Moja kwa moja, Iran yasema haijaalika mataifa yaliyounga mkono mashambulizi dhidi yake
Shughuli za mazishi ya Khamenei zitafanyika kati ya Julai 4 na 8 katika miji ya Tehran, Qom na Mashhad, huku mikutano ya maombolezo pia ikipangwa kufanyika katika miji ya Baghdad, Kazmin, Karbala na Najaf nchini Iraq.
Iran yasema haijaalika mataifa yaliyounga mkono mashambulizi dhidi yake
Chanzo cha picha, Getty Images
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei, amesema kuwa mataifa ya Ulaya yaliyochukua msimamo rasmi wa kuunga mkono mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran hayajaalikwa kuhudhuria mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei.
Hata hivyo, Baghaei amesema ujumbe kutoka baadhi ya mataifa ya Ulaya Mashariki utahudhuria shughuli hizo.
Amesema karibu mataifa 100 yanatarajiwa kutuma ujumbe rasmi, watu mashuhuri au makundi mbalimbali kushiriki katika shughuli za mazishi hayo.
Kwa mujibu wa Baghaei, angalau wakuu wanane wa nchi, wakiwemo marais na mawaziri wakuu, pamoja na maspika wa mabunge kutoka mataifa 12, wamewasili Iran.
Aidha, mawaziri wa mambo ya nje, mawaziri wengine na wawakilishi maalumu kutoka mataifa mengi pia wanashiriki katika shughuli hizo.
Tanzania yaweka utaratibu wa kufuatwa kabla ya maandamano
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Tanzania, Patrobas Katambi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Tanzania, Patrobas Katambi, amefafanua utaratibu wa kisheria unaosimamia maandamano na mikusanyiko ya hadhara, akisisitiza wajibu wa waandaaji kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi angalau saa 48 kabla ya kufanyika kwa shughuli hizo.
Aidha, Katambi amesema utaratibu huo umeainishwa katika Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322, hususan vifungu vya 42, 43, 44, 45 na 46.
Amesema kifungu cha 42 kinaipa Polisi mamlaka ya kusimamia na kuratibu mikusanyiko na maandamano yote yanayofanyika nchini, huku kifungu cha 43 kikielekeza kuwa mtu au waandaaji wanaokusudia kufanya mkusanyiko au maandamano katika maeneo ya umma wanapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi angalau saa 48 kabla ya tukio husika.
Kauli hiyo ya Katambi inakuja kufuatia mjadala ulioibuka kuhusu maagizo yake ya kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya vyama vya siasa.
Kwa sasa, serikali inaeleza kuwa uamuzi wa kusitisha mikutano ya kisiasa unatokana na sababu za kiusalama na juhudi za kuzuia vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza. Wakati huo huo, mitandaoni kumekuwa na miito ya kuitisha maandamano yanayotarajiwa kufanyika Julai 7, 2026.
Oktoba 29, 2025, Tanzania ilishuhudia maandamano yaliyoambatana na vurugu na ghasia katika maeneo mbalimbali, ambapo watu 518 waliripotiwa kupoteza maisha huku maelfu wengine wakijeruhiwa, tukio lililoacha athari kubwa kwa usalama na shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.
Viongozi kutoka mataifa mbalimbali wawasili Iran kuhudhuria mazishi ya Khamenei
Chanzo cha picha, ISNA
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsen Naqvi, amewasili katika mji mkuu wa Iran, Tehran, kuhudhuria mazishi ya Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.
Naqvi alipokelewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Eskandar Momeni.
Pakistan imekuwa ikipatanisha mazungumzo kati ya Iran na Marekani, na Naqvi amezuru Tehran mara kadhaa katika wiki za hivi karibuni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan, Amir Khan Muttaqi, pia amewasili Tehran kwa ajili ya shughuli hizo za mazishi. Jana alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi.
Picha zilizotolewa saa chache zilizopita pia zilimuonyesha He Wei, Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Wananchi la China, akiwasili Tehran kuhudhuria shughuli za leo. Mara baada ya kuwasili, alikutana na Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf.
Maafisa kutoka Turkmenistan, Armenia, eneo la Kurdistan nchini Iraq na mataifa mengine kadhaa pia wamewasili Tehran.
Ujumbe kutoka Vikosi vya Uhamasishaji wa Umma vya Iraq umefika Iran ukiongozwa na Hadi Ameri, mbunge na mmoja wa makamanda wakuu wa kundi hilo.
Iran inatarajia viongozi wa nchi, maspika wa mabunge na mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa kadhaa kuhudhuria mazishi hayo.
Kwa mujibu wa Naibu Msemaji wa serikali ya Taliban, mbali na Waziri wa Mambo ya Nje, kiongozi wa Taliban Abdul Ghani Baradar Akhund pia atahudhuria mazishi hayo.
Vyanzo vimeieleza BBC kuwa ubalozi mdogo wa Iran mjini Herat umetoa zaidi ya visa 2,000 vya bure kwa raia wa Afghanistan wanaotaka kuhudhuria shughuli hizo.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, visa hivyo vya muda mfupi vimetolewa zaidi kwa wanaharakati wa kijamii na kitamaduni wa Afghanistan, wengi wao wakitarajiwa kuingia Iran kupitia Mkoa wa Herat.
Chanzo cha picha, Getty Images
Chanzo cha picha, Getty Images
Majaribio ya dawa zinazoweza kutibu Ebola ya Bundibugyo yaanza
Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuanza kwa majaribio ya kitabibu ya dawa mbili zinazoweza kutibu aina ya virusi vya Ebola vya Bundibugyo, vinavyosababisha mlipuko hatari wa ugonjwa huo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mgonjwa wa kwanza tayari ameanza kushiriki katika majaribio hayo, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa zaidi ya visa 1,400 vya Ebola vimethibitishwa nchini DR Congo, huku watu 438 wakithibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa huo.
Hadi sasa, hakuna chanjo wala dawa iliyoidhinishwa kimataifa kwa ajili ya kutibu aina ya Ebola ya Bundibugyo, ambayo inajulikana kwa kuenea kwa haraka na kuwa na kiwango kikubwa cha vifo.
Majaribio hayo yanaungwa mkono na WHO na yanatekelezwa na watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Umma ya Congo, Taasisi ya Ubelgiji ya Magonjwa ya Tropiki na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.
Akizungumza katika makao makuu ya WHO mjini Geneva, Dkt. Tedros alisema, "Leo tumeanzisha majaribio ya dawa mbili zinazoweza kutibu Ebola, na mgonjwa wa kwanza tayari ameanza kushiriki katika utafiti huo."
Aliongeza, "Ingawa hakuna tiba iliyoidhinishwa kwa sasa, baadhi ya wagonjwa wamepona. Lakini kama tungekuwa na matibabu yaliyothibitishwa kuwa salama na yenye ufanisi, tungeokoa maisha ya watu wengi zaidi."
Mlipuko wa Ebola nchini DR Congo na Uganda ulianza mwezi Mei, na WHO imeutangaza kuwa Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa.
Katika picha: Hali ilivyo katika mahakama ya Rufani kabla ya kesi kuanza
Maelezo ya picha, Baadhi ya wananchi waliojitokeza kusikiliza kesi ya Lissu
Maelezo ya picha, Waliofika mahakamani wakisubiri kesi kuanza
Maelezo ya picha, Mwanasheria wa Serikali Nasorro Katuga (kushoto) akiteta na wanasheria wenzake
Maelezo ya picha, Watendaji mbalimbali wa Mahakama
Lissu afika Mahakama ya Rufani, marejeo ya kesi ya uhaini yasikilizwa leo
Chanzo cha picha, Mwananchi
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, tayari amefika katika Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam ambako mahakama hiyo inatarajiwa kusikiliza maombi ya marejeo yanayohusiana na kesi ya uhaini inayomkabili.
Mahakama hiyo inasikiliza maombi ya marejeo Na. 7440840/2026 katika shauri la Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) dhidi ya Tundu Lissu.
Maombi hayo yanasikilizwa na jopo la majaji watatu linaloundwa na Jaji Mwarija, Jaji Muruke na Jaji Khamis.
Shauri la msingi la kesi ya uhaini lilisimama kwa takriban miezi minne ili kupisha usikilizaji wa rufaa ya Jamhuri iliyopinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali ombi lake la kuwasilisha ushahidi wa nyongeza kupitia shahidi wake, ACP Amini Mahamba.
Lissu alishtakiwa kwa kosa la uhaini mwezi Aprili 2025, miezi mitatu baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA.
Upande wa mashtaka unadai alitoa kauli zilizolenga kuhamasisha wananchi kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mahakama ya Rufani inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu maombi hayo baada ya kusikiliza hoja za pande zote.
Jeneza la Khamenei lapelekwa katika msikiti wa Tehran
Chanzo cha picha, Isna
Jeneza la Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na miili ya baadhi ya wanafamilia wake waliouawa katika shambulio la pamoja la Israel na Marekani la Machi 29, limepelekwa katika msikiti mmoja mjini Tehran.
Shirika la habari la ISNA limesema baadhi ya wageni wa kigeni waliowasili nchini Iran wametoa heshima zao kwa kuhudhuria ibada ya maombolezo mjini Tehran. Shughuli hizo zinatarajiwa kuendelea siku nzima.
Miongoni mwa viongozi waliowasili Tehran kuhudhuria shughuli hizo ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan chini ya utawala wa Taliban, Amir Khan Muttaqi.
Imeelezwa pia kuwa maafisa kutoka Tajikistan, China na India wanatarajiwa kushiriki katika shughuli hizo.
Baadhi ya wanafamilia wa Khamenei, akiwemo mkwe wake, mjukuu wake, mmoja wa mabinti zake na mke wa mwanawe Mojtaba Khamenei, waliuawa pamoja naye katika shambulio hilo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na mamlaka za Iran, shughuli za kuaga na mazishi ya Khamenei zitafanyika kwa hatua kadhaa katika siku mfululizo.
Baada ya shughuli za maombolezo mjini Tehran na baadaye Qom, mazishi yake yanatarajiwa kufanyika mjini Mashhad Alhamisi ijayo. Kabla ya hapo, mwili wake pia unatarajiwa kupelekwa katika miji ya Najaf na Karbala nchini Iraq.
Minyoo 38 yapatikana kwenye ubongo wa mwanamke baada ya kula nyama ya nguruwe India
Chanzo cha picha, Lowri Denman
Laurie Denman aligundua kwa mara ya kwanza kuwa kuna jambo lisilo la kawaida mwilini mwake baada ya kuona minyoo mrefu wa takriban mita moja alipoenda chooni.
"Ilikuwa ya kutisha sana. Ilifanana na utepe wenye mistari midogo midogo," alisema Laurie, mwenye umri wa miaka 42 kutoka Wales.
Hilo lilikuwa ishara ya kwanza ya ugonjwa wa neurocysticercosis, hali iliyosababisha minyoo 38 kupatikana kwenye ubongo wake na kusababisha maumivu makali ya kichwa, degedege na matatizo ya kisaikolojia.
Laurie ni miongoni mwa watu wachache nchini Uingereza waliowahi kugundulika kuwa na maambukizi hayo ya ubongo, yanayosababishwa na mabuu ya minyoo ya nguruwe.
"Daktari aliniambia, tumeangalia picha za uchunguzi wako na tumegundua kuna minyoo 38 kwenye ubongo wako," alisema Laurie.
"Mimi na mama yangu tulitazamana kwa mshangao, tukijiuliza ni kitu gani hiki."
Mwanzoni, madaktari walidhani alikuwa na toxoplasmosis, maambukizi yanayoenezwa kupitia kugusana na kinyesi cha paka aliyeambukizwa.
Hata hivyo, mama yake aliwauliza madaktari kama hali hiyo inaweza kuwa inahusiana na minyoo aliyokuwa ameipata mwaka mmoja uliopita.
Baada ya uchunguzi zaidi, hatimaye aligundulika kuwa na ugonjwa wa neurocysticercosis.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu wanaweza kupata maambukizi hayo kwa kula nyama ya nguruwe mbichi au isiyopikwa vizuri, kunywa maji yaliyochafuliwa na mayai ya minyoo, au kutokana na tabia duni za usafi.
Ugonjwa huo ni nadra sana nchini Uingereza na visa vingi huonekana kwa watu waliotoka katika maeneo ambako ugonjwa huo ni wa kawaida.
Daktari Healy, ambaye alikuwa akimhudumia Laurie, alisema kuwa hiyo ndiyo ilikuwa kisa cha kwanza cha aina hiyo kukiona katika maisha yake yote ya taaluma.
Baada ya miaka kadhaa ya kupona, sasa anataka kutumia uzoefu wake kuhamasisha watu kuhusu ugonjwa huo.
Moto wa nyika wazidi kusambaa kusini mwa Ufaransa, watu 3,000 wahamishwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Moto mkubwa wa nyika unaoendelea kusambaa kusini mwa Ufaransa umesababisha karibu watu 3,000 kuhamishwa kutoka makazi yao, huku mamlaka zikionya kuhusu kuanza mapema kwa msimu wa moto kufuatia wimbi la joto kali lililovunja rekodi.
Kwa mujibu wa vituo vya habari nchini humo, watalii na wakazi wa maeneo ya Sainte Marie la Mer na Canet en Roussillon walilazimika kuondoka baada ya moto kuzuka katika eneo la kambi na kusambaa kwa kasi.
Moto huo umeharibu nyumba kadhaa za muda kabla ya kufika eneo la bandari, ambapo moshi mzito wenye sumu ulitanda juu ya boti na majengo ya karibu.
Kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo, moto mkubwa zaidi umeshuhudiwa katika maeneo ya Aude na Herault, ambapo zaidi ya ekari 900 za ardhi tayari zimeteketea.
Takriban wazima moto 800 na magari 150 ya zimamoto wametumwa kupambana na moto huo, huku juhudi za kuudhibiti zikiendelea.
Kombe la Dunia: Ureno yaibuka na ushindi wa kusisimua dhidi ya Croatia
Chanzo cha picha, Reuters
Timu ya taifa ya Ureno imefuzu kwa hatua inayofuata ya Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2 kwa 1 dhidi ya Croatia katika mchezo uliomalizika kwa tamati ya kusisimua baada ya dakika 18 za nyongeza.
Ivan Perisic aliipa Croatia bao la kuongoza, kabla ya kufunga tena dakika chache baadaye, lakini bao hilo likakataliwa kwa kuotea.
Nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo, aliisawazishia timu yake kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 68 na kuufanya mchezo huo kuingia katika dakika za mwisho ukiwa wazi kwa pande zote.
Gonçalo Ramos aliifungia Ureno bao la ushindi katika dakika ya nne ya muda wa nyongeza.
Hata hivyo, Croatia ilionekana kupata bao la kusawazisha katika sekunde za mwisho za mchezo. Mchezo ulisimamishwa kwa takriban dakika tano ili VAR ipitie tukio hilo, kabla ya kuthibitishwa kuwa mfungaji alikuwa ameotea na bao hilo likakataliwa.
Mashabiki wa Croatia, waliokuwa wakitarajia timu yao kusawazisha na kupeleka mchezo katika muda wa ziada, walishuhudia matumaini yao yakitoweka katika sekunde za mwisho, huku wakionyesha kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi.
Sasa Cristiano Ronaldo ataiongoza tena Ureno katika pambano kubwa dhidi ya Hispania, mataifa mawili jirani yenye historia ndefu na ushindani wa jadi katika soka la kimataifa.
Kabla ya mchezo huo, Hispania iliifunga Austria mabao 3 kwa 0 na kufuzu kwa hatua inayofuata kwa urahisi.
Iran yasema mazishi ya Khamenei yataufanya ulimwengu usikie wito wa kulipiza kisasi
Chanzo cha picha, Getty Images
Spika wa Bunge la Iran na mpatanishi mkuu wa nchi hiyo, Mohammad Baqer Qalibaf, ametoa wito kwa Wairani kushiriki kwa wingi katika mazishi ya Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, akisema ushiriki huo utakuwa sehemu ya kulipiza kisasi kwa kifo chake.
Katika taarifa yake Alhamisi, Qalibaf alisema, "Ninawaomba wananchi wote wa Iran kuandika ukurasa wa kihistoria wa Iran ya Kiislamu kwa kushiriki katika mazishi ya Khamenei."
Aliongeza kuwa, "Wito wa taifa wa kulipiza kisasi lazima usikike duniani kote."
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limesema litachukua hatua za kulipiza kisasi kwa kifo cha Kiongozi Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Katibu wa Baraza hilo, Mohammad Baqer Zolqadr, Iran imesema "kisasi kwa damu ya Ayatollah Ali Khamenei kitachukuliwa dhidi ya waliomuua."
Khamenei aliuawa Februari 28 wakati wa siku ya kwanza ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ametangaza kuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, atashiriki katika shughuli za mazishi ya Khamenei zitakazoanza Jumamosi mjini Tehran.
Kwa mujibu wa BBC Persian, shughuli za mazishi ya Khamenei zitafanyika kati ya Julai 4 na 8 katika miji ya Tehran, Qom na Mashhad, huku mikutano ya maombolezo pia ikipangwa kufanyika katika miji ya Baghdad, Kazmin, Karbala na Najaf nchini Iraq.