Je janga la corona litasababisha watoto wengi zaidi kufanya kazi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mdororo wa kiuchumi katika kipindi hiki cha janga la corona kunaweza kuongeza idadi ya watoto wanaotumikishwa kufanyakazi, Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni (ILO) limeonya.
Katika taarifa iliyochapishwa kuadhimisha Siku ya Kimataifa dhidi ya Ajira ya Watoto, Juni 12, Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kwamba matatizo ya kifedha pia kunaweza kusababisha ulegezaji wa sheria zilizowekwa kulinda watoto dhidi ya kufanyishwa kazi ambako "kunawanyima uhuru wao wa kuwa watoto, uwezo wao na heshima yao na kwamba kunadhuru maendeleo yao ya kimwili na kiakili. "
"Tuna wasiwasi kwamba nchi zitaanza kulegeza sheria zao na kuondoa vipengele vinavyolinda watoto dhidi ya kufanyakazi," Benjamin Smith, mtaalamu wa masuala ya watoto dhidi ya kutumikishwa kazini wa ILO amezungumza na BBC.
"Mtazamo wetu ni kwamba hatua yoyote ya aina hiyo haitakubalika. Janga hili halimaanishi kurejesha nyuma hatua ambazo tumeshapiga."
Je ni watoto wangapi wanafanya kazi?
Shirika la ILO linafafanua utumikishaji wa watoto kufanya kazi kama ukiukaji wa haki ya msingi ya haki za kibinadamu na linahofia kwamba wakati virusi vya corona vinaendelea kusambaa, hilo linaweza kuchangia watoto wengi zaidi kufanyakazi kwasababu sasa hivi shule zimefungwa na familia nyingi zinajikuta zikitumbukia kwenye lindi la umasikini.
Idadi ya hivi karibuni inaonesha kwamba watoto milioni 152 kuanzia umri wa miaka 5 hadi 17 wanachukuliwa kama waathirika wa wanaofanya kazi wakiwa watoto kulingana na shirika hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Karibia nusu yao wanajihusisha na kile kinachofahamika kama kazi zilizo hatari au kujikuta katika mazingira mabaya ya kufanyakazi.
Mtindo huu ni kawaida sana barani Afrika, ambao mtoto mmoja kati ya watano ni sehemu ya wanaolazimika kufanya kazi kulingana na makadirio ya 2016.
Ajira kwa watoto kulingana na shirika la ILO, hilo pia linahusisha kufanya kazi bila kupata malipo ndani ya familia jambo ambalo limezungumziwa katika mikutano kadhaa ya Umoja wa Mataifa kulikoidhinishwa na mataifa zaidi ya 180.
Lengo kimataifa ni kumaliza tatizo la utumikishaji wa watoto kazini kufikia 2025 pia ni sehemu ya Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa na idadi ya walioathirika imekuwa ikipungua kulingana na mashirika mbalimbali yanayofuatilia suala la utumikishaji wa watoto kote duniani.
Lakini pia, Smith anahofia kwamba janga hilo litashinikiza familia zilizoathirika moja kwa moja au vyenginevyo kwasababu ya ugonjwa huo.
Pia kuna wasiwasi kwamba matatizo ya kiuchumi kulikosababishwa na janga la virusi vya corona kutaimarisha wito wa kufikiria tena upigaji marufuku wa watoto kufanyakazi au kutapelekea nchi kulegeza masharti yaliyopo.
"Tunaongeza hatari ya kupoteza kizazi iwapo hatua stahiki haizitachukuliwa," mtaalamu amesema. Kati ya mwaka 2000 na 2016, utumikishaji wa watoto kazini kulipungua kwa asilimia 38 kote duniani. Hiyo inamaanisha, kuna watoto milioni 94 wanaofanyakazi kote duniani.
Lakini pia ni kweli kwamba kuna baadhi ya mataifa ambayo yamechukua hatua tofauti.

2014, Bolivia ilipunguza umri wa mtu kufanyakazi kutoka miaka 14 hadi 10 katika mazingira fulani na chini ya usimamizi wa serikali - hatua ambayo ilisababisha utata na ilikosolewa na mashirika ya haki za kibinadamu.
Nchi zingine huenda hazijahalalishwa sheria kama hii lakini ukweli ni kwamba kuna idadi kubwa ya wafanyakazi ambao ni watoto.
Baadhi ya wataalamu pia wamehoji ufanisi wa marufuku kote duniani ya utumikashaji wa watoto kazini. Mwaka 2016, kundi la wasomi kimataifa lilisema kuwa marufuku hiyo ilikuwa ni yenye kuleta madhara na isokuwa na haja ya kuwepo".
Hoja kubwa yao ilikuwa nini?
Kwamba kufanya kazi kwa watoto kusionekane kama kitu kibaya moja kwa moja.
Wanaopendelea mabadiliko ya kisheria mara nyingi huwa wanazungumzia kisa cha seneta wa Marekani Tom Harkin: Mwaka 1993, alipendekeza mswada ambao ungepiga marufuku uingizaji wa bidhaa kutoka nchi ambazo uzalishaji wa bidhaa zao kunategemea watoto wanaofanya kazi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Harkin, wa chama cha Democrat kutoka jimbo la lowa, hasa alitaka kulenga viwanda vya utengenezaji wa nguo nchini Bangladesh, kufuatia ufichuzi kupitia runinga moja ulioshutumu duka kubwa la kufanya manunuzi la Walmart kwa kutegemea wasambazaji bidhaa nje ya nchi ambao wanatumia watoto katika utengenezaji wa bidhaa hizo.
Mswada huo haukuwahi kupita licha ya majaribio kadhaa zaidi ya mwongo mmoja. Lakini pendekezo la awali liliogopesha wamiliki wa makampuni ya Bangladesh kiasi cha kutaka kusimamisha utumikashaji wa watoto kufanya kazi katika viwanda vyao.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ilikuwa ni karibia watoto 50,000 wakati huo, kulingana na Jo Boyden, profesa wa chuo kikuu cha Oxford.
"Wengi wao waliishia kufanya kazi zenye kuhatarisha maisha yao kama vile ukahaba, na utengenezaji wa matofali. "
Boyden, ambaye amekuwa akifanya utafiti kwa maelfu ya watoto nchini Ethiopia, India, Peru na Vietnam, anaamini kwamba kanuni za kisheria haziakisi uhalisia wa maisha ya watoto ya kila siku.
Je kufanya kazi kunaweza kuwasaidia watoto wa nchi maskini?
Anaelezea kwamba watoto wengi huchanganya kazi na elimu, kwa kutumia pesa wanazopokea kutoka kwa kazi wanazofanya kulipia vitabu vya kusomea na kununua sare za shule pamoja na kuchangia mahitaji ya nyumbani.
Boyden pia alisikia kutoka kwa baadhi ya watoto aliozungumza nao kwamba wako tayari kufanyakazi.
"Kile ninachoona kwa watoto wa nchi maskini ambao wanafanya kazi kwa mara ya kwanza. Wana ujuzi mwingi unaohitajika," alisema.
"Tayari wanajua namna ya kusimamia pesa. Wanajua namna ya kuuza bidhaa."
Tunapokuja suala la kufikiria tena marufuku ya watoto kufanyakazi, baadhi ya watu - ikiwemo watoto wenyewe - wanadai kwamba sheria zilizopo zinazopinga wao kufanyakazi - zinakiuka haki zao na wanataka hilo libadilishwe.

Chanzo cha picha, Getty Images
"'Haina maana yoyote'
Benjamin Smith wa Shirika la ILO, hata hivyo, anasema ni muhimu kwa pendekezo lolote la kulegeza masharti ya watoto kufanya kazi kuangaliwa kwa makini.
Wakati anakiri kwamba ni vigumu kuzuia kila mtoto duniani kufanya kazi na kwamba kufanya kazi huenda ikawa jambo la msingi kabisa hasa kwa watoto wanaotoka matifa maskini, mtaalamu huyo hajakuwa wazi kwamba sheria zilizopo sasa hivi zisifanyiwe marekebisho.
" Tunajua kwamba kuna watoto ambao wanalazimika kufanya kazi, na ambao wanatuambia kuwa wanahitajika kufanya kazi ili kupata lishe yao ya kila siku. Hilo hatujlipinga,"
"Lakini haina maana kupunguza kinga hiyo kwa watoto wote duniani", Smith amesema.
"Watoto kufanya kazi ni ishara ya umaskini kwa watoto na hilo linawanyima kufurahia kuwa mtoto."












