Moja kwa moja, Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi Marekani ikubali masharti sita - Iran

Kauli hiyo inakuja wakati Iran na Oman zikisema mazungumzo kuhusu utaratibu mpya wa kuruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz yamekuwa ya “chanya na yenye kujenga” katika siku za hivi karibuni.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Wahouthi washambulia kiwanda cha kusafisha mafuta Saudi Arabia

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waasi wa Houthi nchini Yemen wamesema wamefanya shambulizi la ndege zisizo na rubani dhidi ya kiwanda cha kusafisha mafuta cha Saudi Arabia, kilichoko katika pwani ya Bahari Nyekundu.

    Msemaji wa kijeshi wa kundi hilo, Yahya Saree, amesema shambulizi dhidi ya kiwanda cha Aramco mjini Jazan lilikuwa kulipiza kisasi dhidi ya kile alichokiita uvamizi wa Saudi Arabia kaskazini magharibi mwa Yemen.

    Wizara ya Nishati ya Saudi Arabia imesema wazima moto wamefanikiwa kuzima moto uliozuka katika eneo la kiwanda hicho.

    Waasi wa Houthi walitangaza mwezi uliopita kuanzishwa kwa kizuizi cha majini dhidi ya Saudi Arabia, hatua iliyochochea tena mzozo kati ya pande hizo na kuongeza shinikizo katika usambazaji wa nishati duniani, ambao tayari umeathiriwa na vita vya Iran.

    Wakati huo huo, chombo cha juu cha usalama nchini Iran kimeonya kuwa Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi Marekani ikubali masharti sita, yakiwemo kulegeza vikwazo dhidi ya Iran, kulipa fidia kwa uharibifu uliosababishwa na vita na kuondoa kizuizi kilichowekwa katika bandari za Iran.

  2. Samia ataka ushirikiano zaidi kati ya Serikali na sekta binafsi kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050

    d

    Chanzo cha picha, Ikulu

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema ushirikiano mkubwa kati ya Serikali na sekta binafsi utakuwa muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

    Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuvutia uwekezaji, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuongeza uwekezaji, kuunda ajira na kuchochea ubunifu.

    Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa zana za utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 na mazungumzo maalumu na viongozi wa sekta binafsi katika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia amesema Serikali na sekta binafsi lazima zishirikiane kama washirika walio sawa ili kufikia malengo ya dira hiyo.

    Zana nne muhimu za utekelezaji zilizozinduliwa ni Mpango wa Taifa wa Muda Mrefu, Mpango wa Nne wa Miaka Mitano wa Maendeleo, mfumo wa kitaifa wa kutathmini matokeo na utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa sekta za umma na binafsi, pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wa Dira ya Maendeleo 2050.

    Akitumia mfano wa ufunguo uliowasilishwa katika hafla hiyo, Rais Samia amesema Serikali inashikilia sehemu moja ya ufunguo huo huku sekta binafsi ikiwa na sehemu inayofungua mlango, akisisitiza kuwa pande zote mbili lazima zishirikiane ili kutimiza malengo ya dira hiyo.

    “Tayari tumezindua zana zinazohitajika kutekeleza Dira ya 2050. Kinachobaki ni sisi sote, Serikali na sekta binafsi, kuzitekeleza kwa pamoja,” amesema.

    Rais Samia amesema Serikali inalenga kuimarisha uhusiano kati ya biashara kubwa na ndogo, biashara rasmi na zisizo rasmi, pamoja na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi kwa upana.

    Amesema uwekezaji unapaswa pia kujenga ujuzi wa ndani na kutoa fursa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika mnyororo wa thamani.

    Rais Samia amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa biashara kuimarisha kampuni za Kitanzania na kuzisaidia kupanua shughuli zao katika masoko ya kikanda na kimataifa.

    “Tungependa kuona kampuni nyingi zaidi za Kitanzania zikiwekeza barani Afrika. Serikali itaendelea kuweka mazingira na kutoa fursa zitakazoiwezesha sekta binafsi kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa,” amesema.

    Amezitaka kampuni binafsi kuunga mkono uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya reli na korido za usafirishaji kwa kuwekeza katika huduma za usafirishaji, uhifadhi na minyororo ya ugavi ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini kwenda katika masoko ya Afrika.

    Rais Samia pia amesema mazingira ya ufadhili duniani yanabadilika, huku mikopo yenye masharti nafuu na misaada ya maendeleo ikipungua. Amesema hali hiyo inafanya ukusanyaji wa rasilimali za ndani na uwekezaji wa sekta binafsi kuwa muhimu zaidi.

    Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 ulianza rasmi Julai 1 mwaka huu, huku sekta binafsi ikitarajiwa kutekeleza takriban asilimia 70 ya ajenda hiyo katika juhudi za kujenga uchumi wa kipato cha juu cha kati ulio mseto, imara, shirikishi na wenye ushindani.

    Rais Samia amesema Tanzania inapaswa kuongeza uzalishaji, kukuza mauzo ya bidhaa nje ya nchi, kupunguza uagizaji usio wa lazima na kutumia rasilimali zake kwa ufanisi, nidhamu na uadilifu.

    Pia amekaribisha kutiwa saini kwa Tamko la Pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi, akisema ni ishara ya dhamira ya pamoja ya kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050.

    Amesema mashirika 11 ya biashara na uwekezaji yaliyotia saini tamko hilo yanapaswa kuhakikisha wanachama wao wanafahamu na kutekeleza ahadi zilizomo, huku mazungumzo endelevu na uwajibikaji kati ya Serikali na sekta binafsi vikiwa muhimu katika kufikia malengo ya dira hiyo.

    Rais Samia amesisitiza pia kuwa amani na utulivu ni rasilimali kubwa zaidi za Tanzania katika maendeleo na kuzitaka sekta zote mbili kuzilinda wakati zikishirikiana kubadilisha uchumi wa nchi katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

    Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi amempongeza Rais Samia kwa kuandaa mazungumzo hayo, akisema yameonyesha dhamira ya Serikali ya kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050.

    Dkt Mwinyi amesema utekelezaji wenye ufanisi wa dira hiyo unahitaji uwekezaji mkubwa katika viwanda, uchumi wa buluu, utalii, maendeleo ya rasilimali watu, kilimo cha kisasa, uchumi wa kidijitali na huduma za kifedha.

    Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Muungano kuunganisha vipaumbele vya dira hiyo katika mipango ya maendeleo, huku akizitaka sekta binafsi kuwekeza katika maeneo muhimu, kutumia teknolojia zinazoibuka na kuimarisha ushirikiano utakaosaidia kufikia malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya Tanzania.

  3. Kenya yaweka kikomo cha matumizi ya dola milioni 47.4 kwa kampeni za urais 2027

    d

    Chanzo cha picha, IEBC

    Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya, IEBC, imechapisha kanuni mpya za ufadhili wa kampeni pamoja na viwango vya juu vya matumizi ya fedha, huku wagombea na vyama vya kisiasa wakianza maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

    Katika notisi iliyochapishwa katika Gazeti rasmi la serikali ya Kenya ya tarehe 7 Agosti 2026, IEBC imeweka kikomo cha matumizi ya kampeni za mgombea urais kuwa Sh6.11 bilioni.

    Kwa mujibu wa tume hiyo, viwango hivyo vimeamuliwa kwa kutumia kanuni inayozingatia idadi ya watu na ukubwa wa eneo, ambapo idadi ya watu ina uzito wa asilimia 70 na eneo la ardhi asilimia 30.

    Viwango hivyo vinahusu uchaguzi wa urais, magavana, wabunge wa Bunge la Kitaifa na Wawakilishi wa Kaunti, pamoja na vyama vya kisiasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo.

    IEBC pia imeweka kikomo cha jumla cha matumizi ya vyama vya kisiasa kuwa $189.6 milioni.

    Chini ya kanuni hizo mpya, mtu mmoja au chanzo kimoja hakitaruhusiwa kutoa zaidi ya asilimia 20 ya jumla ya michango inayoruhusiwa kwa mgombea au chama husika.

    Tume imeonya kuwa wagombea au kamati za vyama vya kisiasa zitakazozidisha viwango vilivyowekwa na kushindwa kuripoti ukiukaji huo zitakuwa zimefanya kosa la jinai.

    ''Mtu atakayepatikana na hatia anaweza kutozwa faini ya hadi Sh2 milioni, kifungo cha hadi miaka mitano jela, au adhabu zote mbili'', yasema IEBC.

    IEBC imewataka vyama vya kisiasa, wagombea, timu za kampeni, wafadhili na watu wengine wanaodhibitiwa na sheria hizo kuanza kufahamu mara moja masharti kuhusu michango na matumizi ya kampeni, utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa taarifa na uwajibikaji.

    Soma Zaidi:

  4. Rais wa Ukraine Volodymr Zelenskyy aomba makombora zaidi ya kujihami

    V

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amezitaka tena nchi washirika wa Kyiv kuipatia Ukraine makombora zaidi ya kuzuia mashambulizi, baada ya mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo kushindwa kuzuia kombora lolote la balistiki la Urusi lililorushwa usiku mmoja.

    Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC wa masuala ya kimataifa Sasha Schlichter, Ukraine kwa kawaida hupokea usambazaji wa mara kwa mara wa makombora ya kuzuia mashambulizi kutoka Marekani. Hata hivyo, akiba ya makombora hayo nchini Marekani imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na vita vya Iran, hali inayozifanya miji kama Kyiv kuwa katika hatari zaidi ya mashambulizi ya Urusi.

    Akiwa ziarani Belgrade Jumamosi, Zelenskyy amezishukuru nchi kama Ujerumani na Poland kwa msaada wao, akisema nchi hizo zina akiba ya makombora ya kujihami ambayo zinaweza kuipatia Ukraine.

    Pia ametaja Japan na Korea Kusini, lakini akasema sheria za ndani katika nchi hizo zinazuia kwa urahisi utoaji wa silaha hizo kwa Ukraine.

    Soma Zaidi:

  5. Dangote atangaza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta Lamu kuanza Oktoba 2026

    Aliko Dangote alitengeneza utajiri wake kupitia sukari na saruji

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Aliko Dangote alitengeneza utajiri wake kupitia sukari na saruji

    Bilionea wa Nigeria na mtu tajiri zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, ametangaza kuwa ujenzi wa kiwanda kinachopendekezwa cha kusafisha mafuta Lamu nchini Kenya utaanza ifikapo Oktoba mwaka huu, huku akifichua kuwa makadirio ya gharama ya mradi huo yamepunguzwa kwa takriban dola milioni 15.5.

    Dangote amesema kiwanda hicho kitahudumia Kenya pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki, huku ujenzi wake ukitarajiwa kukamilika ndani ya kipindi kisichozidi miaka minne baada ya kuanza.

    “Maandalizi ya kiwanda hicho yamepiga hatua kubwa nchini Kenya kwa sababu tunachojaribu kufanya ni kuhakikisha kuwa katika nchi nyingi za Afrika zinakuwa na uwezo wa kujitosheleza kwa mahitaji yao ya nishati,” Dangote aliiambia BBC.

    Amesema maandalizi ya ujenzi yamefikia hatua ya juu, huku hafla ya kuanza rasmi kwa mradi huo ikitarajiwa kufanyika kabla au ifikapo Oktoba, hatua itakayoweka msingi wa ujenzi wa kiwanda hicho kikubwa.

    “Ifikapo Oktoba mwaka huu, tutafanya uzinduzi wa ujenzi. Baada ya kuweka msingi, tutaanza ujenzi rasmi,” Dangote amesema.

    Kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku, jambo litakalokifanya kuwa miongoni mwa vituo vikubwa vya kusafisha mafuta vinavyopangwa kujengwa barani Afrika na kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Kenya katika sekta ya mafuta.

    Dangote pia amesema makadirio ya gharama ya mradi huo yamepunguzwa kutoka takriban dola milioni17.05 hadi dola milioni 15.5.

    “Awali tulifikiri utagharimu dola bilioni 17, lakini utagharimu chini ya hapo, takriban dola bilioni 16,” amesema.

    Ameeleza kuwa kupungua kwa gharama kumetokana kwa kiasi fulani na uzoefu walioupata wakati wa kujenga kiwanda cha kampuni yake nchini Nigeria. Amesema mradi wa Kenya utajengwa kwa haraka zaidi na hivyo kupunguza gharama za fedha zinazohitajika kugharamia ujenzi.

    “Utakuwa na gharama ndogo kwa sababu utajengwa kwa haraka zaidi, hivyo gharama za ufadhili zitakuwa ndogo. Pia, kama kampuni, sasa tuna uzoefu zaidi kuliko tulipokuwa tukijenga kile cha Nigeria,” amesema.

    Dangote amesema mradi huo utafadhiliwa kupitia mchanganyiko wa mtaji wa kampuni na mikopo. Kampuni hiyo inapanga kutoa asilimia 30 ya fedha zinazohitajika kupitia mtaji wake na kutafuta asilimia 70 iliyobaki kupitia mikopo.

    Kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa sekta binafsi nchini Kenya na kuunda maelfu ya nafasi za ajira katika ujenzi, uhandisi, usafirishaji na ugavi, uzalishaji, nishati pamoja na sekta nyingine zitakazohudumia mradi huo.

    Soma Zaidi:

  6. JD Vance: Marekani imeharibu mpango wa nyuklia wa Iran

    D

    Chanzo cha picha, Reuters

    Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema Marekani imeharibu mpango wa nyuklia wa Iran, kuangamiza uwezo wake wa kijeshi wa kawaida na kudhoofisha kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kijeshi wa kutumia makundi washirika.

    Vance amesema hayo katika mahojiano na Fox News Jumamosi, akieleza kuwa Washington kwa sasa inatathmini ikiwa Iran iko tayari kufanya mabadiliko ya muda mrefu ambayo yanaweza kuboresha uhusiano kati ya Iran na Marekani.

    Amesema iwapo Iran haitakuwa tayari kufanya mabadiliko hayo, Marekani itaendelea kuongeza shinikizo dhidi ya Tehran.

    Vance pia amesema serikali ya Marekani inalenga kuongeza uzalishaji wa mafuta na gesi katika Mashariki ya Kati ili kupunguza gharama za mafuta na nishati kwa Wamarekani, huku ikiimarisha upatikanaji wa nishati.

    Soma zaidi:

  7. Oman: Mazungumzo kuhusu Hormuz yapiga hatua

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Oman imesema mazungumzo yake na Iran kuhusu makubaliano ya kuhakikisha usalama wa usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz yanaendelea vyema, huku Tehran ikionya kuwa makubaliano hayo hayamaanishi kwamba njia hiyo muhimu ya majini itafunguliwa mara moja.

    Pande zote mbili zimesema Jumamosi kwamba mazungumzo hayo yanaendelea kwa matumaini, ingawa bado haijafahamika ni lini makubaliano yanaweza kufikiwa.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman imeonya kuhusu mashambulizi dhidi ya meli, ambayo yanaweza kuvuruga juhudi hizo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mazungumzo yako katika hatua za mwisho, lakini akasema kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz bado kunategemea masharti mengine.

    Tehran imezuia kwa kiasi kikubwa matumizi ya njia hiyo ya majini, ambayo kwa kawaida hupitisha takriban theluthi moja ya biashara ya mafuta na gesi duniani, tangu Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi mwezi Februari.

    Soma Zaidi:

  8. FIFA yakosoa kampeni ya kutaka Infantino ajiuzulu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    FIFA imekosoa vikali kile ilichokiita juhudi zinazoendelea za kuidhoofisha taasisi hiyo pamoja na rais wake, Gianni Infantino. Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti zilizomuhusisha Infantino na madai kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi, ambayo FIFA imesema ni madai yasiyo na msingi na ya uongo.

    Infantino pia anakabiliwa na shinikizo kutoka UEFA na baadhi ya vyama vya soka barani Ulaya kufuatia mpango wake uliositishwa wa FIFA Forward Enterprise, uliolenga kuanzisha kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na tiketi za FIFA, huku sehemu ya kampuni hiyo ikiuzwa kwa mwekezaji binafsi.

    Rais wa Shirikisho la Soka la Norway, Lise Klaveness, ametaka Infantino ajiuzulu, huku UEFA ikisema bado iko tayari kususia baadhi ya matukio ya FIFA ikiwa haitapewa uhakikisho kwamba mpango huo hautafufuliwa.

    FIFA imemtetea Infantino ikisema alichaguliwa kidemokrasia na vyama wanachama na anaendelea kuhudumu kwa mamlaka waliompa. Shirikisho hilo limeonya kwamba wanaopinga uongozi wake wanapaswa kutumia taratibu rasmi za kidemokrasia za FIFA badala ya madai au taarifa potofu.

    Upinzani dhidi ya Infantino unatoka zaidi Ulaya, huku Mexico, Conmebol na CAF zikimuunga mkono. CAF, inayowakilisha nchi 54 za Afrika, imesema inaunga mkono Infantino kwa kauli moja.

  9. Masharti ya Iran yapunguza matumaini ya kufikiwa haraka kwa makubaliano

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Masharti yaliyotolewa na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohammad Baqer Zolghadr, kwa kiasi kikubwa yanarudia masharti yaliyokuwa sehemu ya makubaliano ya mfumo yaliyofikiwa kati ya Iran na Marekani mwezi Juni. Lakini sasa, Zolghadr ameyawasilisha masharti hayo kama sharti la lazima ili Mlango wa Hormuz urejee kufanya kazi kikamilifu kama kawaida.

    Masharti hayo yanajumuisha kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo dhidi ya Iran, kulipwa fidia kwa uharibifu uliosababishwa na vita, pamoja na kusitishwa mara moja kwa kizuizi cha Marekani dhidi ya bandari za Iran.

    Iwapo kauli hizo zitatumika kama ishara ya msimamo wa sasa wa Tehran, huenda zikapunguza zaidi matumaini ambayo Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ameyaibua kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano na Iran hivi karibuni.

    Wakati huo huo, Iran na Oman zinaendelea na mazungumzo kuhusu njia mpya ya kuruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz. Mpango huo unatarajiwa kusimamiwa kwa pamoja na Iran na Oman, huku nchi hizo zikitoza ada kwa matumizi ya njia hiyo.

    Makubaliano kama hayo, iwapo yatafikiwa, yangefungua sehemu tu ya njia kuelekea suluhisho pana la mzozo huo. Hata hivyo, yanaweza kumpa Donald Trump njia ya kujiondoa katika vita bila kuhitaji kufikia mara moja makubaliano kamili ya kumaliza mzozo.

    tofauti hizo ni za aina gani.

  10. Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi Marekani ikubali masharti sita - Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohammad Bagher Zolghadr, amesema Iran haitafungua tena Mlango wa Hormuz hadi Marekani itakapokubali masharti sita yaliyowekwa na Tehran.

    Masharti hayo yanajumuisha kupunguza vikwazo dhidi ya Iran, kulipa fidia za uharibifu wa vita, kusitisha mara moja kizuizi cha majini dhidi ya bandari za Iran, kuacha vitisho dhidi ya Iran na kuachilia mali za Iran zilizogandishwa. Kauli yake inaashiria msimamo mkali zaidi wa Tehran katika mazungumzo kuhusu ufunguzi wa njia hiyo muhimu ya mafuta.

    Kauli hiyo inakuja wakati Iran na Oman zikisema mazungumzo kuhusu utaratibu mpya wa kuruhusu meli kupita katika Mlango wa Hormuz yamekuwa ya “chanya na yenye kujenga” katika siku za hivi karibuni. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema mazungumzo hayo yako katika hatua za mwisho, lakini amesisitiza kuwa makubaliano hayatamaanisha mlango huo utafunguliwa mara moja, kwa kuwa ufunguzi wake utategemea masharti mengine.

    Ripoti ya Axios siku moja kabla ilisema, ikinukuu mwanadiplomasia kutoka moja ya nchi zinazosaidia upatanishi, kwamba wajumbe wa Iran walikuwa wakisubiri idhini ya mwisho kutoka Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ili kukamilisha makubaliano na Oman pamoja na Marekani. Mwanadiplomasia huyo alisema idhini hiyo ilitarajiwa kutolewa “hivi karibuni”.

    Reuters pia iliripoti, ikimnukuu afisa wa Marekani, kwamba kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo kati ya Iran na Oman na Washington inatarajia makubaliano kufikiwa hivi karibuni.

    Kwa mujibu wa afisa huyo wa Marekani, Washington itaondoa kizuizi dhidi ya bandari za Iran baada ya kutangazwa kwa makubaliano yatakayohakikisha meli za kibiashara zinapita bila kizuizi katika Mlango wa Hormuz. Kauli ya Zolghadr ni muhimu kwa sababu ametoka katika taasisi hiyo hiyo inayotarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kwa upande wa Iran kuhusu makubaliano hayo.

    Wakati huo huo, kuna taarifa kwamba Zolghadr amewasilisha barua ya kujiuzulu kutoka nafasi yake, lakini Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amepinga hatua hiyo na kumuomba aendelee na kazi. Pezeshkian alipoulizwa kuhusu taarifa hizo amesema kuna “tofauti kadhaa” ambazo wanaendelea kujaribu kuzitatua, bila kueleza zaidi tofauti hizo ni za aina gani.

  11. Salaam na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo 09.08.2026