Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump atishia kushambulia vikali Iran kwa kupiga kambi ya jeshi la Marekani nchini Jordan
CENTCOM imeyahusisha mashambulizi hayo na vikosi vya ulinzi wa mapinduzi ya Iran IRGC na kuongeza kuwa makombora hayo yalizuiliwa.
Muhtasari
- Muqtada al-Sadr: Msiigeuze Iraq kuwa uwanja wa vita
- Mmoja wa marubani Iran waliouawa katika kambi ya jeshi la Marekani nchini Qatar atambuliwa
- Maafisa watano wa polisi wa Kenya wauawa katika shambulio la Al-Shabaab
- Zaidi ya mitetemeko midogo 100 yatikisa Japan
- Venezuela yakerwa na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya nje wa Iran dhidi yake
- Uchunguzi waanzishwa Kenya baada ya tembo 14 kufa katika njia ya kutatanisha
- Iran yakanusha mpango wa kushirikiana na Oman kudhibiti Mlango wa Bahari wa Hormuz - Reuters
- Maafisa watano wa usalama Kenya wauawa katika shambulizi la Al-Shabaab
- Saudi yaungana na Marekani kushambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran
- Kenya na Uingereza kuanza tena mafunzo ya pamoja ya kijeshi
- Hali Ilivyokuwa wakati tetemeko kubwa la ardhi lilipoikumba Japan
- Ghana yaomboleza kifo cha mwanaume mrefu zaidi nchini humo
- Uamuzi wa mahakama ya DRC wamfungulia njia ya muhula wa tatu Tshisekedi
- Zelensky, Netanyahu wakutana na Trump huku vita vya Ukraine na Iran vikiendelea
- Waliofariki kwa tetemeko la ardhi Japan wafikia 13
- WAFCON 2026: Nigeria wachapwa na Malawi 3-2
- Iran na Marekani zashambuliana tena, utulivu wa muda mfupi wasambaratika
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Ambia Hirsi
Trump atishia kushambulia vikali Iran kwa kupiga kambi ya jeshi la Marekani nchini Jordan
Kituo cha habari cha Fox News kinaripoti kuwa Rais Donald Trump amesema Marekani itaishambulia "vikali" Iran baada ya nchi hiyo kufanya shambulio la makombora dhidi ya kambi zake za kijeshi nchini Jordan.
Trump alinukuliwa na Fox News akisema: "Tutawashambulia vikali. Watajutia hatuo yao,"
Kituo hicho cha habari kioliongeza kuwa rais huyo wa Marekani alitumia lugha kali kusisitiza tishio lake, akisema: "Tutawapiga kabla hawajafanya lolote."
Fox News pia iliripoti, ikimnukuu Bw. Trump, kwamba mashambulio ya pamoja ya anga ya Marekani na Saudi Arabia dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran ndani ya Iraq yalipangwa na maafisa wa Iraq.
Kauli hizi zilizohusishwa na Trump zilitolewa wakati ambapo ofisi ya rais wa Iraq imelaani na kuyataja mashambulio hayo ya Marekani na Saudi Arabia kama "ukiukwaji wa wazi wa mamlaka ya Iraq."
Soma Zaidi Hapa:
Marekani yawekea vikwazo meli nane za mafuta na taasisi 10 zenye uhusiano na Iran
Marekani ilitangaza Jumatano awamu mpya ya vikwazo dhidi ya Iran vinavyolenga meli nane za kubeba mafuta na taasisi 10, kulingana na taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha ya Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sita kati ya taasisi hizo zilizowekewa vikwazo zina makao yake nchini China.
Vikwazo hivi vimewekwa wakati ambapo Marekani imekuwa ikiendelea na hatua yake ya kuzuia usafiri wa majini wa Iran katika maeneo ya bahari kusini mwa nchi hiyo kwa muda sasa.
Kama sehemu ya operesheni hiyo, vikosi vya Marekani vimesimamisha au kubadilisha njia ya meli kadhaa.
Vikwazo hivyo vipya vilitangazwa saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuichukulia hatua kali sana Iran katika mahojiano na kituo cha habari cha Fox News.
Awali, jeshi la Marekani lilisema kuwa lilizuia makombora kadhaa ya balistiki yaliyofyatuliwa na Iran yakilenga vikosi vya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Soma zaidi:
Muqtada al-Sadr: Msiigeuze Iraq kuwa uwanja wa vita
Donald Trump anasema kuwa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Saudi Arabia dhidi ya ngome za Vikosi vya Uhamasishaji wa Umma nchini Iraq yaliratibiwa na serikali ya Baghdad, madai ambayo maafisa wa Iraq wameyakanusha.
Ofisi ya Rais wa Iraq imelaani mashambulizi hayo kama "ukiukwaji wa wazi wa mamlaka ya Iraq," na Muqtada al-Sadr ametoa wito kwa vikosi vya wanajeshi na makundi ya wanamgambo wa Iraq kutoingiza Iraq katika "vita visivyo na msingi."
Vikosi vya Uhamasishaji wa Umma (PMF) vilitangaza kuwa angalau wanachama 20 wa kikosi hicho waliuawa na wengine 32 kujeruhiwa katika mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo.
Vyombo vya habari vilivyo karibu na vyanzo vya kijeshi nchini Iran vimetaja kambi za PMF katika mikoa ya Karbala, Nineveh, Diyala, na Kirkuk kuwa miongoni mwa maeneo yaliyolengwa katika mashambulizi hayo.
Wakati wigo wa migogoro ya kikanda ukipanuka hadi Iraq, kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa Kishia, Muqtada al-Sadr, ametoa wito kwa wanajeshi na makundi ya wanamgambo wa Iraq kutoigeuza Iraq kuwa uwanja wa vita.
Aliandika kwenye mtandao wa X kwamba ikiwa Iraq haikuwa chanzo cha shambulio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, basi Kikosi cha wanajeshi hakipaswi kulenga "ardhi huru na takatifu ya Iraq."
Sadr pia aliwataka wanamgambo wa Iraq kutozipa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kisingizio cha kuishambulia Iraq.
Muqtada al-Sadr alilaani vitendo vya makundi ambayo, alisema, yanajaribu kuingiza Iraq katika "vita visivyo na msingi" na kutoa wito kwa serikali kuimarisha usalama na mamlaka ya nchi hiyo pamoja na kulinda maisha ya watu na maeneo matakatifu.
Mmoja wa marubani Iran waliouawa katika kambi ya jeshi la Marekani nchini Qatar atambuliwa
Jeshi la Iran limetangaza utambulisho wa mmoja wa marubani wanne wanaodaiwa kuuawa katika shambulio dhidi ya kambi ya jeshi la anga la Marekani nchini Qatar zaidi ya miezi minne iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mabaki ya rubani huyo yatarudishwa Iran hivi karibuni.
Taarifa kutoka kwa jeshi la Iran inasema, utambulisho wa Brigedia Jenerali Majid Kazemi—rubani wa mojawapo ya ndege za kivita za Iran aina ya Sukhoi Su-24—ulithibitishwa kupitia vipimo maalum na uchambuzi wa chembechembe za vinasaba DNA.
Jeshi la Iran linadai kuwa ndege hizo za kivita zilisababisha "uharibifu mkubwa katika kambi ya Marekani nchini Qatar" mwezi Machi mwaka jana, siku mbili baada ya kuanza kwa mashambulizi ya pamoja ya Israel na Marekani dhidi ya Iran.
Katika taarifa yake inayoelezea jinsi rubani huyo alivyopoteza maisha, jeshi la Iran liliandika kuwa mnamo tarehe 11 Machi, ndege mbili za kivita aina ya Sukhoi-24 za Jeshi la Anga la Iran, katika operesheni moja, "zilifanikiwa kupenya mifumo ya kisasa ya upelelezi na maeneo mengi ya rada za adui, na kuzishambulia kwa mabomu kambi ya Al-Udeid nchini Qatar.
Hata hivyo, ndege hizo za Iran zilishambuliwa na adui wakati zikirejea kupitia anga ya Ghuba ya Uajemi, na jitihada zinaendelea kubaini hali ya marubani hao shupavu wa ndege hizo za kivita."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya jeshi la Iran, "Jitihada za kubaini hali ya marubani wengine watatu wa ndege hizo mbili za kivita zinaendelea kufanywa na taasisi husika, na mara tu taarifa za kina zitakapopatikana, taarifa zitatolewa."
Maafisa watano wa polisi wa Kenya wauawa katika shambulio la Al-Shabaab
Maafisa wa usalama watano wa Kenya waliuawa siku ya Jumanne baada ya kikosi chao kushambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Al-Shabaab katika Kaunti ya Mandera, karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, polisi walisema.
Maafisa hao walikuwa wakishika doria katika eneo la Bwawa la Wantey walipokutana na watu hao wanaoshukiwa kuwa wapiganaji muda mfupi baada ya saa sita mchana. Kulingana na ripoti ya polisi, maafisa hao waliuawa wakati wa makabiliano ya risasi na wapiganaji hao wa kundi hilo lenye msimamo mkali lenye makao yake nchini Somalia.
"Kikosi cha doria kutoka SOG Alungu kilikutana na wapiganaji wa Al-Shabaab katika eneo la Bwawa la Wantey, takriban kilomita sita kusini mashariki mwa kituo hicho. Wakati wa tukio hilo, maafisa wafuatao walijeruhiwa vibaya na kufariki dunia," ripoti hiyo ilieleza.
Polisi walisema timu iliyotumwa katika eneo hilo baadaye iligonga kilipuzi (IED), ambacho kiliharibu gari lao. Hata hivyo, hakuna majeruhi wengine walioripotiwa.
Maafisa waliouawa ni pamoja na maafisa wanne wa Polisi wa Utawala na mmoja wa Polisi wa Akiba wa Kitaifa.
Idara ya usalama baadaye ilianzisha operesheni ya kuwasaka washambuliaji hao, huku polisi wakisema msako huo bado unaendelea kufikia Jumanne jioni.
Kaunti ya Mandera, ambayo iko kando ya mpaka wa Kenya na Somalia, imekuwa ikilengwa mara kwa mara katika mashambulizi ya mpakani yanayohusishwa na wanamgambo wa Al-Shabaab.
Shambulio hilo linajiri huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya kuvizia na mabomu ya barabarani yanayowalenga maafisa wa usalama katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya, ambapo vikosi vya usalama vinaendelea kupambana na wapiganaji wa Al-Shabaab wanaofanya kazi karibu na mpaka.
Zaidi ya mitetemeko midogo 100 yatikisa Japan
Eneo la Kyushu magharibi mwa Japan imekumbwa na zaidiya mitetemeko 100 tangu lilipokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi lililosababisha vifo vya watu 13.
Wengine wengi wanasemekana kupatikana na ''mshtuko wa moyo'' - neno linalotumiwa kuashiria dalili za awali kabla ya mtu kuthibitishwa kuwa amefariki.
IMaafisa wa uokoaji wanapekua vifusi katika kiwanda na kutengeza karatasi na pia katika jumba la maduka huko Kumamoto kuwatafuta manusura.
Jumba hilo la kibiashara lilikumbwa na mlipuko muda mfupi baada ya tetemeko la hilo la ardhi
Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi ameonya kuwa ''muda unayoyoma'' kuwaokoa wale walionaswa chini ya vifusi. Maelfu ya watu wamepelekwa katika hifadhi ya dharura na mengine yakiwa hayana umeme.
Mamlaka ya Hali ya Hewa la Japan (JMA) limetoa wito kwa wakazi kuwa waangalifu kwani bado kuna mitetemeko mingine midogo inayoendelea baada ya tetemeko kuu.
Venezuela yakerwa na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya nje wa Iran dhidi yake
Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela ilitangaza katika taarifa kwamba ilimwita balozi wa Iran siku ya Jumanne ili kuwasilisha malalamiko yake kuhusu kauli ilizozitaja kuwa za "kudhalilisha na zisizofaa."
Bado haijabainika ni hatua au kauli zipi zitakazojumuishwa katika malalamiko hayo ya Venezuela, lakini hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisema katika mahojiano: "Iran sio Venezuela," jambo linaloashiria kuwa kuitwa kwa balozi wa Iran kunahusiana na muktadha huo.
Mnamo mwezi Januari mwaka jana, vikosi vya Marekani vilimteka nyara Rais Nicolas Maduro nchini Venezuela katika operesheni isiyo na kifani na kumfungulia mashtaka nchini humo.
Uchunguzi waanzishwa Kenya baada ya tembo 14 kufa katika njia ya kutatanisha
Mamlaka nchini Kenya zimeanzisha uchunguzi wa dharura kuhusu vifo vya kutatanisha vya tembo 14 kusini mwa nchi hiyo, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Amboseli.
Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) liliiambia BBC kuwa wataalamu wanachunguza mizoga hiyo na kwamba sampuli za tembo hao zimepelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini ikiwa chanzo cha vifo hivyo kilikuwa ugonjwa, sumu au sababu nyingine.
Hifadhi ya Taifa ya Amboseli na maeneo yanayoizunguka, yanayojulikana kama Mfumo wa Ikolojia wa Amboseli, yanachukua eneo kubwa kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania na yanajulikana kwa utajiri wake wa aina mbalimbali za wanyamapori.
Maafisa wanasema hii ni mara ya kwanza katika miongo kadhaa ambapo idadi kubwa kama hiyo ya vifo vya tembo imerekodiwa katika eneo hilo, ambalo limefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu wa tembo katika miaka ya hivi karibuni.
Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya limesema kuwa "kwa sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa kuna chanzo cha vifo vya tembo hawa."
Pi unaweza kusoma:
Iran yakanusha mpango wa usimamizi wa pamoja wa lango la Hormuz na Oman - Reuters
Afisa wa ngazi ya juu wa Iran amepuuzilia mbali uwezekano wa kubuniwa kwa utaratibu wa nchi hiyo kusimamia lango la Bahari la Hormuz kwa ushirikiano na Oman.
Akizungumza na shirika la habari la Reuters kwa sharti la kutotajwa jina afisa huyo alisema: Mfumo wa udhibiti wa pamoja wa Hormuz hautakuwa na manufaa kwa maslahi ya Iran, ingawa Tehran inaichukulia Oman kama jirani mshirika wa thamani.
Siku ya Jumanne Reuters iliripoti likinukuu maafisa wa eneo hilo, kwamba Oman imewasilisha pendekezo jipya kwa Iran la kuanzisha mfumo wa pamoja wa kikanda unaolenga kusimamia Mlango-bahari wa Hormuz.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pendekezo hilo linahusisha michango ya hiari kutoka kwa nchi zinazoshiriki.
Chanzo kimoja katika eneo hilo, ambacho kiliomba kutotajwa jina, kiliiambia Reuters kuwa mpango huo wa Oman unaungwa mkono na nchi za eneo hilo.
Soma zaidi:
Maafisa watano wa usalama Kenya wauawa katika shambulizi la Al-Shabaab
Maafisa watano wa usalama wa Kenya wameuawa katika mapigano na wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa Al-Shabaab Kaunti ya Mandera, karibu na mpaka wa Somalia, polisi wamesema.
Kundi hilo la wanamgambo limekuwa likipigana kwa miaka kadhaa likitaka kuipindua serikali kuu ya Somalia na kuanzisha utawala wake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, kwa kuzingatia tafsiri yake kali ya sheria za Kiislamu (Sharia).
"Timu ya doria kutoka kikosi cha SOG Alungu ilikutana na wanamgambo wa Al-Shabaab katika eneo la Bwawa la Wantey," polisi walisema katika taarifa yao kufuatia mapigano yaliyotokea Jumanne majira ya saa sita mchana.
Polisi waliongeza kuwa wanaendelea kuwafuatilia wanamgambo hao baada ya kikosi cha nyongeza kilichotumwa eneo hilo kukumbwa na mlipuko wa bomu la kutegwa barabarani, ulioharibu gari la kivita lenye kinga dhidi ya mashambulizi
Hata hivyo, hakuna majeruhi walioripotiwa katika tukio hilo.
Pia unaweza kusoma:
Saudi yaungana na Marekani kushambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran
Saudi Arabia imejiunga na Marekani katika mashambulizi dhidi ya kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq, katika hatua inayoweza kuongeza mvutano wa mzozo wa Mashariki ya Kati.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) ilisema mashambulizi hayo yalilenga "magaidi wanaoungwa mkono na Iran ambao walielekezwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kushambulia majeshi ya Marekani na miundombinu ya nishati ya Saudia".
Taarifa hiyo haikutaja jina la kundi la wanamgambo. Hata hivyo, Popular Mobilisation Forces (PMF) ilisema takriban wanachama wake 10 wameuawa.
Tukio hilo limekuja baada ya Iran kurusha makombora kadhaa ya balistiki katika kile ambacho Centcom ilikitaja kuwa "jaribio la kushambulia kwa kushtukiza" vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati. Mvutano huo unaashiria ukomo wa kifupi cha utulivu katika uhasama kati ya Marekani na Iran.
Marekani ilisema shambulio hilo lilitokea saa 17:45 EDT (21:45 GMT) Jumanne, huku makombora yote yakifanikiwa kuzuiwa. Iran ilisema kuwa ililenga kambi ya Marekani nchini Jordan.
Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) pia kilisema kuwa kilishambulia meli tatu za mafuta katika Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim.
Soma Zaidi Hapa:
Kenya na Uingereza kuanza tena mafunzo ya pamoja ya kijeshi
Serikali ya Kenya imetangaza kuanza tena kwa mafunzo ya pamoja ya kijeshi kati ya Kenya na Uingereza katika Kituo cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) kilichopo Nanyuki, siku chache baada ya kuwepo kwa sintofahamu kuhusu kusitishwa kwa zoezi hilo.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Julai 28, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alisema hatua hiyo inaonyesha uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili, unaojengwa kwa kuheshimiana na kushirikiana kwa njia yenye tija.
Mudavadi alisema uamuzi huo unaonyesha kuwa nchi hizo mbili zina uwezo wa kutatua changamoto kupitia mazungumzo huku zikiendelea kudumisha ushirikiano wao wa kimkakati.
"Ushirikiano wa ulinzi kati ya Kenya na Uingereza unaendelea kuimarisha maslahi ya kitaifa ya Kenya. Unaongeza uwezo wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya (KDF), unachangia amani na usalama katika eneo hili, unaunga mkono ajira na biashara za Wakenya, na unaleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa jamii wenyeji," alisema.
Mudavadi aliongeza kuwa Kenya itaendelea kujikita katika kuimarisha ushirikiano wa ulinzi na Uingereza pamoja na kuendeleza juhudi za pamoja za kukuza amani, usalama na utulivu katika eneo la Afrika Mashariki.
Awali, Uingereza ilitoa taarifa ikisema imehamisha shughuli zake za kijeshi kutoka Kenya hadi nchi jirani baada ya leseni kukosa kuidhinishwa na kuongeza kuwa mazoezi yote ya kijeshi yanategemea ruhusa kutoka kwa serikali ya Kenya.
Soma Zaidi:
Ghana yaomboleza kifo cha mwanaume mrefu zaidi nchini humo
Kifo cha Sulemana Abdul Samed, aliyekuwa mwanaume mrefu zaidi nchini Ghana, kimezua majonzi makubwa, hasa kaskazini mwa nchi ambako urefu wake ulimfanya kuwa mtu maarufu katika jamii.
Sulemana mwenye umri wa miaka 33 alifariki dunia akiwa hospitalini Jumatatu katika mji wa Tamale, ulioko takriban kilomita 160 kusini mwa kijiji chake cha Gambaga alikokuwa amelazwa baada ya vidonda vya miguu yake kupata maambukizi.
"Kila mtu alijua jinsi alivyokuwa mkarimu na mwenye moyo mwema. Tangu alipofariki hadi sasa, watu wengi bado wanaendelea kufika nyumbani kujua kilichotokea," amesema ndugu yake, Sulemana Abdul Kudus, alipozungumza na BBC.
Sulemana aligundulika kuwa na ugonjwa nadra unaosababisha watoto kukua kupita kiasi na kufikia urefu usio wa kawaida akiwa katika miaka yake ya ishirini.
Hali Ilivyokuwa wakati tetemeko kubwa la ardhi lilipoikumba Japan
Tetemeko kubwa la ardhi liliikumba kisiwa cha Kyushu nchini Japan tarehe 28 Julai, na kuwalazimu zaidi ya watu 150,000 kuhama makazi yao.
Tetemeko hilo lilikatiza huduma za umeme katika maeneo mbalimbali na kuharibu barabara, kubomoa sehemu ya ukuta wa kasri, na kusababisha daraja la watembea kwa miguu kuporomoka.
Kwa mujibu wa polisi, wakinukuliwa na shirika la utangazaji la umma la Japan, NHK, zaidi ya kaya 40,000 bado hazina umeme.
Aidha, watu kadhaa wanaripotiwa kutoweka baada ya chimni (bomba kubwa la moshi) kuporomoka katika kiwanda cha kutengeneza karatasi mkoani Kumamoto.
Soma Zaidi:
Uamuzi wa mahakama ya DRC wamfungulia njia ya muhula wa tatu Tshisekedi
Uamuzi wa mahakama ya DRC wamfungulia njia ya muhula wa tatu Tshisekedi
Mahakama ya Kikatiba ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeidhinisha sheria muhimu ya kura ya maoni, hatua ambayo huenda ikamfungulia Rais Félix Tshisekedi njia ya kugombea muhula wa tatu madarakani.
Mwenyekiti wa Mahakama hiyo amesema muswada huo, uliopitishwa na Bunge la Seneti mnao mwezi Juni, unaendana na Katiba, hivyo kuidhinisha vifungu vinavyoruhusu kufanyiwa marekebisho.
Upinzani umelaani sheria hiyo, ukisema suala hilo linarejesha nyuma juhudi za kutatua mzozo wa muda mrefu unaoendelea mashariki mwa Congo.
Maelfu ya watu wameandamana katika miji ya mashariki wa Goma na Bukavu kupinga hatua hiyo.
Rais Tshisekedi amebakisha miaka miwili katika muhula wake wa pili na wa mwisho wa uongozini.
Zelensky, Netanyahu wakutana na Trump huku vita vya Ukraine na Iran vikiendelea
Rais Donald Trump amefanya mikutano tofauti na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, mikutano ambayo Ikulu ya Marekani ilielezea kuwa ya "kujenga na yenye tija".
Viongozi hao wawili walikuwa Washington kuhudhuria maziko ya Seneta Lindsey Graham, ambaye alikuwa mfuasi mkubwa wa Israel na mtetezi wa misaada ya Marekani kwa Ukraine, ambaye alifariki dunia mapema mwezi huu.
Zelensky na Trump walijadili matumaini ya Kyiv kwamba Marekani ingesaidia kuimarisha mifumo yake ya ulinzi wa anga, ingawa hakuna ahadi rasmi iliyotolewa hadi sasa.
Kwa upande wake, Netanyahu aliwasili wakati ambapo uhusiano kati ya Marekani na Israel ulikuwa umetetereka kutokana na mitazamo tofauti kuhusu Iran.
Kabla ya ziara hiyo, ilitarajiwa kuwa Zelensky angemshinikiza Trump kutimiza ahadi aliyotoa katika mkutano wa kilele wa NATO mwezi huu ya kuipa Ukraine kibali cha kutengeneza makombora ya Patriot ya kuzuia mashambulizi ya anga.
Kwa muda mrefu Ukraine imekuwa ikitaka makombora ya Patriot ya Marekani; Kyiv inasema makombora hayo yanaweza kutumika kuilinda miji ya Ukraine dhidi ya mashambulizi yanayoongezeka ya ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu kutoka Urusi kote nchini humo.
Hata hivyo, mkutano huo uliofanyika kwa faragha ulimalizika bila tangazo lolote thabiti kuhusu msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine.
Trump aliandika kwenye mtandao wa Truth Social kwamba mkutano huo "ulienda vizuri sana!"
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Zelensky alimshukuru rais wa Marekani kwa "kila tunachofanya kwa pamoja kulinda maisha ya raia wa Ukraine".
Aliongeza kuwa wawili hao walijadili kuhusu vibali vya Patriot na "mawazo kadhaa ambayo yanaweza kusaidia".
"Tulizungumzia pia masuala ya kidiplomasia," aliandika. "Ni muhimu mchakato wa kidiplomasia ufufue nguvu mpya."
Katika ujumbe mwingine tofauti, Zelensky amesema alikutana na wawakilishi wa kampuni ya Marekani inayotengeneza zana za kijeshi ya Lockheed Martin ili kujadili "kuendeleza zaidi ushirikiano wao.
Soma Zaidi:
WAFCON 2026: Nigeria wachapwa na Malawi 3-2
Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake huko Morocco zimezidi kuchangamka.
Mabingwa watetezi Nigeria maarufu Super Falcons wameangukia pua baada ya kukubali kichapo cha magoli 3-2 mbele ya Malawi.
Bila kutarajiwa na wengi, mabingwa hao mara 10 wa Afrika walijikuta wapo nyuma kwa magoli 2-0 yaliyopishana kwa dakika 6 tu mpira ukielekea ukingoni.
Dakika za mwisho zilishuhudia magoli matatu na kuibua shangwe kwa Malawi ambayo magoli yake matatu yalitiwa kimiani na Temwa Chawinga, huku ya Nigeria yakifungwa na Uchenna Kanu na Rasheedat Ajibade.
Katika mchezo wa mapema, Zambia waliwafundisha kandanda Misri kwa kichapo cha magoli 6-0 huku Barbra Banda akitia nyavuni magoli matatu.
Hii leo kuna michezo miwili ya Kundi D: Ghana itakabiliana na Cape Verde, kabla ya Cameroon kupambana na Mali.
Pia unaweza kusoma:
Waliofariki kwa tetemeko la ardhi Japan wafikia 13
Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, amesema kuwa watu wasiopungua kumi na tatu sasa wamethibitishwa kufariki dunia kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Jumanne katika kisiwa cha Kyushu, kusini mwa Japan.
Bi. Takaichi amesema watu wengi bado wanahesabika kuwa hawajulikani walipo au wanasubiri kuokolewa, huku akieleza kuwa vikosi vya uokoaji vinapambana ili kuokoa manusura.
Operesheni za uokoaji zinaendelea katika duka moja kubwa nchini Japan la Aeon Mall, ambako watu watatu wamethibitishwa kufariki dunia.
Awali, idara ya zimamoto ya eneo hilo ilisema watu kadhaa walikuwa wamenaswa ndani ya duka hilo huku pia kukiwa na taarifa za matetemeko madogo.
Eneo la Kumamoto, ambako duka kubwa Aeon Mall liko ni mji ulioko katika kisiwa cha Kyushu, kimoja kati ya visiwa vinne vikuu nchini Japan. Kisiwa hicho cha kusini ni cha tatu kwa ukubwa na cha pili kwa idadi ya watu nchini Japan.
Afisa wa Mawasiliano ya Umma wa Mkoa huo Akino Sonoda, amesema watu wanane wameokolewa kutoka katika kituo hicho cha Aeon Mall.
Iran na Marekani zashambuliana tena, utulivu wa muda mfupi wasambaratika
Iran imefyatua makombora kadhaa ya masafa marefu kuelekea vikosi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati, katika kile ambacho jeshi la Marekani limesema kilikuwa jaribio la kushtukiza.
Tukio hilo limekatiza kipindi kifupi cha utulivu kilichokuwa kimeanza kurejesha matumaini ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), mashambulizi hayo yalitokea Jumanne saa 5:45 jioni kwa saa za Mashariki mwa Marekani (21:45 GMT). Jeshi hilo linasema makombora yote yalidunguliwa kabla ya kufika maeneo yaliyolengwa, ingawa halikutaja yenyewe.
Wakati huohuo, Marekani kwa kushirikiana na Saudi Arabia ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo yaliyodaiwa kutumiwa na makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq.
CENTCOM imesema hatua hiyo ilikuwa ni kulipiza kisasi mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa dhidi ya maeneo ya Marekani katika kipindi cha saa 72 zilizopita.
Hadi sasa, Iran haijatoa tamko rasmi kuhusu madai hayo.
Mapigano haya yanahitimisha kipindi kifupi cha utulivu ambacho kilitarajiwa kutoa fursa kwa juhudi za kidiplomasia na mazungumzo kati ya Marekani na Iran.
Soma Zaidi: