudumu kwa miaka 10 kama katiba ya Kenya inavyoruhusu.

Mgogoro na uhusiano baina ya Rais Kenyatta na naibu wake huenda ukachacha zaidi kufuatia kutolewa kwa ripoti ya marekebisho ya katiba BBI. Bwana Ruto anatofautiana na Rais kuhusiana na jambo hili. Ruto anasema kwamba hakuna dharura katika kuifanyia marekebisho katiba ya Kenya na kwamba fikra ya kutaka kuipanua serikali hasa katika ngazi na nyadhifa za juu kupitia kwa marekebisho haya ni jambo lisilofaa.

Kwa sasa, wengi nchini Kenya wanaamini kwamba Ruto amekasirishwa na kuvunjwa moyo baada ya kugundua kwamba Rais Kenyatta huenda asimuunge mkono katika uchaguzi wa 2022.

Kutafuta mrithi wa Rais Kenyatta

Kutokana na tofauti hizi, ni bayana kwamba wandani wa karibu wa Rais Kenyatta na viongozi wa chama cha Jubilee wamekuwa wakijikuna vichwa kuhusu uteuzi wa atakayefaa kumrithi ambaye ataweza kukubalika na Wakenya baada ya kupendekezwa.

Huku mchakato wa BBI ukiwa umeanza na ripoti yenyewe kupokelewa na Rais Kenyatta na Raila Odinga, kuna uwezekano kwamba atakayemrithi Rais Kenyatta anaweza kupendekezwa kupitia mchakato huu na kuweza, na hatimaye, kuchukua hatamu za kuongoza Kenya. Hata hivyo, hali hii ya mrithi wa Rais Kenyatta itategemea hatma ya mchakato wa BBI.

Kundi lenye kipaumbele

Kwanza kabisa, kuna kikundi ambacho kinajumuisha kinara wa chama cha ODM ambaye pia ni kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, ambaye chama chake kimeingia kwenye makubaliano na chama Jubilee, kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi na kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka. Tayari kuna ripoti ambazo zinaonyesha kwamba kati ya viongozi hawa, ndipo kuliko na wale watakaochuana na kuongoza Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Kwa umbali, mpango wa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta unaonekana kuwa mpango wa muda mrefu ambao unaendelezwa hadi kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2027.

Chini ya mpango huu wa kisiasa ambao yamkini ni fiche lakini unaonekana kwenye shughuli zinazoendelea za kisiasa, viongozi wanaofanya kazi kwa karibu na Rais Kenyatta wanataka kuwa na muundo wa serikali ambao utakuwa na Rais wa nchi, waziri mkuu, manaibu wawili wa waziri mkuu na naibu wa rais. Nafasi nyingine ambazo zinasemekana kuwa katika mpango huu wa wandani wa rais ni maspika wa mabunge ye seneti na lile la kitaifa.

Hata hivyo, mpango huu utaanza kubainika zaidi baada ya mchakato wa BBI na kura ya maoni nchini Kenya. Hii ndio sababu ya sheria kuhusu kura ya maoni kuwasilishwa bungeni ili iweze kushughulikia masuala haya yote.

Raila Odinga na BBI

Pili, kuna Raila Odinga ambaye ndiye mshirika wa karibu wa Rais Kenyatta katika mchakato wa BBI na ndiye walianzisha naye safari nzima ya BBI. Yamkini jinsi siasa zinavyokwenda, duru zinaarifu kwamba Raila Odinga yuko kifua mbele kumrithi Rais Kenyatta "kama daraja la muda" kabla ya kutoa nafasi kwa "anayefaa" katika uchaguzi utakaofuata kwa sababu, kwa sasa, mwanasiasa huyo hana uungwaji mkono wa kutosha kitaifa. Nafasi hii ya miaka mitano itampa nafasi ya kujijenga kisiasa.

Orodha ya wanasiasa wanafikiriwa zaidi kwenye mpango huu ni pamoja na seneta wa Baringo Gideon Moi (Kanu), Bwana Kalonzo Musyoka (Wiper) na Bwana Musalia Mudavadi (ANC).

Wiki mbili zilizopita, mwanasiasa Peter Kenneth aliongoza kundi la wazee wa jamii ya Wakikuyu kukutana na Raila Odinga nyumbani kwake, Bondo. Mkutano huu ulionekana kama njia mojawapo ya kuleta jamii za Agikuyu na Luo pamoja, jamii ambazo zimekuwa na uhasama wa kisiasa tangu Kenya kujipatia uhuru. Mipango inaendelea kufanyika kwa wazee wa jamii ya Luo kutembelea eneo la Mlima Kenya kuendelea kujenga uhusiano huo wa kisiasa na kijamii. Jambo hili linaonyesha taswira ya mambo.

Hata ingawa kiongozi wa upinzani Raila Odinga anaonekana kuwa mbele kwenye kinyanganyiro cha kuwania urais kwa sababu ya kuwa mmoja wa waanzilishi wa BBI pamoja na Rais Kenyatta, duru nyingine zinaarifu pia kwamba kuna makundi mengine yenye ushawishi mkubwa serikalini wasiompendelea. Hata hivyo, bwana Odinga ana sifa ambazo zinamweka kipuaumbele kwenye kinyanganyiro cha mwaka wa 2022 kwa sababu ya umri, raslimali za kuwezesha kampeini ya urais na sifa zake nzuri za kufanya kampeini kambambe za kitaifa.

Ikiwa mpango huu wa kisiasa utaafiki, Bwana Odinga atawania urais, Bwana Gidoen Moi awe naibu wake huku Bwana Kalonzo au Bwana Mudavadi akiwa mmoja wa manaibu. Mpango mbadala ni kutokuwepo kabisa kwa Uhuru Kenyatta kwenye mahesabu haya, na ambapo, Gideon Moi atawania urais ili kugawanya kura za eneo la bonde la ufa na William Ruto, huku Raila Odinga akiwa waziri Mkuu. Hali hii itamwacha Bwana Kalonzo Musyoka na kiongozi mwingine kutoka magharibi mwa Kenya wakichukua naibu wa waziri mkuu kwani makamu wa rais itabidi afikiriwe kutoka kwenye eneo la Mlima Kenya.

Aidha, kuna mpango mbadala wa kumhusisha kiongozi kutoka magharibi mwa Kenya-hasa Bwana Mudavadi - awanie Urais, mwanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya awe naibu wake, huku Bwana Odinga akiwa Waziri Mkuu na Gideon Moi na Bwana Kalonzo Musyoka wakiwa manaibu.

Aidha, kuna mpango wa kumhusisha mtu mashuhuri kutoka sehemu za pwani ya Kenya ili kupewa nafasi kubwa ya kitaifa, kama spika wa seneti ama bunge la kitaifa.

Hata hivyo, kufikia sasa, haijabainika wazi mipango ya kisiasa itakavyokwenda maana Bwana Musyoka na Mwana Mudavadi wote wanashikilia kwamba watawania urais mwaka wa 2022 huku Raila Odinga akieleza kwamba ataeleza mpango wake wazi baada ya kura ya maamuzi.

Sifa za Mwaniaji Urais

"Wanafikiria kwa sababu Uhuru anaondoka uongozini na kwenda nyumbani mwaka wa 2022, hatakuwa na nguvu zozote kuhusu ni nini kitatokea kwenye siasa za Kenya. Ninawaambia kwamba wakati mwafaka ukifika, nitakuwa na cha kusema," Rais Kenyatta alisema kwenye mkutano wa kisiasa mjini Nyeri, mnamo Novemba, 2018.

Kuna masuala mbali mbali ambayo Rais Kenyatta atazingatia kuhusiana na ni mwaniaji yupi ambaye atamuunga mkono kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022 pamoja na "uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa kwa sababu hataki kuwa kwenye mchezo wa pata potea na mipango yake na kukumbukwa visivyo."

Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba Rais Kenyatta atakuwa na ushawishi mkubwa kuhusu atakayemrithi baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2022. Hili ni bayana zaidi kwa sababu Raila Odinga ambaye wanashirikiana kwa sasa chini ya mwavuli wa BBI amekuwa kwenye siasa za Kenya kwa muda mrefu na anawazia zaidi pia jinsi atakavyokumbukwa, jinsi ilivyo kwa Rais Uhuru Kenyatta mwenyewe ambaye atakuwa akiondoka uongozini baada ya miaka 10.

Kinachojitokeza wazi sasa ni kuwa Rais Kenyatta ameanza kuonyesha mpango kuhusu atakayemrithi kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2022 ambao, yamkini, inavyokwenda kwa sasa, haumhusishi William Ruto.

Mpango unaoendelea wa kuwa na ushirikiano wa vyama vikuu vikiwemo Jubilee, Wiper, ANC, CCM na labda Ford-K na vingine ni moja kati ya mikakati yenye lengo la kuhakikisha kuwa Rais Kenyatta anapata nafasi mwafaka kumteua mrithi wake apendavyo.