Netanyahu kuukataa mpango wa Trump wa vipengele 15 kuhusu Gaza huenda si kauli ya mwisho

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huenda amekataa kabisa mpango mpya wa Bodi ya Amani ya kuwapokonya silaha Hamas huko Gaza, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba hilo halitakuwa neno la mwisho.
Ikulu ya Marekani, White House, haijatoa maoni rasmi. Hata hivyo, inaripotiwa kuwa Marekani “haijasumbuliwa” na kauli ya Netanyahu na inaiona kama kauli ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wenye ushindani mkubwa.
“Tunaelewa mahitaji ya kisiasa ya Bibi,” mwanahabari wa Israel Barak Ravid anamnukuu afisa mwandamizi wa Marekani akisema, akitumia jina la utani la Netanyahu. “Hatuna tatizo na hilo mradi tu anaendelea kufanya kile tunachomtaka, hasa kuhusu kuzuia mashambulizi huko Gaza.”
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na kusitishwa kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, angalau kwa kiwango fulani, jambo ambalo Hamas ililitaka wakati ilipokubali mpango wa vipengele 15 unaoungwa mkono na Marekani.
Pia kuna dalili nyingine kwamba Israel iko tayari kuendeleza mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa Gaza, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kupelekwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Utulivu (ISF). Kikosi hicho kinaundwa na wanajeshi kutoka nchi mbalimbali, na mpango ni kwamba watashirikiana na kikosi kipya cha polisi wa Palestina katika kuhakikisha usalama wa eneo hilo.
Ujenzi wa kituo cha kwanza cha ISF bado unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu, miongoni mwa magofu ya Rafah, kusini mwa Gaza, kwa mujibu wa redio ya umma ya Israel, Kan News. Hatua hiyo itawezesha hatimaye kuanza kwa ujenzi upya wa eneo hilo.





































