Moja kwa moja, Saudi yaungana na Marekani kushambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran

Marekani ilisema shambulio hilo lilitokea saa 17:45 EDT (21:45 GMT) Jumanne huku Iran ikisema ililenga kambi ya Marekani nchini Jordan.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Venezuela yakerwa na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya nje wa Iran dhidi yake

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela ilitangaza katika taarifa kwamba ilimwita balozi wa Iran siku ya Jumanne ili kuwasilisha malalamiko yake kuhusu kauli ilizozitaja kuwa za "kudhalilisha na zisizofaa."

    Bado haijabainika ni hatua au kauli zipi zitakazojumuishwa katika malalamiko hayo ya Venezuela, lakini hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisema katika mahojiano: "Iran sio Venezuela," jambo linaloashiria kuwa kuitwa kwa balozi wa Iran kunahusiana na muktadha huo.

    Mnamo mwezi Januari mwaka jana, vikosi vya Marekani vilimteka nyara Rais Nicolas Maduro nchini Venezuela katika operesheni isiyo na kifani na kumfungulia mashtaka nchini humo.

  2. Uchunguzi waanzishwa Kenya baada ya tembo 14 kufa katika njia ya kutatanisha

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka nchini Kenya zimeanzisha uchunguzi wa dharura kuhusu vifo vya kutatanisha vya tembo 14 kusini mwa nchi hiyo, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Amboseli.

    Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) liliiambia BBC kuwa wataalamu wanachunguza mizoga hiyo na kwamba sampuli za tembo hao zimepelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini ikiwa chanzo cha vifo hivyo kilikuwa ugonjwa, sumu au sababu nyingine.

    Hifadhi ya Taifa ya Amboseli na maeneo yanayoizunguka, yanayojulikana kama Mfumo wa Ikolojia wa Amboseli, yanachukua eneo kubwa kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania na yanajulikana kwa utajiri wake wa aina mbalimbali za wanyamapori.

    Maafisa wanasema hii ni mara ya kwanza katika miongo kadhaa ambapo idadi kubwa kama hiyo ya vifo vya tembo imerekodiwa katika eneo hilo, ambalo limefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu wa tembo katika miaka ya hivi karibuni.

    Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya limesema kuwa "kwa sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa kuna chanzo cha vifo vya tembo hawa."

    Pi unaweza kusoma:

  3. Iran yakanusha mpango wa usimamizi wa pamoja wa lango la Hormuz na Oman - Reuters

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Afisa wa ngazi ya juu wa Iran amepuuzilia mbali uwezekano wa kubuniwa kwa utaratibu wa nchi hiyo kusimamia lango la Bahari la Hormuz kwa ushirikiano na Oman.

    Akizungumza na shirika la habari la Reuters kwa sharti la kutotajwa jina afisa huyo alisema: Mfumo wa udhibiti wa pamoja wa Hormuz hautakuwa na manufaa kwa maslahi ya Iran, ingawa Tehran inaichukulia Oman kama jirani mshirika wa thamani.

    Siku ya Jumanne Reuters iliripoti likinukuu maafisa wa eneo hilo, kwamba Oman imewasilisha pendekezo jipya kwa Iran la kuanzisha mfumo wa pamoja wa kikanda unaolenga kusimamia Mlango-bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pendekezo hilo linahusisha michango ya hiari kutoka kwa nchi zinazoshiriki.

    Chanzo kimoja katika eneo hilo, ambacho kiliomba kutotajwa jina, kiliiambia Reuters kuwa mpango huo wa Oman unaungwa mkono na nchi za eneo hilo.

    Soma zaidi:

  4. Maafisa watano wa usalama Kenya wauawa katika shambulizi la Al-Shabaab

    .

    Chanzo cha picha, AP

    Maafisa watano wa usalama wa Kenya wameuawa katika mapigano na wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa Al-Shabaab Kaunti ya Mandera, karibu na mpaka wa Somalia, polisi wamesema.

    Kundi hilo la wanamgambo limekuwa likipigana kwa miaka kadhaa likitaka kuipindua serikali kuu ya Somalia na kuanzisha utawala wake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, kwa kuzingatia tafsiri yake kali ya sheria za Kiislamu (Sharia).

    "Timu ya doria kutoka kikosi cha SOG Alungu ilikutana na wanamgambo wa Al-Shabaab katika eneo la Bwawa la Wantey," polisi walisema katika taarifa yao kufuatia mapigano yaliyotokea Jumanne majira ya saa sita mchana.

    Polisi waliongeza kuwa wanaendelea kuwafuatilia wanamgambo hao baada ya kikosi cha nyongeza kilichotumwa eneo hilo kukumbwa na mlipuko wa bomu la kutegwa barabarani, ulioharibu gari la kivita lenye kinga dhidi ya mashambulizi

    Hata hivyo, hakuna majeruhi walioripotiwa katika tukio hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Saudi yaungana na Marekani kushambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran

    .

    Chanzo cha picha, Handout photo by US. Navy via Getty Images

    Saudi Arabia imejiunga na Marekani katika mashambulizi dhidi ya kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq, katika hatua inayoweza kuongeza mvutano wa mzozo wa Mashariki ya Kati.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) ilisema mashambulizi hayo yalilenga "magaidi wanaoungwa mkono na Iran ambao walielekezwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kushambulia majeshi ya Marekani na miundombinu ya nishati ya Saudia".

    Taarifa hiyo haikutaja jina la kundi la wanamgambo. Hata hivyo, Popular Mobilisation Forces (PMF) ilisema takriban wanachama wake 10 wameuawa.

    Tukio hilo limekuja baada ya Iran kurusha makombora kadhaa ya balistiki katika kile ambacho Centcom ilikitaja kuwa "jaribio la kushambulia kwa kushtukiza" vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati. Mvutano huo unaashiria ukomo wa kifupi cha utulivu katika uhasama kati ya Marekani na Iran.

    Marekani ilisema shambulio hilo lilitokea saa 17:45 EDT (21:45 GMT) Jumanne, huku makombora yote yakifanikiwa kuzuiwa. Iran ilisema kuwa ililenga kambi ya Marekani nchini Jordan.

    Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) pia kilisema kuwa kilishambulia meli tatu za mafuta katika Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim.

    Soma Zaidi Hapa:

  6. Kenya na Uingereza kuanza tena mafunzo ya pamoja ya kijeshi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Kenya imetangaza kuanza tena kwa mafunzo ya pamoja ya kijeshi kati ya Kenya na Uingereza katika Kituo cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) kilichopo Nanyuki, siku chache baada ya kuwepo kwa sintofahamu kuhusu kusitishwa kwa zoezi hilo.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Julai 28, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alisema hatua hiyo inaonyesha uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili, unaojengwa kwa kuheshimiana na kushirikiana kwa njia yenye tija.

    Mudavadi alisema uamuzi huo unaonyesha kuwa nchi hizo mbili zina uwezo wa kutatua changamoto kupitia mazungumzo huku zikiendelea kudumisha ushirikiano wao wa kimkakati.

    "Ushirikiano wa ulinzi kati ya Kenya na Uingereza unaendelea kuimarisha maslahi ya kitaifa ya Kenya. Unaongeza uwezo wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya (KDF), unachangia amani na usalama katika eneo hili, unaunga mkono ajira na biashara za Wakenya, na unaleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa jamii wenyeji," alisema.

    Mudavadi aliongeza kuwa Kenya itaendelea kujikita katika kuimarisha ushirikiano wa ulinzi na Uingereza pamoja na kuendeleza juhudi za pamoja za kukuza amani, usalama na utulivu katika eneo la Afrika Mashariki.

    Awali, Uingereza ilitoa taarifa ikisema imehamisha shughuli zake za kijeshi kutoka Kenya hadi nchi jirani baada ya leseni kukosa kuidhinishwa na kuongeza kuwa mazoezi yote ya kijeshi yanategemea ruhusa kutoka kwa serikali ya Kenya.

    Soma Zaidi:

  7. Ghana yaomboleza kifo cha mwanaume mrefu zaidi nchini humo

    .

    Kifo cha Sulemana Abdul Samed, aliyekuwa mwanaume mrefu zaidi nchini Ghana, kimezua majonzi makubwa, hasa kaskazini mwa nchi ambako urefu wake ulimfanya kuwa mtu maarufu katika jamii.

    Sulemana mwenye umri wa miaka 33 alifariki dunia akiwa hospitalini Jumatatu katika mji wa Tamale, ulioko takriban kilomita 160 kusini mwa kijiji chake cha Gambaga alikokuwa amelazwa baada ya vidonda vya miguu yake kupata maambukizi.

    "Kila mtu alijua jinsi alivyokuwa mkarimu na mwenye moyo mwema. Tangu alipofariki hadi sasa, watu wengi bado wanaendelea kufika nyumbani kujua kilichotokea," amesema ndugu yake, Sulemana Abdul Kudus, alipozungumza na BBC.

    Sulemana aligundulika kuwa na ugonjwa nadra unaosababisha watoto kukua kupita kiasi na kufikia urefu usio wa kawaida akiwa katika miaka yake ya ishirini.

  8. Hali Ilivyokuwa wakati tetemeko kubwa la ardhi lilipoikumba Japan

    Maelezo ya video, Wakati tetemeko kubwa la ardhi lilipoikumba Japan japo jana siku ya Jumanne.

    Tetemeko kubwa la ardhi liliikumba kisiwa cha Kyushu nchini Japan tarehe 28 Julai, na kuwalazimu zaidi ya watu 150,000 kuhama makazi yao.

    Tetemeko hilo lilikatiza huduma za umeme katika maeneo mbalimbali na kuharibu barabara, kubomoa sehemu ya ukuta wa kasri, na kusababisha daraja la watembea kwa miguu kuporomoka.

    Kwa mujibu wa polisi, wakinukuliwa na shirika la utangazaji la umma la Japan, NHK, zaidi ya kaya 40,000 bado hazina umeme.

    Aidha, watu kadhaa wanaripotiwa kutoweka baada ya chimni (bomba kubwa la moshi) kuporomoka katika kiwanda cha kutengeneza karatasi mkoani Kumamoto.

    Soma Zaidi:

  9. Uamuzi wa mahakama ya DRC wamfungulia njia ya muhula wa tatu Tshisekedi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Uamuzi wa mahakama ya DRC wamfungulia njia ya muhula wa tatu Tshisekedi

    Mahakama ya Kikatiba ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeidhinisha sheria muhimu ya kura ya maoni, hatua ambayo huenda ikamfungulia Rais Félix Tshisekedi njia ya kugombea muhula wa tatu madarakani.

    Mwenyekiti wa Mahakama hiyo amesema muswada huo, uliopitishwa na Bunge la Seneti mnao mwezi Juni, unaendana na Katiba, hivyo kuidhinisha vifungu vinavyoruhusu kufanyiwa marekebisho.

    Upinzani umelaani sheria hiyo, ukisema suala hilo linarejesha nyuma juhudi za kutatua mzozo wa muda mrefu unaoendelea mashariki mwa Congo.

    Maelfu ya watu wameandamana katika miji ya mashariki wa Goma na Bukavu kupinga hatua hiyo.

    Rais Tshisekedi amebakisha miaka miwili katika muhula wake wa pili na wa mwisho wa uongozini.

  10. Zelensky, Netanyahu wakutana na Trump huku vita vya Ukraine na Iran vikiendelea

    .

    Chanzo cha picha, Zelensky Social Media Account/Handout

    Rais Donald Trump amefanya mikutano tofauti na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, mikutano ambayo Ikulu ya Marekani ilielezea kuwa ya "kujenga na yenye tija".

    Viongozi hao wawili walikuwa Washington kuhudhuria maziko ya Seneta Lindsey Graham, ambaye alikuwa mfuasi mkubwa wa Israel na mtetezi wa misaada ya Marekani kwa Ukraine, ambaye alifariki dunia mapema mwezi huu.

    Zelensky na Trump walijadili matumaini ya Kyiv kwamba Marekani ingesaidia kuimarisha mifumo yake ya ulinzi wa anga, ingawa hakuna ahadi rasmi iliyotolewa hadi sasa.

    Kwa upande wake, Netanyahu aliwasili wakati ambapo uhusiano kati ya Marekani na Israel ulikuwa umetetereka kutokana na mitazamo tofauti kuhusu Iran.

    Kabla ya ziara hiyo, ilitarajiwa kuwa Zelensky angemshinikiza Trump kutimiza ahadi aliyotoa katika mkutano wa kilele wa NATO mwezi huu ya kuipa Ukraine kibali cha kutengeneza makombora ya Patriot ya kuzuia mashambulizi ya anga.

    Kwa muda mrefu Ukraine imekuwa ikitaka makombora ya Patriot ya Marekani; Kyiv inasema makombora hayo yanaweza kutumika kuilinda miji ya Ukraine dhidi ya mashambulizi yanayoongezeka ya ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu kutoka Urusi kote nchini humo.

    Hata hivyo, mkutano huo uliofanyika kwa faragha ulimalizika bila tangazo lolote thabiti kuhusu msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine.

    Trump aliandika kwenye mtandao wa Truth Social kwamba mkutano huo "ulienda vizuri sana!"

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Zelensky alimshukuru rais wa Marekani kwa "kila tunachofanya kwa pamoja kulinda maisha ya raia wa Ukraine".

    Aliongeza kuwa wawili hao walijadili kuhusu vibali vya Patriot na "mawazo kadhaa ambayo yanaweza kusaidia".

    "Tulizungumzia pia masuala ya kidiplomasia," aliandika. "Ni muhimu mchakato wa kidiplomasia ufufue nguvu mpya."

    Katika ujumbe mwingine tofauti, Zelensky amesema alikutana na wawakilishi wa kampuni ya Marekani inayotengeneza zana za kijeshi ya Lockheed Martin ili kujadili "kuendeleza zaidi ushirikiano wao.

    Soma Zaidi:

  11. WAFCON 2026: Nigeria wachapwa na Malawi 3-2

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake huko Morocco zimezidi kuchangamka.

    Mabingwa watetezi Nigeria maarufu Super Falcons wameangukia pua baada ya kukubali kichapo cha magoli 3-2 mbele ya Malawi.

    Bila kutarajiwa na wengi, mabingwa hao mara 10 wa Afrika walijikuta wapo nyuma kwa magoli 2-0 yaliyopishana kwa dakika 6 tu mpira ukielekea ukingoni.

    Dakika za mwisho zilishuhudia magoli matatu na kuibua shangwe kwa Malawi ambayo magoli yake matatu yalitiwa kimiani na Temwa Chawinga, huku ya Nigeria yakifungwa na Uchenna Kanu na Rasheedat Ajibade.

    Katika mchezo wa mapema, Zambia waliwafundisha kandanda Misri kwa kichapo cha magoli 6-0 huku Barbra Banda akitia nyavuni magoli matatu.

    Hii leo kuna michezo miwili ya Kundi D: Ghana itakabiliana na Cape Verde, kabla ya Cameroon kupambana na Mali.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Waliofariki kwa tetemeko la ardhi Japan wafikia 13

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, amesema kuwa watu wasiopungua kumi na tatu sasa wamethibitishwa kufariki dunia kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Jumanne katika kisiwa cha Kyushu, kusini mwa Japan.

    Bi. Takaichi amesema watu wengi bado wanahesabika kuwa hawajulikani walipo au wanasubiri kuokolewa, huku akieleza kuwa vikosi vya uokoaji vinapambana ili kuokoa manusura.

    Operesheni za uokoaji zinaendelea katika duka moja kubwa nchini Japan la Aeon Mall, ambako watu watatu wamethibitishwa kufariki dunia.

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Awali, idara ya zimamoto ya eneo hilo ilisema watu kadhaa walikuwa wamenaswa ndani ya duka hilo huku pia kukiwa na taarifa za matetemeko madogo.

    Eneo la Kumamoto, ambako duka kubwa Aeon Mall liko ni mji ulioko katika kisiwa cha Kyushu, kimoja kati ya visiwa vinne vikuu nchini Japan. Kisiwa hicho cha kusini ni cha tatu kwa ukubwa na cha pili kwa idadi ya watu nchini Japan.

    Afisa wa Mawasiliano ya Umma wa Mkoa huo Akino Sonoda, amesema watu wanane wameokolewa kutoka katika kituo hicho cha Aeon Mall.

  13. Iran na Marekani zashambuliana tena, utulivu wa muda mfupi wasambaratika

    .

    Chanzo cha picha, Handout photo by US. Navy via Getty Images

    Iran imefyatua makombora kadhaa ya masafa marefu kuelekea vikosi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati, katika kile ambacho jeshi la Marekani limesema kilikuwa jaribio la kushtukiza.

    Tukio hilo limekatiza kipindi kifupi cha utulivu kilichokuwa kimeanza kurejesha matumaini ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili.

    Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), mashambulizi hayo yalitokea Jumanne saa 5:45 jioni kwa saa za Mashariki mwa Marekani (21:45 GMT). Jeshi hilo linasema makombora yote yalidunguliwa kabla ya kufika maeneo yaliyolengwa, ingawa halikutaja yenyewe.

    Wakati huohuo, Marekani kwa kushirikiana na Saudi Arabia ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo yaliyodaiwa kutumiwa na makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq.

    CENTCOM imesema hatua hiyo ilikuwa ni kulipiza kisasi mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa dhidi ya maeneo ya Marekani katika kipindi cha saa 72 zilizopita.

    Hadi sasa, Iran haijatoa tamko rasmi kuhusu madai hayo.

    Mapigano haya yanahitimisha kipindi kifupi cha utulivu ambacho kilitarajiwa kutoa fursa kwa juhudi za kidiplomasia na mazungumzo kati ya Marekani na Iran.

    Soma Zaidi:

  14. Hujambo Msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara tarehe ni 29/07/2026.