Uefa yaikosoa Fifa baada ya Trump kuingilia kati kadi nyekundu
Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa) imekosoa vikali uamuzi wa kushangaza wa Fifa wa kutounga mkono kadi nyekundu dhidi ya mchezaji Folarin Balogun katika Kombe hili la Dunia, na kusema "haujawahi kutokea, haueleweki na haukubaliki."
Mshambuliaji wa Marekani Balogun, ambaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu wakati wa mechi dhidi ya Bosnia-Herzegovina, alipaswa kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi ya raundi ya 16 dhidi ya Ubelgiji itakayochezwa siku ya Jumanne.
Lakini waandaaji wa Kombe la Dunia, Fifa, ambao ni shirikisho linaloongoza soka duniani, walichagua kutotekeleza adhabu hiyo kwa mchezaji huyo wa miaka 25, ikimaanisha kuwa mfungaji bora wa timu hiyo atacheza mechi ijayo.
Uefa, shirikisho linaloongoza soka barani Ulaya, limesema kuingilia kati ili kufuta kadi nyekundu katika mashindano hayo ni "kuvuka mstari mwekundu".
Kati ya kadi 188 nyekundu zilizotolewa tangu kuanzishwa kwa Kombe la Dunia, ni mchezaji mmoja tu aliyeondolewa adhabu hiyo.
Ni Garrincha ya Brazili mwaka 1962, ambapo kulikuwa na tuhuma za kuingiliwa kisiasa.
CBS News imethibitisha kwamba kurejea kwa Balogun kunakuja baada ya rais wa Marekani, Donald Trump kumpigia simu rais wa Fifa, Gianni Infantino siku ya Alhamisi na kuzungumza naye kuhusu kadi nyekundu hiyo.
Siku ya Jumapili, Rais Trump aliishukuru Fifa kwa kuondoa kadi nyekundu kwa mchezaji huyo.
Chama cha Soka cha Ubelgiji (RBFA) kilisema katika taarifa Jumatatu kwamba "hakina njia nyingine ila kupinga uhalali wa mchezaji huyo katika mechi ijayo".
Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Maxime Prevot alisema: "Ikiwa simu ndiyo sababu ya uamuzi huu usioeleweka, itakuwa ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za mpira wa miguu."
Rais wa zamani wa Fifa Sepp Blatter, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Infantino mwaka 2016 baada ya kashfa ya ufisadi, amenadika kwenye X kwamba "mpira wa miguu haupaswi kamwe kuwa uwanja wa nguvu za kisiasa".
Uefa imesema kusimamishwa kwa mchezaji "sio chaguo la hiari" bali ni "kanuni iliopo katika kanuni".
“Sheria zisiposimamiwa na wasimamizi, uadilifu wa mchezo uko hatarini na uaminifu wa shindano hudhoofishwa," Uefa imesema katika taarifa.
"Tunaeleza mashaka yetu kwa uamuzi huo ambao haujawahi kutokea, usioeleweka na usio na msingi."
Glenn Micallef, kamishna wa michezo wa Umoja wa Ulaya, amesema maamuzi kuhusu michezo "ni ya mashirika ya michezo, si ya wanasiasa".
Uefa na Fifa zimekuwa zikizozana kuhusu maamuzi kadhaa katika miezi ya hivi karibuni.
Baada ya Omar Artan kukataliwa kuingia Marekani kuchezesha Kombe la Dunia, Uefa ilimwalika Msomali huyo kuchezesha Kombe la Super Cup kati ya Paris St-Germain na Aston Villa Agosti 12.