Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Odinga na Kenyatta: Mambo yalivyokuwa siku ya Uchaguzi Mkuu Kenya 2017 tarehe 8 Agosti
Muungano wa upinzani nchini Kenya umepinga matokeo ya urais ambayo yamekuwa yakitangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi IEBC.
Moja kwa moja
Mji wa Nakuru wabaki 'mahame'
Maeneo mengi ya miji yamebaki bila watu, wengi wakielekea katika vituo vya kupigia kura kupiga kura. Mwandishi wetu Idris Situma amepiga picha hizi mjini Nakuru.
John Kerry, mmoja wa waangalizi wa uchaguzi awasili kituo cha kupigia kura cha Moi Avenue, Nairobi
Wapiga kura wakipata chai ya asubuhi wanaposubiri kupiga kura
IEBC: Tunaangazia changamoto zinazoshuhudiwa
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC amekuwa akiwahutubia wanahabari ukumbi wa Bomas.
Amesema anafahamu kwamba baadhi ya Wakenya walirauka hata kabla ya vituo kufunguliwa.
Amewahimiza wapiga kura ambao hawajafika vituoni kufanya hivyo.
Bw Chebukati amesema anafahamu kwamba katika baadhi ya vituo kumeshuhudiwa changamoto na wanaangazia kuzitatua.
Katika baadhi ya maeneo, amesema mvua kubwa ilitatiza uchukuzi na wamelazimika kutumia helikopta.
"Katika vituo vilivyochelewa kufunguliwa, tutaongeza muda wa kufunga vituo, sawia na muda uliocheleweshwa."
Mtindo wa mavazi katika kupiga kura
Wapiga kura wamekuwa wakijitokeza kwa njia mbalimbali na wakiwa wamevalia mavazi mbalimbali. Lakini utafanyaje kuonesha uzalendo? Pengine uvalie kama watatu hawa katika kituo cha Mutomo, Gatundu ambapo Rais Kenyatta anatarajiwa kupiga kura baadaye.
Upigaji kura kituo cha William Ruto
Upigaji kura unaendelea katika kituo cha Kosachei katika kaunti ya Uasin Gishu ambapo Naibu Rais William Ruto anatarajiwa kupiga kura yake baadaye leo.
IEBC: Tunafahamu kuna vituo vilichelewa
Tume huru ya uchaguzi nchini Kenya imesema inafahamu kwamba kuna baadhi ya vituo vya kupigia kura ambavyo vilifunguliwa kwa kuchelewa.
Tume hiyo imeandika kwenye Twitter kwamba maafisa wake wanashughulikia hilo na tahakikisha hakuna mpigaji kura anayetatizika.
Foleni katika baadhi ya vituo
Katika baadhi ya vituo, kuna foleni ndefu. Mfano ni katika kituo hiki cha Kipsigis County Council mjini Kericho kama alivyoshuhudia mwandishi wa BBC Rob Wilson.
Je, wewe ni Mkenya, hali iko vipi ulipo?
Yasemavyo magazeti ya Kenya kuhusu uchaguzi
Wakenya wapiga kura nchini Tanzania
Raia wa Kenya waishio Tanzania wamekuwa wakipiga kura nchini Tanzania katika miji ya Dar es Salaam na Arusha.
Mwandishi wa BBC Halima Nyanza yupo katika kituo cha kupigia kura mjini Arusha ambapo ameshuhudia upigaji kura ukiendelea.
Hitilafu za kimitambo kituo cha Kibra
Mwandishi wa BBC Abdinoor Aden anasema mitambo ya kuwatambua wapiga kura katika kituo cha shule ya Olympic, Kibra imeanza kukubwa na hitilafu.
Shughuli ya upigaji kura imesimama kwa muda maafisa wa tume ya uchaguzi wakijaribu kutatua tatizo hilo.
Afisa msimamizi wa ucahguzi kituo hicho Aggrey Mulera amesema wanajaribu kutafuta suluhu.
Hakuna kuachwa nyuma
Watu wa jamii ya Kalasinga hawajaachwa nyuma katika mji wa Kisumu, magharibi mwa Kenya. Mwandishi wetu Odeo Sirari amekutana na wawili hawa kwenye foleni kituo cha Ukumbi wa Aga Khan.
Kukanganywa na rangi Kisumu
Mpiga kura huyu anasema hakuweza kutofautisha rangi za karatasi za kupiga kura, rangi ya karatasi za wawakilishi wa wadi na wawakilishi wa wanawake.
Rangi ya karatasi ya kupigia kura inafanana na rangi ya vifuniko vya masanduku ya kutumbukiza kura.
Rangi ya karatasi ya urais ni nyeupe na vivyo hivyo, masanduku ya kura za urais yana vifuniko vyeupe.
Ugavana rangi ni ya samawati. Kura ya seneta ni ya manjano, mbunge ni kijani kibichi na mwakilishi wa wanawake ni ya kizambarau nazo za mwakilishi wa kaunti biji.
Upigaji kura wachelewa kuanza Garissa
Upigaji kura katika kituo cha kupigia kura cha Maktaba ya Garissa umechelewa kuanza. Mwandishi wa BBC Bashkas Jugsodaay anasema upigaji kura umeanza dakika chache zilizopita.
Wapiga kura wa kwanza Kisumu
Mwandishi wetu Odeo Sirari yupo katika kituo cha Aga Khan mjini Kisumu na amewapiga piga wapiga kura hawa ambao walikuwa miongoni mwa waliopiga kwanza kituoni humo.
Wapiga kura wa kwanza Kwale
Upigaji kura umeanza katika kituo cha Wabungo, Kwale pwani ya Kenya na baadhi ya watu washamaliza kupiga kura.
Pichani ni mmoja wa waliopiga kura kwanza.
Garissa raia kupiga kura maktabani
Shughuli ya upigaji kura imeanza katika kaunti ya Garissa, mashariki mwa Kenya. Usalama umeimarishwa.
Pichani ni maafisa wa Tume ya Uchaguzi wakijiandaa kwa upigaji kura.
Hali ilivyo Mwabungo eneo la Kwale pwani ya Kenya
Hivi ndivyo hali ilivyo kituo cha kupigia kura cha Mwabungo kaunti ya Kwale. Hapa, watu wa jamii ya Makonde watapiga kura mara ya kwanza baada ya kutambuliwa kuwa raia wa Kenya.
Habari za hivi punde, Vituo vya kura vyafunguliwa
Vituo vya kupigia kura nchini Kenya vimefunguliwa rasmi.