Tanzania yaweka utaratibu wa kufuatwa kabla ya maandamano
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Tanzania, Patrobas Katambi, amefafanua utaratibu wa kisheria unaosimamia maandamano na mikusanyiko ya hadhara, akisisitiza wajibu wa waandaaji kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi angalau saa 48 kabla ya kufanyika kwa shughuli hizo.
Aidha, Katambi amesema utaratibu huo umeainishwa katika Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322, hususan vifungu vya 42, 43, 44, 45 na 46.
Amesema kifungu cha 42 kinaipa Polisi mamlaka ya kusimamia na kuratibu mikusanyiko na maandamano yote yanayofanyika nchini, huku kifungu cha 43 kikielekeza kuwa mtu au waandaaji wanaokusudia kufanya mkusanyiko au maandamano katika maeneo ya umma wanapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi angalau saa 48 kabla ya tukio husika.
Kauli hiyo ya Katambi inakuja kufuatia mjadala ulioibuka kuhusu maagizo yake ya kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya vyama vya siasa.
Kwa sasa, serikali inaeleza kuwa uamuzi wa kusitisha mikutano ya kisiasa unatokana na sababu za kiusalama na juhudi za kuzuia vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza. Wakati huo huo, mitandaoni kumekuwa na miito ya kuitisha maandamano yanayotarajiwa kufanyika Julai 7, 2026.
Oktoba 29, 2025, Tanzania ilishuhudia maandamano yaliyoambatana na vurugu na ghasia katika maeneo mbalimbali, ambapo watu 518 waliripotiwa kupoteza maisha huku maelfu wengine wakijeruhiwa, tukio lililoacha athari kubwa kwa usalama na shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.