Kurejea shuleni baada ya corona: 'Watoto watakuwa na wasiwasi hasa - lakini ni kawaida'

A teenager lying on her bed at home

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuhisi kutengwa na kuwa na wasiwasi kumeongezeka miongoni mwa vijana, wataalamu wanasema
Iliyochapishwa

Emma, 14, ambaye jina lake halisi limebadilishwa, anapitia wakati mgumu baada ya kuwa ndani kwa wiki kadhaa kama moja ya hatua zinazotekelezwa nchini Uingereza.

Kuwa na rafiki zake kumemwezesha kukabiliana na msongo wa mawazo, lakini kwa sasa anahisi kutengwa.

"Nipo tu ndani ya nyumba na sijui ni lini nitarejea shuleni au kuona rafiki zangu," amezungumza na Tume ya Watoto Uingereza.

"Hili linanipa msongo wa mawazo kweli.

Lakini analopitia sio jambo geni.

Wataalamu wameonya kuhusu athari za afya ya akili kwa watoto na vijana ambao watahisi kutengwa na kutenganishwa na marika zao kwasababu ya hatua ya kusalia ndani na kufungwa kwa shule.

A girls scrolling through her phone screen

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watoto na vijana wameonesha kuwa na hofu dhidi ya virusi vya corona kupitia utafiti uliofanywa na Unicef

Kulingana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa- Unicef, watoto walioshiriki utafiti katika hatua ya awali ya janga la corona walikuwa na wasiwasi wa kutengwa na familia zao na rafiki zao na pia kuhusiana na suala la kupata virusi hivyo na kufa.

"Pengine wiki ya kwanza, walifurahia kusalia nyumbani kwasababu hakukuwa na shule. Lakini kwa haraka haraka, watoto walianza kupata wasiwasi," Ursula Grass, mkuu wa shule ya Waldhauschulle kusini magharibi mwa Ujerumani ameiambia BBC.

"Walilazimika kukabiliana na tatizo la kutengwa nyumbani."

Kukosa kutangamana

Shirika la Unicef linasema watoto bilioni 1.6 waliathirika na kufungwa kwa shule katika nchi 145. Na sio tu kwamba masomo yao yamekatizwa.

"Walimu hawasomeshi tu masomo kama vile hisabati, lugha na kadhalika. Pia wanawafundisha namna ya kutangamana, kuwa na huruma, na pia kucheza na wengine," anasema Bi. Grass.

A girl in a school in Gaza, 20 May 2020

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, kuna maanisha watoto bilioni 1.6 walikatiza masomo yao na hivyo kukosa kuonana na rafiki zao

Katika nchi iliyoendelea kama Ujerumani, walimu wanaweza kuweka kazi za wanafunzi kwa intaneti, na kuendeleza mawasiliano kwa njia ya simu na barua pepe.

"Lakini ule uhusiano wa karibu haukuwepo, na kwamba kwa watoto wengi lilikuwa tatizo kubwa," Bi. Grass amesema.

"Shule zinatoa ratiba ya kawaida ya kufanya mambo, eneo salama ambapo vijana wanaweza kuzungumza na watu wazima wanaowaamini pamoja na rafiki zao ana kwa ana," amesema Tom Madders, mkurugenzi wa chama cha kuangalia maslahi ya watoto.

Wakati ambapo nchi nyingi zinajitayarisha kuanza kulegeza masharti, "shule zitakuwa na jukumu muhimu katika kuunga mkono vijana," amesema bwana Madders.

Katika nchi kadhaa, watoto wanaanza kurejea shuleni lakini Bwana Madders ametahadharisha kwamba shule zinastahili kufunguliwa tu ikiwa hali ni shwari na usalama wa uhakika.

Sheria mpya

A boy washes his hands in a school in France, 14 May 2020

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kanuni za kunawa mikono sasa zinahitajika kutekelezwa kikamilifu shuleni

Kama ilivyo kwa maeneo mengine, shuleni ni maeneo tofauti kabisa ikilinganishwa na ilivyokuwa wiki kadhaa zilizopita.

Sheria za usafi kama vile watoto wanavyohitajika kuosha mikono kila wakati na kuhakikisha wanaingia chooni mmoja mmoja.

Denmark na Ujerumani, watoto wanawekwa kwa makundi ya idadi ndogo ndogo.

Makundi haya yanafika kwa nyakati tofauti na pia wanakula chakula cha mchana kwa nyakati tofauti, wanacheza kwa makundi hayo tofauti tofauti na wanafundiswha na mwalimu mmoja.

Ni vigumu, hasa kwa watoto wadogo pale ambapo hawawezi kuwa na rafiki zao, wanapotengwa madarasani na pia wakati wa mapumziko," anasema Bi. Grass.

Pupils observe social distancing rules in a school playground in the Netherlands, 15 May 2020

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Watalaamu wanasema kutekeleza hatua za kutokaribiana miongoni mwa watoto itakuwa changamoto kubwa

Nchini Uingereza, shule bado zimefungwa hadi Juni, lakini Megan, 14, anahofia kwamba hataweza kutangamana na rafiki zake tena.

Ameiambia BBC kwamba ni kheri aendelee kuonana nao kupitia mtandao kwasababu hataweza tena kuwakumbatia.

Helen Dood, profesa wa saikolojia ya watoto katika Chuo Kikuu cha Reading Uingereza, anasema kujitahidi kutekeleza hatua ya kutokaribiana itakuwa vigumu kwa watoto wadogo.

"Njia pekee ya kuwezesha hilo ni kuweka hatua za kudhibiti kukaribiana kabisa, na hili sio jambo jema kwa wanafunzi hasa afya yao ya akili," Profesa Dodd amezungumza na BBC.

"Watoto wanastahili kuhisi kwamba wana uhuru, kuwa wanaweza kujifanyia maamuzi na kujidhibiti."

Kufunguliwa tena kwa shule 'inaweza kuwa changamoto'

Pupils at the Waldhausschule in Germany
Maelezo ya picha, Wanafunzi wa shule ya Waldhausschule nchini Ujerumani wakiwa wamevalia barakoa za rangi mbalimbali

Zeinab Hijazi, mtaalamu wa masuala ya afya ya akili na kisaikolojia kutoka Unicef, anasema kufunguliwa tena kwa shule ni mchakati ambao unahitaji kusimamiwa vizuri.

"Bila shaka kunaweza kuwa changamoto kubwa," alizungumza na BBC.

"Kuwa na wasiwasi kwa watoto ni jambo lisiloepukika. Lakini ni kawaida kwa nyakati ngumu kama hizi."

Bi Hizaji anasema walimu wanahitaji kuwa na maarifa na uwezo wa kusaidia watoto ambao wanapitia changamoto kihisia.

"Walimu wanatumia muda mwingi na watoto kuliko mwengine yeyote, na wao ndio walio na uwezo mkubwa wa kubaini changamoto zozote walizonazo za kiafya," anasema.

Kusini magharibi mwa Ujerumani, wanafunzi wa Grass ni wale wanaotakiwa kupata mahitaji maaalum kumaanisha kwamba wako katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya afya ya akili.

Anasema kwamba kazi yake kubwa imekuwa "kupunguza hofu hiyo".

Pupils at the Waldhausschule in Germany pictured outdoors
Maelezo ya picha, Angalizo lake kubwa limekuwa katika suala zima la kupnguza hofu, anasema Bi. Grass

"Tulifanya baadhi ya miradi nao," Bi Grass anasema, kama vile kwenda msituni, kuoka pizza na kushona barakoa zao.

Baada ya Ujerumani kupendekeza rasmi matumizi ya barakoa, Bi Grass pamoja na wanafunzi wake walianza kuzishona kwa kujitolea.

Hatua hiyo ya kutengeneza barakoa, anasema kumefanya wanafunzi wake wamejifunza kuhusu hatua za kujikinga na kuondoa hofu waliokuwa nayo.

'HKupona kihisia'

Bi Grass anasema, "Mwalimu anahitaji kuona wanafunzi sio tu wakisoma bali pia wakiwa na amani."

Lakini nchini Uingereza, Megan, 14, anahisi kwamba badala ya walimu kufundisha, wamekuwa wakitoa kazi tu".

Tatizo kubwa linaanzia pale ambapo anajitahidi kutafuta utaratibu aliouzoea akiwa nyumbani.

Children read a book together in a library

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Lazima tuwape watoto muda wa kupona, anasema Profesa Dodd

Profesa Dodd anasema shuleni na wazazi watakuwa wa msaada mkubwa kwa watoto wakati wanapoanza tena maisha na sio kwa kuwalazimisha kufanya mambo fulani.

"Ili watoto waweze kusoma kadiri ya uwezo wao kipindi hiki cha mwaka, tunahitaji kuwapa muda huu kupona kwanza kisaikolojia kwa yale wanayopitia kabla ya kuanza kwa masomo rasmi tena kama ilivyo kawaida," Profesa Dodd amesema.

"Ujumbe uko wazi kwamba katika kipindi cha muda mrefu, hili litafaidi watoto katika masomo yao."

Na sio ujumbe utakaopokelewa vyema na kila mtu, katika jamii ambayo utamaduni umekuwa kutoa kipaumbele kwa mafanikio ya elimu.

Nchini Vietnam, Unicef inaomba serikali kupanga tena upya kalenda ya shule kwa watoto inaweza kuwa na mwaka ujao wote ili kufidia miezi minee ya kufungwa kwa shule.

“Hili linaweza kusaidia pakubwa kupunguza shinikizo inayokumba watoto hawa wakati huu,” Simone Vis, mtaalamu wa elimu wa Unicef nchini Vietnam amezungumza na BBC.

Children do gymnastic exercise in Phuc Dien elementary school Hanoi, Vietnam, 11 May 2020.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Mei, shule nchini Vietnam zilifunguliwa baada ya kufungwa kwa miezi minne

Utafiti uliofanywa Aprili na walimu 8,000 na nyanja mbalimbali unaonesha kwamba watoto wana wasiwasi kuhusu kukatishwa kwa masomo yao na vile hatua hii itakavyoathiri matokeo yao.

"Na pia sio jambo la kustaajabisha hasa ukizingatia kwamba shinikizo iliyopo kwa wazazi wa Vietnam dhidi ya watoto wao katika suala zima la kusoma na kufanya vyema shuleni," Bi Vis anasema.

"Shinikizo hili linatoka kwa jamii na marika yao na huenda hilo likawa na athari hasi kwa masomo ya wanafunzi."

'Ni wakati wa kuwasikiliza'

Serikali na shirika la Unicef wamezindua kampeni awali mwezi huu katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kunakolenga kuanza mijadala ya kitaifa kuhusu afya ya akili.

Watoto wamekuwa wakishirikishana michoro, video na aina nyengine za mawasiliano kuhusu virusi vya corona na kufanya hofu yao kuwa jambo la kawaida.

Masks coloured by pupils at the Waldhausschule in Germany
Maelezo ya picha, Barakoa za rangi zinaweza kusaidia watoto kukubali hali,amesema mwalimu Grass kutoka Ujerumani

Walimu wanaombwa kuwaarifu watoto wao "ni kawaida kuwa na hisia kama hizo," Bi Vis anasema.

Kampeni hiyo inajumuisha mapendekezo ya wazazi kuhusu namna wanavyoweza kujibu watoto nyumbani kwa namna ya kuwasaidia kihisia dhidi ya virusi vya corona.

"Ni muhimu kwa wazazi kuzingatia kusikiliza watoto, ili waweze kuhisi kujiamini zaidi katika suala zima la kushirikishana wengine hisia zao," Bi Vis amesema.

"Wazazi wanatakiwa kuchukua muda kuwafariji na kuwaonesha upendo na kuwapa hakikisho," aliongeza.

"Ni muhimu kuwapongeza kila mara kwasababu watoto hawa wameonesha ujasiri kupitia janga hili."