Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Lissu: Msiruhusu upande wa mashitaka kuleta vitu ambavyo hawajanituhumu navyo

Kesi hiyo ya uhaini iliyosimama kwa miezi mitano inasikilizwa mfululizo kuanzia leo hadi Septemba 7, 2026, chini ya Jopo la Majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Mapigano katika kambi ya kijeshi nchini Mali yamewaua wapiganaji kadhaa, jeshi limesema

    Mamlaka nchini Mali zimesema wanajeshi wao waliwaua wapiganaji kadhaa wa Kiislamu wenye msimamo mkali walipokuwa wakizuia shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi siku ya Jumapili.

    Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), kundi la kijihadi linalohusishwa na al-Qaeda, limesema ndilo lililohusika na shambulio hilo, ambapo wapiganaji wake walidai kuchukua udhibiti wa kambi hiyo katika mji wa San.

    Jeshi, ambalo pia lilipata hasara katika shambulio hilo, limekanusha kwamba lilipoteza udhibiti wa kambi hiyo. Hata hivyo, limesema wanajeshi wake walilazimika “kujiondoa kwa muda.”

    Tukio hilo limetokea wakati hali ya usalama nchini Mali ikionekana kuzidi kuwa mbaya, zaidi ya muongo mmoja tangu uasi wa makundi ya kijihadi uanze kushika mizizi kaskazini mwa nchi hiyo.

    “Adui ameangamizwa na shambulio limedhibitiwa kwa mafanikio. Takribani magaidi 40 wameangamizwa,” alisema Luteni Kanali El Oumrani, kamanda wa kikosi cha 23 katika kambi ya San, kwenye video.

    Aliwataka wakazi kuwa waangalifu, akisisitiza kwamba wanajeshi wake “hawajaondoka popote” na kwamba kambi hiyo bado iko chini ya udhibiti wa jeshi.

    “Kambi ya kikosi cha 23 haiko tupu; iko chini ya ulinzi wa jeshi.”

    Mashahidi walionukuliwa na kituo cha redio cha Ufaransa RFI walisema shambulio hilo lilianza karibu saa 05:00 asubuhi kwa saa za Mali (GMT) siku ya Jumapili, na lilidumu kwa takribani saa mbili.

  2. Ushahidi waendelea kutolewa mahakamani

    Jaji: shahidi kiapo chako kinaendelea naamini unakumbuka ulipoishia

    Wakili: Baada ya kupata taarifa kwa ma RCO wa mikoa mbalimbali nini kiliendelea

    Shahidi: Hatua iliyofuata niliitisha majalada nikiwa na lengo la kusoma na kufahamu ushahidi uliopo ndani ya hayo majalada

    Wakili: ni mikoa ipi na ipi?

    Shahidi: Mfano mkoa wa kilimanjaro lenye KR/CIB/PE/18/2025 hili lilikuwa jalada la uchunguzi toka Kilimanjaro, Arusha Ars/CIB/PE/40/2025, Mbeya MBE/CID/PE/54/2025 pia kuna jalada lilitoka Ruvuma likiwa na kumbukumbu namba …. ambalo lilikuwa na kosa la kula njama za kuandamana

    Pia kulikuwa na jalada toka mkuu wa upelelezi Kinyerezi

    Wakili: Baada ya kuitisha haya majalada unakumbuka nini?

    Shahidi: Baada ya kuyapokea niliyasoma

    Wakili: Baada ya kuyasoma yalikuwa kwenye hatua gani za upelelezi Shahidi: Baada ya kuyasoma tulibaini wengi waliokuwa kule walikuwa wamehamasika na kauli ya mshitakiwa na tukabaini wengi wao walikuwa wafuasi wa Chadema na wengine wachache wa vyama vingine

    Wakili: Baada ya kugundua wengi wao walikua ni wafuasi kilifuata nini?

    Shahidi: Nilielekeza majalada yarudi mikoani na nikaelekeza hawa watu watafutwe na waandikwe maelezo kama mashahidi.

    Wakili: Waandikwe maelezo kama mashahidi kwenye kesi gani?

    Shahidi: Kwenye kesi hii tuliyonayo ya uhaini jambo ambalo liletelekezwa wahusika walipatikana na wakaandikishwa maelezo

    Wakili: Baada ya kupata hayo maelezo hasa wewe ulifanya nini?

    Shahidi hayo maelezo yaliwekwa kama sehemu ya jalada la ushahidi dhidi ya mtuhumiwa.

    Wakili: Unakumbuka nini juu ya tarehe 9/4/2025

    Shahidi: Hii ndio tarehe aliyokamatwa mshitakiwa akiwa ziarani mbinga wakili alafu baada ya kukamatwa

    Shahidi: Alisafirishwa siku hiyo hiyo na kuletwa Dar es salaam na alifika kesho yake tarehe 10/04/2025 na kufikishwa kituo cha kati cha polisi alifikishwa na kusomewa tuhuma zake na mtuhumiwa alisema hakua tayari kutoa maelezo pale na alisema atatolea maelezo yake mahakamani.

    Wakili: Kisha nini kikaendelea? Shahidi: Baada ya kupata maelezo yako ofisi ya taifa ya mashtaka ya kanda ya DSM ilipofika majira ya mchana iliandaa mashitaka dhidi ya mshitakiwa na jioni ya hiyohiyo siku alifikishwa mahakama ya hakimu mkazi kisutu.

    Wakili: Nini kikafuata?

    Shahidi: Nakumbuka baada ya kusomewa mashitaka Jalada la upelelezi lilirejeshwa kwetu kwa ajili ya upelelezi zaidi.

    Wakili: Nini unakumbuka kingine?

    Shahidi:Tukiwa tunaendelea na upelelezi tulipokea malalamiko toka kwa baadhi ya mashahidi kuwa kuna matishio kwao iwapo wangetoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa.

    Wakili: Hao waliokua wanatoa vitisho mlibaini ni nani?

    Shahidi: Wengi walikuwa ni wafuasi wa chadema tena wakitumia maneno ya kuwasalimia na kwenda mbali ya kusema waombewe mabaya wapate mikosi na laana.

    Wakili: Baada ya kupokea hiyo taarifa mlifanya nayo nini?

    Shahidi: Na sisi kwa nafasi zetu tuliingia kwenye mitandao na comments zenyewe zilikuwa na vitisho kwenye mitandao ya facebook, tiktok instagram na x

    Wakili: Baada ya kujiridhisha...?

    Shahidi: Baada ya kujiridhisha nilifanya mawasiliano na ofisi ya taifa ya mashitaka kueleza juu ya matishio hayo kwa mashahidi ili kuomba wafichwe (ulinzi)

    Wakili: Nini kikafuata?

    Shahidi: Baada ya hapo nilikwenda kuchukua kiapo maalumu toka ofisi ya taifa ya mashitaka ili mashahidi hao wapatiwe ulinzi

    Wakili: Mheshimiwa jaji baada ya kuwauliza wenzangu hakuna swali la nyongeza.

    Unaweza kusoma;

  3. Marais wa mashirikisho ya soka: Infantino alivunja uaminifu

    FIFA na rais wake, Gianni Infantino, wametuhumiwa kuvunja uaminifu “kupitia udanganyifu” katika barua ya wazi iliyotolewa na UEFA, Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia (AFC).

    Barua hiyo, iliyotiwa saini na marais na makatibu wakuu wa mashirikisho hayo, ilisema kuwa mzozo wa hivi karibuni kuhusu pendekezo la Fifa Forward Enterprise (FFE) kimsingi ulihusu “uadilifu wa mchezo, pamoja na uadilifu wa wale waliochaguliwa kuuongoza.”

    FFE ingesababisha kuanzishwa kwa kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na tiketi za mashindano yote ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia, huku 21% ya kampuni hiyo ikiuzwa kwa kampuni binafsi ya uwekezaji.

    Mpango huo ulisitishwa baada ya kukosolewa vikali na mashirikisho kadhaa, yakiongozwa na UEFA, ambayo ilitishia kususia mashindano yote ya FIFA.

    “Uaminifu unapovunjwa kupitia udanganyifu, na mtu anapojiona kuwa yuko juu ya jumuiya iliyomkabidhi mamlaka, basi ameachana na wajibu huo,” ilisema barua hiyo.

    Barua hiyo iliongeza:

    “Uongozi katika soka si mali ya mtu. Sio suala la kushikilia au kudai mamlaka ili yaendelee kushikiliwa. Ni wajibu wa kuitumikia familia ya soka iliyokukabidhi dhamana hiyo.”

    Ingawa taarifa hiyo haikumtaja Infantino kwa jina, vyanzo vimeiambia BBC Sport kwamba inapaswa kuonekana kama fursa kwake kujiuzulu na kuondoka katika nafasi yake kwa heshima.

    Taarifa hiyo imekuja baada ya FIFA kutoa taarifa Jumamosi jioni, ambapo ilikosoa vikali kile ilichokiita “juhudi zinazoendelea na zilizoratibiwa” za kuidhoofisha taasisi hiyo pamoja na Infantino.

    Unaweza kusoma;

  4. China yawahamisha watu milioni moja kutoka kwenye makazi yao huku dhoruba kubwa ikikaribia

    Mamlaka nchini China zimewahamisha zaidi ya watu milioni moja kutoka kwenye makazi yao mashariki mwa China, ikiwemo mji mkuu Shanghai, baada ya Kimbunga Dolphin kutua nchi kavu.

    Kimbunga hicho kilileta mvua kubwa na kusababisha usafiri kusimama katika maeneo mbalimbali ya kanda hiyo. Takribani ndege 1,000 ziliahirisha safari mjini Shanghai pekee siku ya Jumatatu.

    Ingawa mamlaka zimepunguza hadhi ya Dolphin na kukitaja sasa kuwa dhoruba ya kitropiki, bado zinaonya kuhusu mvua kubwa sana, mafuriko makubwa na hatari ya maporomoko ya ardhi hadi Jumatano, wakati dhoruba hiyo ikielekea kaskazini.

    Awali, mamlaka za China zilitoa onyo kuhusu Dolphin. Kilikuwa kimbunga chenye nguvu zaidi kuikumba China mwaka huu.

    Kimbunga hicho kilikuwa na kasi ya juu ya upepo ya kilomita 150 kwa saa kilipotua kwa mara ya kwanza huko Yuhuan, katika mkoa wa Zhejiang, saa 17:30 (09:30 GMT) Jumapili.

    Takribani saa moja baadaye, kilitua kwa mara ya pili katika mji wa Wenzhou, kwa mujibu wa mamlaka za hali ya hewa.

    Mvua kubwa ilitabiriwa Jumatatu katika mikoa ya Shandong, Henan, Hubei, Anhui, Jiangsu na Zhejiang, pamoja na mji wa Shanghai.

  5. "Msiruhusu upande wa mashitaka kuleta vitu ambavyo hawajanituhumu navyo"

    Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, leo amefikishwa mahakamani ambapo Shauri la Uhaini linaendelea kusikilizwa.

    Wakili amesema ‘waheshimiwa majaji ushahidi unapimwa na mahakama, na hazuiwi kusema, huyu ni mpelelezi sasa anazuiwa vipi asiseme walichokibaini na huu sio ushahidi mpya. Mashahdi wengine walisema pia uchaguzi ungezuia vipi kumzuia kusema sio sawa na mahakama hii nina amini inatenda haki’.

    Baada ya majadiliano kidogo, Jaji alimruhusu wakili wa serikali kuendelea na akaanza kumuelezea Jaji msingi wa swali alilomuuza shahidi hasa kwenye kipengele cha kukinukisha.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, shahidi hana haki ya kutoa ushahidi anaoufikiria. Anatoa ushahidi unaoendena na shauri husika kitu anachosema kiwe kinaendana na kesi, kuna maneno mengi sana kwenye kesi hii tutakinukisha, na mengine yako kwenye hati ya mashtaka lakini hakuna maneno ya kuchana karatasi za kura, tutapiga watu. Mkiruhusu haya meneno, mtafungua sanduku la wadudu wabaya kuingia na mtashindwa kuendesha kesi hii vyema.

    Ni rai yangu msiruhusu upande wa mashtaka kuleta vitu ambavyo hawajanituhumu navyo, hatari ni kwamba mkiruhusu ukaingia kwenye rekodi mtalazimika kuutolea uamuzi na wanafahamu hivyo mkiruhusu tutahama kwenye kesi ya uhaini na kwenda kwenye kuchoma karatasi za kura sisi tuna haki ya kupinga ushahidi unapokuwa sio sahihi na msiruhusu mambo ambayo hayapo naomba msiruhusu.

    Baada ya hapo, majaji waliongea tena kidogo.

    Tukitazama hapa notisi tuliyotoa awali naona ndio huko tunataka kuelekea wakili muongoze shahidi vizuri hataki kwenda kwenye mambo ya Oktoba, 29 ambayo tulishakataa tangu awali.

    Wakili: Serikali inaomba mahakama iwaruhusu kuendelea maana hata mashahidi waliopita walisema mambo yaliyofungamana na mambo kama kuzuia kura na mengine hii haitakuwa sawa.

    Baada ya hapo, Jaji Nduguru akamwambia asuburi kwanza.

    Wakili: Walikua wamewakamata watu kwa sababu gani?

    Shahidi: Ilikuwa ni kwa kuchochea na kushawishi watu kufanya maandamano

    Shahidi: Na wakaniambia tayari walikuwa wameshafungua majalada kwa baadhi ya maeneo.

    Shahidi aliomba ruhusa atoke akajisitiri na majaji wakamruhusu

    Kesi hii itaendelea kusikilizwa mwendo wa saa nane.

    Mbali na Shitaka la uhaini Tundu Lissu anatuhumiwa kwa kuchapisha taarifa za uongo kuhusu kuharibiwa kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024, kutumika kwa Polisi kuiba kura na Majaji kutotenda haki kwa kuwa ni wateule wa Rais.

    Tundu Lissu alikamatwa tarehe Aprili 9, 2025 huko Mbinga, mkoani Ruvuma, alipokuwa akiongoza mkutano wa kisiasa. Alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mnamo Aprili 10, 2025, akikabiliwa na shtaka la uhaini kutokana na kauli zake za kushinikiza mageuzi na kuzuia Uchaguzi Mkuu.

  6. Lissu: "Sikuwaambia watu wachome na kuchana kura"

    Shahidi: Baada ya kutazama ile video tulibaini kulikuwa na kulikuwa na kosa kutokana na maneno mengi aliyotamka ila kwa kesi hii naomba nirejee machache “Wanasema kitu kimoja sahihi hapa, msimamo huu unaashiria uasi… akaendelea kusema ni kweli kwa sababu tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko kwa sababu tunaenda kukinukisha sana huu uchaguzi tutauvuruga kwa sababu tunaenda kukinukisha vibaya sana” Mwisho wa kunukuu

    Wakili: "Sasa shahidi embu iambie Mahakama haya maneno baada ya kuyasikia ilipata tafsiri gani?

    Shahidi: "Kwa mujibu wa yale maneno aliyoyasema mimi pamoja na timu yangu ndipo tuliona mshitakiwa Tundu Antipass Lissu alikuwa na nia ya kuitisha serikali ili ifanye anayotaka, kitendo cha kuitisha serikali kwa kuzuia uchaguzi na kuhamasisha uasi ndio uhaini wenyewe huo

    Wakili: "Unasema uhaini kwa mujibu wa kifungu gani Shahidi Hilo kosa lipo kwa mujibu wa kifungu ….. Kwa mujibu wa uchunguzi wetu tuliofanya tulibaini Tundu Lissu alikuwa akihutubia raia na kwa kuwa ni Raia wa Tanzania anawajibu wa utii kwa Jamhuri ya Muungano, serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

    Wakili: "Hayo maneno yalikuaje ya kitisho kwa serikali embu waambie majaji

    Shahidi: "Mshitakiwa alipotamka yale maneno yanaviashiria vikubwa vya uvunjifu wa amani na kutamka yale maneno ni kuitishia serikali kwa uwazi"

    Wakali: "Alafu'

    Shahidi: "Aliidhirishia serikali nia yake kwa kuchapisha maneno hayo kwemye mtandao wa youtube wa Jambo TV"

    Wakili: "Kingine mlichokiona cha kuigusa serikali ambayo ni wajibu wake kulinda amani'

    Shahidi: "Uchaguzi ulizungumziwa ni uchaguzi wa wabunge madiwani na Rais na uchaguzi upo kwa mujibu wa katiba"

    Wakili: "Waambie majaji ni nani mwenye jukumu la kulinda nchi"

    Shahidi: "Ni wajibu wa serikali"

    Wakili: "Na nini ambaye anachukua hatua sheria pale inapokuwa imevunjwa"

    Shahidi: "Ni serikali"

    Wakili: "Unapotishia kuvunja amani nani anaathirika"

    Shahidi: "Anayeathirika unapotishia kuvuruga uchaguzi ni ule muhimili mmoja wa serikali ambao ndio unajukumu la kusimamia na kutekeleza sheria ndani ya nchi"

    Wakili: "Tuambia kama uliwahi kufanya uchunguzi juu ya haya maneno ulifahamu uchaguzi ungevurugwa vipi"

    Shahidi: Katika upelelezi wetu tulioufanya hayo maneno ya kukinukisha yalilenga kufanyika kwa matendo ambayo yangezuia uchaguzi usifanyike

    Lissu anazungumza: "Waheshimiwa majaji ninapinga aina hii ya uhojigi wa shahidi mimi ni mshaitakiwa wa uhaini sikuwaambia watu wachome na kuchana kura haya maneno wanaokoteza na wanayaleta kwa mlango wa nyuma na sikubaliani nao"

    Majaji wanajalili kidogo…….. Minong'ono Mahakamani…….

    Wakili: "Waheshimiwa Majaji ushahidi unapimwa na Mahakama, na hazuiwi kusema huyu ni mpelelezi sasa anazuiwa vipi asiseme walichokibaini na huu sio ushahidi mpya mashahdi wengine walisema pia uchaguzi ungezuiwa vipi kumzuia kusema sio sawa na Mahakama hii nina amini inatenda haki

    Majaji wanajadili kidogo......

  7. M23 yakataa kuwapokea wafungwa sita katika makabidhiano DRC

    Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wamekataa kuwapokea wafungwa sita kati ya 15 waliokabidhiwa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, katika mchakato wa kubadilishana wafungwa unaosimamiwa na Qatar.

    Kwa mujibu wa M23, wafungwa hao sita hawakuwa katika orodha ya watu wanaopaswa kushirikishwa katika makubaliano hayo.

    Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, ilisaidia kuwaachilia na kuwahamisha wafungwa hao kati ya tarehe 6 na 7 Agosti.

    Waliondoka katika mji wa Beni, wakapitia Uganda na kuelekea Bunagana, mji unaodhibitiwa na M23 katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

    Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, amesema kati ya watu 15 waliokabidhiwa, ni tisa pekee waliokuwa katika orodha ya wafungwa 768 iliyowasilishwa na kundi hilo kwa wapatanishi mwaka 2025.

    Amesema mmoja ni raia wa Uganda ambaye hana uhusiano na M23, huku wengine watano wakiwa hawapo katika orodha hiyo.

    Makabidhiano hayo ni sehemu ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa yaliyofikiwa Septemba 2025, ambapo serikali ya DRC ilikubali kuwaachilia wafungwa 311 wa M23, huku waasi wakikubali kuwaachilia watu 166 wenye uhusiano na serikali.

    Hata hivyo, muda wa makubaliano hayo wa Aprili ulipita bila kubadilishana wafungwa.

    M23 imesema bado iko tayari kuwaachilia wafungwa wake 166.

    Haya ndiyo makabidhiano ya kwanza yaliyothibitishwa ya wafungwa kwenda kwa M23 tangu kundi hilo lilipoteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa DRC, mwanzoni mwa mwaka 2025.

    Pia Soma:

  8. Shahidi kesi ya Lissu - 1: "Tulizama video (ya Lissu) kwa masaa mawili"

    Shahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CHADEMA, Amini Mahamba Kamishna Msaidizi wa Polisi anatoa ushahidi wake akiongozwa na wakili wa Serikali.

    "Nilipokea taarifa na nikaanza safari kuelekea ofisi za mkuu wa upelelezi kanda maalumu ya DSM ZCO baada ya kufika nilikutana na maofisa wengine kisha nikakaribishwa ofisini na kupewa mrejesho juu ya walipofikia yeye na timu yake ya upelelezi"

    "Na kwemye Jalada niliona jina la mshitakiwa ambayae yuko mbele yetu ambaye ni Tundu Antipas Lissu. Baada ya hatua hizo niliwapangia majukumu, kupeleleza, kukusanya taarifa kuhoji"

    Wakili wa Serikali: "Wewe unasema ndio ulisimamia upelelezi kwenye hizo timu kama unakumbuka kulikuwa na nani na nani"

    Shahidi Mahamba: "Timu ya ukamataji, Mkaguzi wa polisi msaidizi Michael ndio alikuwa kiongozi wao ……. Inspekta Nunu na wengine. Shahidi anaendelea kuwataja kwa majina

    "Baada ya kupanga majukumu mimi na ile timu tulitazama ile video picha mjongeo toka akaunti ya youtube ya Jambo TV".

    Wakili Mahamba: "Waambie majaji ni video gani hiyo"

    Shahidi: "Ilikua ni video ya Tundu Lissu akihutubia"

    Wakili: "Mliweza vipi kuiangalia".

    Shahidi: "Tukiwa pale ofisini kuna kompyuta maalumu ambayo anaitumia iInspecta Michael ndio tuliitumia kuangalizia hiyo video"

    Wakali: "Mahakama inataka kujua mliitazama kwa kiwango gani?

    Shahidi: "Tuliitazama kuanzia mwanzo mpaka mwisho, hiyo video ilikua ndefu na tulitazama kwa masaa mawili na zaidi"

    Wakali: "Katika hiyo video ulimwona nani"

    Shahidi: "Nilimuona Tundu Lissu na alikua amevaa vazi rasmi la chama la rangi ya kaki akiwa amesimama kwemye mimbari akitoa hotuba na kulikuwa na bendera ya chama na nyuma bendera kama ya taifa"

    Wakili: Iambie Mahakama rangi za bendera ya taifa ni zipi"

    Shahidi: "Rangi za bendera ya taifa ni bluu, njano kijani na nyeusi"

    Wakili: Haya rangi za bendera ya chadema ni zipi"

    Shahidi: "Kuna nyeupe, blue bahari nyekundu na nyeusi"

    Wakili: "Tuambie kipi kingine uliona

    Shahidi: "Pia alikuwa amevaa miwani na alikua akihutubia umma

    Wakili: "Unaweza ukaimbia Mahakama lugha aliyokua akitumia mshitakiwa

    Shahidi: "Lugha iliyokua ikitumika ni lugha yetu ya taifa kiswahili"

    Wakili: "Wewe ulikua ukiratibu zoezi zima la upeleleze ulipata nini kwemye hiyo video kilichoonesha hapa kinafungamana na jalada lilokuwa mbele yenu".

  9. Makaburi ya pamoja yenye miili ya raia 25 yagunduliwa Sudan

    Makaburi ya pamoja yenye miili ya raia 25 waliouawa na wanamgambo wa RSF, yamegunduliwa katika mji wa Kurmuk, jimboni Blue Nile, kusini mashariki mwa Sudan.

    Kwa mujibu wa Sudan Tribune, taarifa hizo zimetolewa na kamishna wa Kurmuk, Abdel Aty Mohamed al Faki.

    Jeshi la Sudan lilitwaa tena udhibiti wa Kurmuk tarehe 8 Julai, baada ya mji huo kutekwa na RSF mwezi Machi katika operesheni iliyofanywa kwa pamoja na kundi la waasi la Sudan People’s Liberation Movement Army North, SPLM A N, kutoka mpakani mwa Ethiopia.

    Al Faki amesema makaburi hayo yaligunduliwa wakati jeshi lilipokuwa likifanya msako katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa mji huo, zaidi ya mwezi mmoja baada ya RSF kuondolewa.

    Amesema waathiriwa walinyongwa karibu na Jebel Fankat, kilima ambacho RSF ilikitumia kurusha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani wakati wa kuuteka mji huo.

    Kurmuk imekuwa moja ya maeneo yenye migogoro mikubwa nchini Sudan na imekuwa ikibadilisha udhibiti kati ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi katika vita vya sasa na vya zamani.

    Mashirika yanayofuatilia haki za binadamu yamekuwa yakiishutumu RSF kwa kutekeleza ukatili mkubwa wakati wa udhibiti wake wa Kurmuk na maeneo ya jirani, ikiwemo mauaji yasiyo ya kisheria, uporaji na kuwalazimisha raia kuyahama makazi yao.

    Soma Zaidi:

  10. Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu yaendelea baada ya kusimama kwa miezi 5

    Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amefikishwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo, Agosti 10, 2026, kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili.

    Kesi hiyo imeanza tena baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano tangu Februari 24, 2026.

    Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalohusishwa na kauli alizotoa kuhusu kusudio la kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

    Kesi hiyo inasikilizwa kwa mfululizo kuanzia leo hadi Septemba 7, 2026, chini ya Jopo la Majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

    Vikao vya maandalizi ya uendeshaji wa kesi hiyo vilifanyika kuanzia Agosti 5, 2026, vikihusisha Mahakama, upande wa Jamhuri, mshitakiwa Tundu Lissu pamoja na mawakili wake.

    Kwa sasa, kesi hiyo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi.

    Baadhi ya mashahidi, wakiwemo askari polisi na mashahidi wasiokuwa askari ambao ni mashahidi wanaolindwa, tayari wametoa ushahidi wao.

    Lissu amekuwa akishikiliwa gerezani tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025, na kushtakiwa siku iliyofuata kwa makosa ya uhaini na uchochezi.

  11. Uganda yaanzisha msako dhidi ya magari aina ya Subaru yanayotoa kelele

    Polisi nchini Uganda wameanzisha msako dhidi ya madereva wa magari aina ya Subaru yaliyofanyiwa marekebisho ya mfumo wa kutolea moshi na kutoa milio mikubwa.

    Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia malalamiko ya wakazi wa Lugazi kuhusu kelele zinazotokana na magari hayo, hasa nyakati za usiku.

    Polisi katika Manispaa ya Lugazi, wilayani Buikwe, wamemkamata dereva mmoja anayekabiliwa na tuhuma za kusababisha uchafuzi wa mazingira kwa kelele.

    Dereva huyo alikamatwa Jumamosi akiwa anaendesha Subaru yenye mfumo wa kutolea moshi uliorekebishwa, na gari hilo limezuiliwa na polisi.

    Msako huo unalenga kukabiliana na magari yanayotoa kelele kupita kiasi na kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za usalama na utulivu wa jamii.

  12. Uganda na Tanzania zakubaliana kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati kikanda

    Uganda na Tanzania zimezindua ushirikiano mpya wa nishati unaolenga kuifanya bandari ya Tanga kuwa kitovu muhimu cha nishati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Mpango huo unatarajiwa kuvutia uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 20, huku ukiwa na mpango wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta pamoja na miundombinu mingine ya nishati.

    Makubaliano hayo yamesainiwa kati ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta Uganda, UNOC, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, TPDC, pamoja na kampuni ya Vitol Bahrain EC.

    Mpango huo utaweka msingi wa ushoroba jumuishi wa nishati itakayounganisha Uganda na Tanzania kupitia mabomba ya kusafirisha bidhaa mbalimbali za mafuta, pamoja na miundombinu ya mafuta na gesi na vituo vya kuhifadhi nishati.

    Uganda na Tanzania zinasema ushirikiano huo unaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya mafuta na nishati katika Afrika Mashariki, huku Bandari ya Tanga ikitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mnyororo huo wa nishati.

    Haya yanajiri baada ya tajiri mkubwa barani Afrika Aliko Dangote kuchagua bandari ya lamu kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta, badala ya Tanzania kama ilivyokuwa imependekezwa.

  13. Mahakama ya Afrika Mashariki yaipa Uganda siku 45 kujibu kesi ya mateso kwa washukiwa

    Mahakama ya Afrika Mashariki ya Haki, EACJ, imeipa serikali ya Uganda siku 45 kuwasilisha majibu yake katika kesi inayopinga uamuzi wa Mahakama ya Katiba kuhusu ulinzi wa washukiwa wa uhalifu dhidi ya mateso.

    Kesi hiyo imewasilishwa na Chama cha Wanasheria Uganda, ULS, kikidai kuwa uamuzi wa Mahakama ya Katiba unadhoofisha ulinzi wa kisheria dhidi ya mateso kwa watu wanaoshukiwa kutenda uhalifu.

    Mahakama hiyo yenye makao yake Arusha, Tanzania, imeagiza Mwanasheria Mkuu wa Uganda kuwasilisha majibu ya serikali ndani ya siku 45.

    Mahakama imeonya kuwa iwapo serikali ya Uganda haitawasilisha majibu ndani ya muda huo, kesi inaweza kuendelea kusikilizwa na kuamuliwa bila majibu yake.

    Hatua hiyo inafungua njia kwa Mahakama ya Afrika Mashariki kuchunguza iwapo uamuzi unaolalamikiwa unaendana na wajibu wa Uganda wa kulinda haki za binadamu na kuzuia vitendo vya mateso dhidi ya washukiwa wa uhalifu.

  14. Wanajeshi 50,000 wa Korea Kaskazini wanatarajiwa kupelekwa Urusi - Zelensky

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema hadi wanajeshi 50,000 wa Korea Kaskazini wanaweza kupelekwa nchini Urusi kusaidia katika vita dhidi ya Ukraine.

    Zelenskyy amesema idadi hiyo ni ongezeko kutoka makadirio ya awali ya wanajeshi 30,000, huku akionya kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Moscow na Pyongyang unaendelea kuimarika.

    Amesema Ukraine imegundua makombora ya Korea Kaskazini katika ardhi yake na kwamba Pyongyang inaendelea kupata uzoefu wa vita vya kisasa pamoja na teknolojia na zana za kijeshi kutoka Urusi.

    Kwa mujibu wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine, kikosi cha makombora cha Korea Kaskazini kimeanza kupeleka wanajeshi na vifaa magharibi mwa Urusi. Kikosi hicho kinaweza kuwa na makombora 120 ya balistiki na vifaa sita vya kurushia makombora.

    Korea Kaskazini tayari ilipeleka takriban wanajeshi 14,000 katika eneo la Kursk nchini Urusi mwaka 2024, kusaidia vikosi vya Urusi katika mapigano dhidi ya Ukraine.

    Kutokana na kuongezeka kwa ushirikiano huo, Zelenskyy ameiomba Korea Kusini kuisaidia Ukraine kwa mifumo ya ulinzi wa anga, ambako Kyiv inakabiliwa na upungufu mkubwa wa silaha za kuzuia mashambulizi ya makombora ya balistiki.

    Wakati huo huo, mashambulizi ya Urusi yameendelea kulenga miji na miundombinu ya Ukraine, huku ripoti za hivi karibuni zikieleza kuwa raia wameuawa na wengine kujeruhiwa katika maeneo mbalimbali.

    Zelenskyy pia amewataka washirika wa Ukraine kuongeza msaada wa ulinzi wa anga, akisema uwezo huo ni muhimu katika kukabiliana na kuongezeka kwa mashambulizi ya makombora ya Urusi.

    Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Wes Streeting amezitaka nchi washirika kuongeza msaada wa mifumo ya ulinzi wa anga kwa Ukraine kabla ya majira ya baridi, akisema Rais Vladimir Putin anaweza kutumia msimu huo kama silaha dhidi ya Kyiv.

    Naye Papa Leo ametoa wito wa kusitishwa kwa vita kati ya Urusi na Ukraine, akisema idadi ya raia wanaouawa na kujeruhiwa, wakiwemo watoto, inaongezeka.

    Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake ukisema zaidi ya raia 16,000 wameuawa tangu kuanza kwa vita, huku wengi wao wakiwa raia wa Ukraine.

  15. Iran yamteua kiongozi mpya wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa

    Iran imemteua kiongozi mpya wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, katika mabadiliko muhimu ya uongozi wakati nchi hiyo ikikabiliana na mzozo kati yake, Marekani na Israel.

    Mohsen Rezaei, kamanda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameteuliwa kushika wadhifa huo wenye jukumu muhimu katika kuamua namna Iran itakavyokabiliana na mzozo huo.

    Rezaei amewahi kusema Iran inapaswa kudumisha udhibiti wa Mlango wa Hormuz, akisema hilo ni muhimu zaidi kuliko kumiliki silaha za nyuklia.

    Kwa kuzingatia historia yake ndefu ya kushika nyadhifa za juu serikalini, uteuzi wake unaonekana kuashiria kuwa kizazi cha zamani cha wanasiasa wa Iran bado kinaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika uongozi wa nchi hiyo.

    Hata hivyo, kumekuwa na utabiri kwamba wanasiasa vijana wanaweza kuanza kupewa nyadhifa za juu katika uongozi wa Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  16. CENTCOM yafichua meli zilizozuiwa tangu kuanza kwa vikwazo vya Marekani

    Kamandi Kuu ya Marekani CENTCOM, inayosimamia operesheni za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati, imesema tangu kuanza kwa zuio la baharini dhidi ya Iran, imezuia meli 55 za kibiashara na kusimamisha meli mbili kwa kutumia mashambulizi ya risasi.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, CENTCOM imesema zaidi ya meli 20 za kivita za Marekani zinafanya shughuli katika Mashariki ya Kati kuunga mkono operesheni za kijeshi, ikiwemo utekelezaji na ufuatiliaji wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

    CENTCOM pia imesema vikosi vya Marekani viliingia na kukagua meli mbili wakati wa utekelezaji wa zuio hilo la baharini.

  17. Trump: Iran imekuwa na utovu wa nidhamu kwa miaka 51

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran imekuwa na utovu wa nidhamu kwa miaka 51.

    Trump amesema hayo katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, akidai Iran imeiongoza dunia katika kile alichokiita tabia mbaya kwa kipindi cha miaka 51.

    Trump pia alichapisha picha inayoonyesha kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya Iran, rial, tangu mwanzoni mwa mwaka 2025 hadi sasa.

    Akiambatanisha picha hiyo, Trump amesema, “Iran haina pesa,” na kuongeza, “fedha yao haina thamani.”

    Soma Pia:

  18. Trump akanusha Marekani kuishiwa silaha za kivita

    Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa kwamba Marekani imepungukiwa na silaha na risasi, akisema nchi hiyo ina akiba kubwa ya silaha na kwamba nyingine zinaendelea kutengenezwa.

    Trump pia ameonya kuwa watu wanaoshukiwa kuvujisha taarifa za siri za serikali wataadhibiwa vikali.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye X Alhamisi, Trump amesema Marekani ina “idadi kubwa ya silaha na risasi”, hasa za aina fulani, huku akisema uzalishaji wa silaha hizo unaendelea na zinatumwa pale zinapohitajika.

    Trump na Wizara ya Ulinzi ya Marekani wanakabiliwa na maswali kuhusu hali ya akiba ya silaha nchini humo, huku vita vikiingia mwezi wa sita na makubaliano ya amani yakitarajiwa kuchukua muda kufikiwa.

    Kwa upande mwingine, Iran imesema silaha zinazozalishwa nchini humo zinaiwezesha kukabiliana na “tishio lolote”.

    Waziri wa Ulinzi wa Iran, Majid Ibn Reza, amesema dalili za kupungua kwa uwezo wa adui zinaendelea kuonekana kila siku, huku akisisitiza kuwa majeshi ya Iran yako tayari kukabiliana na hatari yoyote.

    Amesema teknolojia inayozalishwa nchini Iran ni bora kuliko teknolojia nyingine yoyote ya kijeshi katika eneo hilo.

    Taarifa hiyo inafuatia mashambulizi makubwa ya makombora yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Iran katika operesheni iliyopewa jina Epic Fury, pamoja na mashambulizi mengine ya kijeshi.

    Kwa mujibu wa CBS News, mshirika wa BBC, Marekani imetumia sehemu kubwa ya akiba yake ya kimataifa ya makombora ya masafa marefu na makombora yanayoongozwa kwa usahihi. Taarifa hiyo ilinukuu vyanzo viwili vinavyofahamu hali hiyo, vilivyozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina.

    Soma zaidi:

  19. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 9/08/2026.